Monday, January 9, 2012

Magufuli hajasema kweli; Anaficha Udhaifu wa Serikali na Wizara yake

TAARIFA KWA UMMA

UTANGULIZI

Tarehe 4 na 5 Januari 2011 Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa John Magufuli alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akitoa madai mbalimbali juu yangu wakati akijibu kauli za Wabunge wa Dar es salaam juu ya ongezeko la nauli katika vivuko vya Kigamboni na maeneo mengine nchini.Toka Waziri Magufuli atoe kauli zisizokuwa za kweli dhidi yangu badala ya kujibu hoja za msingi nilizotaka maelezo toka wizara yake na serikali kwa ujumla sikutoa tamko kwa kuwa nilikuwa katikati ya kazi mbalimbali jimboni Ubungo na majukumu mengine ya kitaifa.

Hata hivyo, kuna msemo kwamba ‘uongo ukiachwa ukarudiwa rudiwa unaweza kuaminika kuwa ndio ukweli’; hivyo naomba kutoa taarifa kwa umma kujibu madai hayo kwa lengo la kuweka rekodi sahihi.Namheshimu Waziri Magufuli, hata hivyo kauli alizozitoa dhidi yangu zinadhirisha kuwa ameanza kulewa sifa kwa kiwango cha kuwa mpotoshaji na mzushi. Ni vyema umma ukachukua tahadhari kwamba imani ya wananchi juu yake ameanza kuitumia vibaya kulinda uzembe, ubabe na ufisadi.Aidha, ni muhimu akawa anajielekeza kujibu madai ya msingi ya wananchi badala ya kuibua masuala mengine kwa lengo la kuhamisha mjadala; hivyo nitarudia tena masuala ambayo nilitaka ayatolee maelezo na vielezo kwa maslahi ya umma.

KUHUSU KIINGILIO KATIKA KITUO KIKUU CHA MABASI UBUNGO (UBT)

Waziri Magufuli amezusha na kupotosha kwamba sijawahi kuhoji kupandishwa kwa kiingilio katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT) cha 200. Ukweli ni kwamba kama ambavyo napinga ongezeko holela la nauli za vivuko nchini, nilipinga ongezeko la kiingilio katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo kwa maslahi ya wananchi wa jimbo letu na ya wasafiri wote nchini wanaotumia kituo hicho. Ukweli zaidi ni kwamba viingilio vya Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo pamoja na ongezeko lake vilipitishwa kwa kutungiwa sheria ndogo (by law) na jiji kabla ya mimi kuchaguliwa kuwa mbunge. 

Hata hivyo, pamoja na kuwa sikuwa mbunge wakati kiingilio kinawekwa mara baada ya kuwa mbunge niliendelea na harakati nilizozianza kabla ya kuwa mbunge za kupinga ufisadi wa mapato katika kituo hicho. Tarehe 28 Januari 2011 nilifanya ziara ya kituoni hapo kama sehemu ya kutimiza wajibu wa kibunge ambapo pamoja na mambo mengine nilikutana na mawakala wa kituo kusikiliza malalamiko yao ikiwemo kuhusu kiingilio. Kufuatia kupinga huko Tarehe 11 Mei 2011 Kamati ya Fedha na Uongozi ya Jiji la Dar es salaam ilipitisha azimio la kupendekeza kwamba utekelezaji wa sheria ndogo iliyoongeza kiingilio usitishwe. 

Kwa kuwa sheria ndogo imetungwa na baraza la madiwani, nilikwenda mbele zaidi kupinga kiwango cha kiingilio na ufisadi katika Kituo cha Mabasi Ubungo kwa kuwasilisha hoja binafsi Tarehe 15 Mei 2011. Kutokana na ukubwa wa hoja ya ufisadi katika kituo hicho kwa mujibu wa vyanzo vyetu na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali suala hilo limekuwa likichukua muda kushughulikiwa na nimeendelea kupinga na kuhoji kwenye vikao vya jiji, kupitia vyombo vya habari na hata bungeni Waziri Magufuli akisikia. 

Kwa sasa tayari jiji limekubaliana na hoja hiyo kinachofuata ni baraza la madiwani kupitisha azimio la kufanya mabadiliko husika. Hivyo, Waziri Magufuli hakusema ukweli alipodai kwamba sijawahi kupinga ongezeko la kiingilio katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo. Jaribio lake dhaifu la kutaka kuonyesha kwamba nimeacha ya kwetu nakwenda kushughulikia ya wengine hatimaye litashindwa ukweli utakapotamalaki.

