Awali
ya yote niwatikie nyinyi wanahabari kheri ya sikukuu na kupitia kwenu nifikishe
salamu kwa ndugu zetu waislam na watanzania wote katika kuadhimisha Iddi
Ell-Hajj.
Tarehe
15 Oktoba 2012 nilitoa taarifa kwa umma kuwa niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge
kusudio la kuwasilisha Muswada Binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka
2012 kwa hati ya dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za
Bunge (Toleo la Mwaka 2007) iwapo Serikali haitatoa kauli kwa umma ya ratiba ya
kupata mapendekezo toka kwa wadau wa hifadhi ya jamii pamoja na kamati husika
ya kudumu ya Bunge na kuwasilisha muswada husika bungeni kama ilivyoazimiwa
bungeni tarehe 6 Julai 2012.
Kufuatia
hatua yangu na hatua za wadau wengine Serikali kinyume na msimamo wa awali
ambalo ulielezwa na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Makongoro Mahanga tarehe 14 October
2012 ambaye alieleza kuwa marekebisho ya kurejesha fao la kujitoa hayatafanyika
mpaka mkutano wa kumi wa Bunge mwezi Februari mwaka 2013; Serikali imechapa
katika gazeti la Serikali Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na. 40
Juzuu namba 93 ambao katika sehemu ya 6 vifungu vya 13, 14 na 15 imependekeza
kurejesha fao la kujitoa kwa upande wa mfuko mmoja wa mashirika ya umma (PPF)
hata hivyo muswada huo haujawasilishwa kwa hati ya dharura kama ilivyoazimiwa
na kuahidiwa.
Kwa
upande mwingine, sehemu hiyo ya sita ya muswada huo wa marekebisho ya sheria
mbalimbali haijakidhi mahitaji na matakwa ya azimio la bunge la tarehe 6 Agosti
2012 lililoungwa mkono na wabunge katika kikao cha 41 cha Mkutano wa Nane wa
Bunge na itasababisha mgogoro mwingine katika ya serikali na wafanyakazi kwa
upande mmoja, wafanyakazi na waajiri kwa upande mwingine na kuathiri uchumi wa
nchi na maisha ya wafanyakazi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutoresha fao
la kujitoa katika mifuko mingine ikiwemo NSSF, PSPF na LAPF.
Kwa
kuzingatia kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara imeeleza kuwa
Rais ndiye mkuu wa Nchi na Kiongozi wa Serikali na Ibara ya 34 imeeleza kwamba
mamlaka yote yapo mikononi mwake na kwamba madaraka hayo yanaweza kutekelezwa
na watu wengine kwa niaba yake na kwamba Ibara ya 35 imeeleza bayana kwamba
shughuli zote za serikali zitatekelezwa na watumishi wa serikali kwa niaba
yake; wakati umefika sasa wa wafanyakazi na wadau wengine kuchukua hatua za
kuwezesha Rais kuingilia kati kabla ya mkutano
wa Bunge kuanza tarehe 30 Oktoba 2012 kutumia madaraka na mamlaka yake kuondoa
udhaifu uliojitokeza wa Waziri wa Kazi na Ajira Gaudencia Kabaka, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Fredrick Werema na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko
ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) Irene Isaka kutokutekeleza kwa wakati na kwa
ukamilifu mapendekezo na maamuzi ya Bunge pamoja na ahadi za Serikali kwa
wabunge.
Mosi;
Rais azingatie masharti ya Kanuni za Kudumu za Bunge na kutia saini hati
ya dharura ya kuwezesha muswada wa
marekebisho ya sheria mbalimbali wenye vifungu vya nyongeza vinavyowezesha fao
la kujitoa kurejeshwa kwa mifuko yote ikiwemo NSSF, PSPF na LAPF kuwasilishwa
bungeni. Kanuni ya 80 Fasili ya 4 inaelekeza kwamba “Muswada wowote wa sheria
wa Serikali wa dharura hautaingizwa kwenye shughuli za Bunge bila ya kuwa na
hati iliyowekwa saini na Rais inayoelekeza kuwa muswada uliotajwa kwenye hati
hiyo ni wa dharura”.
Iwapo
Rais hataweka saini hati ya dharura au Serikali haitawasilisha bungeni hoja kwa
mujibu wa Kanuni ya 93 fasili ya 4 bunge litabanwa na fasili ya 1 ambayo
inakataza bunge kushughulikia hatua zaidi ya moja katika mkutano mmoja wa
bunge; tafsiri yake ni kwamba sheria hii itasubiri kupitishwa katika mkutano wa
kumi wa Bunge mwezi Februari 2012 na hivyo wafanyakazi kuendelea kunyimwa mafao
ya kujitoa kinyume na azimio la Bunge.
Pili,
Rais atengue tangazo na agizo la Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii
(SSRA) kueleza kuwa “kufuatia kuanza
kutumika kwa Sheria hiyo (ya 13 Aprili 2012) maombi mapya ya kujitoa
yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili
kuwezesha Mamlaka na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau” ambalo
limesababisha mifuko yote kuacha kutoa mafao ya kujitoa hata kwa wafanyakazi .
Hii
ni kwa sababu marekebisho ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa upande wa
kusitisha fao la kujitoa yaliyofanyika tarehe 13 Aprili 2012 yalihusu zaidi
Mfuko wa Mashirika ya Umma (PPF); hivyo hayakupaswa kabisa kutumika kama sababu
ya kusitisha mafao kwa mifuko yote ikiwemo NSSF, PSPF na LAPF na kwa upande
mwingine wafanyakazi wanaodai mafao hayo kabla ya kujiunga na mifuko hiyo
walijiunga wakiwa wameelezwa kama kati ya haki na stahili zao ni pamoja na
kupata fao la kujitoa mazingira yakilazimisha hivyo kabla ya pensheni ya
uzeeni. Hivyo, kusubiriwa kwa marekebisho ya sheria hakupaswi kuwa kisingizio
cha kuendelea kusitisha mafao yao ya kujitoa, ama sivyo Rais aeleze sababu za
ziada za kuzuia mafao ya kujitoa kwa kuzingatia Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa
Serikali juu ya uendelevu wa mifuko katika siku
chache zijazo kufuatia kushindwa kwa makampuni na Serikali yenyewe
iliyokopeshwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kuheshimu matakwa ya malipo ya
mikopo kutoka mifuko husika ambayo fedha zake zinatokana na makato ya pensheni
toka kwa wafanyakazi na waajiri.
Rais
arejee kumbukumbu rasmi ya Bunge (Hansard) ya tarehe 7 Agosti 2012 za kikao cha
42 cha Mkutano wa Nane wa Bunge ambao nilishika mshahara wa Waziri Bunge
lilipokaa kama kamati na “nilitaka
ufafanuzi wa kisera wa Serikali pamoja na uamuzi wa kuahidi kwamba kwenye
mkutano wa Bunge ujao italeta Muswada wa dharura kuhusiana na Fao la Kujitoa,
nilitaka kauli ya Serikali juu ya agizo lilitolewa na SSRA la kusitisha
utoaji wa mafao ya kujitoa katika kipindi hiki cha miezi sita (6) na kuhusiana
na wafanyakazi waliosimamishwa katika hatua ya kudai hayo mafao.
Sasa
iwapo Wizara inatoa kauli ya kutengua sitisho hilo na vilevile inatoa kauli ya
kutaka kurejeshwa kwa wafanyakazi waliosimamishwa katika hatua ya madai ya fao
hili la kujitoa”. Waziri wa Kazi na Ajira alijibu kuwa “tutalifanyia kazi agizo
hilo”, hata hivyo mpaka sasa agizo hilo la SSRA halijatenguliwa na wafanyakazi
waliosimamishwa wengine hawajarudishwa mpaka hivi sasa na baadhi wamefukuzwa
kazi kabisa kutokana na mgogoro uliosababishwa na Serikali kusitisha fao la
kujitoa bila kuzingatia haki za binadamu, mazingira ya ujira nchini na
ushirikishwaji wa wafanyakazi na wadau wengine muhimu wa hifadhi ya jamii.
Wenu
katika utumishi wa umma,
John
John Mnyika (Mb)
26/10/2012
1 comment:
Mkuu, nguvu zako hazikupotea bure,hili limezaa matunda, and as we speek tumeshaanza process na tumeahidiwa malipo by 22nd Nov 2012. Tunashukuru kwa jitihada zako.
Post a Comment