Kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) na (3) mamlaka ya bunge ni kutunga sheria na kusimamia serikali. Kutokana na mamlaka hayo kazi za mbunge ni kuwakilisha wananchi, kushiriki katika kutunga sheria pamoja na kuisimamia serikali na viongozi wake.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dr Shukuru Kawambwa aliahidi bungeni kwenye mkutano wa nne kwamba serikali imepata mkakati wa kumaliza migogoro na matatizo katika vyuo vikuu nchini na kwamba hatua za haraka zingechukuliwa kama sehemu ya utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2012/12.
Hata hivyo, badala ya migomo na migogoro kumalizika inaelekea kuongezeka. Katika siku za karibuni pamekuwepo na maandamano ya mara kwa mara katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS). Aidha, hali ya mambo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) haijatulia mpaka sasa, huku wanafunzi 567 wakiwa bado wamesimamishwa. Katika kipindi cha mwezi mmoja imekuwa ikijirudia rudia hali ya mvutano baina ya wanafunzi na utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).
Hali katika vyuo vikuu hivi na vingine haiendani na ahadi ambayo Waziri Kawambwa alizitoa bungeni na kwa umma miezi kadhaa iliyopita. Leo nimeingia ofisini jimboni na kukatizwa kazi za kufuatilia masuala mengine ya wananchi na habari za mgomo katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam Mlimani.
Pamoja na kuwa bado sijapokea taarifa rasmi ya toka kwa Utawala wa Chuo au kwa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO); wakati nikifuatilia taarifa zaidi nimeona nichukue hatua za kiutendaji za kuwasiliana na wizara yenye dhamana ili waweze kuingilia kati kama sehemu ya kutimiza ahadi iliyotolewa bungeni.
Katika kukabiliana migomo na migogoro katika elimu ya juu serikali imekuwa ikichukua hatua dhidi ya matokeo badala ya kushughulikia vyanzo vya matatizo hivyo natarajia wakati huu Waziri husika atajielekeza katika madai ya msingi ya wanafunzi na wahadhiri.
Serikali izingatie kwamba chimbuko la mgogoro wa MUHAS ni tofauti katika utekelezaji wa agizo la serikali la tarehe 12 Juni 2009 (GN. 178) ambayo limefanya mabadiliko ya makubwa kwenye uendeshaji wa serikali za wanafunzi katika vyuo vikuu na hivyo kuanzisha mivutano baina ya wanafunzi na utawala katika chuo hicho na vyuo vingine nchini.
Serikali irejee kwamba chanzo cha migomo UDOM ni madai ya wanafunzi kuhusu mafunzo kwa vitendo na malalamiko mengine kutoka kwa wahadhiri. Toka wanafunzi wasimamishwe mwezi Juni 2011 mpaka sasa ikiwa imepita karibu miezi sita wanafunzi 567 bado wamesimamishwa masomo huku zoezi la kumhoji mmoja mmoja likisuasua na kutarajiwa likiwa limepangwa kumalizika mwishoni mwa Mwezi Machi mwaka 2011. Serikali inaweza kabisa kwa kushirikiana na chuo kuharakisha taratibu za kinidhamu wakati huo huo kushughulikia madai ya msingi ya wanafunzi ili kuepusha mazingira ya mivutano kudumu kwa muda mrefu.
Serikali itambue kwamba chanzo cha migomo ya hivi karibuni UDSM ni kugeuzwa kwa taratibu za utoaji mikopo na hatimaye kuchelewa kwa malipo ya wanafunzi na wengine kupata pungufu au kukosa kabisa. Katika mazingira hayo ni muhimu kwa Waziri Kawambwa kuweka wazi kwa umma ripoti ya Tume ya Rais iliyoundwa tarehe 14 Februari 2011 na kukabidhi taarifa yake tarehe 29 Aprili yenye mapendekezo ya jinsi ya kuboresha utaratibu wa sasa wa ugharamiaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu.
Kuwekwa wazi kwa taarifa hii kutawezesha wawakilishi wa wananchi, wanafunzi, wazazi, vyuo vikuu na wadau wengine wote kuunganisha nguvu katika kushughulikia matatizo yanayoendelea kujitokeza katika elimu ya juu hivi sasa.
Ikumbukwe kwamba Rais Jakaya Kikwete aliahidi mwaka 2007 kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wanafunzi wa elimu juu nchini ili kupunguza migomo na migogoro. Katika Mkutano wake na wanafunzi wa vyuo vikuu mwezi Februari 2007 alikwenda mbali zaidi kwa kuwaeleza kwamba hakuna mtoto wa maskini atayeshindwa kuendelea na masomo kutokana na masharti ya mikopo.
Miaka mitano imepita toka ahadi hizo zitolewe migomo katika vyuo vikuu inaendelea na pia wapo watoto wa walalahoi ambao wamefaulu kidato cha sita lakini wemeshindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa mikopo; hivyo Waziri asipochukua hatua za haraka itadhihirika kwamba ahadi za serikali zimekuwa za ‘kiini macho’.
John Mnyika (Mb)
13/12/2011
7 comments:
Shukuru Kawambwa hakuna wizara ambayo aliiweza. huyu jamaa anabebwa tu na uswahiba alionao na JK na vile wametoka sehemu moja. lkn hana uwezo wa kuongoza wizara hii na ningemshauri ajiuzulu tu. Uwezo kwakweli hana
Huko Wizarani ni sawa na kupoteza muda tu.... hatua za kuchukua ni NGUVU ya umma na ya wanafunzi wenyewe itumike. Ingawa wanasingizia Al-shababu kwa mikusanyiko ya msingi. Ila kwenye mikusanyiko yao ya kula Bilion 50 kwa kuadhimisha 50yrs ya Tanganyika Al-shabaab hawasemwi.
Shida iko hapa,watendaji wote wa serikali kuanzia rais wa jamhuri hadi mtendaji wa mtaa hawafanyi kazi pasipo shuruti.
Mfano; madai ya waalimu yameahidiwa kufanyiwa kazi baada ya walimu kuitisha mgomo,'boom' halikuongezwa pasipo mgomo,matatizo ya wanafunzi hayasikilizwi pasipo mgomo,
na mgomo unaathali kubwa sana kwa wanafunzi
ili wanafunzi wasiendelee kuathirika na migomo wakati huohuo wakipewa haki zao
ni vema
mawaziri,ma-VC na ma-DEAN FACULTIES wasomee uongozi angalau ngazi ya diploma
kuwepo na evaluation forms kwa wadau husika ili watathmini management zinazowaongoza
CHADEMA(chama kikuu cha upinzani) waelimishe wananchi kwa kuwapa vipeperushi vinavyoonesha haki zao kwa nukuu za katiba na sheria ili (mfano mwanafunzi wa chuo) ajue haki zake kwa kunukuu vifungu vya katiba,kanuni na sheria na sio blaablaa
kwanza hongera kwa kusimamia haki za wanyonge, inaniuma sana kusimamishwa masomo Udom kosa likiwa ni kudai mafunzo kwa vitendo ambayo ni haki yangu ya msingi, lakin serikali yetu pia ambayo ni kiziwi na kipofu isiyo ona matatizo yanayotukumba wanachuo ambayo mwisho wa siku watoto wa walala hoi ndo tunahukumiwa kwa kosa la serikali, pia sioni umuhimu wa TCU kwasababu nilikuwa naamini kuwa ipo kwa kazi ya kuhakikisha ubora wa elimu katika vyuo vya umma na vya binafsi hautofautiani lakin leo degree program ambazo ni sawa UDSM wanaenda mafunzo kwa vitendo lakini hizo hizo degree program UDOM haziendi mafunzo kwa vitendo sijui huwa wanaangalia nini wakati wa kuvisajili hivi vyuo? nina mengi ya kuongea ila bdo cjapata nafasi ya kuyasemea na nakuomba Mh Mnyika Mungu akujaze nguvu na ujasili ili usije choka kupigania hiki za wanyonge kwani wanyonge tupo nyuma yako kwa maombi. "THE ROOTS OF EDUCATION IS BITTER BUT ITS FRUITS ARE SWEET"
GN 178 itaua upatikanaji wa viongozi bora na tena wenye uthubutu wa kuonya, kufundisha na kuelekeza kama ilivyosifa ya kiongozi bora. zaidi italeta viongozi wababaishaji na vibaraka watakaoshindwa hata kutetea maslahi ya taifa na kutuuza kwa wanaowatumikia. watanzania tuwaunge mkono wanafunzi wa MUHAS wanaodai uwajibikaji katika ngazi ya Uwanafuzi,upatikanati wa katiba zilizo huru na kwa maslahi ya taifa.
hapa inaonesha kuwa waziri mwenyedhamana hajui kinachoendelea na kama anajua,basi anauzembe ktk utendaji wake...
thamahani; naomba nitumike lugha ya kigeni (kiingereza)
What you said in your posts is true. but what this country needs is a complete change of leadership. and this will only be possible through a nation wide strike. All uni students should meet at DSM and we strike till JK listens to our demand.
worse come, we have to copy what happened in Egypt and Libya.
paralyse the nation and bring about the necessary change. the army will hit us, but if we keep the media on our side, international pressure will bring about the change.
all together for change :)
Post a Comment