KUHUSU MADAI KWAMBA SIJAWAHI KUPENDEKEZA BARABARA ZA KUPANDISHWA HADHI NA KUFANYIWA KAZI KWA AJILI YA KUPUNGUZA FOLENI

Waziri Magufuli amezusha na kupotosha kwamba sijawahi kupendekeza barabara za kupandishwa hadhi ili zishughulikiwe na serikali kuu kwa ajili ya kupunguza foleni katika jimbo la Ubungo na Dar es salaam kwa ujumla. Ukweli ni kwamba mara baada ya kuchaguliwa katika kikao changu cha kwanza kabisa kushiriki cha Bodi ya Barabara ya Mkoa mwezi Februari 2011 ambacho chombo cha Wizara yake cha utendaji cha Wakala wa Barabara (TANROADS) kikiwepo nilitoa mapendekezo ya barabara husika na hatua ambazo serikali ilipaswa kuchukua katika maandalizi ya kupandisha hadhi na pia katika bajeti, hatimaye orodha ya barabara husika za kupandishwa hadhi ziliwasilishwa na kupitishwa katika vikao vilivyofuatia. 

Pia, nimeandika barua rasmi mbili zenye mapendekezo mahususi kwa TANROADS na Waziri wa Ujenzi barabara za kushughulikiwa kupunguza foleni (Aprili na Mei 2011); lakini Waziri Magufuli hajawahi kujibu barua hata moja huku miezi zaidi ya sita ikiwa imepita. Baada ya ukimya kwa kutokutekelezwa kwa mapendekezo ya kikao cha bodi ya barabara na kutokujibiwa kwa barua nilichukua hatua za kuwasilisha mapendekezo bungeni ya barabara muhimu kwa ajili ya kupunguza foleni na kutaka majibu ya kuzipandisha hadhi barabara husika wakati nachangia kwenye mjadala wa Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano Tarehe 14 Juni 2011. 

Nikaeleza zaidi hatua zinazopaswa kuchukuliwa na serikali kupunguza foleni jimbo la Ubungo na Dar es salaam kwa ujumla Tarehe 2 Agosti 2011 wakati nachangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi ikiwemo kuhusu kupandisha hadhi barabara husika na kuongeza kiwango cha bajeti. Waziri Magufuli kuzusha na kupotosha kwamba sijawahi kupendekeza kupandishwa hadhi kwa barabara inadhirisha kwamba amekuwa msahaulifu na amefanya jaribio dhaifu la kunichonganisha na wananchi wa jimbo letu kuwa sifuatilii masuala yetu. Ukweli ni kwamba foleni inaendelea kuwepo kwa sababu ya uzembe wa Wizara ya Ujenzi na serikali kwa ujumla kushindwa kutenga Fedha za kutosha kwa ajili ya kulimaliza tatizo pamoja na kupata hasara ya mabilioni kila siku, kiwango ambacho kimetengwa kwa ajili ya barabara za pembezoni za kupunguza msongamano ikiwemo za Ubungo na Dar es salaam nzima kwa mwaka wa Fedha 2011/2012 ni bilioni tano tu; hivyo suala la msingi ambalo Waziri Magufuli anapaswa kulijibu ni iwapo serikali imekubaliana na ushauri wangu wa kufanya mapitio ya bajeti na kuongeza Fedha kwenye mkutano ujao wa bunge kwa ajili ya mkakati wa kuondoa foleni Dar es salaam.

KUHUSU MADAI YA KUSHINDWA KUJA NA WAZO LA KUSHIRIKISHA WAKALA WA NYUMBA (TBA) KWENYE KUTAFUTA SULUHISHO LA MALAZI KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU:

Waziri Magufuli amezusha suala tofauti la madai ya kushindwa kuja na wazo la kushirikisha Wakala wa Nyumba (TBA) kwenye kutafuta suluhisho la malazi kama sehemu ya nyingine ya jaribio lake dhaifu la kuhamisha mjadala na kujaribu kutafuta huruma ya kuungwa mkono na wanafunzi wa vyuo vikuu jimboni Ubungo. Ukweli ni kwamba kazi kubwa ya TBA ambayo iko chini ya Wizara ya Ujenzi na kujenga nyumba za watumishi wa umma, na katika mwaka wa Fedha 2011/2012 ina rasilimali chache za kumalizia miradi iliyopo na kutafuta viwanja vya kujenga nyumba za serikali. 

Kwa hiyo, katika kufanya kazi za kibunge kuhusu TBA ninachofuatilia kwa sasa ni nyumba za watumishi wa umma na masuala ya malazi ya wanafunzi nayafuatilia kwa vyombo na mamlaka nyingine. Ingekuwa TBA ina fursa hiyo anayodai Waziri Magufuli angeiwezesha kuwepo katika harambee iliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete jimboni Ubungo kwa ajili ya Kituo cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ambao taasisi na watu mbalimbali tulichangia kwa ajili ya ustawi wa wanafunzi. Katika hali ya sasa, TBA haina uwezo wa kuanza kujenga maeneo ya malazi ya wanafunzi wakati haijaweza hata kuziba pengo la nyumba za serikali zilizouzwa kinyemela kwa uratibu wa Waziri Magufuli. 

Wanafunzi wa Vyuo Vikuu hawawezi kupotoshwa na Waziri Ujenzi kwamba ana dhamira ya kuwajengea maeneo ya malazi wakati ambapo amesababisha mpaka mawaziri na watumishi wenzake wa umma kukaa mahotelini au kupanga kwa gharama kubwa kwa sababu ya watangulizi wao akiwemo Magufuli kujiuzia nyumba za serikali kwa upendeleo. Waziri Magufuli anapaswa kuwaeleza wanafunzi wa vyuo vikuu na watanzania kwa ujumla kiwango cha ubadhirifu na madeni kwa taifa kinachopunguza uwezo wa serikali kuwapatia mikopo ya elimu ya juu, kuwajengea maeneo ya malazi na kutekeleza miradi mingine ya msingi ya maendeleo na athari ambazo TBA imepata kutokana na kuuzwa kiholela kwa nyumba za serikali.

KUHUSU KUKUTANA KUZUNGUMZIA MAAFA YA MAFURIKO YALIYOLIKUMBA JIJI LA DAR ES SALAAM

Waziri Magufuli amezusha na kupotosha kwamba hatujawahi kukutana kwa ajili ya kuzungumzia maafa ya mafuriko. Ukweli ni kuwa kauli kuhusu suala la kivuko tulizitoa tukiwa tunajiandaa kuingia kwenye kikao cha kamati ya maafa ya mkoa kujadili masuala ya mafuriko, na kabla ya siku hiyo wabunge tumejumuika kwenye vikao vingine vya maafa katika Mkoa wetu. Aidha, toka maafa ya mafuriko yatokee Tarehe 20 Disemba 2011 nimeshiriki kwa hali na mali katika hatua zote ikiwemo hatua aliyoitaja Waziri Magufuli ya kupendekeza njia bora za kuwasaidia wanaoishi mabondeni. Hivyo, kauli hii ni jaribio linguine dhaifu la kujaribu kujenga hisia kuwa hatujali matatizo ya msingi ya wananchi ya wakati huu ili kuhamisha mjadala.

KUHUSU MADAI KWAMBA NILIPASWA KUSHUGHULIKIA MAMBO YA UBUNGO NA SI YA KIGAMBONI

Waziri Magufuli amejaribu kujenga dhana potofu kwamba nilipaswa kushughulikia masuala ya jimbo letu la Ubungo na si kujiingiza kwenye kero za jimbo linguine. Ukweli ni kuwa kero zote tatu alizodai kuwa nimeziacha jimboni bila kuzifuatilia za kiingilio cha Ubungo, kupandisha hadhi barabara za kupunguza foleni na suala la kutumia TBA katika kupata suluhisho la malazi ya wanafunzi wa vyuo vikuu nimezitolea maelezo yenye kuonyesha kwamba nimetimiza wajibu husika wa kibunge. 

Maelezo hayo yanayonyesha kwamba ili tuweze kushughulikia kwa haraka zaidi kero za msingi za wananchi mabadiliko ya mfumo wa utendaji kazi yanahitajika kufanya serikali na viongozi wake waweze kuwajibika ipasavyo. Hii inahitaji kuunganisha nguvu ya wengine na mamlaka zingine katika kuisimamia serikali suala ambalo haliwezi kutimia kwa kazi za ndani ya jimbo pekee. Ukweli ni kwamba mbunge pamoja na kuwakilisha wananchi wa jimbo waliomtuma, anawajibika vile vile kwa nchi, kwa chama na kwa nafasi yake. Hivyo, katika kutimiza majukumu ya kibunge yanatokana mamlaka ya bunge ya kuisimamia serikali kwa mujibu wa Ibara ya 63; mbunge anapaswa kuwasimamia mawaziri na serikali kwa ujumla. 

Matokeo ya kuwezesha mabadiliko ya kiutendaji na uwajibikaji yanatija kwa wananchi wote ikiwemo wa jimbo la Ubungo. Aidha, kama katibu wa wabunge wa Mkoa wa Dar es salaam nina wajibu wa kushughulikia suala lolote linalomgusa mbunge yoyote wa Mkoa wetu iwapo linahitaji nguvu ya pamoja kwa maslahi ya umma. Izingatiwe pia, mwingiliano wa Dar es salaam wapo wananchi wa Ubungo wanaofanya kazi ama kufanya biashara Kigamboni ambao nao wametaka niwawakilishe kwenye suala hili kama ninavyofanya kwa mengine. Pia, ifahamike kwamba kilichotukutanisha wabunge siku tuliyotoa kauli ni kikao na kamati ya maafa ya mkoa tofauti na madai potofu aliyotoa kwamba wabunge hatujawahi kukutana kwa ajili ya masuala ya maafuriko yaliyoukumbuka mkoa wa Dar es salaam.

KUHUSU KIWANGO CHA UPANDISHWAJI WA NAULI KATIKA KIVUKO CHA KIGAMBONI NA VIVUKO VINGINE NCHINI

Waziri Magufuli ameamua kupotosha kwamba nilichompinga na kupanda kwa nauli kutoka shilingi 100 mpaka 200, na kuacha kujibu hoja kuu ambazo nilitaka azitolee maelezo na vielelezo. Ukweli ni kuwa nilichotaka kisitishwe ni utekelezaji wa agizo kupitia gazeti la serikali (GN 367) ya tarehe 4 Novemba 2011 na kuanza kutumika kwa nauli mpya kwa ujumla wake kutokana na kukiukwa kwa misingi ya utawala bora na pia baadhi ya viwango kutokuzingatia hali halisi. Kwa upande wa kupanda kwa nauli nilisisitiza kuwa kero kuu sio kupanda nauli ya mtu mzima toka shilingi 100 mpaka 200 bali kupandishwa kupindukia kwa nauli za vyombo vya usafiri na usafirishaji hali ambayo itasababisha kupanda kwa bei ya bidhaa katika eneo la Kigamboni na kuathiri watu wengi zaidi. 

Mathalani, Baskeli za matairi matatu (Guta) toka Tsh 200 hadi Tsh 1800 (Asilimia 800); bei ambayo ni kubwa kuliko ya gari ndogo; bajaj zimepanda toka Tsh 300 hadi Tsh 1300 (Asilimia 333); mikokoteni imeongezeka toka Tsh 200 hadi Tsh 1500 (Asilimia 650) na mizigo nayo inatozwa kati ya shilingi 200 mpaka 500. Sasa kwa kuwa utekelezaji wa agizo unafanyika kwa ujumla, nikataka viwango vipya kwa ujumla wake visitishwe mpaka kwanza serikali itoe maelezo na vielezo vya msingi wa kufanya ongezeko kubwa la kiwango hicho. Nilitaka serikali itoe maelezo ikizingatia kwamba vivuko ni huduma sio biashara kwa kuwa maeneo mengi yenye vivuko yalipaswa kuwa na madaraja kwa ajili ya vyombo hivyo vya usafiri na wananchi kuweza kupita. 

Nilieleza wazi kwamba kazi ya msingi ya Wizara ya Ujenzi ni kujenga barabara, madaraja na miundombinu mingine sio kufanya biashara ya vivuko hivyo, ongezeko la kuangalia soko linaweza kushawishi ucheleweshaji wa ujenzi wa madaraja. Ieleweke kwamba kazi kuu ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) sio kuendesha vivuko na kama tunataka suala hili kuwa ndio kipaumbele tunayo Wizara ya Uchukuzi ambayo inahusika pia na uchukuzi majini na inashirika la meli. Kumekuwepo na kukosekana na uwazi na udhibiti wa kutosha wa mapato na matumizi ya kivuko hivyo tulitaka serikali ieleze kwa mchanguo badala ya kauli za ujumla kuhusu suala hili ili kujenga uhalali wa kupandisha nauli husika kwa hoja ya kupanda kwa gharama za uendeshaji. Nilipinga ongezeko kubwa la bei ya umeme kwa kisingizio hicho hicho, kwa kuwa mchakato ulikuwa shirikishi naamini kutokana na maoni ya wadau yako ambayo yatarekebishwa na TANESCO tofauti na mapendekezo yao ya awali. 

Haiwezekani suluhisho la kupanda kwa gharama za maisha kwa wabunge ikawa kujiongezea posho za vikao na suluhisho kwa taasisi za umma kama Wizara ya Ujenzi na TEMESA ikiwa ni kijiongeza mapato kwa kuongeza nauli bila kuzingatia kubana matumizi na kumjali mtanzania wa kipato cha chini ambaye anabeba mzigo mkubwa wa kupandwa kwa gharama za maisha na sasa anapindishiwa hata na serikali yake nauli za vyombo vya usafiri kuvuka tu kwenye kivuko. Hivyo, Wizara ya Ujenzi kupitia vyombo vyake inapaswa kuhusisha mapato yanayokusanywa kwenye barabara na ujenzi wa miundombinu na uendeshaji wa vivuko vya muda wakati miundombinu inasubiriwa.

Pia, pamoja na nauli, msingi wa uendeshaji wa vivuko unapaswa pia kuwa mapato kutoka kwenye barabara na vyanzo vingine. Badala ya kujibu hoja ya msingi, Waziri Magufuli amejikita katika ongezeko la shilingi 100 mpaka 200 na kulinganisha pia na mazingira yasiyoendana baina ya kivuko cha Kigamboni na vivuko vingine nchini ambavyo vinatofautiana umbali, muda na gharama za uendeshaji.

KUHUSU SHERIA NA UTARATIBU AMBAO UMETUMIKA KUPANDISHA VIWANGO HUSIKA

Waziri Magufuli amezusha na kupotosha kwamba nilisema amekiuka sheria ya uendeshaji wa vivuko. Ukweli ni kwamba katika kauli yangu nilisema wazi kwamba Waziri Magufuli amepandisha viwango vya kivuko hicho kwa mamlaka aliyopewa na sheria mbovu ya vivuko (Ferries Act), hata hivyo nilisisitiza kwamba mamlaka hayo ameyatumia kibabe na kwa kutozingatia misingi ya utawala bora. Nilisema kwamba Waziri Magufuli anapaswa kuzingatia kwamba nchi haiongozwi kwa sheria moja, na ikiwa anataka kutumia sheria moja basi sheria mama ni katiba ya nchi. 

Nilisema kwamba kwa mujibu wa ibara ya 8 ya katiba ya taifa letu wananchi ndio msingi wa mamlaka, ibara ya 18 inataka wananchi wapewe taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali kwa maisha na shughuli zao na ibara ya 21 inatoa haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi ama moja kwa moja au kupitia wawakilishi. Hivyo, katika kutekeleza sheria ya vivuko na kanuni zake badala ya kutumia ubabe Waziri Magufuli alipaswa kuzingatia misingi hiyo muhimu lakini hakufanya hivyo kwa sababu nauli zimepandishwa bila kuwa na uwazi wala ushirikishwaji. Wananchi na wadau hawakushirikishwa katika kutoa maoni kuhusu suala linalowahusu kama ambavyo mamlaka zingine za kiserikali zinafanya wakati wa michakato ya kupandisha bei, mathalani mashirika ya umma ya umeme, mafuta na gesi hufanya michakato hiyo kupitia EWURA. 

Nikasema kwamba pamoja na kuwa sheria hailekezi kwa kina jambo hili, Waziri Magufuli na Wakala wa Serikali wa Ufundi na Umeme (TAMESA) walipaswa kuonyesha mfano hasa kwa kuwa walishaombwa kufanya hivyo kwa barua ya mwaka 2011 mwanzoni ambayo wizara yake haikutimiza wajibu hata wa walau kujibu. Nikaeleza kwamba Serikali imeweka mfumo kama huu kwa usafiri wa nchi kavu na majina kupitia SUMATRA kwa upande wa watoe huduma wengine, hivyo ilipaswa na yenyewe kuonyesha mfano. Ndio msingi wa kusema kwamba kwa kuwa suala hili limelalamikiwa na wananchi na wabunge ni vizuri agizo likasitishwa na taratibu shirikishi zikatumika kwa kushauriana na SUMATRA. 

Nilieleza kwamba suala hili linatokana na udhaifu wa mifumo yetu ya utendaji na uendeshaji ambapo taasisi za kiserikali zinahodhi michakato muhimu ya kitaifa na linakuwa zito zaidi kwa kuwa halikuelezwa bayana hata wakati bunge linajadili makadirio ya mapato na matumizi ya serikali bungeni ya Wizara ya Ujenzi Tarehe 1 na 2 Agosti 2011. Nikaeleza kwamba mjadala huu ni muhimu kwa taifa kwa ajili ya kubadili sheria na taratibu husika pamoja na kuweka mfumo mzuri zaidi wa utendaji na uwajibikaji bila kuwa na mivutano kwenye masuala ambayo kama yangekuwepo mawasiliano na mashauriano yasingefikia hatua ya kuwa malumbano. Hivyo, tukiachia hali hii ikiendelea bila uwazi, ushirikishaji na uwajibikaji itaendelea kwenye masuala yanayowagusa wananchi wa maeneo mengine nchini ikiwemo wa jimbo letu la Ubungo. Kwa hiyo, kuunga kwangu mkono suala hili ilikuwa ni sehemu ya kutekeleza ahadi ambayo niliwaahidi wananchi wa Ubungo wakati wa uchaguzi kwamba nitasimamia vyombo vyote vinavyohusika na masuala ya usafiri na mengine ya huduma za msingi wa umma.

KUHUSU KAULI ZISIZOZINGATIA MISINGI YA UONGOZI NA UTAWALA BORA

Nilipinga kauli za Waziri Magufuli zisizozingatia uongozi na utawala bora mathalani kuwaambia wananchi wapige mbizi au kumshambulia mbunge katika jambo ambalo kama Waziri Magufuli na TEMESA wangezingatia misingi ya utendaji bora kwa kujibu barua lisingefikia kuwa na malumbano hadharani. Waziri Magufuli angeweza kabisa kujenga hoja bila kuzusha vioja visivyo vya lazima, kisingizio cha kauli ya watendaji wa Wizara yake kwamba alifanya hivyo baada ya kuzomewa na wananchi hakiwezi kuhalalisha misingi muhimu ya uongozi wa busara na unyenyekuvu badala ya ubabe na uropokaji. Jambo hili lisingekuwa na uzito kama ingekuwa ni makosa ya mara ya kwanza, hata hivyo nililazimika kutoa kauli ya kumtaka aombe radhi nikikumbuka pia kauli zake ambazo mpaka sasa hajawahi kuomba radhi kwa umma wakati akijibu wananchi na viongozi waliokuwa wakilalamikia uuzwaji holela wa nyumba za serikali kwamba ‘nyie mwaona wivu’ ama ‘mlie tu’. Hivyo, ameendeleza tu hulka yake na sitarajii kwamba itabadilika hata baada ya taarifa hii kwa umma kuhusu masuala ambayo amezusha na kupotosha juu yangu. Kwa heshima niliyonayo kwake natarajia kwamba atabadilika, na natarajia utakubali ndani ya wiki moja kunijibu kukubali kupokea changamoto hizi na kuzifanyia kazi. Asipofanya hivyo, tutakutana bungeni na nitafuatilia mabadiliko ya kisheria, kikanuni, kimfumo na kiutendaji katika Wizara yake kwa karibu zaidi kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu ya wananchi wa Jimbo la Ubungo na Taifa kwa ujumla.Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
08/01/2012

2 comments:

Anonymous said...

Safi sana, afadhali umefanunua mbunge wetu

Alvin Leon said...

umemaliza kaka, ccm na magufuli wao wamejaa misifa bureee