Wednesday, September 26, 2012

Shiriki mkutano wa EWURA na wananchi kuhusu udhibiti wa huduma ya maji kwa magari na visima binafsi kesho 27 Septemba, 2012; toa maoni kuandaliwe kanuni za kudhibiti ubora na kuwezesha kutolewa kwa bei elekezi


Natoa mwito kwa wananchi wa Jimbo la Ubungo kuhudhuria mkutano wa wadau, wananchi na watoa huduma ya maji kwa magari na visima binafsi katika Jiji la Dar es salaam ulioitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) tarehe 27 Septemba 2012 katika Ukumbi wa Land Mark Hotel River Side Ubungo kuanzia saa 3 asubuhi.

Aidha, katika kujadili ajenda za mkutano huo zilizotolewa naitaka EWURA kuweka mkazo katika kupokea maoni ya wananchi ili kuwezesha kuandaliwa kwa haraka kwa kanuni za usimamizi na bei elekezi ya maji katika jiji la Dar es salaam ikiwemo katika visima na malori binafsi kwa kuzingatia kuwa katika ziara yangu katika kata nane za Jimbo la Ubungo katika kipindi cha mwezi Agosti na Septemba 2012 nimepokea malalamiko mengi juu ya ongezeko la bei ya maji ambayo imefikia mpaka shilingi mia tano kwa dumu moja la lita 20 bila udhibiti wowote.

Kwa mujibu wa Tangazo la EWURA lililotolewa mwezi Septemba 2012 Mkutano huo ambao wadau wote wa maji ikiwemo wananchi wanaalikwa kushiriki utajadili haki na wajibu wa watoa huduma ya maji Jijini Dar es salaam; mwongozo wa watoa huduma ya maji kwa visima na magari binafsi na utaratibu utakaotumiwa na DAWASCO kusajili watoa huduma wa maji ya visima na wasambazaji wa maji kwa magari binafsi.

Izingatiwe kuwa katika mikutano yangu na wananchi ya awamu ya pili katika kata nane za Jimbo la Ubungo kati ya Agosti na Septemba 2012 nilisisitiza kuwa EWURA ina wajibu kama ilivyo kwenye mafuta na umeme kusimamia sekta ya maji siyo ya umma tu hata binafsi, hata hivyo kwa sasa inasimamia zaidi bei na ubora kwa upande wa mamlaka za umma.

Hivyo, nilitoa mwito kwa wananchi kuungana kuitaka EWURA kueleza hatua iliyofikiwa katika kuandaa kanuni za usimamizi wa sekta binafsi ya maji juu ya mfumo wa bei elekezi na viwango vya ubora kama ambavyo mamlaka husika iliahidi kwenye Kongamano la Maji Ubungo mwaka 2011 suala ambalo lipaswa kuzingatiwa na wadau watakaoshiriki kwenye mkutano unaofanyika tarehe 27 Septemba 2012.

Itakumbukwa tarehe 2 Machi 2012 nilifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo masuala mengine niliitaka EWURA kutoa kauli ndani ya kipindi cha wiki moja kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya kanuni husika pamoja na udhibiti wa bei ya maji ikiwemo kwenye sekta binafsi katika jiji la Dar es salaam.

Katika mkutano wangu na wanahabari tarehe 2 Machi 2012 nilieleza kuwa kupitia ziara ya kikazi katika kata saba za Jimbo la Ubungo nilibaini kwamba  kubwa ya ubora na bei ya maji jijini Dar es salaam katika sekta binafsi; bei ya maji iko juu sana hali ambayo inashawishi biashara haramu yenye kuhusisha hujuma katika miundombinu ya maji na ufisadi wenye kuharibu ratiba ya mgawo wa maji ili kupanua soko kinyemela.

Tarehe 8 Machi 2012 Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa EWURA Titus Kaguo alinukuliwa vyombo vya habari akinijibu kuwa mamlaka hiyo haiwezi kutoa bei elekezi kwenye maji kwa kuwa tayari ilishafanya hivyo mwaka 2010 bila kuzingatia kuwa bei elekezi pekee iliyotolewa na EWURA ni katika visima, maghati na mabombo ya umma yanayoendeshwa na DAWASA na DAWASCO.

Kufuatia majibu hayo tarehe 8 Machi 2012 nilitoa taarifa kwa umma kuwa kauli ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) iliyonukuliwa na vyombo vya habari tarehe 8 Machi 2012 kuwa mamlaka hiyo haiwezi kutoa bei elekezi ya maji kwa kuwa imekwishatoa tayari mwaka 2010 haipaswi kukubaliwa na wananchi na wadau wa sekta ya maji katika Jiji la Dar es salaam.

Katika taarifa hiyo niliitaka EWURA kutimiza kwa ukamilifu wake wajibu wake kwa mujibu wa Sheria mbili muhimu za usimamizi wa sekta ya maji nchini (Water Supply and Sanitation Act of 2009 and The Energy and Water Utilities Regulatory Authority Act)

Katika taarifa hiyo nilitoa mwito kwa EWURA kutoa maelezo ya kina kuhusu hatua iliyofikiwa katika kuandaa kanuni za usimamizi wa sekta binafsi ya maji juu ya mfumo wa bei elekezi na viwango vya ubora kama ambavyo mamlaka husika iliahidi kwenye Kongamano la Maji Ubungo mwaka 2011.

Pamoja na kutoa taarifa hiyo kwa umma niliiandikia  barua EWURA itimize wajibu wake wa kusimamia ubora na bei hata hivyo nilipokea majibu kuwa muongozo bado haujaandaliwa, hivyo mkutano huu wa tarehe 27 Septemba 2012 ni fursa muhimu ya kuharakisha maandalizi ya kanuni na utaratibu husika.

Ufumbuzi wa kudumu wa kushusha bei ya maji ni DAWASA na DAWASCO kuongeza uzalishaji, usafirishaji na usambazaji hata hivyo udhibiti wa EWURA kuhusu ubora na bei katika kipindi hiki cha upungufu ni muhimu kuepusha madhara kwa umma ya kuuziwa maji yasiyo na ubora na kwa bei ya kuruka hali ambayo inawathiri zaidi wananchi wa kipato cha chini.

Imetolewa tarehe 26 Septemba 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo


Thursday, September 20, 2012

MREJESHO: Matatizo ya Maji Kata ya GOBA


Pamoja na manispaa ya Kinondoni kutoa shilingi milioni moja na nusu tarehe 14 Septemba 2012 kwa ajili ya kufunga mita na kuanza kusukuma maji ya mradi wa Goba, tarehe 19 Septemba 2012 wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani nimemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kuwawajibisha watendaji waliozembea na kusababisha matatizo hayo kudumu kwa muda mrefu.

Izingatiwe kuwa kiasi hicho ni nyongeza baada ya awali kutolewa milioni tatu na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo la Ubungo (CDCF) kwa ajili ya kuwezesha huduma ya maji kupitia mradi huo kurejea.

Ikumbukwe kuwa mwezi Agosti 2011 maji yalikatwa kwenye kata ya Goba kutokana na DAWASCO kuidai kamati ya mradi wa maji shilingi milioni 18 na katika kufuatilia deni hilo nilipata taarifa za Kamati ya Maji kuwasilisha malalamiko DAWASCO ya kutokukubaliana na kiwango hicho cha deni na pia kwa Manispaa ya Kinondoni kuhusu matatizo ya kiutendaji na kifedha katika mradi huo wa maji ikiwemo ya upotevu wa fedha.

Tarehe 5 Septemba 2011 niliwaunganisha wananchi kwa pamoja tukaandamana kwenda ofisi ya DAWASCO makao makuu ambapo tulikutana na mtendaji mkuu wa kampuni husika na kufanya mazungumzo ambayo yalisaidia baadhi ya hatua za msingi kuchukuliwa ikiwemo DAWASCO kurejesha huduma ya maji katika bomba kuu baada ya sehemu ya deni kulipwa na makubaliano kufikiwa kuhusu malipo ya kiwango kilichobaki.

Pia tarehe 24 Oktoba 2011 niliandika barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kutoa mwito wa hatua za dharura kuchukuliwa ili kuhakikisha uhakiki unafanyika wakati huo huo wananchi wengine wanaendelea kupata huduma ya maji; lakini udhaifu wa kiutendaji umefanya hatua ziwe za kusuasua.

Hata hivyo, pamoja na huduma ya maji kurejeshwa katika bomba kuu haikuweza kusambazwa kwenye mabomba ya wananchi pamoja na vioski vya kutolea huduma kwa sababu ya udhaifu wa utendaji katika ngazi ya kata na katika kamati ya maji hivyo tarehe 26 Januari 2012 niliwaunganisha wananchi kufika Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya hatua za haraka za Mkurugenzi wa Manispaa.

Kufuatia hatua hiyo Mkurugenzi wa Manispaa Fortunatus Fwema alifanya ziara katika kata ya Goba tarehe 31 Januari 2012 na kuagiza kwamba ndani ya tano maji yatoke katika kata hiyo na kuagiza Mhandisi wa maji na timu yake waweke kambi katika kata ya Goba mpaka maji yatoke kwa gharama za halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Hata hivyo, muda huo ulimalizika bila maji kupatikana na kikosi kazi kilikabidhiwa jukumu tarehe 28 Februari 2012 kushughulikia kile kilichoelezwa kuwa ni kuanza uchunguzi wa Bomba la Maji kuanzia Tanki Bovu hadi kwenye tanki la Matosa ili kubaini wizi, upotevu wa maji na uharibifu wa miundombinu.

Katika kipindi cha kati ya Februari mpaka Agosti 2012 nimefuatilia Manispaa kwa njia mbalimbali na wakati wote maelezo yamekuwa kazi hiyo inachukua muda mrefu kwa sababu ya urekebishaji wa miundombinu ambapo Manispaa ya Kinondoni ilikubali kutoa mita 15 pamoja na stendi za bomba mpya kwa ajili ya kufunga katika bomba kubwa kwenye njia zinazoelekea kwa wananchi ili kudhibiti wizi na upotevu wa maji pamoja na kufanya marekebisho katika mabomba na gate-valves zilizohujumiwa.

Ikumbukwe kuwa matatizo ya maji kata ya Goba yanafahamika kwa mamlaka zote husika kuanzia Wizara ya Maji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Kinondoni na vyombo vya dola kuanzia mwaka 2007 mpaka mwaka 2012 lakini hatua kamili hazijachukuliwa kwa wakati.

Wananchi wa Goba wamepoteza uvumilivu kwa kuwa hatua hazichukuliwi kwa haraka na kutokana na hali hiyo mbunge kama mwakilishi wa wananchi nimeumua kuungana nao katika kutaka uwajibikaji wa watendaji wote waliozembea na kusababisha matatizo hayo kudumu kwa muda mrefu.

Nimefikia hatua hiyo kwa sababu njia zote za kawaida kupitia vikao na mawasiliano ya kiofisi zinaelekea kukwamishwa na uzembe, hujuma na urasimu na udhaifu wa kiutendaji katika ngazi mbalimbali.

Katika kushughulikia masuala la maji kwenye kata ya Goba, narudia kusisitiza hatua zifuatazo kuendelea kuchukuliwa kwa haraka na mamlaka zifuatazo:

Mosi; Mamlaka za Manispaa ya Kinondoni zikiongozwa na Meya na Mkurugenzi zinapaswa kufuatilia kwa haraka kuhakikisha maji yanarejeshwa Goba. Hatua hii iende sambamba na kupanua wigo wa maji Goba kwa kutekeleza kwa haraka upatikanaji wa maji kutoka pia mradi wa maji toka Madale Kisauke. 

Manispaa izingatie matatizo yaliyopo kwenye miradi ya maji inayoendeshwa na manispaa pamoja na kamati za wananchi au vyama vya watumia maji katika maeneo mbalimbali. Hivyo, pamoja na kuchukua hatua kuhusu mradi wa maji wa Goba, Manispaa ichukue hatua juu ya miradi iliyokwamba ukiwemo wa Mbezi Msumi na Makabe. Pia, Manispaa ya Kinondoni inapaswa kufanya mabadiliko kwenye idara ya maji kwa kuwa ina udhaifu mkubwa wa kiutendaji.

Pili; Wizara ya Maji, Mamlaka ya maji safi na maji taka (DAWASA) na Kampuni ya maji safi na maji taka (DAWASCO) zizingatie kwamba maeneo ya pembezoni ya Dar es salaam ambayo awali yalikuwa vijiji sasa ni mitaa yenye wakazi wengi. Hivyo, maeneo kama kata ya Goba na mengine ya pembezoni yanapaswa kuunganishwa moja kwa moja na mtandao wa maji chini ya mamlaka husika kwa mujibu wa sheria iliyounda DAWASA badala ya mfumo uliopo ambalo haulingani na mahitaji.

Tatu; vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kushughulikia vyanzo vya migogoro badala ya kusubiri mpaka matatizo yanapoibuka kwa kushughulikia kwa wakati malalamiko yanayotolewa. Mathalani, Jeshi la Polisi (Ofisi ya DCI) na TAKUKURU wanapaswa kutoa kauli kuhusu hatua zilizochukuliwa juu ya tuhuma za ufisadi na ukiukwaji wa sheria katika mradi wa maji Goba ambazo zimetolewa na wananchi kwa mamlaka husika kuanzia mwa 2007.

Mamlaka husika zizingatie kuwa tarehe 27 Februari 2011 na 6 Machi 2011 nilifanya mikutano na wananchi katika kata ya Goba ambapo risala ya wananchi pamoja na ripoti ya ukaguzi wa mradi wa mradi wa maji Goba ya mwaka 2007 zilizosomwa ambazo zilieleza bayana matatizo yaliyokuwepo kwenye kamati ya maji pamoja na mradi kwa ujumla ikiwemo yaliyohusu upotevu wa fedha ambayo vyombo vya dola vilipatiwa taarifa lakini hatua hazikuchukuliwa kwa wakati. 

Kwa nyakati mbalimbali nimeziandikia barua rasmi mamlaka husika kuhusu masuala haya na mengine  na kutokana na kutochukua hatua kwa wakati mwezi Agosti 2012 kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge nilikutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na kumweleza haja ya kuingilia kati ili ufumbuzi upatikane mapema.

John Mnyika (Mb)
19/09/2012


Wednesday, September 19, 2012

Hatimaye ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Maziwa mpaka External pamoja na daraja unaanza!!


Tayari taratibu za zabuni zimeshakamilika na mkandarasi anapaswa kuanza ujenzi. Manispaa ya Kinondoni imeshaweka alama ya "X" katika majengo ambayo yatapaswa kubomolewa kuwezesha upanuzi wa barabara husika unaofanywa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Dar es salaam (TANROADS).

Tarehe 15 Septemba 2012 nilifanya mkutano wa hadhara Jimboni Ubungo kwenye kata ya Makuburi ambapo pamoja na maswali mengine niliulizwa ni lini ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami kutoka Maziwa mpaka External ukiambatana na ujenzi wa daraja katika barabara husika utaanza.

Pamoja na kueleza hatua iliyofikiwa mpaka sasa nilitoa mwito wananchi wote ambayo makazi yao yamewekewa alama ya "X" ikiwa si wavamizi wa barabara wawasilishe kwa Manispaa ya Kinondoni maelezo na vielelezo vyao kwa kuzingatia Wakala wa Barabara Mkoa wa Dar es es salaam (TANROADS) wao wana bajeti ya ujenzi pekee na madai ya fidia kwa wenye uhalali yako chini ya Manispaa ya Kinondoni; tayari 17 Septemba 2012 baadhi ya wananchi wamewasilisha nyaraka zao.

Ikumbukwe pia kuwa kwa kutambua umuhimu wa suala hili nilichukua hatua mbalimbali za kibunge kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2011 ili barabara husika iweze kupandishwa hadhi na kujengwa kwa kiwango cha lami kwa haraka zaidi kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kuliko ilivyopangwa awali.

Niliziandikia mamlaka husika hususan Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuzingatia barabara tajwa katika bajeti kwa lengo la kuchangia katika kupunguza msongamano, Wizara ya Ujenzi awali ilisema serikali kuu haiwezi kushughulikia barabara hiyo kwa kuwa iko chini ya Manispaa ya Kinondoni. Lakini, nikaendelea kuchukua hatua zaidi kwa njia za kibunge na za uwakilishi wa wananchi na hatimaye TANROADS ikaingiza barabara hiyo katika vipaumbele vyake na kutenga fedha za ujenzi wa kiwango cha lami kiasi cha shilingi bilioni 1.2.

Aidha, pamoja na kiwango hicho cha fedha kilichotengwa na TANROADS, tarehe 5 Machi 2012 Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alieleza kuwa amewasilisha maombi mengine kupitia Mfuko wa Barabara (Road Fund) kwa ajili ya ujenzi wa  daraja kubwa zaidi katika barabara hiyo kwenye eneo la Ubungo Kisiwani/External suala ambalo pia kwa nyakati mbalimbali nilihoji utekelezaji wake.

Izingatiwe kwamba tarehe 21 Machi 2012 niliunganisha wananchi kuchangia hatua za dharura za kufanya matengenezo ili kupunguza kero lakini nikasisitza kuwa suluhisho muhimu zaidi ni kupanua daraja la External katika Eneo la Ubungo Kisiwani ili kupunguza msongamano wa magari na kujenga barabara husika kwa kiwango cha lami hatua ambayo sasa inaelekea kuchukuliwa kwa haraka.

John Mnyika (Mb)
18 Septemba, 2012

Tuesday, September 18, 2012

“Waziri Tibaijuka aeleze uendelezaji wa Mji wa Luguruni Kibamba na eneo la Kwembe Kati”.




MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kuueleza umma kuwa mwendelezaji mwenza aliyepatikana kwa ajili ya mji wa kisasa wa Luguruni anatoka kampuni gani.





Mbali na kueleza jina la kampuni hiyo, Mnyika pia amemtaka waziri huyo kueleza kazi hiyo itaanza lini na nafasi ya serikali na wananchi ni ipi katika mradi huo na kisha aweke hadharani mkataba ulioingiwa baina ya mwendelezaji mwenza huyo kutoka sekta binafsi na serikali, ili wananchi watambue mipaka yao.





Mnyika alitoa kauli hiyo juzi katika eneo la Kibamba mji mpya alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara, baada ya kufanya kazi ya kichama ya kufungua matawi saba (7) ya CHADEMA katika kata ya Kwembe.

Alisema serikali ilichagua eneo la Luguruni kuwa moja ya sehemu zitakazojengwa miji ya kisasa kwa lengo la kupunguza msongamano mjini na ikaingia gharama za kupima viwanja kulipa fidia kwa wananchi wa maeneo hayo na kueleza kuwa kitendo cha kuacha kuwa pori ni kuhatarisha usalama wa wananchi wa maeneo hayo.

“Mwaka huu serikali iliahidi bungeni juu ya kupatikana mwendelezaji mwenza sasa watufahamishe basi ni nani kwa kuwa leo wananchi wanalalamikia eneo hili kuwa sehemu ya maangamizi yao, wanakabwa wanaibiwa na hata kubakwa kama walivyosema lakini pia kuendelea kuacha eneo hili kuwa pori ni kuwaruhusu watu wavamie kisha serikali iingie gharama nyingine ya kuwaondoa,” alisema Mnyika.

Habari hii imeandikwa na Abdallah Khamis na kuchapwa na gazeti la Tanzania Daima rejea: http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=40614

KAULI KUHUSU TAARIFA YA TANESCO JUU YA MAAMUZI YA MAHAKAMA KUU KWENYE KESI YA DOWANS

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tarehe 7 na 8 Septemba 2012 haijatoa ufafanuzi kuhusu masuala niliyotaka Serikali kupitia kwa Waziri wa Nishati na Madini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuyatolea majibu hivyo bado nasubiri kauli zao kuhusu maamuzi ya mahakama kuu kwenye kesi ya TANESCO na Dowans na kuhusu matumizi katika kesi ya IPTL.

Aidha, taarifa hiyo imeibua tena mjadala kuhusu ufanisi wa makampuni binafsi ya wanasheria yanayoishauri TANESCO na kuiwakilisha mahakamani hivyo narudia kutoa mwito kwa Serikali kuagiza ukaguzi na uchunguzi unaoendelea kuhusu tuhuma za ufisadi na ubadhirifu ndani ya TANESCO kuhusisha pia ukaguzi na uchunguzi wa matumizi ya fedha na ufanisi wa huduma za kisheria ambazo TANESCO ikitumia katika kesi za Dowans na IPTL.

Jana tarehe 7 Septemba 2012 nilitoa kauli kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ya kuitaka serikali isitumie kizingizio cha maamuzi ya Mahakama Kuu ya juzi tarehe 6 Septemba 2012 kuharakisha mpango wa kuilipa Dowans kwa fedha za walipa kodi watanzania au kubebesha mzigo huo kwa wateja wa TANESCO.

Sunday, September 16, 2012

MAJARIBIO YA USAFIRI WA TRENI DAR ES SALAAM NI HATUA MUHIMU, TRL NA RAHCO WANAPASWA KUCHUKUA HATUA ZA HARAKA ZAIDI KWA KUSHIRIKIANA NA HALMASHAURI KAMA NILIVYOZIELEZA BUNGENI AGOSTI 2012 KUHUSU MAENEO YA MABIBO NA UBUNGO

Tarehe 10 Septemba 2012 majaribio ya usafiri wa treni katika jiji la Dar es salaam yalifanywa kuanzia Stesheni mpaka Ubungo Maziwa. Kufuatia majaribio hayo kauli kuhusu changamoto zilizopo ilitolewa na Naibu Waziri Dkt Charles Tizeba na maoni mbalimbali yametolewa na wadau wengine kwenye vyombo vya habari tarehe 11 na 12 Septemba 2012.

Kwa nafasi yangu ya Mbunge wa Ubungo katika Jiji la Dar es salaam natambua kuwa majaribio hayo ni hatua muhimu katika suala ambalo tangu mwaka 2010 kwa nyakati mbalimbali nimeihoji Serikali kutaka utekelezaji wa haraka kwa kuzingatia kuwa suala hilo lilikuwa kwenye mipango zaidi ya miaka 10 iliyopita hata hivyo hatua zaidi na za haraka zinahitajika kwa huduma ya usafiri wa reli kuanza tarehe 1 Oktoba 2012 na kuweka mazingira bora ya usafiri huo kupunguza msongamano.

Natoa mwito kwa Waziri na Naibu Waziri wa Uchukuzi kuzingatia mchango wangu nilioutoa bungeni mwezi Agosti 2012 ili kuhakikisha kwamba TRL na RAHCO zinashirikiana kwa karibu na Halmashauri za Jiji la Dar es salaam kushughulikia changamoto zinazohusu uvamizi wa maeneo ya hifadhi za njia za reli na ufinyu wa eneo la kugeuzia vichwa vya treni sehemu ya Ubungo Maziwa.

Thursday, September 13, 2012

SIJARIDHIKA NA MAJIBU YA TANESCO KUHUSU UCHAFUZI WA MAZINGIRA, FIDIA YA WANANCHI WANAOISHI MAENEO HATARISHI YA KARIBU NA MITAMBO YA KUFUA UMEME UBUNGO IHARAKISHWE


Tarehe 9 Septemba 2012 baadhi ya vyombo vya habari viliandika habari kwamba wakazi zaidi ya 500 wa eneo la Ubungo Darajani karibu na Riverside wanalalamika kuishi kwenye mfereji wa maji taka wenye mafuta ya mitambo na mchanganyiko wa kemikali kadhaa zinazodaiwa kuzalishwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Sijaridhika na majibu yaliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Felichism Mramba kwamba shirika hilo limedhibiti mfumo wa maji taka na haihusiki na tatizo hilo la kuchafua makazi na mazingira.
Kufuatia kauli hiyo, natoa wito kwa Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO kutoa majibu ya wazi kwa wananchi ni kampuni gani hasa inahusika na uchafuzi huo wa mazingira na kuchukua hatua zinazostahili kurekebisha mfumo uliopo.

Ikiwa hatua hazitachukuliwa nitaungana na wananchi kufikisha malalamiko yao kwenye mamlaka zinazohusika na usimamizi wa mazingira katika Manispaa ya Kinondoni na katika Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Waziri wa Nishati na Madini na Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO watoe majibu ya wazi kwa wananchi ni lini fidia ya wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayozunguka mitambo ya kuzalishia umeme ya Ubungo itaanza kulipwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 kutokana na kiasi cha shilingi bilioni 10 ambacho tayari kimeshaingizwa kwenye bajeti.

Izingatiwe  kwamba tarehe 04 Aprili 2012 nilifanya mkutano na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga zaidi ya 500 katika kata ya Ubungo ambapo pamoja na mambo mengine nilitoa siku tatu kwa Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO kueleza hatua walizochukua katika kutekeleza ahadi waliyoniahidi  kwa nyakati mbalimbali kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 wakati wa vikao vya kamati ya nishati na madini nilipohoji kuhusu hatma ya wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi jirani na mitambo ya umeme ikiwemo kuhusu uchafuzi wa mazingira unaoendelea.

Ikumbukwe kwamba mwaka 2004 baada ya mitambo kulipuka serikali iliahidi kuwalipa fidia wananchi husika na kuwahamisha, mwaka 2009 Serikali ikarudia tena ahadi hiyo lakini mpaka tarehe 4 Aprili 2012 ilikuwa haijatekelezwa hata kwa mtu mmoja.

Ndani ya siku hizo tatu, TANESCO ilitoa ahadi ya kuwa suala la fidia kwa wananchi litaingizwa katika bajeti ya serikali mapema iwezekanavyo na tayari kiasi cha shilingi bilioni 10 kimetengwa kwa ajili ya kuanza kulipa fidia ikiwa ni sehemu ya  Mradi wa Kuboresha Mifumo ya Umeme Katika Jiji la Dar es salaam (Kasma 3154).

Ili kuhakikisha kwamba mpango wa kulipa fidia ikiwa ni sehemu pia ya kuboresha mazingira ya eneo husika tarehe 27 Julai 2012 katika hotuba yangu bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Wizara ya Nishati na Madini ieleze iwapo kiasi cha 10,000,000,000 kilichotengwa kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayozunguka mitambo ya kuzalishia umeme ya Ubungo kitatosha kukamilisha kazi hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ili kuepusha uwezekano wa gharama kuongezeka kutokana na riba ya kuchelewa kufanya malipo kama ilivyotokea kwa miaka iliyopita.

John  Mnyika (Mb)
09 Septemba 2012





Monday, September 10, 2012

Unatumia barabara ya Kimara-Mavurunza-Bonyokwa: Chukua Hatua, Shiriki sasa!!


Nawaomba wananchi na wadau wa sekta binafsi mnaotumia Barabara ya Kimara-Mavurunza-Bonyokwa muwasiliane na Diwani wa Kimara Pascal Manota 0784954657 awape utaratibu wa kuchangia kuwezesha kukodi grader kusawazisha na malori kuweka vifusi kwenye maeneo korofi kwa dharura wakati tukisubiri matengenezo ya haraka yanayopaswa kufanywa na Serikali kwa kodi zetu; mimi tayari nimeshampatia mchango wangu wa shilingi laki mbili kati ya milioni moja zinazohitajika, wewe je?

Izingatiwe kwamba tayari Wizara ya Ujenzi ilishakubali kuihudumia barabara hii na wiki chache zilizopita niliandika barua kwa meneja wa TANROADS Mkoa wa Dare es Salaam kutaka hatua zake kwa hali mbovu ya barabara hiyo pamoja na kuwa kero wa wananchi inamwaibisha Rais Kikwete mbele ya wakazi husika kwa kuwa alitembelea mwaka 2010 na kuahidi itajengwa kwa kiwango cha lami.
Aidha, mwaka 2011 ilifanyiwa matengenezo ya kawaida lakini kwa sasa imeharibika tena kufuatia mvua zilizonyesha, hali mbovu ya barabara hiyo inaathiri pia hatua za kupunguza msongamano kwenye barabara ya Morogoro wakati huu ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART) unapoendelea kwa kuwa barabara hiyo hutumika kama njia mbadala kutoka Manispaa ya Kinondoni mpaka Manispaa ya Ilala.

Leo na kesho nitakuwa kwenye mfululizo wa mikutano ya baraza la madiwani wa jiji hivyo wakati nikiendelea kufuatilia majibu ya hatua za haraka za serikali kuwezesha matengenezo makubwa, naomba  utaratibu kwa kushirikiana na diwani na watendaji kwa ajili ya kuunganisha wananchi wa maeneo husika na wadau wengine ili kufanya matengenezo madogo kupunguza kero uendelee. 

John Mnyika (Mb)
10/09/2012


Friday, September 7, 2012

CHADEMA wamtaka Kikwete awasimamishe vigogo Polisi

na Nasra Abdallah

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwasimamisha kazi vigogo wote wa Jeshi la Polisi, ambao wamekuwa wakitoa taarifa tata kuhusu mauaji ya mwandishi Daudi Mwangosi, kujiuzulu nyadhifa zao na kupisha uchunguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Mahusiano na Habari wa chama hicho, John Mnyika, aliwataja vigogo hao wa polisi kuwa ni Kamanda wa Operesheni wa Polisi, Paul Chagonja na RPC wa Iringa, Michael Kamhanda, ambao katika nyakati tofauti walidai kuwa Mwangosi alifikwa na mauti baada ya kuchoropoka kutoka kundi la wafuasi wa CHADEMA na kukimbilia mikononi mwa polisi na ghafla kulitokea mlipuko wa bomu la machozi uliosababisha kifo cha mwandishi huyo jambo ambalo sio la kweli.

Mnyika alisema maneno hayo yanatofautiana na ukweli na kuyaita kuwa ni ya uongo, ikizingatiwa kwamba picha mbalimbali zimeonesha kilichotokea, ikiwemo waandishi waliokuwemo eneo la tukio kutoa ushuhuda wao.

Sunday, September 2, 2012

Shughuli za kimaendeleo na ujenzi wa chama jimboni Ubungo


Kwa mwezi huu wa Septemba, katika siku za katikati ya wiki nitaendelea na kazi za kuwawakilisha wananchi kwa lengo la kuisimamia  serikali jimboni na kitaifa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa siku za mapumziko ya mwisho wa wiki, nitakuwa nafanya matukio na mikutano ya kichama jimboni kwa malengo;
Mosi, kutekeleza programu ya demokrasia na ujenzi wa chama ngazi ya chini katika kata na mitaa mbalimbali.
Pili, kuhamasisha viongozi na wanachama kufuatilia kazi za maendeleo jimboni na kujiandaa kutoa maoni ya mabadiliko ya Katiba Mpya.

Jana Septemba 1, 2012 nilianza kata ya Msigani-Makondeni, Mbezi Hii, Malambamawili, Msingwa, Bwaloni na Masaki ambapo nilizindua misingi, matawi,ofisi na nimepokea wanachama. Aidha nimesomewa risala za masuala ya kufuatilia, nimeulizwa maswali na nimehutubia kama njia moja wapo ya kujibu baadhi ya hoja zenye kuhitaji majibu na ufafanuzi.

Leo Septemba 2, 2012 nitakuwa kata ya Mbezi-Luis; Kilimahewa, Msumi, Msakuzi, Makabe na Mshikamano.

Njoo ushiriki, tulijenge jimbo letu. Kwa pamoja tunaweza.
Maslahi ya Umma Kwanza.

John Mnyika (MB)
Jimboni Ubungo
02 Septemba, 2012