Wednesday, August 3, 2011

Kuhusu maamuzi dhaifu ya CC ya CCM juu ya nishati na madini

Maamuzi yaliyofanywa na kamati kuu ya CCM katika kikao chake cha tarehe 31 Agosti 2011 kuhusu masuala mbalimbali yanayolikabili taifa hususani kuhusu nishati na madini imethibitisha ulegelege na kupoteza mwelekeo kwa serikali na chama hicho kwa ujumla.

Aidha maagizo hayo bado ni legelege na hayawezi kutoa muongozo thabiti kwa serikali katika kukabiliana na changamoto za msingi zinazolikabili taifa kwa sasa katika sekta za nishati na madini.

Kwa nyakati mbalimbali kuanzia mwaka 2005 nimekuwa nikitoa kauli za kueleza kwamba CCM na serikali yake ni legelege kiuongozi na kimaadili hali ambayo inaathiri maisha ya wananchi na mustakabali wa nchi kwa ujumla.

Hatimaye mwezi Februari mwaka 2007 wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya CCM Mwenyekiti wa chama hicho Rais Jakaya Kikwete akatambua hali hiyo na kurejea kauli ya Mwalimu Julius Nyerere kwamba “chama legelege huzaa serikali legelege’ na kueleza dhamira ya kuondoa ulegelege huo kuanzia kwenye chama na hatimaye katika serikali.
Hata hivyo, maagizo yaliyotolewa na kamati kuu katika kikao chake cha tarehe 31 Agosti 2011 kuhusu bei ya mafuta ya taa, matatizo ya umeme na masuala ya madini yamedhihirisha kwamba CCM na serikali yake bado hawajaondokana na ulegelege ambao kama usipodhibitiwa ni hatari kwa hatma ya nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Ni muhimu watanzania wakatambua kwamba Mwenyekiti wa CCM Rais Kikwete ambaye ndiye aliyeongoza kikao cha kamati kuu kilichotoa maagizo kuhusu bei ya mafuta ya taa, matatizo ya umeme na migogoro migodini ndiye kiongozi mkuu wa shughuli za serikali na mwenyekiti wa baraza la mawaziri ambalo vikao vyake vimejadili masuala hayo hayo na kupitisha maamuzi mabovu.

Aidha umma ukumbuke kwamba kabla ya Mkutano wa Nne wa Bunge hili la bajeti palifanyika vikao vya vyombo vya maamuzi vya CCM hususani sekretariati, kamati kuu na halmashauri kuu ambavyo vilijadili pamoja na ajenda nyingine hali ya siasa ikiwemo maandalizi ya bajeti na kushindwa kutoa maagizo muafaka kwa serikali hali ambayo imelitumbukiza taifa katika matatizo ya sasa.

Hivyo, maagizo yaliyotolewa kwa serikali na Kamati Kuu ya chama hicho ni ya kisiasa yenye kulenga kumkosha Rais Kikwete na CCM kufuatia malalamiko ya wananchi juu ya ugumu wa maisha na tishio la maandamano ya CHADEMA kuhusu maamuzi mabovu yaliyofanywa na serikali yaliyopitishwa kwa kura za wabunge walio wengi wa CCM bila kuzingatia maslahi ya wananchi.

Ikiwa maagizo hayo yametolewa kwa dhamira ya kweli ya chama kuisimamia serikali yanapaswa kuambatana na hatua ya Rais Kikwete kuvua magamba kwa kuvunja baraza la mawaziri kwa kushindwa kumshauri vizuri katika kuiongoza serikali.

Agizo la kamati kuu ya CCM la kuitaka serikali ‘kutafuta njia ya kushusha bei ya mafuta ya taa’ ni dhaifu kwa kuwa sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta hayo inajulikana wazi kuwa ni kupandishwa kwa kodi kulikofanywa tarehe 22 Juni 2011 hivyo; Kamati Kuu ya CCM ilipaswa kutoa agizo la kukubaliana na maoni tuliyotoa kwenye Bajeti Mbadala ya Nishati na Madini tarehe 15 Julai 2011 na kuiagiza serikali kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria ya fedha katika mkutano wa bunge unaoendelea ili kupunguza gharama za maisha kwa wananchi kwa kuondoa ongezeko kubwa lililofanywa kwenye kodi ya mafuta ya taa na pia kupunguza kodi zaidi kwenye dizeli na petroli.

Azimio la kamati kuu kueleza kusikitishwa na tatizo la umeme halionyeshi CCM kuwaomba radhi watanzania kutokana na kuliingiza taifa katika hali hiyo kutokana na uzembe, ufisadi na udhaifu wa kiuongozi. Aidha, azimio hilo halionyeshi kamati kuu kutambua uzito wa tatizo hilo kwa kulitangaza kuwa janga la taifa au hali ya dharura yenye kuhitaji uwajibikaji wa pamoja ikiwemo wa Rais Kikwete badala yake imelichukulia kuwa ni suala la kurekebisha bajeti ya nishati na madini kwa kuambatanisha mpango wa dharura. Kamati Kuu ya CCM ingetambua tatizo la ukosefu wa nishati linavyoathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kuwa ni janga la taifa ingetoa maagizo ya kukabiliana na maoni tuliyotoa kwenye bajeti mbadala ya nishati na madini tarehe 15 Julai 2011 ya kutaka sio tu kufanya marekebisho ya bajeti ya nishati na madini bali pia kwa Wizara ya Fedha kuwasilisha bajeti ya nyongeza (supplementary budget) ili kurekebisha kasoro zilizotokana na kupitishwa kwa bajeti finyu tarehe 21 Juni 2011. Aidha, kamati kuu ya CCM ingetambua kwamba taifa lipo kwenye hali ya dharura lingemtaka Rais Kikwete ambaye pia na mwenyekiti wa chama hicho kuwajibika kutumia mamlaka yake ya kikatiba ikiwemo ya hali ya dharura kuwezesha hatua za haraka kuchukuliwa.

Taarifa ya kwamba kamati kuu ya CCM imejadili masuala mengine kama ‘migogoro migodini’ na ‘kuagiza serikali kuyashughulikia kwani yanatatulika’ inaonyesha ulegelege na udhaifu wa chama hicho katika kuishauri na kuisimamia serikali. Kamati Kuu ya CCM ilipaswa kutoa maelekezo mahususi ya maeneo ya migogoro migodini kwa kuzingatia maoni tuliyoyatoa kwenye bajeti mbadala ya nishati na madini tarehe 15 Julai 2011. Aidha, Kamati Kuu ya CCM imejikita katika kutoa agizo la ujumla kuhusu migogoro migodini bila kutoa maagizo kuhusu suala muhimu zaidi kuhusu mapato katika madini na ufisadi katika sekta hiyo pamoja na gesi asilia. Kamati Kuu ya CCM ilipaswa kukubaliana na maoni tuliyotoa kwenye bajeti mbadala ya nishati na madini na kuiagiza serikali kuwasilisha muswada wa marekebisho ya kitabu cha mapato na sheria ya fedha ili kuongeza wigo wa mapato kwenye sekta ya madini na pia kuchukua hatua za kushughulikia ufisadi pamoja na kupanua uwekezaji katika gesi asilia ikiwemo ujenzi wa bomba la gesi.

Watanzania warejee hotuba ya bajeti mbadala ya nishati na madini ya kambi rasmi ya upinzani bungeni ambapo tulieleza bayana vyanzo vya matatizo kwenye sekta za nishati na madini ikiwemo suala la bei ya mafuta ya taa, tatizo la umeme, migogoro migodini na changamoto zingine na kueleza kwamba matatizo yamezidi kuongezeka baada ya kupitishwa kwa bajeti mbovu tarehe 21 Juni 2011 kwa kura za ndio za wabunge wa CCM bila kutanguliza mbele maslahi ya umma.

Umma ufahamu kwamba bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha Mustapha Mkullo tarehe 8 Juni 2011 ilishindwa kutenga fedha za kutosha za kushughulia matatizo ya umeme pamoja na upungufu wa gesi asilia ilipitia katika baraza la mawaziri chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete. Hata baada ya kambi rasmi ya upinzani kuwasilisha bajeti mbadala na serikali haikukubali kuzingatia maoni yaliyotolewa kwa uzito unaostahili.
Aidha muswada wa sheria ya fedha na marekebisho yake yaliyowasilishwa tarehe 22 Juni 2011 ambao uliongeza kodi kubwa katika mafuta ya taa na kuongeza misamaha ya kodi katika madini badala ya kupanua wigo wa mapato ulitokana na serikali inayoongozwa na CCM. Ikumbukwe kwamba wakati wa kujadiliwa sheria husika niliwasilisha marekebisho kwenye muswada yenye lengo la kupunguza kiwango cha kodi ambacho serikali ya CCM ilidhamiria kuongeza kwenye mafuta ya taa lakini yalikataliwa na serikali pamoja na wabunge wa CCM.

Bajeti ya Serikali pamoja na Sheria ya Fedha vyote vilipitishwa kwa kura ya ndio na wabunge wa CCM kwa kufuata kilichoelezwa kuwa ni msimamo wa chama uliofikiwa katika kikao cha kamati ya wabunge wa chama hicho (party caucus) kwa maelezo kwamba ni utekelezaji wa sera na ilani za chama hicho.

Sehemu kubwa ya Kamati Kuu ya CCM ni wabunge ambao tayari walishapiga kura bungeni kupitisha bajeti na sheria bila kuzingatia mahitaji ya nishati na madini kwa kuongeza gharama za maisha kwa wananchi kupitia kupandisha bei ya mafuta ya taa, kupitisha bajeti isiyokidhi mahitaji ya kukabiliana na matatizo ya umeme na kushindwa kupanua wigo wa mapato katika madini.

Hivyo, ni muhimu Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM akaliomba radhi taifa kutokana na hali hiyo na pia CCM ikawaagize wabunge wake kuwaomba radhi wananchi wa majimbo yao na watanzania kwa kupiga kura ya ndio kwa kutanguliza mbele maslahi ya chama badala ya maslahi ya umma.

Aidha natoa mwito kwa kamati kuu za vyama vingine vyenye uwakilishi bungeni ikiwemo CHADEMA inayoongoza kambi rasmi ya upinzani bungeni kuitisha vikao vya dharura kabla ya mkutano wa bunge unaoendelea hivi sasa kumalizika kujadili hali ya siasa ili kutoa ushauri kwa wabunge wake na serikali kwa ujumla kwa ajili ya kulinusuru taifa kwa kuwa nchi ipo katika hali tete.

Izingatiwe kuwa Kwa sehemu kubwa matatizo katika sekta za nishati na madini yamechangiwa na sababu za kibinadamu za kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji kwa viongozi wa kiserikali kuanzia kwa viongozi wakuu wa nchi, wizara na watendaji wengine na hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi.

Uwajibikaji unahitajika ukiambatana na hatua za haraka za kusimamia sera sahihi, uongozi makini na taasisi thabiti zenye kuelewa kwamba sekta ya nishati ni moyo wa taifa na sekta ya madini ni mtaji wetu kwa sasa na kuchukua hatua kali dhidi ya ufisadi uliofanyika katika sekta husika, kufanya mapitio ya mikataba, kuharakisha utekelezaji wa mipango kwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
Bungeni, Dodoma-02/08/2011

1 comment:

Anonymous said...

JM
Nakuaminia sana na nakubali uwjibikaji wako.

Kama kuna uwezekano wa kutoa article hii kwenye magazeti (kama tangazo au vinginevyo) naamini watanzania wengi tunahitaji utambuzi.

kila la heri!!!!!!!!!!