Wednesday, January 22, 2014

Ufafanuzi kuhusu upanuzi na mgogoro wa kuhusu upana wa barabara ya Morogoro

Kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2004 na 2013 nimezungumzia haja ya upanuzi wa Barabara ya Morogoro kutoka Jimboni Ubungo kupitia Kibaha mpaka Chalinze na mgogoro uliodumu muda mrefu kuhusu upana wa Barabara hiyo.

Ningependa kutoa ufafanuzi kwamba nyakati zote nimeunga mkono upanuzi wa Barabara hiyo ikiwemo ujenzi wa barabara hiyo kuwa njia sita (tatu kwenda na tatu kurudi).

Hata hivyo, mara nyingi nimekosoa masuala manne kuhusu upanuzi na mgogoro kuhusu upana wa barabara ya Morogoro:

Mosi, Serikali kutoa ahadi bila utekelezaji kwa miaka mingi. Mwaka 2012 na 2013 Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli amekuwa akirudia kauli kwamba ujenzi wa Dar Es Salaam-Chalinze express road kuanza. Katika mkutano wangu na wananchi jimboni tarehe 19 Januari 2014 kuhusu ujenzi wa Barabara hiyo, nimesisitiza kwamba fedha za ujenzi wa barabara hiyo hazijatengwa hivyo ujenzi hauwezi kuanza. Badala yake nilifafanua kwamba Serikali inachokifanya kwa sasa ni kutafuta mkandarasi mwenye uwezo wa kutafuta fedha na kujenga. Hivyo, ni muhimu Serikali ikawaeleza wananchi ukweli na kuharakisha kutekeleza ahadi zilizotolewa kwa miaka mingi.

Pili; badala ya Serikali kuja na wazo la kujenga njia zaidi ya 6, ianze kwanza kutekeleza ahadi ya njia hizo sita; kwa kuanza na ujenzi katika umbali wa mita 60 zilizopo. Hivyo, sioni haja ya Serikali kujenga kwa sasa mpaka eneo la upana wa mita 241 wakati ambapo kuna barabara nyingine muhimu za pembezoni ya Barabara ya Morogoro ambazo zikiharakishwa kujengwa zinaweza kupunguza foleni mf. Barabara ya Goba-Mbezi-Msigani-Malambamawili-Kinyerezi na nyinginezo ambazo ujenzi wake unasuasua.

Tatu; Serikali kupotosha kwa miaka mingi kuhusu upana wa barabara hiyo. Mwaka 2011, 2012 na 2013 Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli amekuwa akidai kwamba upana wa barabara hiyo unahusisha pia maeneo yenye upana wa mita 242 ( mita 121 kutoka katikati ya barabara kwa kila upande) kuanzia Jimboni Ubungo hadi Kibaha; na kwamba wananchi wanaoishi katika maeneo ya ndani ya upana huo ni wavamizi wasiostahili kulipwa fidia. Kwa nyakati mbalimbali nimepinga kauli hiyo ya Waziri na yamekuwepo malumbano kuhusu suala hilo. Mara zote nimesisitiza kwamba upana wa barabara hiyo ni mita 60 (yaani 30 kwa kila upande kutoka katika kati ya barabara). Hivyo, wakazi katika eneo hilo hawajavamia barabara na wamehamia kihalali kwa msukumo wa Serikali kuanzia wakati wa Operesheni vijiji ya mwaka 1970.

Mkutano wangu na wananchi wa tarehe 19 Januari 2014 ulijadili suala hili kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kupitia shauri Na 80 la 2005 na kutoa hukumu tarehe 31 Mei 2013 ambayo pamoja na mambo mengine imetamka kuwa The Highway Ordinance Cap 167 Government Notice No 161 of 5/5/1967 ambayo hutumiwa na Wizara ya Ujenzi na Tanroads kuingia katika ardhi za wananchi “ni batili kwa kutofautiana na vifungu vya 15 na 16 vya Sheria ya Ardhi ya Vijiji na 5 ya 1999”.

Tatu; kwa nyakati zote nimesisitiza kwamba iwapo Serikali inataka kutwaa maeneo ya nyongeza kwa ajili ya ujenzi nje ya nafasi ambayo tayari inawezesha ujenzi wa barabara hiyo basi Serikali ihakikishe inalipa kwanza fidia kwa wananchi kabla ya kubomoa nyumba za wananchi na kuwasababishia umaskini. Suala hili nalo nililisisitiza katika mkutano wangu na wananchi tarehe 19 Januari 2014 katika eneo la Luguruni.

Hivyo, habari iliyoandikwa na Gazeti la Tanzania Daima 21 Januari 2014 (uk 2) kwamba Mnyika “alisema haoni ya kupanua barabara kutoka Kibaha hadi Dar es Salaam wakati maeneo mengine ya nchi hayana barabara zinazopitika kwa kirahisi” si sahihi.

Aidha, kauli ya Wakala wa Barabara (TANROADS) kupitia Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar Es Salaam Julius Ndyamkama kwamba “watu waliojenga kinyume cha sheria ndani ya hifadhi ya barabara pembezoni mwa barabara ya Morogoro kuanzia Ubungo hadi Kibaha wamekuwa wakidaganyana kuwa nyumba zinatakiwa kuwa umbali wa mita 30 kutoka barabarani, lakini ukweli ni kwamba nyumba zinaruhusiwa kujengwa umbali wa mita 121 kutoka katika barabara za TANROADS” nayo sio sahihi.

Katika muktadha huo, namshauri Rais Jakaya Kikwete kukaa na mawaziri wake kuwaelekeza kuipitia, kuiheshimu na kuwezesha utekelezaji wa maamuzi ya mahakama pamoja na kuharakisha ujenzi wa barabara huku ikilinda haki za msingi za wananchi wa majimbo ya Ubungo, Kisarawe, Kibaha Mjini na Chalinze walioshi pembezoni mwa barabara hiyo wenye haki zilizotambuliwa tangu wakati wa Operesheni Vijiji.

Kadhalika, badala ya kuendeleza malumbano Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli na Watendaji wake wa Wakala wa Barabara (TANROADS) waelekeze nguvu za haraka katika kusimamia ujenzi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka (BRT) ambapo Mkandarasi (Starbag) na Wakala (DART) hawatekelezi ipasavyo masharti ya mikataba.

Masharti hayo yanayokiukwa na ni pamoja na kushindwa kuweka njia mbadala za kutosha na alama inavyostahili na hivyo kusababisha msongamano mkubwa katika barabara ya Morogoro wenye athari kwenye uchumi wa nchi na kuleta usumbufu kwa umma.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
21/01/2014

No comments: