Sunday, July 20, 2014

Mnyika amnusuru Waziri Makala

16 Julai, 2014 Na Abdallah Khamis

Naibu Waziri wa Maji, Amos MakalaMBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemnusuru Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala asiendelee kuzomewa na wananchi wakati wa  ziara yake ya ukaguzi wa miundombinu ya maji jimboni humo.
Mapema wanachama wa CCM wakiwa na bendera zao, walionekana kupangwa ili kumzomea Mnyika ambaye hata hivyo hakuwajali, badala yake aliendelea kuhutubia mkutano huku Makala akionekana kufurahishwa na hali hiyo.
Mnyika alieleza jinsi alivyowapigania wakazi wa Kimara Mavurunza na maeneo mbalimbali ya jiji kupata maji pasipo kujali itikadi zao za vyama.
Alisema ziara hiyo ya naibu waziri ni matokeo yake ya kumbana Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe, pamoja na watendaji wa Kampuni ya kusambaza maji ya Dawasa kuhakikisha maji yanapatikana kwa wakazi wa Dar es Salaam.

Alisema kama si kushindwa kwa Serikali ya CCM kuzuia wizi wa maji unaofanywa na watu wanaoyauza, hususan viongozi wa serikali, tatizo hilo lisingekuwa kwa kiasi kinachotisha kama ilivyo sasa.
Alimtaka Naibu Waziri Makala ahakikishe wakazi wa Ubungo na maeneo mengine ya jiji wanapata maji kwa kuwa ni haki yao ya msingi, na kwamba wawabane watu wanaouza maji.
Baada ya Mnyika kumaliza, Makala alisimama na kabla hajaanza kuzungumza wananchi walimueleza kuwa hawataki porojo zaidi ya maji.
“Kiongozi hapa tunataka maji, hizo porojo zako za kisiasa peleka huko huko kwa kuwa tumechoka na ahadi zisizotekelezeka kwa muda wa miaka hamsini,” alisema mwananchi ambaye hakufahamika jina.
Makala badala ya kutulia, alimueleza mwananchi huyo kuwa kama hataki porojo aondoke katika mkutano hali iliyozua zomea zomea kutoka kwa wananchi.
Akiwa amekasirika, Makala aliwatishia wananchi kuwa atawakamata kwa kuwaita polisi, lakini kitisho hicho hakikufua dafu.
Katika jitihada zake za kuendelea kuwatisha wananchi, Makala aliinuka mithili ya kutaka kuwafuata, lakini Mnyika alimzuia na kumueleza hali hiyo isingekuwepo kama CCM wasingeingiza siasa katika masuala ya kiserikali.
Mnyika aliwasihi wananchi wampe nafasi kiongozi huyo aweze kuwaeleza mipango ya serikali.
Baada ya ombi hilo, wananchi walitulia na Makala akaeleza kuwa serikali imeshatenga sh. bilioni 362 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Ruvu Juu na Chini na kwamba miradi hiyo itakamilika ifikapo Septemba mwakani.
Chanzo: Gazeti la TanzaniaDaima (http://www.freemedia.co.tz/daima/mnyika-amnusuru-waziri-makala/)

No comments: