Saturday, February 19, 2011

Mitambo ya Dowans itaifishwe, Waziri ajieleze kuhusu mgawo wa umeme

Naomba kutoa taarifa kwa umma kwamba sijawahi kutoa kauli popote ya kushauri Dowans ipewe mkataba wa miezi mitatu kama ilivyonukuliwa na chombo kimoja cha habari.

Gazeti la Mtanzania toleo namba 5388 la tarehe 16 Februari 2011 limeandika katika ukurasa wake wa kwanza kwamba “ Wabunge: Dowans iwashwe”; “January, Mnyika washauri mkataba wa miezi mitatu”.

Gazeti la Mtanzania limetaja kuwa chanzo chake ni mahojiano ya kipindi cha Jambo Tanzania kilichorushwa na TBC1 asubuhi ya tarehe 15 Februari 2011.

Napenda watanzania wenzangu wakumbuke kwamba kipindi hicho kilirushwa LIVE na katika kipindi husika hakuna kauli yoyote niliyoitoa ya kutaka mitambo ya Dowans iwashwe kwa mkataba wa miezi mitatu badala yake niliitaka serikali itumie sheria hususani ya uhujumu uchumi kuiwasha mitambo husika kwa maslahi ya taifa.

Katika kipindi hicho nilitoa kauli hiyo na kueleza kwamba nisingependa kwenda ndani zaidi katika hatua kwa wakati huo. Kauli yangu hiyo imenukuliwa kwa usahihi na Gazeti la Mwananchi toleo namba 03888 la tarehe 16 Februari 2011 katika ukurasa wa nne.

Ningependa kutumia fursa hii kusisitiza mtazamo wangu kwamba ni muhimu ili kupunguza adha ya mgawo wa umeme serikali itumie mamlaka yaliyopo kwenye katiba na sheria ikiwemo sheria ya uhujumu uchumi, sheria ya kupambana na rushwa, sheria ya mali zilizopatikana isivyo halali nk itaifishe mitambo hiyo haraka iwezekanavyo na kuiwasha kwa maslahi ya umma.

Ikumbukwe kwamba kampuni ya Dowans ilirithi mkataba toka kampuni ya Richmond ambayo ilithibitishwa kwa maazimio ya bunge kuwe ilipata mkataba katika mazingira ya ukiukwaji wa sheria ikiwemo sheria ya kupambana na rushwa. Pia, hata kampuni yenyewe ya Dowans kuna utata kuhusu usajili, umiliki na uhamasishaji wa mkataba wake kama suala zima likitazamwa kwa undani wake yakirejewa yaliyojiri Costa Rica na Tanzania.

Kampuni ya Dowans kama inataka kuepusha kutaifishwa basi wamiliki wake popote pale walipo duniani wajitokeze hadharani wakiri kwamba walipotoshwa na Richmond pamoja na vyombo vya kiserikali wakati wa kuhamishwa mkataba ili wajijengee uhalali wa kufanya majadiliano ikiwemo ya kufuta madai ya fidia inayotaka kutolewa kwa mujibu wa hukumu ya ICC.

Aidha wakati mjadala kuhusu MW 120 za Dowans ukiendelea na kwa kuwa kiasi hicho hakiwezi kuziba pengo la takribani MW 240 ambalo linakabili taifa hivi sasa, ni muhimu kwa Waziri wa Nishati na Madini kutoa maelezo ya kina kuhusu hatua ambayo serikali inataka kuchukua ya kukodi mitambo ya MW 260. Aidha, Waziri atoe ufafanuzi wa kutokukamilika kwa mipango ya serikali wakati ambapo dharura ya umeme ilijulikana toka mwaka 2002, serikali ikaijadili kwa kina mwaka 2006, bunge likapitisha maazimio mwaka 2008 na serikali ikaahidi tena mwaka 2009 kuweka utaratibu wa kukabiliana na dharura hiyo. Katika muktadha huo ni muhimu kwa bunge kupata fursa ya kujadili kwa kina suala la umeme katika mkutano unaoendelea wa bunge kama jambo la dharura ili kuweza kulinusuru taifa. Nitatoa tamko la kina hivi karibuni kwa nafasi yangu ya uwaziri kivuli kuhusu suala la umeme kwa kuzingatia hali ya mgawo inavyoendelea sanjari na kupanda kwa gharama za nishati hiyo kunakoongeza ugumu wa maisha kwa watanzania walio wengi baada ya majadiliano na baraza kivuli na mamlaka nyingine husika.

Imetolewa Dodoma leo tarehe 16/02/2011

John Mnyika (Mb)
0784222222

No comments: