Vyombo mbalimbali vya habari vya leo tarehe 11 Disemba 2011 vimeeleza kwamba kesho tarehe 12 Novemba 2011 Waziri Mkuu Mizengo atakuwa mgeni rasmi katika shughuli maalumu ya kufunga Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru itakayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Mkoani Dar es salaam.
Kwa makadirio ya vyanzo mbalimbali kiwango cha fedha kilichotumiwa mwaka huu kwa ajili ya ‘sherehe’ za miaka 50 ya uhuru kinazidi bilioni 50; hivyo natarajia kwamba Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ndiye mwenyekiti wa maandalizi ya maadhimisho hayo atatumia shughuli hiyo ya kufunga kueleza pia kiwango halisi cha fedha ambacho kimetumiwa hivi sasa na Serikali kupitia Wizara na taasisi zake.
Toka wakati wa bunge la bajeti nimekuwa nikisikitishwa na kiwango kikubwa cha fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya ‘sherehe’ za uhuru katika bajeti za Wizara mbalimbali huku kukiwa na upungufu wa fedha za miradi ya maendeleo.
Gharama za maisha kwa wananchi ziko juu na uchumi wa nchi uko kwenye hali tete kwa sababu ya pamoja na mambo mengine mfumuko wa bei na kuporomoka kwa shilingi. Hali hii inachangiwa pia na ubadhirifu na matumizi ya anasa ya fedha za umma ambapo ‘sherehe’ hizi ni sehemu za matumizi hayo.
Wakati wa bunge la bajeti nilipiga kura ya HAPANA ya kukataa bajeti ambayo ilitenga fedha nyingi kwenye posho za vikao na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima huku mipango mingine muhimu ya maendeleo mathalani ya kuwezesha jiji la Dar es salaam kupata maji, ujenzi wa barabara za pembezoni kwa ajili ya kupunguza foleni, malipo ya madeni ya walimu, askari na watumishi wa umma pamoja na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ikiwa haijatengewa fedha za kutosha.
Majibu ya serikali wakati wote yamekuwa ni kwamba hakuna fedha za kutosha sasa ni muhimu Waziri Mkuu Pinda watanzania mabilioni ya ‘sherehe’ hizo yametoka wapi; kwa kuwa kiwango cha matumizi yaliyofanyika kinaonyesha kuwa juu hata ya kile ambacho kimekuwepo kwenye bajeti iliyopitishwa bungeni.
Kiwango hicho cha fedha kingeweza kugharamia masuala yafuatayo ambayo yangefanyika katika kipindi cha mwaka mmoja maadhimisho ya uhuru yangekuwa na maana zaidi kwa sababu tarehe 9 Disemba 1961 Mwalimu Nyerere akihutubia taifa alieleza kuwa ‘uhuru ni kazi’ wala hakusema ‘uhuru ni sherehe’.
Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru yangekuwa na maana kama yangeacha kumbukumbu ya mwaka 2011 kwa kulipa madeni yote ya walimu, askari na watumishi wengine wa umma; pamoja na kuelekeza fedha hizo kwenye miradi iliyotengewa fedha kidogo.
Mathalani ujenzi wa barabara za pembezoni za kupunguza foleni Dar es salaam umetengewa bilioni tano tu, ujenzi wa bwawa la maji la Kidunda umetengewa bilioni sita, na kuna watoto wa maskini ambao wamekosa mikopo na kushindwa kuendelea na elimu tofauti na ahadi ya Kikwete; fedha hizi zingetosha kufanya matumizi haya yote na mengine.
Aidha katika kufunga maonyesho hayo Waziri Mkuu Pinda afafanue pia sababu za maonyeshoya Wizara na Taasisi mbalimbali kufanyika zaidi mkoani Dar es salaam kama vile miaka 50 ya Uhuru ilikuwa kwa ajili ya watu wa Dar es salaam pekee. Fedha hizi za umma zingekuwa na maana kama zingetumiwa kuzunguka nchi nzima kuhamasisha maendeleo mitaani na vijijini ili kusonga mbele kama taifa kwa kuwa mafanikio ya miaka 50 ya Uhuru yanapaswa kujionyesha yenyewe katika maisha ya wananchi.
Wakati Wizara na Taasisi hizo zikiwa zinatumiwa fedha nyingi kufanya maonyesho kwa gharama za posho, machapisho na matumizi mengine yasiyokuwa na lazima; watumishi wa umma wako kwenye hali mbaya na mishahara katika taasisi zao imekuwa ikicheleweshwa. Hivyo, pamoja na kufunga maonyesho Waziri Mkuu Pinda anapaswa kufuatilia kwa kina matumizi ya wizara zote na taasisi zote zinazowahusu ili kuwa na uwajibikaji kutokana na matumizi haya.
Izingatiwe kwamba matumizi haya yamehusisha pia matumizi ya mara nyingi ya fedha za umma kwenye masuala yale yale ya maonyesho kwa kuwa toka mwaka huu uanze Wizara na Taasisi zimekuwa zikifanya maonyesho yao kila moja pekee na kutumia fedha za umma. Wizara na Taasisi hizo hizo nyingi zikashiriki tena maonyesho ya Saba Saba na Wizara na Taasisi hizo hizo zimerudia tena kushiriki maonyesho ya Uhuru katika viwanja hivyo hivyo; katika mkoa huu huu mmoja wa Dar es salaam.
Haya yanafanyika wakati wakina mama wajawazito na wagonjwa wengine wanafariki katika Hospitali ya Mwananyamala, Temeke, Amana, Muhimbili na Ocean Road kwa ajili ya kukosa madawa na huduma nyingine za msingi miaka 50 baada ya uhuru; haya yanafanyika wakati bado kuna shule nyingi za msingi na sekondari katika Mkoa huu huu wa Dar es salaam ambazo hazina vifaa muhimu ikiwemo madawati miaka 50 ya Uhuru.
Hivyo, ili kushughulikia mianya ya ufujaji na ubadhirifu kutokana na maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru ni kamati ya maandalizi iliyoongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda itoe taarifa ya mapato na matumizi. Aidha, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aingize kipengele maalum cha matumizi ya fedha za ‘sherehe’ za uhuru katika ukaguzi wake wa kila Wizara, Taasisi za Umma , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika ukaguzi wa Matumizi ya fedha za mwaka wa fedha 2011/2012.
John Mnyika (Mb)
11/12/2011
4 comments:
hakika atueleze mantiki ya kutumia pesa zote hizo na wakati zingeweza kufanya kitu kingine cha msingi kwa maslahi ya taifa... yaan inasikitisha sana kuona watu wanatafuta mwanya wowote wa kuchota fedha za umma,, hakika uzalendo umetoweka kabisa,, Mungu atusaidie maana kwa mwenendo huu taifa linaangamia
Yani there is no way wanasikia maoni ya watu hawa viongozi wetu wanachofanya ni kututukomesha kwa kutowachagua maana walijua wenyewe walikopata kura za kuwarudisha madarakani tena, so they are not accountable to wananchi may be kwa shetani yani nina hasira nao za kutosha tu, hela wamepata kwenye mishahara yetu pay as you earn of course
Ni balaa kubwa kuishi maisha ya sherehe katikati ya dalili zote za kushindwa kupambana na maadui watatu walioainishwa vizuri kuwa ni Ujinga,maradhi,na umaskini.Mwalimu angekuwepo angekumbusha kama alivyofanya marehemu BABU ABDULRAHMAN,kulikumbusha taifa na wananchi kuwa kumeongezeka adui wa nnne wa hatari anayefifisha vita dhidi ya maadui zetu watatu ambaye ni UFISADI!Tafadhali Mheshimiwa ukipata forum toa hoja binafsi!Hawa watawala ni hatari!
Tz si masikini,hali ikiendelea hivyo ya kutowajali wananchi wadogo,viongozi mkiendelea kufuja pesa za walipa kodi,ipo siku mtajutia jambo hilo jirekebisheni
Post a Comment