Thursday, December 29, 2011

Kuhusu matatizo ya maji kata ya Goba; uvumilivu unakaribia kikomo

Matatizo ya maji kata ya Goba ni matokeo ya udhaifu wa watendaji katika ngazi mbalimbali na natoa mwito kwa mamlaka zinazowasimamia watendaji hao kuchukua hatua stahiki na kutoa taarifa kwa wananchi katika kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa.

Kazi ya mbunge kwa mujibu wa katiba na sheria ni kuwakilisha wananchi, kuisimamia serikali na kutunga sheria. Utekelezaji ni jukumu la mamlaka, vyombo na ngazi mbalimbali za kiserikali. 

Matatizo ya maji kata ya Goba yanafahamika kwa mamlaka zote husika kuanzia Wizara ya Maji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Kinondoni na vyombo vya dola kuanzia mwaka 2007 mpaka mwaka 2011 lakini hatua kamili hazijachukuliwa.

Wananchi wamepoteza uvumilivu na kama hatua hazitachukuliwa kwa haraka viongozi wa kuchaguliwa hatutakuwa na sababu ya kuendelea kuwaambia wavute subira; tutaungana nao katika kushinikiza uwajibikaji. 
Katika kipindi cha wiki mbili huduma ya maji isiporudishwa kwenye kata ya Goba nitatangaza mgogoro na Manispaa ya Kinondoni pamoja na mamlaka zingine husika na kuwaunganisha wananchi kuchukua hatua watakazoona zinafaa.

Nimefikia hatua ya kutoa kauli hii nzito kwa sababu njia zote za kawaida kupitia vikao na mawasiliano ya kiofisi zinaelekea kukwamishwa na uzembe, hujuma na urasimu na udhaifu wa kiutendaji katika ngazi mbalimbali.

Kufuatia DAWASCO kutokutoa majibu kwa suala hili na mengine tarehe 5 Septemba 2011 niliwaunganisha wananchi kwa pamoja tukaandamana kwenda ofisi ya DAWASCO makao makuu ambapo tulikutana na mtendaji mkuu wa kampuni husika na kufanya mazungumzo ambayo yamesaidia baadhi ya hatua za msingi kuchukuliwa.

Kufuatia maandamano na mazungumzo hayo DAWASCO wametekeleza wajibu wao kwa hatimaye kukubali kurejesha maji kwenye kata ya Goba na kupanga utaratibu wa deni kulipwa kwa awamu.

Katika kuchangia kuwezesha hatua hiyo kuchukuliwa kwa wakati nilishawishi kiwango cha milioni tatu kutolewa kwa ajili ya mradi wa maji Goba kutoka katika Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo (CDCF).

Hata hivyo, pamoja na kutengwa kwa fedha hizo kikwazo cha huduma ya maji kurejeshwa katika vituo vya kutoa huduma ya maji katika kata ya Goba ni matatizo katika kamati ya maji kwa upande mmoja na udhaifu mkubwa wa watendaji wa manispaa ya Kinondoni idara ya maji mpaka ngazi ya kata. 

Kisingizio wakati wote kimekuwa ni zoezi la kufukua mabomba kwa ajili ya uhakiki; hali ambayo imefanya matatizo ya maji yadumu Goba kwa zaidi ya miezi minne na kufanya watanzania wa kipato cha chini wanunue maji kwa bei ya juu au kuyapata kwa umbali mrefu.

Tarehe 24 Oktoba 2011 niliandika barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kutoa mwito wa hatua za dharura kuchukuliwa ili kuhakikisha uhakiki unafanyika wakati huo huo wananchi wengine wanaendelea kupata huduma ya maji; lakini udhaifu wa kiutendaji umefanya hatua ziwe za kusuasua.

Katika kushughulikia masuala la maji kwenye kata ya Goba, narudia kusisitiza hatua zifuatazo kuendelea kuchukuliwa kwa haraka na mamlaka zifuatazo:

Mosi; Mamlaka za Manispaa ya Kinondoni zikiongozwa na Meya na Mkurugenzi zinapaswa kufuatilia kwa haraka kuhakikisha maji yanarejeshwa Goba. Hatua hii iende sambamba na kupanua wigo wa maji Goba kwa kutekeleza kwa haraka upatikanaji wa maji kutoka pia mradi wa maji toka Madale Kisauke. Manispaa izingatie matatizo yaliyopo kwenye miradi ya maji inayoendeshwa na manispaa pamoja na kamati za wananchi au vyama vya watumia maji katika maeneo mbalimbali. Hivyo, pamoja na kuchukua hatua kuhusu mradi wa maji wa Goba, Manispaa ichukue hatua juu ya miradi iliyokwamba ukiwemo wa Msewe Golani. Pia, Manispaa ya Kinondoni inapaswa kufanya mabadiliko kwenye idara ya maji kwa kuwa ina udhaifu mkubwa wa kiutendaji.

Pili; Wizara ya Maji, Mamlaka ya maji safi na maji taka (DAWASA) na Kampuni ya maji safi na maji taka (DAWASCO) zizingatie kwamba maeneo ya pembezoni ya Dar es salaam ambayo awali yalikuwa vijiji sasa ni mitaa yenye wakazi wengi. Hivyo, maeneo kama kata ya Goba na mengine ya pembezoni yanapaswa kuunganishwa moja kwa moja na mtandao wa maji chini ya mamlaka husika kwa mujibu wa sheria iliyounda DAWASA badala ya mfumo uliopo ambalo haulingani na mahitaji.

Tatu; vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kushughulikia vyanzo vya migogoro badala ya kusubiri mpaka matatizo yanapoibuka kwa kushughulikia kwa wakati malalamiko yanayotolewa. Mathalani, Jeshi la Polisi (Ofisi ya DCI) na TAKUKURU wanapaswa kutoa kauli kuhusu hatua zilizochukuliwa juu ya tuhuma za ufisadi na ukiukwaji wa sheria katika mradi wa maji Goba ambazo zimetolewa na wananchi kwa mamlaka husika kuanzia mwa 2007. 

Mamlaka husika zizingatie kuwa tarehe 27 Februari 2011 na 6 Machi 2011 nilifanya mikutano na wananchi katika kata ya Goba ambapo risala ya wananchi pamoja na ripoti ya ukaguzi wa mradi wa mradi wa maji Goba ya mwaka 2007 zilizosomwa ambazo zilieleza bayana matatizo yaliyokuwepo kwenye kamati ya maji pamoja na mradi kwa ujumla ikiwemo yaliyohusu upotevu wa fedha ambayo vyombo vya dola vilipatiwa taarifa lakini hatua hazikuchukuliwa kwa wakati. 

Itakumbukwa kwamba tarehe 1 Septemba 2011 nilitoa taarifa ya awali kuhusu ufuatiliaji ambao nilifanya na hatua ambazo nilikusudia kuzichukua kuhusu maji kukatwa katika kata ya Goba na tuhuma juu ya kamati mpya ya maji.

Katika taarifa hiyo nilieleza kwamba , iwapo DAWASCO isingetoa majibu kabla tarehe 3 Septemba 2011 kuhusu masuala mbalimbali ya maji katika Jimbo la Ubungo ikiwemo kuhusu malalamiko juu ya deni la maji katika kata ya Goba nitawaongoza wananchi wa kata mbalimbali kwenda makao makuu ya DAWASCO wiki ijayo ili kuunganisha nguvu ya umma hatua za haraka zaidi ziweze kuchukuliwa.

Aidha, nilitoa mwito kwa Manispaa kuitisha na kuijadili ripoti ya mkaguzi wa ndani kuhusu mradi husika pamoja na taarifa ya kamati ya kufuatilia mfumo mzima wa uendeshaji wa mradi.

Katika taarifa hiyo nilieleza pamoja na mambo mengine kuwa katika ufuatiliaji wangu nimebaini kwamba Matatizo ya Maji katika Kata ya Goba kama ilivyo katika kata zingine katika Jimbo la Ubungo na Mkoa wa Dar es salaam kwa ujumla yanatokana na matatizo ya kimfumo, kiuongozi, kifedha na kiutendaji yanayosababishwa na Kamati ya mradi wa Maji Goba, DAWASCO, DAWASA, Halmashauri za Jiji la Dar es salaam na Wizara ya Maji ambayo nimekuwa nikiipa taarifa na kutaka iingilie kati kwa nyakati mbalimbali.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)

30/12/2011

2 comments:

Anonymous said...

Mh. Hongera sana kwa jitihada unazo zifanya na kweli tunashukuru sana and we real appreciate.
Pamoja na pongezi zangu napenda kuchukua fursa hii kukumbusha kwamba sisi wakati wa Mbezi Misumi tumesahaulika hususani kuhusiana na huduma muhimu za kijamii. Kwa mfano mpaka wakati huu barabara zetu zimekuwa mbovu sana, hakuna umeme na kikubwa maji pia yamekuwa tatizo kubwa sana. Adha ya barabara inaweza pia kuwadhulu wanafunzi wanao soma shule ya sekondari misumi mwisho kwani magari ni machache sana na hivyo ulazimika kutembea kwa miguu na wakati mwingine kupanda boda boda.
Hatua hii ni hatarishi kwa watoto wa kike kwani ni rahisi sana kurubuniwa na kukatizwa masomo kama watapata mimba na magonjwa hatari likiwemo ukimwi.
Mh. Maji limekuwa tatizo sugu sana sana watu wengi wanategemea visima hasa wakati wa masika na wakati wa kiangazi watu ufikia kununua ndoo moja hadi shilingi 500-1000!! hali ni mbaya sana mh.
Mheshiwa tungeomba mkutano wa hadhara ili tuweze kujadili kwa pamoja ni jinsi gani tunaweza kutatua matatizo yetu. Tunaamini kwamba uwezi wewe kama wewe kutuwekea mabomba ya maji au nguzo za umeme lakini pamoja tunaweza kusonga mbele.

Anonymous said...

Kwanza hongera mbunge kwa kuwa mstari wa mbele katika kufuatilia swala la maji katika kata yetu ya Goba.Mimi napata mashaka sana tatizo la maji huku goba; Maji yamekatwa sababu ya deni sawa, Lakini kama haitoshi wameamua kung'oa mabomba na kuchukuwa baadhi ya mita za maji za wananchikwa kisingizio cha kuzichunguza.

Ni uchunguzi gani ambaoumepelekea kung'oa hadi mabomba? Pia kuchukuwa mita za maji za wananchi na kutokomea nazo mpaka leo.

Wananchi wanaendelea kupata tabu na hadha ya maji kwa kununua maji kwa shillingi 250/= hadi 300/= kwa ndoo ya lita 20. Kwa kweli inaumiza sana sisi wananchi wa hali ya chini.

Jambo la msingi nadhani uitishwe mkutano wa wananchi wote ili wao wawezekuamua hatima ya tatizo la maji Goba, manalimekuwa sugu sana.