Monday, December 19, 2011

Kuhusu Serikali kulinda Viwanda vya ndani

Leo tarehe 19 Disemba 2011 vyombo mbalimbali vya habari vimemnukuu Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwahakikishia wafanyabiashara kwamba Serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete itaendelea kulinda viwanda vya ndani ili viweze kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa na kuongeza ajira.

Hata hivyo, kauli hiyo haipaswi kuleta matumaini ya kweli kwa wafanyabiashara na watanzania kwa ujumla katika kipindi hiki cha kuathirika kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kutokana na mfumuko mkubwa wa bei na kuporomoka kwa kasi kwa shilingi ya Tanzania ukilinganisha na dola kunakochangiwa pamoja na sababu mbalimbali ikiwemo kupungua kwa uzalishaji nchini katika kilimo na viwanda pamoja na ongezeko kubwa la uingizaji wa bidhaa kutoka nje.

Waziri Mkuu Pinda anapaswa kutoa kwa wafanyabiashara wenye viwanda na umma wa watanzania mpango wa haraka wa kukuza uchumi wa nchi na kupunguza gharama za maisha ambao pamoja na mambo mengine utajikita katika kuongeza uzalishaji nchini, kupanua wigo wa ajira, kupunguza kiwango cha uagizaji wa bidhaa kutoka nje ili kuboresha urari wa biashara na kudhibiti bei ya bidhaa muhimu.



Aidha, Waziri Mkuu Pinda amewaeleza wafanyabiashara wenye viwanda kuwa kama sehemu kulinda viwanda vya ndani Rais Jakaya Kikwete ameweka msisitizo katika ujenzi wa kanda huru za kibiashara (EPZ/SEZ) ili wawekezaji wasipate shida ya ardhi na miundombinu mingine; bila kueleza umuhimu wa kuweka mkazo katika kufufua na kuokoa viwanda vya ndani ambavyo vingi vimeathirika kutokana na ubinafsishaji holela na vingine kutokana na kutowekewa mazingira mazuri ya kibiashara ya kuviwezesha kuchangia katika kukuza uchumi na kuongeza ajira.

Hivyo, natoa mwito kwa Waziri Mkuu Pinda kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni kuonyesha mfano kwa vitendo vya kulinda viwanda vya ndani kwa kushughulikia matatizo ya viwanda ambavyo serikali ina hisa kwa kupitia kumbukumbu za bunge na kufuatilia kuhakikisha ahadi mbalimbali ambazo serikali imezitoa bungeni zinatekelezwa.

Kati ya hatua hizo mahususi ni muhimu kwa serikali kufanya uchunguzi wa dharura kuhusu Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kilichopo katika jimbo la Ubungo ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kunusuru kiwanda hiki ambacho kina hali mbaya ya uzalishaji, migogoro ya wafanyakazi na uuzwaji au ukodishwaji wa mali za kampuni bila kuzingatia taratibu na maslahi ya umma.

Aidha, Rais Kikwete kwa nafasi yake ya kiongozi wa serikali na mwenyekiti wa baraza la mawaziri awaagize Waziri wa Fedha, Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Kazi na Ajira kutekeleza mipango ya kulinda viwanda vya ndani hususani kiwanda cha Nguo cha Urafiki ambacho kina hali mbaya lakini kina fursa ya kuchangia katika kuongeza ajira na pato la serikali iwapo hatua za haraka zitachukuliwa.

Kama inavyofahamika, moja ya viwanda vikubwa vya nguo hapa nchini vilivyojengwa wakati wa Awamu ya Kwanza ya Utawala wa nchi yetu chini ya Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kiwanda cha Nguo cha Urafiki ambacho kilijengwa miaka michache baada ya uhuru kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka nchi ya China. Baadaye kiwanda kilibinafsishwa kiholela na sasa kinaendeshwa kwa ubia kuanzia mwaka 1997 ambapo serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 49 ya hisa huku asilimia 51 zikiwa chini ya kampuni ya nchini China.

Pamoja na kuwa mwenye hisa nyingi ndiye anawajibika zaidi katika uendeshaji wa kiwanda kiuendeshaji na maslahi ya wafanyakazi, serikali kwa kuwa na hisa 49% kwa niaba ya watanzania ina wajibu wa pekee wa kufuatilia kwa karibu hali ya kiwanda kama sehemu ya kulinda viwanda vya ndani, kudhibiti hasara kwa serikali na kuzuia upotevu wa mali za umma. Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka kumi wajibu huu umekuwa hautekelezwi ipasavyo hali ambayo imedidimiza kiwanda kwa kiwango kikubwa na kuathiri uzalishaji pamoja na kupunguza ajira.

Baada ya kubaini hali hiyo tarehe 4 Februari 2011 nilitembelea Kiwanda cha Nguo cha Urafiki Ubungo na kufanya mazungumzo na wafanyakazi pamoja na wawakilishi wa menejimenti. Kutokana na mkutano huo na vyanzo vingine nilipata maelezo ya kina kuhusu hali mbaya ya kiwanda ikiwemo kusimama kwa uzalishaji wa nguo na maslahi duni ya wafanyakazi.

Kufuatia taarifa hizo nilichukua hatua ya kuziandikia mamlaka husika kuweza kuchukua hatua za haraka kunusuru hali ya kiwanda. Kutokana na mamlaka husika kuchelewa kuchukua hatua nilikwenda mbele zaidi kwa kutumia mamlaka ya kibunge kuhoji mawaziri husika wakati wa mkutano wa nne wa Bunge wakati wa kujadiliwa kwa bajeti za wizara mbalimbali.

Baadhi ya Wizara nilizozitaka kuchukua hatua ni pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha hususani ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika Hodhi la Mali ya Mashirika ya Umma (CHC), Wizara ya Kazi na Ajira na mamlaka zingine. Hatua ambazo zimechukuliwa mpaka sasa zimekuwa za kususua na hazionyeshi kama serikali inayachukulia matatizo ya Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kwa uzito unaostahili.

Pamoja na kuitaka serikali kuchukua hatua pia nilitoa mwito kwa kamati husika za bunge kuchukua hatua ambapo kamati ya Viwanda na Biashara iliitikia mwito huo na Novemba 2011 ilitembelea kiwanda na kushuhudia ukweli wa madai ambayo tumekuwa tukiyatoa kuhusu hali mbaya ya kiwanda. Kamati hiyo ilitoa kauli ya kutaka uchunguzi wa ziada ufanyike hatua ambayo haijatekelezwa mpaka hivi sasa.

Izingatiwe kuwa kabla ya Kuingia ubia, Serikali ilifanya ukarabati mkubwa wa mitambo kwa gharama za walipa kodi watanzania. Aidha, mara baada ya ubia serikali ya Tanzania iliingia mkataba mwingine na Serikali ya China wa mkopo wa dola milioni 27 (zaidi ya bilioni 30) kwa ajili ununuzi wa mitambo mipya badala yake kwa sehemu kubwa fedha hizo zikatumika kununua mitambo chakavu.

Matokeo yake uzalishaji ukaanza kupungua na wafanyakazi wakaanza kupunguzwa na hivyo kusababisha kushuka kwa mapato ya serikali na kuongezeka kwa matatizo ya ajira. Pia, kutokana na matatizo hayo baadhi ya mitambo imeondolewa na kuuzwa kinyemela kama vyuma chakavu hali ambayo imesababisha wafanyakazi kupewa likizo wengi bila malipo na wengine kwa malipo pungufu kwa visingizio mbalimbali. Kutokana na hali hiyo nilizitaka Wizara na Mamlaka husika kuchunguza madai hayo na kuongeza ukaribu wa serikali katika uendeshaji wa kiwanda husika.

Kwa upande mwingine maslahi ya wafanyakazi nayo yamezidi kuwa duni badala kuboreshwa baada ya ubia kuingiwa na hivyo kushusha motisha ya ufanyaji wa kazi. Pia wafanyakazi hawalipwi mishahara kwa viwango vipya vilivyotangazwa na serikali katika hatua za awali. Hali hizi zimesababisha migogoro mbalimbali kati ya kampuni na serikali kwa upande mmoja na wafanyakazi walioko kazini na walioachishwa kwa upande mwingine na hivyo kuongeza mizigo ya madeni kupitia hukumu za mahakama, mamlaka zingine na madai lukuki. Kufuatia hali hiyo kudumu kwa muda mrefu zaidi ya miaka kumi, nilitoa mwito kwa Wizara na Mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kumaliza matatizo ya wafanyakazi katika Kiwanda cha Nguo cha Urafiki ili kuelekeza nguvu katika uzalishaji.

Katika mikutano ya tatu na nne ya Bunge kwa nyakati na njia mbalimbali nilizieleza pia Wizara na mamlaka mbalimbali za serikali kuwa hali mbaya ya kiwanda inahusisha pia kukosekana kwa udhibiti katika mali za kampuni na pia kiwanda kuanza kufanya shughuli ambazo ziko nje ya kazi ya msingi ya ubia wa uzalishaji wa nguo. Niliitaka serikali kuchunguza na kuchukua hatua juu ya shughuli zinazoendelea kufanywa na Kiwanda cha Nguo cha Urafiki nje ya mikataba na misingi ya ubia mathalani: upangishaji wa Nyumba za wafanyakazi, upangishaji wa maeneo ya wazi, upangishaji wa maghala ya kiwanda, uuzaji wa nyumba za wafanyakazi, mfano mzuri ni nyumba 50 za THB eneo la Manzese, na ukodishaji wa maeneo kwa ajili ya kufanya biashara ya mafuta. Hali hii imeambatana na uingizaji wa bidhaa za nje kwa mgongo wa kampuni ya Urafiki na zingine tanzu kinyume na ubia wenye msingi wa kulinda na kuendeleza viwanda vya ndani hali ambayo imeleta athari katika uchumi wa taifa na kupunguza ajira za uzalishaji.

Kutokana na hali hiyo nilitoa mwito kwa Serikali kuingilia kati kupitia Wizara ya Fedha hususani Ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) na Wizara ya Viwanda na Biashara kuchukua hatua zinazostahili juu ya kiwanda cha Urafiki. Aidha, kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara kuchukua hatua za kuisimamia serikali ili kuharakisha hatua za kunusuru kiwanda hiki kama ili kuonyesha pia mfano wa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhusu viwanda vingine. Hata hivyo, mpaka sasa hakuna hatua kamili zilizochukuliwa na Wizara na Mamlaka husika hivyo Waziri Mkuu Pinda anapaswa kuingilia kati kusukuma hatua kuchukuliwa baadala ya kutoa kauli za ujumla kwamba serikali inalinda viwanda vya ndani.

Aidha, ili dhamira hiyo ya Rais Kikwete kuendeleza uwekezaji katika viwanda vya ndani iweze kudhihirika serikali iweke wazi kwa umma taarifa ya uchunguzi kuhusu hali ya viwanda vilivyobinafsishwa ambayo imebaini ufisadi na matatizo makubwa ya kiutawala katika uwekezaji ili kuweka msingi wa hatua kuchukuliwa kunusuru viwanda hivyo pamoja na kudhibiti hali kama hiyo isijitokeze katika uwekezaji katika maeneo maalum ya kiuchumi unaoendelea hivi sasa.

John Mnyika (Mb)

Ps: Taarifa hii niliitoa jana 19/12/2011

1 comment:

Wikedzi said...

Inatisha sana unapoona maplaza yanajengwa kwa wingi yakiwa yamefurika bidhaa za nje wakati viwanda vyetu havifanyiwi mkakati wowote ili vitufae.