Wednesday, January 15, 2014

TAARIFA KWA UMMA: Kero ya maji Dar na taarifa za kina


Rais Jakaya Kikwete amwondoe Prof. Jumanne Maghembe nafasi ya Waziri wa Maji kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka za kuongeza upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar Es Salaam na nchini kwa ujumla.

Rais Kikwete azingatie kwamba tarehe 10 Januari 2014 nilimtumia ujumbe Waziri Maghembe kumshauri ajiuzulu kutokana na kujirudia rudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam kinyume na maelezo yake ya uongo aliyoyatoa bungeni tarehe 4 Februari 2013.

Aidha, kufutia maelezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) Hawa Sinare kuhusu sababu za kuchelewa kwa miradi ya maji Jijini na majibu ya Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO) Jackson Midala kuhusu kujirudia kwa matatizo ya maji; Rais Kikwete akumbuke ahadi yake ya kuitisha kikao Ikulu kujadili masuala maji mwezi Machi 2013 ambayo mpaka sasa hajaitekeleza.

Ikumbukwe kwamba mara baada ya kujirudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam niliwasiliana na mamlaka husika ziweze kuchukua hatua na pia nilitaka Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Mamlaka zinazohusika na huduma ya maji jijini (DAWASA na DAWASCO) watoe maelezo kwa umma juu ya sababu za kweli za matatizo za matatizo hayo.


Kwa nyakati mbalimbali kati ya tarehe 10 na 14 Januari 2013 viongozi na watendaji mbalimbali wa DAWASA na DAWASCO walitoa maelezo yenye kuonyesha kwamba matatizo ya maji Jijini Dar Es Salaam yanayoendelea hivi sasa ni matokeo ya kudaiwa fedha za kulipia umeme na TANESCO, uchakavu wa mitambo, kuchelewa kutekelezwa kwa miradi, wizi na upotevu wa maji.

Rais Kikwete azingatie kwamba maelezo yaliyotolewa yanadhihirisha kwamba Wizara ya Maji, DAWASA na DAWASCO pekee hawawezi kukamilisha hatua za haraka hivyo mamlaka za juu ziingilie kati kuepusha Serikali kuendelea kupata hasara, uchumi wa nchi kuathirika na ugumu wa maisha kwa wananchi kuongezeka kwa kuzingatia kwamba maji huduma ya msingi ya kijamii na malighafi muhimu katika uzalishaji.

Rais Kikwete arejee hoja binafsi niliyowasilisha bungeni tarehe 4 Februari 2013 kuhusu hatua za haraka za kuongeza upatikanaji wa maji safi na kuboresha ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar Es Salaam (Nimeambatanisha nakala ya sehemu ya hoja hiyo inayohusu mapendekezo ya hatua nane za haraka).

Rais Kikwete atambue kwamba ingejadiliwa na maazimio yote kutekelezwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam na nchini kwa ujumla mpaka hatua ya sasa yangekuwa yamepungua katika maeneo mbalimbali kutokana na hatua ambazo nilipendekeza zichukuliwe.

Hata hivyo, badala ya kuunga mkono hoja hiyo ambayo ingeisaidia Wizara yake na kurekebisha udhaifu uliokuwepo na hivyo kumrejeshea imani kwa umma ambavyo ilikuwa imepungua; Waziri Maghembe akaamua kinyume cha kanuni za Bunge kutoa hoja ya kuondoa hoja niliyowasilisha kwa maelezo kuwa Serikali inaendelea vizuri na utekelezaji.

