Saturday, January 28, 2012

Taarifa ya Hoja kuhusu utekelezaji wa maazimio juu ya Richmond

Tarehe 25 Januari 2012 nimewasilisha kwa Katibu wa Bunge taarifa ya hoja kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007 Kanuni 54 (4) na 55 (1) kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Richmond Development Company LLC.

Hoja hiyo ikipewa nafasi ya kuwasilishwa na kujadiliwa itaongeza msukumo wa utekelezaji wa maazimio ya bunge na hivyo kuchangia katika mapitio ya mikataba yenye kuongeza bei ya umeme; kuweka mfumo wa kulihusisha bunge katika maandalizi ya mikataba yenye maslahi ya taifa ikiwemo katika mafuta, gesi asilia na ujenzi na kuwezesha uwajibikaji na hatua kamili kuchukuliwa kwa waliohusika na ufisadi na uzembe uliolisababishia hasara taifa.

Taaarifa hii ya hoja niliiwasilisha awali tarehe 13 Aprili 2011 na kupatiwa majibu; hata hivyo niliijibu ofisi ya bunge kupatiwa taarifa ya utekelezaji uliofanywa na serikali baada ya Februari 2010 bila kupatiwa majibu hivyo nimeiwasilisha tena ili hoja husika ijadiliwe.

Lengo la Hoja Binafsi nitakayoiwasilisha kufuatia taarifa hiyo ni kutaka uamuzi wa Bunge uliofanyika katika Bunge la Tisa Mkutano wa 18 mwezi Februari 2010 kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya mkataba baina ya TANESCO na kampuni ya Richmond Development Company LLC; UBADILISHWE.


Katika muktadha huo, hoja binafsi husika itawezesha mjadala kuhusu uamuzi husika kufunguliwa na kutoa fursa kwa jambo hilo kufikiriwa tena ili kuwezesha hatua kamili kuchukuliwa juu ya maazimio 23 ya Bunge yaliyopitishwa tarehe 15 Februari 2008 katika Mkutano wa 10 wa Bunge la Tisa.

Taarifa ya tatu ya Serikali Februari 2010 ilitanguliwa na Taarifa mbili zilizowasilishwa Bungeni na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, tarehe 28 Agosti, 2008, tarehe 11 Februari, 2009 na Taarifa moja iliyokabidhiwa na kujadiliwa na Kamati, ambazo zililitaarifu Bunge kuwa utekelezaji wa Maazimio 10 kati ya 23 yaliyotolewa na Bunge, yamefanyiwa kazi hadi mwezi Februari, 2009 na Maazimio 13 bado yalikuwa hayajakamilika. Maazimio hayo 13 ni: Nambari 1,2,3,5,7,8,9,10,11,13,14,15 na 18. Hoja binafsi itakapojadiliwa bungeni itawezesha Bunge na wananchi kwa ujumla kupata taarifa ya utekelezaji wa maazimio hayo 13.

Kati ya maazimio hayo 13, baadhi ya maazimio ambayo utekelezaji wake haujakamilika ni pamoja:

Azimio Na. 3, ambalo liliagiza kwamba “Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC (uliorithiwa na Dowans Holdings S.A.) na ile kati ya TANESCO na IPTL, SONGAS, AGGREKO na Alstom Power Rentals, ipitiwe upya mapema iwezekanavyo kama ambavyo Mikataba ya Madini ilivyopitiwa upya na Serikali”. Iwapo Azimio hili lingetekelezwa kwa ukamilifu wake, gharama za uzalishaji TANESCO zingepungua na hivyo bei ya umeme isingepandishwa kwa kiwango kikubwa kama ilivyo sasa, ambapo Januari 2011 ilipandishwa kwa wastani wa 18.5% na Januari 2012 imepandishwa tena kwa wastani wa 40.29 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mzigo mkubwa wa ufisadi na ubovu wa mikataba.

Azimio Na. 8 na 14, maudhui ya maazimio hayo yanafanana kwa sababu yaliitaka “Serikali iwawajibishe Viongozi wenye dhamana ya kisiasa waliokuwa Mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini ambao wakati ule alikuwa ni Mheshimiwa Dkt. Ibrahim Msabaha na Mheshimiwa Nazir Karamagi.” Bunge lilielezwa kwamba vyombo vya Dola vimekamilisha uchunguzi wake wa ndani ya Nchi kuhusu suala hili. Hata hivyo zoezi lililoendelea toka Februari 2010 ni kufanya uchunguzi wa nje ya Nchi kwa kushirikiana na Vyombo vya Dola vya Kimataifa ambapo mwaka mmoja umemalizika bila hatua zozote kuchukuliwa kwa wahusika katika kashfa ambayo maazimio ya bunge yalipitishwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita hali ambayo inaweza kusababisha hata mashahidi na ushahidi kupotea.

Azimio Na. 13, “Serikali izihusishe Kamati za Kudumu za Bunge kwenye hatua za awali za maandalizi ya Mikataba mikubwa ya muda mrefu ya kibiashara ili kuondokana na utaratibu uliopitwa na wakati kwamba Mikataba ya Kibiashara ni siri hata kwa walipa kodi wenyewe. Aidha, Serikali ihakikishe kuwa, Kamati zote za Bunge zinapitia Mikataba mikubwa ya muda mrefu ya kibiashara chini ya sekta zao ili kuliondolea Taifa mizigo isiyo ya lazima”. Azimio hili halijaanza kutekelezwa kwa ukamilifu wake matokeo yake ni kwamba serikali katika kipindi cha kati ya mwaka 2008 mpaka 2011 imeendelea kuwa siri katika hatua za awali za maandalizi na pia mikataba mingi haijafanyiwa mapitio. Hoja binafsi itawezesha mjadala kuhusu suala hili kufunguliwa na utaratibu thabiti kuwekwa katika kipindi hiki ambacho taifa linaingia katika mikataba mingi ya ujenzi na miundombinu na pia mikataba ya utafutaji na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia ambayo ina umuhimu wa pekee kwa uchumi na usalama wa nchi. Aidha, azimio hili lingetekelezwa kwa ukamilifu lingesaidia kuwa na mfumo mzuri zaidi wa maandalizi ya mikataba wakati huu ambapo serikali inaingia mikataba mingi ya gharama kubwa ya utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme hali ambayo imeongeza mzigo mwingine wa gharama za maisha kwa wananchi.

Azimio Na. 10, “Gavana wa Benki Kuu pamoja na Bodi ya Wakurugenzi, wachunguze kwa makini uhalali wa malipo ya ziada (US$ 4,865,000) yaliyofanywa kwa Dowans Holdings S.A iliyorithi majukumu ya Richmond Development Company LLC na kuwachukulia hatua waliohusika na uzembe huo.” Hoja Binafsi itawezesha mjadala kufunguliwa na mambo zaidi yaliyojiri kuhusu suala hili na mengine kuweza kujulikana na hatua kuchukuliwa kwa wote waliozembea ili kuimarisha misingi ya uwajibikaji katika taifa.

Masuala zaidi kuhusu maazimio mengine nitayaweka katika Maelezo ya Hoja na Hoja Husika ili niwasilishe katika Mkutano wa Sita wa Bunge la 10 uliopangwa kuanza tarehe 31 Januari 2011 kwa kadiri itakavyoelekezwa.

Imetolewa tarehe 27 Januari 2012 na:

John Mnyika (Mb)

Mbunge wa Ubungo



1 comment:

Anonymous said...

that is good John, never give up, u gonna face a very stiff competion due to the nature of the contarct itself, beneficiaries of that contracts and other stakeholders of the said!it will awake another hope if it will be approved to be discused!its Japhet