Wednesday, March 21, 2012

Soma, Shiriki na Shirikisha na wengine kuwezesha mabadiliko ya kweli

Soma, Shiriki na Shirikisha na wengine: Mabadiliko Arumeru Mashariki (Arusha) na Vijibweni (DSM) yatawezeshwa na wewe, mimi na wenzetu.


Kesi ya uchaguzi wa Ubunge Ubungo imenifanya nishindwe kurudi Arumeru Mashariki mapema kwa kuwa nawajibika kuandaa ushahidi na mashahidi. Kiroho nipo pamoja na makamanda wengine katika mapambano kuhakikisha Nassari anaungana nasi kupunguza hodhi ya chama kimoja bungeni. Katika siku hizi ambazo nalazimika kuwepo DSM, kiakili na kimwili pamoja na kesi na majukumu mengine ya kibunge naelekeza nguvu katika uchaguzi wa udiwani kata ya Vijibweni Jimbo la Kigamboni Manispaa ya Temeke.

Marafiki zangu na wote mnaouniunga mkono mlio Arusha naomba muwezeshe uwepo wangu kiroho kwa kushiriki katika harambee ya kuchangia chama itakayofanyika Naura Spring Hotel tarehe 23 Machi 2012 kuanzia saa 1 Usiku. Wasilianeni na Mwigamba 0784815499 au 0713953761 kwa maelezo na maelekezo. Mkishashiriki mnipe mrejesho kuhusu ushiriki wenu kupitia mnyika@chadema.or.tz ili Mungu akipenda nikija Arumeru Mashariki mwishoni mwa kampeni kuongeza nguvu tuweze kuonana. Hakuna Kulala; Mpaka Kieleweke.

Marafiki zangu na wote mnaoniunga mkono katika Jiji la Dar es salaam naomba mshirikiane nami kwa hali na mali kuhakikisha kwamba Manispaa ya Temeke ambayo ndio pekee katika mkoa wa Dar es salaam isiyokuwa na Diwani yoyote wa kata wa CHADEMA inapata walau mwakilishi mmoja kutoka chama mbadala. Wasilianeni na Kilewo 0714225960 au 0756091748 kwa ajili ya maelezo na maelekezo na mnipe mrejesho kupitia mnyika@chadema.or.tz. Kwa kipindi cha mwaka mmoja cha utumishi wa umma nimeshuhidia umuhimu wa kuchanganya vyama katika mabaraza ya madiwani katika kuongeza uwajibikaji kwenye usimamizi wa fedha za umma katika serikali za mtaa ambazo ndio zinashughulikia kwa kiwango kikubwa masuala ya maendeleo katika maeneo yetu. Tuunganishe nguvu ya umma kuwezesha mabadiliko ya kweli. Shiriki sasa na shirikisha na wengine; Maslahi ya Umma Kwanza.

John Mnyika (Mb), Mkurugenzi wa Habari na Uenezi (CHADEMA)-22/03/2012

1 comment:

Anonymous said...

nakusalim kaka,pamoja na juhudi ambazo mmekua mkizifanya mimi nawalaumu kwa kushindwa kulinda kura zenu hasa katika chaguzi ndogo,nina ushahidi wa namna mambo yalivyofanyika igunga kwakua kaka yangu yuko usalama wa taifa,hivi majuzi vijana zaidi ya 200 wa CCM wameondoka hapa dodoma wakielekea Arumeru,kwa uelewa wao na uwezo wao sidhani kama wanaenda kusaidia kampeni mimi nahisi kuna kitu wanaenda kufanya,hapo ni dodoma tu sijajua mikoa mingine wamekwenda wangapi,nawasihi muwe makini la sivyo hii michezo mibaya itaendelea kuwanufaisha ccm kila siku,mwisho nikupe moyo wa kuendelea na mapambano na uwe imara kupigania haki yako kwani nimeona tuhuma za huyo mama sijazielewa kabisa na natumaini kwa uelewa wako huwezi kukosea kujumlisha,kazi njema JJ