Thursday, January 9, 2014

Waziri Prof. Maghembe ajiuzulu: DAWASA/DAWASCO warejeshe huduma ndani ya wiki moja katika maeneo yaliyokuwa yakipata mgao wa maji kabla

Nimemtumia ujumbe Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kumshauri ajiuzulu kutokana na kujirudia rudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam kinyume na maelezo yake ya uongo aliyoyatoa bungeni tarehe 4 Februari 2013.

Aidha, Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Mamlaka zinazohusika na huduma ya maji jijini (DAWASA na DAWASCO) watoe maelezo kwa umma juu ya sababu za kweli za matatizo ya maji kujirudia rudia katika Jiji la Dar Es Salaam.

Pia, wajieleze kwa umma ni kwanini wananchi wasipendekeze Rais awachukulie kwa uzembe, kuisababishia hasara Serikali, kuathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa kukosa maji mara kwa mara ambayo ni huduma ya msingi ya binadamu na malighafi muhimu katika uzalishaji.

Itakumbukwa kwamba tarehe 4 Februari 2013 niliwasilisha hoja binafsi bungeni juu ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji katika jiji la Dar Es Salaam, nikipendekeza Bunge kuingilia kati kuweza kuisimamia Serikali kuchukua hatua za haraka.

Iwapo hoja hiyo ingejadiliwa na maazimio yote kutekelezwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam mpaka hatua ya sasa yangekuwa yamepungua katika maeneo mbalimbali kutokana na hatua ambazo nilipendekeza zichukuliwe.

Hata hivyo, badala ya kuunga mkono hoja hiyo ambayo ingeisaidia Wizara yake na kurekebisha udhaifu uliokuwepo na hivyo kumrejeshea imani kwa umma ambavyo ilikuwa imepungua; Waziri Maghembe akaamua kinyume cha kanuni za Bunge kutoa hoja ya kuondoa hoja niliyowasilisha.

Katika hatua hiyo nilijaribu kutumia kanuni za Bunge kuweza kutoa ufafanuzi juu ya uongo wa Waziri Prof. Maghembe na hatua ambazo Bunge lilipaswa kuchukua. Hata hivyo Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai aliamua kukiuka kanuni kumlinda hali ambayo ilichochea vurugu bungeni.

Mara baada ya kurejea bungeni tarehe 10 Februari 2013 nilihutubia wananchi na kuwaeleza kusudio la kuandaa maaandamano kwenda Wizara ya Maji iwapo katika kipindi cha ndani ya wiki mbili Waziri Prof. Maghembe asingejitokeza kutoa maelezo kwa umma kuhusu masuala yote ambayo alipaswa kuyajibu bungeni juu ya hatua za haraka zilizopaswa kuchukuliwa.

Ndani ya wiki hizo mbili Waziri Maghembe alijitokeza mara mbili kuzungumzia masuala ya maji Dar Es Salaam; kupitia mikutano ya CCM ikiwemo katika kata ya Goba jimboni Ubungo na katika mkutano wake na wafanyakazi DAWASA na DAWASCO tarehe 21 Februari 2013 na kueleza hatua za haraka ambazo angesimamia zichukuliwe.

Hata hivyo, baada ya wiki moja bila ya Waziri wa Maji na Wizara kwa ujumla kuonyesha kwa matendo kuisimamia kwa karibu EWURA, DAWASA, DAWASCO na Manispaa ya Kinondoni kuchukua hatua za haraka ambazo nilizieleza kwenye hoja binafsi, niliamua kuchukua hatua zaidi.

Nilitangaza kuongoza maandamano ya wananchi tarehe 16 Machi 2013 kwenda Wizara ya Maji ili kupata majibu na kuisimamia Serikali kuchukua hatua za haraka. Hata hivyo maandamano hayo yalizuiliwa na Jeshi la Polisi kwa sababu zisizo za msingi na kuombwa kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Nilikata rufaa lakini toka wakati huo mpaka anaondelewa katika nafasi yake Waziri Dr Emmanuel Nchimbi alikwepa kuchukua hatua dhidi ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela kwa kuvunja sheria, kusababisha hasara na kuwanyima haki ya msingi wananchi ya kufikisha ujumbe kwa Serikali.

Maandamano hayo yangefanyika na hatua kuchukuliwa matatizo yangepungua tofauti na ilivyo sasa, hivyo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Pereira Silima anapaswa kueleza umma lini rufaa hiyo itashughulikiwa maandamano yaweze kufanyika wananchi wapate majibu ya hatua za haraka nilizopendekeza ndani na nje ya Bunge.

Zaidi ya nusu mwaka umepita toka Waziri Prof. Maghembe atoe ahadi ambazo ameshindwa kusimamia utekelezaji wake na hivyo kupaswa kujiuzulu. Iwapo Waziri Prof. Maghembe hatajiuzulu nitaeleza hatua zaidi ambazo nitachukua.

Wakati hatua hizo zikisubiriwa, natoa mwito kwa DAWASA na DAWASCO kuhakikisha kwamba katika kipindi kisichozidi wiki moja huduma za maji zinarejea katika maeneo ambayo yalikuwa yakipata mgawo wa maji.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
10/01/2013

No comments: