Monday, July 28, 2014

Mnyika ataka matengenezo ya barabara ya Sinza-Tandale-Magomeni yaharakishwe

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika amemtumia mjumbe Meya wa Manispaa ya Kinondoni kutaka afuatilie kwa karibu matengenezo ya Barabara ya Sinza-Tandale-Magomeni (Barabara ya Mlandizi) kuharakishwa.

Mbunge amechukua hatua hiyo baada ya kupita katika barabara hiyo kuanzia maeneo ya Sinza Kijiweni-Mtogole hadi Makanya na kubaini kwamba bado ukarabati haujaanza na hali ya barabara ni mbaya.

Mnyika amewasiliana pia na Mkurugenzi wa Halmashauri kutaka Ofisi yake itoe taarifa kupitia vyombo vya habari tarehe ngapi matengenezo hayo yataanza na lini yanatarajiwa kumalizika.

Mnyika amekumbusha kwamba pamoja na kero ambazo wananchi wanapata hivi sasa Serikali inapaswa kutambua kwamba barabara hiyo ni muhimu katika kupunguza msongamano kwenye Barabara ya Morogoro na inapaswa kupewa kipaumbele wakati huu ambapo ujenzi wa mradi wa mabasi ya haraka (DART) unaendelea na hivyo kuhitajika kwa barabara mbadala.

Itakumbukwa kwamba mara baada ya barababara hiyo kuharibika kufuatia mvua za masika Mbunge alipendekeza kwamba barabara hiyo iingizwe katika orodha ya miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko.

Katika Mkutano wa Baraza la Ushauri la Mkoa (RCC) Mbunge alitaka majibu kutoka kwa Mkuu wa Mkoa juu ya maombi ya fedha kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). 

Mkuu wa Mkoa alieleza kwamba maombi yaliyowasilishwa na Manispaa ya Kinondoni yalifikia bilioni 12 ilielekezwa yapunguzwe ambapo ilitaarifiwa kwamba yalipungua mpaka bilioni 8.

Hata hivyo, majibu yaliyotolewa baada ya maombi kuwasilishwa ni Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa tayari kutoa bilioni 4 ambapo mpaka sasa kwa taarifa tulizonazo ni kuwa kiasi cha shilingi bilioni 1 kimeshawasilishwa kwenye akaunti ya Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya matengenezo ya dharura ya miundombinu mbalimbali.

Kwa kuwa fedha zimeshapatikana Manispaa ya Kinondoni inapaswa kuchukua hatua za haraka kutokana na umuhimu wa barabara hiyo katika kupunguza msongamano wa magari na pia katika kuhudumia wananchi wa majimbo ya Ubungo na Kinondoni katika kata mbalimbali ambapo barabara hiyo inapita.



Imetolewa tarehe 22 Julai 2014 na:

Azizi Himbuka

Katibu Ofisi ya Mbunge

Jimbo la Ubungo


No comments: