Thursday, December 29, 2011

Serikali itoe taarifa uchunguzi wa kashfa ya UDA

Serikali inapaswa kutoa taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa juu ya ukaguzi na uchunguzi wa tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa sheria, kanuni na maslahi ya wananchi katika mchakato wa ubinafsishaji wa Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA).

Taarifa hiyo inapaswa kutolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, vyombo vya dola na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa umma umeanza kupoteza matumaini juu ya hatma ya ukaguzi na uchunguzi huo ambao serikali iliahidi ungefanyika katika kipindi cha mwezi mmoja lakini mpaka sasa miezi minne imepita huku ukimya na usiri ukitawala.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kutoa taarifa kwa kuwa alitoa agizo bungeni tarehe 4 Agosti 2011 wakati wa kipindi cha maswali kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kifungu cha 38 (4) ya kuelekeza vyombo vya dola hususan Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) , Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Ofisi ya Upepelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma husika.

Toka agizo hilo litolewe umma wala wabunge hatujawahi kuelezwa hatua ambayo vyombo vya dola hususani TAKUKURU na ofisi ya DCI imefikia katika uchunguzi wa tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa sheria, kanuni na maslahi ya wananchi katika mchakato wa ubinafsishaji wa Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA).
Taarifa pekee ambayo imetolewa mpaka sasa na ofisi ya Waziri Mkuu ni kuwa tarehe 13 Agosti 2011 Waziri wa Nchi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) George Mkuchika alikabidhi barua kwa CAG ya kutaka ufanyike ukaguzi maalum katika kipindi cha mwezi mmoja. Hata hivyo, miezi miwili ilipita bila ukaguzi husika kukamilika na hatimaye mwezi Oktoba CAG akatangaza kwa umma kwamba ameshindwa kumalizia ukaguzi husika kutokana na kutingwa na majukumu mengine.

Kutokana na hali hiyo CAG alieleza kwamba ofisi yake imeiteua kampuni binafsi ya KPMG kufanya ukaguzi husika katika kipindi cha mwezi mmoja. Hatahivyo, takribani miezi miwili imepita bila ukaguzi huo kukamilika hivyo; CAG Ludovick Utouh anapaswa kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatua iliyofikiwa juu ya ukaguzi huo na kuhakikisha kwamba ukaguzi unakamilika kwa haraka.

Ni muhimu umma ukafahamu kwamba uchunguzi uliokuwa ufanywe na Kamati iliyoundwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) bado haujaanza kutokana na uongozi wa Bunge kuelekeza kwamba uchunguzi huo unapaswa kusubiri ukaguzi wa CAG.

Aidha, ieleweke kwamba madiwani wa jiji la Dar es salaam nao ni vigumu kuchukua hatua kamili kutokana na suala hilo kuwa katika uchunguzi wa maelekezo ya ofisi ya Waziri Mkuu.

Hivyo vyombo vya uwakilishi wa wananchi yaani bunge na baraza la madiwani vimebanwa kiufundi kuchukua hatua vikisubiri uchunguzi huo wakati ambapo ukaguzi haujakamilika na kampuni ya Simon Group imeshaingizwa katika umiliki na uendeshaji wa kampuni ya UDA.

Pia, wakati ukaguzi huo ukiendelea kuchelewa maofisa waliohusika katika jiji, kampuni ya UDA, wizara mbalimbali na taasisi za serikali wanaendelea na utumishi kama kawaida katika mazingira ambayo yanaacha mianya ya hujuma kwa mali za kampuni na vielelezo mbalimbali. 

Pamoja na kuhimiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi, narudia kutoa mwito kwa Serikali kuagiza kusitishwa mara moja kwa mkataba batili na maamuzi haramu yaliyofanyika ya kukabidhi hisa, mali na uendeshaji wa kampuni ya UDA kwa Kampuni ya Simon Group Limited ili katika kipindi hiki cha uchunguzi masuala yote ya kampuni hiyo yaratibiwe na bodi huru itayoundwa na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria.

Izingatiwe kwamba tarehe 4 Agosti 2011 wabunge wa Dar es salaam tulitoa tamko kwamba tuko tayari kutoa ushahidi kwa vyombo hivyo pamoja na kushirikiana na serikali kwa ujumla wake ili kuwezesha hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa haraka kuhusu tuhuma hizo. Hata hivyo, mpaka sasa kama katibu wa wabunge sijaitwa na chombo chochote cha serikali kuhusu suala la UDA na sijapokea taarifa toka kwa mbunge yoyote mwingine iwapo maelezo yametakiwa toka kwa wabunge juu ya ukaguzi unaoendelea.

Ni vizuri umma wa wakazi wa mkoa wa Dar es salaam na watanzania kwa ujumla ukakumbuka kwamba maamuzi yote yaliyofanywa na Mstahiki Meya Didas Massaburi kuhusu kampuni ya UDA yanayotajwa kuridhiwa na vikao vya jiji ni batili kwa kuwa yalifanyika kwenye vikao visivyokuwa halali bila kuzingatia sheria, kanuni na maslahi ya wananchi wa Dar es salaam; bila ridhaa ya wabunge ambao ni Wajumbe wa Baraza la Halmashauri ya Jiji. 

Maamuzi hayo yalifanyika bila kuheshimu maelekezo ya barua ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya tarehe 28 Februari 2011 yenye kumbu. Na CAB. 185/295/01/27 ambayo iliagiza kusitisha mara moja mchakato wa kuuza hisa ambazo hazijagawiwa barua ambayo nakala yake iliwasilishwa kwa mkurugenzi wa Jiji na Meneja Mkuu wa UDA pamoja na Wizara zingine zinazohusika.

Katika kufanya ukaguzi na uchunguzi ni muhimu kwa serikali kuzingatia kwamba pamoja na udhaifu kwenye uongozi wa Jiji la Dar es salaam matatizo ya UDA yamechangiwa pia na Ofisi ya Msajili wa Hazina kutokuwa makini katika hatua zote kwa kushirikiana na CHC katika masuala ya ubinafsisaji wa UDA. Pia, CHC katika hatua ya sasa nayo ina udhaifu wa kushindwa kushughulikia masuala husika kutokana na migogoro ya kiutawala inayosababishwa pia na Waziri wa Fedha. Hivyo, pamoja na kutaka taarifa za taasisi husika ni muhimu Waziri Mkuu Pinda kutoa kauli kuhusu utekelezaji wa agizo alilolitoa bungeni kuhusu kashfa ya UDA.

Nahitaji kauli ya serikali kuhusu suala hili kama sehemu ya kutimiza wajibu wa kibunge wa uwakilishi na usimamizi ili kulinda mali za umma na pia kutetea maslahi ya wakazi wa Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla wanaohangaika na adha ya usafiri.

John Mnyika (Mb)

29/12/2011.

No comments: