Itakumbukwa kwamba tarehe 19 Februari 2014 Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum Pandu Kificho aliteua Kamati ya Wajumbe ishirini yenye uwakilishi wa makundi yote yanayounda Bunge Maalum kwa ajili ya kumshauri kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum.
Rasimu ya kwanza ya Bunge Maalum iliandaliwa na Kamati ya Maandalizi chini ya Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (nakala yake niliwapa hapa: http://goo.gl/hEI4aw ).
Kazi ya mjumbe ni kuwakilisha na kuwasilisha; katika kutekeleza wajibu huo, jana 26 Februari 2014 tulikuwa na Semina ya Bunge Maalum kuhusu Rasimu ya Pili ya Kanuni za Bunge Maalum toleo la 2014.
Katika mjadala wa jana niliunga mkono mapendekezo ya rasimu katika sehemu ya nne kuhusu kupunguzwa kwa mamlaka na madaraka makubwa ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum, tofauti na rasimu ya kwanza; sasa maamuzi ya mwenyekiti hayatakuwa ya mwisho. Mjumbe asiporidhika anaweza kukata rufaa na pia rasimu sasa inapendekeza kwamba mwenyekiti au makamu wanaweza kuondolewa kwa kura ya kutokuwa na imani.
Niliunga mkono kuruhusiwa kwa utaratibu wa kuwasilisha Taarifa ya Maoni Kinzani (dissenting opionion); hii ni kwa sababu rasimu ya kwanza haikuwa na utaratibu wa uwasilishaji bungeni wa hoja za wabunge, hoja zote ilikuwa ni kamati. Njia pekee ya kuwezesha mawazo mbadala kuweza kufika katika ukumbi wa Bunge kwa ukamilifu ukiondoa michango ya wabunge ni kupitia Taarifa za Maoni Kinzani.