Monday, February 21, 2011

Tamko langu la awali kuhusu kuwekwa X katika majengo ya pembeni ya Barabara ya Morogoro

Katika kipindi cha wiki moja mfululizo kuanzia tarehe 11 mpaka 17 Februari 2011 nikiwa bungeni Dodoma nimekuwa nikipokea simu na sms toka kwa wananchi wakilalamikia hatua ya wafanyakazi wa wakala wa Barabara Mkoa wa Dar es salaam (TANROADS) kupita katika nyumba zao zilizopembezoni mwa barabara ya Morogoro bila wakazi kupewa notisi na kuweka alama za “X” ama “BOMOA TNRD”.

Aidha nimesoma kwenye baadhi ya vyombo vya habari (mf. NIPASHE Toleo na. 056929 la tarehe 18 Februari 2011 Uk 1 na 8) habari yenye kichwa “bomoa bomoa nyingine kukumba wakazi wa Ubungo/Dar”

Habari hiyo imemnukuu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es salaam, James Nyabakari akiwataka watu wote waliojenga kwenye hifadhi ya Barabara kubomoa wenyewe na kwamba serikali haitawalipa kwa kuwa ni wavamizi na kwamba watakaolipwa ni wale tu ambao serikali itahitaji maeneo yao.

Taarifa zinazoelezwa ni kwamba alama hizo zimewekwa mita 90 pande zote mbili za barabara kuanzia maeneo ya Ubungo mpaka Kimara, na kwamba hali hiyo itawagusa pia wananchi wa Mbezi mpaka Kiluvya katika hatua za baadaye.

Nikiwa mwakilishi wa wananchi wa maeneo husika nimeshangazwa na hatua kubwa kama hizi za kiserikali kuchukuliwa bila kufanyika kwa mikutano ya umma ama walau kutoa taarifa ya kuelimisha umma kuhusu mipango husika inayotarajiwa kufanyika. Aidha nimeshangazwa zaidi na hatua kama hizo kuchukuliwa bila walau wawakilishi wa wananchi kama wenyeviti wa mitaa, madiwani na wabunge kuelezwa kwa kina mipango inayokusudiwa kufanyika na athari zake kwa wananchi wa maeneo husika. Utendaji kazi wa namna hii ni kinyume na misingi ya utawala bora inayotaka uwazi na pia ni chanzo cha migogoro isiyo ya lazima katika jamii.

Nachukua fursa hii kutoa mwito kwa serikali ngazi ya wizara ya ujenzi, mkoa na wilaya kuhakikisha kwamba mikutano na wananchi inafanyika ama walau matangazo kwa umma yanatolewa kuhusu suala husika.

Aidha mamlaka husika za kiserikali zitoe maelezo ya wazi kuhusu wananchi wanaostahili fidia na kutoa notisi ya muda wa kutosha kwa wakazi wenye majengo yanayostahili kubomolewa ili kupitisha barabara ya mradi wa mabasi yaendayo kwa haraka (DART) na mipango mingine.

Katika kufanya hivyo Serikali izingatie kuwa wapo wakazi wengi wenye kustahili kulipwa fidia kutokana na historia ya Barabara hiyo ya Morogoro kuliko ambavyo suala hili linavyotazamwa kijuujuu.

Ikumbukwe kwamba Mwaka 1932, wakati wa mkoloni, ilitungwa sheria ya barabara nchini, sheria hii inatambua na kuelezea uwapo wa barabara za umma nchini. Kiambatanisho cha sheria hii kinaitaja barabara itokayo Morogoro mpaka Iringa, maarufu kama barabara ya Morogoro kama barabara ya umma, pamoja na mambo mengine, sheria hii inampa waziri mwenye dhamana na barabara uwezo wa kuamua juu ya upana muafaka wa barabara za umma kwa kutoa tangazo kwenye gazeti la serikali.

Mnamo mwaka 1967, waziri mwenye dhamana ya barabara nchini alitoa notisi namba 161 kwenye gazeti la serikali, kupitia tangazo hilo upana wa barabara uliongezwa kutoka futi 33 za mwaka 1932 na kufikia futi 75, hii ni kutoka katikati.

Sheria hii ya mwaka 1967 ndio umekuwa msingi wa 'bomoa bomoa' na 'chukua chukua' inayotekelezwa na serikali chini ya mwavuli wa kile kinachojuulikana kama upanuzi wa barabara ya Morogoro. Hata hivyo ni vyema ikumbukwe kuwa tangazo hilo la serikali halikueleza juu ya maeneo yanayo milikiwa na watu binafsi.

Hivyo mamlaka husika zirejee kwamba utekelezaji wa sheria hauzingatii kikamilifu wakazi ambao wameyamiliki maeneo hayo kabla ya mwaka 1967 ambao kimsingi sheria hii imewakuta,hivyo wanahaki ya kulipwa fidia. Pamoja na ukweli kuwa katika miaka hiyo majengo yalikuwa bado hayajatamalaki lakini sehemu kubwa ya ardhi ilikuwa ni ama mashamba ya watu au maeneo ya ufugaji ambayo kwa muda wote huo yamekuwa yakirithishwa au kuuzwa vizazi hadi vizazi mpaka kufikia hatua ya sasa ya kuendelezwa. Kwa serikali inayofuata sheria zinazojali haki, watu hawa wanastahili fidia kwa kuwa sheria hii iliwakuta.

Ikumbukwe pia kwamba baada ya Barabara ya Morogoro kukamilika miaka ya mwanzoni mwa sabini, serikali ya Awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere ilianzisha kote nchini vijiji vya ujamaa na kuhamishia watu katika vijiji hivyo. Maeneo ya kati ya Ubungo na Kiluvya yalikuwa sehemu ya vijiji hivyo na watu wakahamishiwa katika maeneo hayo kwa ajili ya makazi. Dar es salaam ilitangazwa kama eneo la mjini mwaka 1985 bila ya wananchi wa maeneo husika kushirikishwa kwa ukamilifu.

Hivyo ni muhimu kwa mamlaka husika kurejea ukweli kwamba Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999 kifungu cha 15 kinatambua haki za watu walioishi katika vijiji kati ya tarehe 1 Januari 1970 na tarehe 31 Disemba mwaka 1977; hivyo kimsingi haki za wananchi wa eneo kati ya Ubungo na Kiluvya walioanza makazi yao katika kipindi husika zinapaswa kuthaminiwa na kulindwa.

Mamlaka husika zikumbuke kwamba mwaka 2001 bila kuzingatia sheria hiyo ya ardhi Wizara ya husika iliingilia makazi ya wananchi na kuongeza ukubwa wa eneo la hifadhi ya barabara kuwa mita 120 kila upande wa Barabara ya Morogoro.

Izingatiwe pia kwamba mwaka 2009 Waziri wa Miundombinu wa wakati huo Dr Shukuru Kawambwa alitoa kanuni kupitia gazeti la serikali namba 21 na 23 la Januari 2009 zilizopunguza eneo hilo kutoka mita 120 mpaka mita 60 kwa pande zote mbili za barabara katika maeneo mengi, mchakato huu nao ulifanyika kimya kimya bila wananchi kupewa taarifa za wazi na za kina.

Katika kanuni hizo maeneo mengi ya barabara ya Morogoro nchi nzima yametengwa kuwa mita kati ya 30 na 60 kwa pande zote mbili isipokuwa ya kutoka Ubungo mpaka Kiluvya ambayo yametengwa kwa kiwango kikubwa zaidi bila kuzingatia kwamba baadhi ya maeneo hayo yalishatolewa kihalali kwa wananchi kupitia sheria nyingine kama maeneo ya makazi kama nilivyoeleza awali. Hivyo, katika mazingira hayo, ikiwa serikali ina mpango wa kuongeza ukubwa wa barabara ziada ya eneo ambalo tayari lilishatolewa kwa wananchi na wajibu wa serikali kuhakikisha wananchi hao wanapata fidia stahili.
Baada ya sheria zingine kuwapa haki ya kuanzisha vijiji na baadaye miji Serikali iliwapa uhalali zaidi wa kuwa na makazi rasmi katika maeneo hayo kwa kuwapelekea huduma za msingi ambazo kisheria hutolewa maeneo halali yanayo tambulika kisheria. Serikali imewawekea miundo mbinu ya umeme, maji, simu na wengine wamepewa mpaka hati miliki na wizara ya ardhi. Iweje wizara ya ujenzi imwambie mtu kuwa ardhi anayo imiliki si halali wakati amesha milikishwa ardhi hiyohiyo na wizara ya ardhi? Au wizara ya ujenzi na ile ya ardhi ziko chini ya serikali mbili tofauti?

Kimsingi mimi kama mwakilishi wa wananchi wa eneo husika, naunga mkono suala la miradi ya maendeleo katika maeneo yetu; hata hivyo miradi hiyo lazima izingatie vile vile haki na stahili za wananchi wanaoondolewa kupisha miradi husika. Na ni muhimu kwa mchakato mzima kuwa shirikishi na taarifa sahihi kutolewa kwa wakati. Hivyo, pamoja na mikutano na taarifa ambazo nahimiza mamlaka husika kuzitoa na mimi kwa upande wangu nitatembelea maeneo yanayogusudiwa kubomolewa na nitafanya mikutano na wananchi kuhusu suala husika pindi nikirejea Dar es salaam. Aidha, natoa rai kwa wananchi wote wa maeneo husika ambao wanaamini kwamba haki zao zinavunjwa waweze kuunganisha nguvu ya umma katika kuhimiza uwajibikaji na kufuatilia stahili zao kama sehemu ya kutimiza wajibu wao wa kiraia kwa maendeleo ya kaya zao na taifa kwa ujumla.

Imetolewa safarini toka Dodoma tarehe 20 Februari 2011:

John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo

6 comments:

Filipo Lubua said...

Mimi nakupongeza sana Muheshimiwa kwa jitihada za kupigania haki za wananchi. Serikali imekuwa ikijifanya ina mipango ya maendeleo bila hata kuzingatia kuwa mipango hiyo inatakiwa iwafae wananchi na wala si kuwaangamiza.

Inaonekana kuwa mipango ya wizara moja na nyingine inakinzana na hivyo huwafanya wananchi wataabike na kunyanyasika. Jitihada zote hizo za kubomoa makazi ya wananchi tena bila utaratibu mzuri, inatufanya tupoteze imani na serikali hii isiyotutambua kama wanachi halali katika maeneo yetu husika. Ni katika programu hizihizi za kimaendeleo tunaposhuhudia rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma, licha ya wao kutukandamiza.

Lazima tusimame kutetea haki zetu.

Cou. Martin Godwin said...

'Haya ndio mambo tunayoyapata tunapokuwa na wataalamu wa vyeti, umeyaweka maelezo vizuri sana Mr. Mnyika, tatizo la watu ndani ya mamlaka wanaona watu ni wajinga, walikosea kuwa walipo, hawana haki na maeneo yao, bila hata kutambua historia ya eneo wanatoa tu matamko kwa mwonekano na utetezi wa sheria moja, sasa Kunduchi-Mtongani eneo la Machimbo linalopigiwa kelele lina Umeme na Maji kuliko hata maeneo mengine halali. Kazi yenu itakuwa ngumu kidogo Bungeni. MUNGU AWABARIKI' Cou. Martin Godwin

Temu, A.B.S said...

Tufuate mipango miji na tuweke mipango miji kabambe ya 100 years ahead.

Wananchi waelimishwe na haki zifuatwe na mawasiliano yafanyike ili taarifa ziwe timely.

Lingine kubwa kabisa, hizi VUNJA VUNJA in the name of modernization, sometimes ni wholly mislaced. Haswa pale inapoharibu heritage, environment and traditions. Hakuna hazina kubwa kwenye maendeleo kama kujua culture and tradition yako, na historia yako. Hivyo, hizi bomoa bomoa lazima zizingatie heritage - kama kuna vijiji vya Ujamaa hata kama vimebadilika, why destroy them? Jenga around these and if you say it is expensive, try destroying and see how expensive that is selling out own tradition or erasing it!

Willy Migodela said...

tanzania ni nchi inayoendeshwa kwa kuvunja sheria kitu ambacho kinapelekea watanzania kuwa waoga kudai haki zao. serikali inatumia udhaifu huo kuwaburuza watanzania. hata wabunge wengi hawajui sheria wanabaki kuwa watu wa ndio mzee kwa ujinga wao na kwa kuogopa kuongea ukweli ili waendelee kushikiria nafasi walizopewa. hongera wanaubungo kwa kupata mbunge wa ukweli. hongera mnyika, watanzania tuko pamoja nawe.

Arnold said...

Ubabe, Ubabe, Ubabe!!! Serikali ya mawaziri wa 'Ratili Moja, Pesa Moja". Siku yao inakaribia.

Relief said...

Utawala shirikishi ndio maana thabiti ya Utawala bora, mwananchi asipopewa taarifa sahihi juu ya mambo yanayomgusa yeye moja kwa moja lazima atatoa kilio lakini taarifa ikija sahihi kama hii hapa hatakama itakuwa inamuumiza mwananchi kiasi fulani, hatolalamika wala kutoa kilio kwani anakuwa amekwishaelewa. Tunahitaji ufafanuzi wa vina namna hii mara zote. We got your back broda!!

Salut,
MalkiaRelief.