Friday, January 31, 2014

Mwito kwa wananchi kutoa maoni kuhusu sheria ndogo

 
Nimerejea jimboni kikazi, pamoja na ufuatiliaji kuhusu kasoro za ujenzi unaendelea katika Barabara ya Morogoro na matengenezo yanayohitajika katika barabara zinaunganika na barabara hiyo katika maeneo ya pembezoni kupunguza foleni, lipo suala linalohitaji mjadala na maoni ya haraka toka kwa wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Tangu mwaka 2013 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imekuwa katika mchakato wa kutunga sheria ndogo nne: ya matumizi ya barabara, ushuru wa masoko, ada na ushuru na ushuru wa huduma. Mwanzoni mwa mwaka huu 2014 katika kikao cha Baraza la madiwani ilibainika kwamba sheria hizo zilikaribia kupitishwa bila ya ushirikishwaji wa kutosha wa wadau na wananchi.

Halmashauri iliongeza muda wa kupokea maoni; hata hivyo muda ukiwa unaelekea ukiongoni, ikiwa imesalia takribani wiki moja, tathmini ya ofisi ya mbunge Jimbo la Ubungo inaonyesha kwamba sheria hizo hazijasambazwa vya kutosha kwa wananchi na wadau kwa ajili ya kutoa maoni yao katika kata na mitaa mbalimbali.

Hivyo, ofisi ya mbunge Jimbo la Ubungo leo tarehe 31 Januari 2014 itafanya kazi ya kusambaza Sheria hiyo kwa njia mbalimbali kwa ajili ya wadau na wananchi kupitia na kutoa maoni yao. Mkazi wa Jimbo la Ubungo anayehitaji kutoa nakala anaweza kuwasiliana na Katibu Msaidizi Aziz Himbuka kupitia 0784379542 au 0715379542 au kwa kuwasiliana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni moja kwa moja.

Wednesday, January 22, 2014

Ufafanuzi kuhusu upanuzi na mgogoro wa kuhusu upana wa barabara ya Morogoro

Kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2004 na 2013 nimezungumzia haja ya upanuzi wa Barabara ya Morogoro kutoka Jimboni Ubungo kupitia Kibaha mpaka Chalinze na mgogoro uliodumu muda mrefu kuhusu upana wa Barabara hiyo.

Ningependa kutoa ufafanuzi kwamba nyakati zote nimeunga mkono upanuzi wa Barabara hiyo ikiwemo ujenzi wa barabara hiyo kuwa njia sita (tatu kwenda na tatu kurudi).

Hata hivyo, mara nyingi nimekosoa masuala manne kuhusu upanuzi na mgogoro kuhusu upana wa barabara ya Morogoro:

Mosi, Serikali kutoa ahadi bila utekelezaji kwa miaka mingi. Mwaka 2012 na 2013 Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli amekuwa akirudia kauli kwamba ujenzi wa Dar Es Salaam-Chalinze express road kuanza. Katika mkutano wangu na wananchi jimboni tarehe 19 Januari 2014 kuhusu ujenzi wa Barabara hiyo, nimesisitiza kwamba fedha za ujenzi wa barabara hiyo hazijatengwa hivyo ujenzi hauwezi kuanza. Badala yake nilifafanua kwamba Serikali inachokifanya kwa sasa ni kutafuta mkandarasi mwenye uwezo wa kutafuta fedha na kujenga. Hivyo, ni muhimu Serikali ikawaeleza wananchi ukweli na kuharakisha kutekeleza ahadi zilizotolewa kwa miaka mingi.

Wednesday, January 15, 2014

TAARIFA KWA UMMA: Kero ya maji Dar na taarifa za kina


Rais Jakaya Kikwete amwondoe Prof. Jumanne Maghembe nafasi ya Waziri wa Maji kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka za kuongeza upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar Es Salaam na nchini kwa ujumla.

Rais Kikwete azingatie kwamba tarehe 10 Januari 2014 nilimtumia ujumbe Waziri Maghembe kumshauri ajiuzulu kutokana na kujirudia rudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam kinyume na maelezo yake ya uongo aliyoyatoa bungeni tarehe 4 Februari 2013.

Aidha, kufutia maelezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) Hawa Sinare kuhusu sababu za kuchelewa kwa miradi ya maji Jijini na majibu ya Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO) Jackson Midala kuhusu kujirudia kwa matatizo ya maji; Rais Kikwete akumbuke ahadi yake ya kuitisha kikao Ikulu kujadili masuala maji mwezi Machi 2013 ambayo mpaka sasa hajaitekeleza.

Ikumbukwe kwamba mara baada ya kujirudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam niliwasiliana na mamlaka husika ziweze kuchukua hatua na pia nilitaka Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Mamlaka zinazohusika na huduma ya maji jijini (DAWASA na DAWASCO) watoe maelezo kwa umma juu ya sababu za kweli za matatizo za matatizo hayo.

Taarifa kwa Umma-Nishati ya Umeme


Kufuatia ukimya wa Wizara ya Nishati na Madini na Mamlaka nyingine tangu nitoe mwito kwao tarehe 9 Januari 2014 juu ya ongezeko la bei ya umeme; namshauri Rais Jakaya Kikwete katika mchakato wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri kumtaka Waziri Prof. Sospeter Muhongo kujieleza kwake na kwa umma kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa.

Rais Kikwete akumbuke kwamba Waziri Muhongo alisema uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013 alipowahakikishia wananchi kwamba bei ya umeme haitapanda hata baada ya TANESCO kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha bei ya umeme.

Kinyume na kauli za Waziri Prof. Muhongo; Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), katika kikao chake cha tarehe 10 Desemba 2013 pamoja na mambo mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja hatua ambayo itaongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi na itaathiri uchumi wa nchi.

Maamuzi hayo yamefikiwa kufuatia tarehe 11 Oktoba 2013, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa EWURA. TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari 2014 na asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015.

Vilevile TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi ya kitanzania hatua ambazo nazo zina athari katika uchumi na maisha ya wananchi.

Thursday, January 9, 2014

Waziri Prof. Maghembe ajiuzulu: DAWASA/DAWASCO warejeshe huduma ndani ya wiki moja katika maeneo yaliyokuwa yakipata mgao wa maji kabla

Nimemtumia ujumbe Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kumshauri ajiuzulu kutokana na kujirudia rudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam kinyume na maelezo yake ya uongo aliyoyatoa bungeni tarehe 4 Februari 2013.

Aidha, Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Mamlaka zinazohusika na huduma ya maji jijini (DAWASA na DAWASCO) watoe maelezo kwa umma juu ya sababu za kweli za matatizo ya maji kujirudia rudia katika Jiji la Dar Es Salaam.

Pia, wajieleze kwa umma ni kwanini wananchi wasipendekeze Rais awachukulie kwa uzembe, kuisababishia hasara Serikali, kuathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa kukosa maji mara kwa mara ambayo ni huduma ya msingi ya binadamu na malighafi muhimu katika uzalishaji.

Itakumbukwa kwamba tarehe 4 Februari 2013 niliwasilisha hoja binafsi bungeni juu ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji katika jiji la Dar Es Salaam, nikipendekeza Bunge kuingilia kati kuweza kuisimamia Serikali kuchukua hatua za haraka.

Iwapo hoja hiyo ingejadiliwa na maazimio yote kutekelezwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam mpaka hatua ya sasa yangekuwa yamepungua katika maeneo mbalimbali kutokana na hatua ambazo nilipendekeza zichukuliwe.

Kauli ya awali kuhusu ongezeko la bei za umeme

Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), katika kikao chake cha tarehe 10 Desemba 2013 pamoja na mambo mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja hatua ambayo itaongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi na itaathiri uchumi wa nchi.

Maamuzi hayo yamefikiwa kufuatia tarehe 11 Oktoba 2013, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa EWURA. TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari 2014 na asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015.

Vilevile TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi ya kitanzania.

Maamuzi hayo ya Bodi ya EWURA ambacho ni chombo cha Serikali yamethibitisha kwamba Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo alisema uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013 alipowahakikishia wananchi kwamba bei ya umeme haitapanda hata baada ya TANESCO kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha bei ya umeme.

Monday, January 6, 2014

Kauli kuhusu Uongo wa Waziri Profesa Muhongo

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ametoa kauli za uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013 ndani na nje ya Bunge kuhusu utafiti na uendelezaji wa gesi asilia.

Waziri Muhongo alijibu uongo kwamba hafanyi kazi kwa vyombo vya habari nilipohoji kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya kuanzia Novemba 2011 ya kushughulikia ufisadi uliothibitika katika mapato ya mauzo ya gesi na udhaifu mwingine uliobanishwa.

Aidha, Waziri Muhongo aliahidi uongo alipounda alipounda kamati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na kuahidi kwamba kamati hiyo itafanya mapitio ya mikataba na kuandaa ripoti itakayowezesha mikataba mibovu ya utafiti wa mafuta na gesi asili kufanyiwa marekebisho. Hata hivyo, Wizara ya Nishati na Madini baadaye iliyoa taarifa kwamba matokeo ya ripoti hiyo hayatatumika kwa ajili ya mikataba iliyopita bali mikataba ijayo.

Sunday, January 5, 2014

Mapendekezo ya Mgawanyo Mpya wa Manispaa za Jiji la Dar es Salaam

Nimepokea mwaliko wa kikao maalumu cha kikao cha fedha na uongozi wa tarehe 3/01/2014 kikao kufanyika tarehe 06/01/2013 saa nane mchana kujadili mapendekezo ya kuongeza maeneo mapya ya utawala katika Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na ajenda zingine.

Nimeonelea tija kuwasilisha mapendekezo yangu kwa maandishi kwa umma na baadae katika kikao tajwa. Kwa hatua hii, ni fursa kwa kila mwananchi kutoa maoni yake juu ya haya;

Kwa ukuaji wa kasi wa Dar es Salaam ambao ndiyo mji mkubwa nchini Tanzania, jiji kitovu cha biashara na viwanda ambalo kadiri ya takwimu linakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni nne na nusu. Jiji hili limeshika nafasi ya tatu katika miji inayokuwa kwa kasi barani Afrika na miongoni mwa miji kumi inayokuwa kwa kasi duniani.

Ifahamike pia, Jiji la Dar es Salaam ndilo linashikilia asilimia themanini na tatu (83%) ya mapato ya serikali kitaifa na takribani asilimia sabini (70%) ya kodi zote zinazokusanywa nchini Tanzania.

Yafuatayo ndiyo mapendekezo yangu ya wasilisho la nyaraka ya mapendekezo yaliyoletwa katika ofisi yangu toka Manispaa ya Kinondoni;

Mosi, Pendekezo la kutumia “Manispaa” badala ya “Wilaya”:
Kadiri ya wasilisho, imetumika pendekezo la “wilaya”. Ningeshauri na kupendekeza kutokana na uhalisia na ukuaji wa kasi kutumika kwa “Manispaa” badala ya wilaya.

Pili, Pendekezo bora la mgawanyo wa Manispaa:
Katika wasilisho lenye uwepo wa mapendekezo saba. Ninaungana na kuafiki utumiaji wa pendekezo la pili lililowasilishwa la kuwa na Manispaa tano (5) ambazo ni;
i.                    Manispaa ya Ilala
ii.                 Manispaa ya Temeke
iii.               Manispaa ya Kinondoni
iv.                Manispaa ya Kigamboni
v.                  Manispaa ya Ubungo

Sababu muhimu:
1.        Ukubwa kijiografia: Kwa kuongeza wilaya mbili mpya yaani Manispaa ya Kigamboni na Manispaa ya Ubungo hii itasaidia wilaya hizi kuweza kuhimili ukubwa wa eneo wa kijiografia ambalo kwa sasa inaelemea wilaya hizi za sasa yaani Manispaa ya Kinondoni na Manispaa ya Temeke.
2.      Ukuaji wa kasi wa jiji: Katika ukuaji wa kasi unaoendelea jiji la Dar es Salaam maeneo yaliyopo katika wilaya hasa ya Kinondoni na Temeke ndiyo ambayo yanaongoza pia katika ukuaji huo wa kasi wa kimakazi na shughuli za kiuchumi kama viwanda na uwekezaji. Hivyo kwa kuwa na Manispaa mpya mbili(Manispaa ya Ubungo na Manispaa ya Kigamboni) zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kusimamia vyema mipango miji, kuujenga vyema mji na kusimamia kihuduma.
3.       Uwepo wa mipango ya kuimarisha ukuaji wa jiji kupitia miji ya pembezoni “satellite cities”: tayari serikali imeweka dhamira ya kuimarisha ukuaji wa jiji kupitia satellite cities. Hivyo uwepo wa wilaya mbili yaani Kigamboni (Satellite city Kigamboni) na Ubungo (“Luguruni Satellite City” ndani ya Kata ya Kwembe na Kata ya Kibamba) zitamudu kusimamia vyema ujenzi imara wa satellite cities na pia kuwezesha wilaya zitakazoachwa kama wilaya ya Kinondoni kuwa na ahueni ya kuelemewa na kazi hivyo nazo kusimamia vyema mipango ya ujenzi wa satellite cities zilizomo ktk maeneo hayo