Kwa kuwa toka Februari 2013 mpaka Januari 2014 imebainika kwa nyakati mbalimbali kwamba utekelezaji hauendi kama Serikali ilivyoahidi na kwamba kuna udhaifu wa usimamizi katika ngazi mbalimbali ikiwemo wizarani, ni muhimu Rais amwondoe Prof. Maghembe kuwa Waziri wa wizara hiyo.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)

14/01/2014




Kiambatanisho:

MAPENDEKEZO YA MAAZIMIO YA HOJA  KUHUSU HATUA ZA HARAKA ZA KUBORESHA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA USHUGHULIKIAJI WA MAJI TAKA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM

(Kwa mujibu wa Kanuni 55 (10) ya  Kanuni za Kudumu za Bunge)

Kwa kuingiza maneno:

“KWA KUWA, Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini ikiwemo katika Manispaa za Jiji la Dar es Salaam ilipaswa kutekelezwa kuanzia mwaka 2005/2006 na kukamilika mwaka 2010/2011 kwa kugharimu dola za kimarekani milioni 292 hata hivyo tathmini ya miaka miwili na nusu ya utekelezaji (mid term review) imebanisha kasoro nyingi katika utekelezaji.

KWA KUWA, Kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi.

NA KWA KUWA, Wizara ya Maji iliandaa waraka maalum wa kuiomba Serikali kutenga kiasi cha shilingi bilioni 653.85 Mpango Maalum 2011-2013 wa kuboresha huduma za majisafi na uondaji wa majitaka katika Jiji la Dar es salaam na kupitishwa na Baraza la Mawaziri mwezi Machi 2011 lakini utekelezaji wake unaelekea kucheleweshwa mpaka mwaka 2016.

NA KWA KUWA , katika mwaka wa fedha 2011/2012 na 2012/13 Serikali haikutenga kiwango kamili cha fedha kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulioidhinishwa na Bunge na kwa kuzingatia mgawanyo wa Mpango Maalum wa Maji Safi na Maji Taka katika Jiji la Dar Es Salaam na kauli ya Serikali ya tarehe 7 Novemba 2012.

NA KWA KUWA, kwa mujibu wa ibara ya 62 (2)  na (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 , Bunge ndicho chombo kikuu chenye madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu.

NA KWA KUWA, kwa mujibu wa ibara ya 63(3) katika utekelezaji wa madaraka yake bunge laweza kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutunga sheria pale utekelezaji unapohitaji kuwapo sheria.

NA KWA KUWA, Malengo ya Kitaifa yalikuwa ni kuwapatia wakazi wa Mjini maji kwa asilimia 90 ifikapo mwaka 2010 na kwamba malengo hayo kwa Jiji la Dar es Salaam yamesogezwa mbele na kuwekwa malengo mapya ya upatikanaji wa huduma ya maji safi kufikia asilimia 90 na uondoaji wa maji taka kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.

KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali ichukue hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam:

NA KWAMBA, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi  maalum wa matumuzi ya fedha matumizi ya bilioni 96.4 za mradi wa maji safi na mazingira vijijini katika Jiji la Dar es salaam na Halmashauri zingine na kuwezesha hatua za ziada kuchukuliwa.

NA KWAMBA, Kufuatia kauli iliyotolewa bungeni tarehe 7 Novemba 2012 kuhusu Mpango Maalum wa kutatua tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 Serikali izingatie makisio ya awali ya gharama za mpango huo na kuingiza mahitaji yaliyobaki kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka 2013/2014 na Bajeti ya mwaka 2013/2014.

NA KWAMBA, Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 29 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 uwekewe muda wa ukomo wa kukamilika kwa dharura katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa ikiwemo iliyozinduliwa Oktoba 2012 yenye kuhitaji miundombinu ya ziada kufikia wananchi zaidi.

NA KWAMBA, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa thamani ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.

NA KWAMBA, EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali.

NA KWAMBA, EWURA iharakishe kukamilisha mchakato ulioanza wa kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es salaam.

NA KWAMBA, Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on the management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012 ili maoni na mapendekezo yazingatiwe wakati wa kujadili na kushauri kuhusu mapendekezo ya mpango wa taifa na bajeti ya nchi.

NA KWAMBA, Serikali iwasilishe bungeni haraka iwezekanavyo muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka (Water Supply and Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili kushughulikia upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.”

Naomba kuwasilisha.

…………………

John John Mnyika(Mb)

Jimbo la Uchaguzi-Ubungo
04/02/2013

 

 

No comments: