Wednesday, September 3, 2008

SERIKALI IACHE KUMLINDA LOWASSA

Siku chache zilizopita. Nilitoa taarifa hii kwa vyombo vya habari. Hata hivyo, kwa sababu ambazo sizifahamu, habari hii haikutoka katika magazeti mengi ya kila siku. Pengine inaweza ikawa ni njia iliyotumika kufikisha ujumbe(barua pepe) lakini kuna uwezekano mkubwa sababu ikawa ni kuwa Lowassa hakutajwa kuchukuliwa hatua kama hizi ambazo nimezieleza hapa katika yale Maazimio 23 ya Bunge. Yeye aliambiwa tu atakafakari na kuchukua maamuzi ambayo ataona yanafaa. Yeye akaamua kujiuzulu. Lakini bado siridhiki sana na sababu hii kwa kuwa maazimio hayo 23 hayajasema Karamagi na Msabaha wachunguzwe kuhusu Rushwa kama serikali ilivyoamua. Kama imeamualiwa na Serikali hawa wachunguzwe, kwanini serikali haikumjumuisha na Lowassa? Hii inafanya niamini kwamba bado msimamo huu hapa chini ni mwafaka:

TAARIFA KWA UMMA

SERIKALI IACHE KUMLINDA LOWASSA

  • Ni mmoja wa mizizi ya ufisadi wa Richmond
  • Akamatwe, ahojiwiwe na achukuliwe hatua za kisheria.

Tarehe 25 Februari, 2008 Vijana wa CHADEMA tulitoa taarifa kwa umma tukikemea jitihada zilizokuwa zikiendelea za Lowassa kujisafisha na kusafishwa na tukahimiza achukuliwe hatua za haraka kutokana na tuhuma za ufisadi na/ama matumizi ya madaraka katika kashfa ya RICHMOND. Pamoja na taarifa yetu hiyo kwa umma katika kipindi chote ambacho Serikali ilipewa na Bunge kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu suala hilo hatua tulizopendekeza hazikuchuliwa. Aidha tumefadhaishwa zaidi na Taarifa ambayo Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo ameiwasilisha Bungeni Alhamisi 28 Agosti, 2008 pamoja na kutaja hatua ambazo zimechukuliwa kuhusu watuhumiwa wengine ikiwemo kuandikiwa Barua za kujieleza na/ama kuanza kuchunguzwa na vyombo vya dola/usalama; Waziri Mkuu hakueleza hatua ambazo zimeaanza kuchukuliwa dhidi ya Bwana Lowassa.

Tunatambua kuwa Waziri Mkuu katika taarifa yake ameeleza kuhusu hatua ambazo serikali imeanza kuchukua ikiwemo za marekebisho ya Sheria ama mifumo ya uwajibikaji, ikiwemo ile ya manunuzi. Hata hivyo, tungependa kuweka bayana kwamba matatizo ya msingi ya taifa letu hayasababishwi na mapungufu katika sheria pekee, ila kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na kulegea kwa misingi ya utawala wa sheria na uwajibikaji miongoni mwa viongozi. Hivyo, tunapenda kuwajulisha Watanzania kuwa kama watuhumiwa wa ufisadi hawatachukuliwa hatua mapema, misingi ya utawala wa sheria itazidi kutetereka na matokeo yake ni kuwa mageuzi yoyote katika mifumo ya kiutawala hayatatekelezwa kikamilifu. Kwa ujumla tunaamini kwamba utamaduni huu wa kulindana katika serikali unatoa mfano mbaya kwa vijana wa kitanzania kuhusu uongozi na utawala bora.

Tungependa kusisitiza kuwa Bwana Lowassa, akiwa Waziri Mkuu wa nchi yetu wakati huo alikuwa mmoja wa mizizi mikuu ya ufisadi wa RICHMOND. Hivyo, tunaona kuwa Taarifa ya Utekelezaji ya Waziri Mkuu Pinda imejikita katika kushughulikia matokeo badala ya mzizi wa tatizo lenyewe na hivyo kama hali hii ikiendelea itaporomosha nidhamu na uwajibikaji katika taifa letu. Tunaamini kwamba kama Bwana Lowassa aliyekuwa kinara wa Serikali wakati huo, ataweza kuchukuliwa hatua kikamilifu basi itakuwa rahisi kwa waliokuwa chini yake kuweza kuchukuliwa hatua za haraka na hatimaye kurejesha maadili katika utawala. Lakini kama Serikali itaendelea kumlinda Bwana Lowassa na kuwatoa kafara maafisa wa chini, bado haitakuwa imetekeleza kikamilifu dhana ya uwajibikaji na utawala wa Sheria. Kujiuzulu kwa Waziri Mkuu na mawaziri wenzake kadhaa ni hatua ndogo sana katika kashfa iliyohusisha uvunjaji wa Sheria za nchi yetu, mazingira ya ufisadi na hasara kubwa kwa taifa.

Sisi tunaona kutotajwa kikamilifu kwa hatua zilizochuliwa juu ya Bwana Lowassa ni mwendelezo wajitihada za miezi ya karibuni za Bwana Lowassa(Mb) kupita akijitetea kuanzia katika hotuba yake alipokwenda Jimboni Monduli na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari na hata mahojiano yake maalumu na Televeshioni ya Taifa(TVT).

Aidha, taarifa ya Waziri Mkuu Pinda imeakisi uamuzi wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu Bwana Edward Lowassa kujitokeza miezi ya karibuni kujitetea kuhusu kuhusika kwake katika kashfa ya Richmond ambayo kwa ujumla ni ishara ya unafiki wa kisiasa. Itakumbukwa kuwa baada ya Kamati Teule kuwasilisha taarifa yake, Bwana Lowassa alipata nafasi bungeni takribani mara mbili kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni wakati akiwa Waziri kuzungumzia suala hili lakini hakutoa utetezi ambao Mwezi Februari alijaribu kuutoa kwa umma. Waziri Mkuu Pinda inabidi auleze Umma kama uamuzi wa kumtomtaja katika Taarifa yake ya utekelezaji kuhusu hatua ambazo amechuliwa ni ishara kuwa serikali imekubaliana na utetezi wa Bwana Lowassa.

Itakumbukwa kuwa Vijana wa CHADEMA tulieleza wazi kwamba katika kujitetea kwake mwezi Mei, Bwana Lowassa alithibitisha wazi uzembe na matumizi mabaya ya madaraka ambayo aliyafanya alipokuwa Waziri Mkuu wakati wa sakata zima la Richmond. Hivyo, tunarudia kutoa mwito kwa vyombo vya dola kuweza kumkamata, kumhoji na kumchukulia hatua za kisheria dhidi ya uzembe na matumizi hayo mabaya ya madaraka kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Badala ya Bwana Lowassa kuendelea kupita akijitetea kuwa Kamati Teule haikumuita kuweza kujieleza; vyombo vya dola vimkamate akatoe maelezo yake panapohusika. Vyombo vya dola vimekuwa vikiwakamata raia wa kawaida wenye taarifa za uhalifu kuweza kuisadia polisi, inashangaza Bwana Lowassa amejieleza wazi kuwa alikuwa anafahamu uhalifu uliokuwa ukitendeka lakini bado yuko nje akijitetea na pia Taarifa za kiserikali zikielekea kumlinda. Tunaamini akikamatwa yeye, atawezesha watuhumiwa wakuu wa kashfa ya Richmond kuweza kupatikana. Tulieza wazi katika tamko letu na Mwezi Februari kuwa , jitahada zozote za kumlinda na kumtetea zingeweza kuathiri mwekekeo wa hatua ambazo zitanatarajia kupendekezwa na Kamati ya Waziri Mkuu mpya Mheshimiwa Mizengo Pinda. Kutokana na Taarifa ya Waziri Mkuu Pinda aliyowasilisha Bungeni Alhamisi tarehe 28 Agosti, 2008 ni wazi kuwa kuna kila dalili kuwa mwelekeo huo umeanza kuathiriwa, hivyo tunarudia tena kutaka Bwana Lowassa achukuliwe hatua kabla ya Bunge la Mwezi Novemba, 2008.

Bwana Lowassa akiwa Waziri Mkuu amethibitisha kwamba maneno yake mwenyewe kuwa alikiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 na Sheria ya Makosa ya Udhibiti wa Uhujumu wa Uchumi wa nchi ya Mwaka 1984.

Bwana Lowassa alikiri kwamba alikuwa anafahamu kwamba Richmond ni kampuni ya kitapeli, lakini katika kipindi chote cha uongozi wake aliinyamazia hali hii na kwa kiasi kikubwa aliitetea kampuni hiyo mbele ya macho ya umma. Wakati wa Viongozi mbalimbali wa upinzani walipoweka bayana kwamba Richmond ni kampuni isiyo na uwezo, serikali ilitetea kampuni hiyo. Vyombo mbalimbali vya habari vilimtuhumu Bwana Lowassa mwaka 2006 na 2007 kama kiongozi wa Shughuli za serikali bungeni, kwamba alishiriki ‘kuwaziba midomo’ wabunge wa CCM wasijadili suala hili. Pia, ni Bwana Lowassa huyo huyo, alinukuliwa akiwa Arusha akiwataka watanzania wasiijadili kampuni ya Richmond baada ya mvua kuanza kunyesha. Kama Bwana Lowassa wakati wote huo alijua kama ni kampuni ya kitapeli kama anavyojaribu alivyojaribu kujitetea, uamuzi wake wa kuwaasa watanzania wasiijadili ulikuwa ni wa kulinda ufisadi ambao aliufahamu. Inashangaza pia ni Lowassa huyo huyo alisema alijua kuwa Richmond ni kampuni ya kitapeli; ni Lowassa huyo huyo alisema kwamba alishauriwa vibaya na watumishi wa umma aliowataja kuhusu uwezo wa Richmond; Ni Lowassa huyo huyo aliyesema kwamba alijua kuwa TANESCO chini ya Menejimenti ya Net Group Solution walitaka kuhujumu mchakato wa tenda na hivyo ‘kuwanyang’anya’. Lakini ni Lowassa huyo huyo aliyekuwa Waziri Mkuu ambaye angeweza kuviagiza vyombo vya dola kumwezesha kuthibitisha ‘utapeli wa Richmond’; hivyo, maelezo ya sasa yanayotolewa kuhusu ushiriki wake yanaonyesha kuwa sasa kuna mwelekeo wa kumlinda.

Tunaendelea kushangazwa na Serikali na Bwana Lowassa kutumia utetezi wake kueleza tu nia yake ya kutaka mkataba wa Richmond usitishwe; nia ambayo kama ni kweli alikuwa na uwezo wa kuitekeleza na hakuitekeleza. Tunaitaka Serikali na Bwana Lowassa kuweka bayana ni kwa vipi Richmond ilipewa tenda hiyo na kwa shinikizo la nani. Bwana Lowassa anakwepa kuyazungumzia haya kwa kuwa anajua kabisa kwamba ni yeye aliyetumia madaraka yake vibaya alipokuwa Waziri Mkuu kwa kukiuka Sheria na Taratibu za Ununuzi kwa ‘kupora’ mchakato uliokuwa ukiendeshwa na TANESCO, ‘kuunda kamati yake’ na kuzisukuma mamlaka za ununuzi hali iliyopelekea Richmond kupewa tenda ili hali haikuwa na uwezo uliotakiwa. Ni uzembe huu ambao umelisababishia hasara taifa kwa kulipa shilingi milioni 152 kila siku kwa kampuni ya Dowans iliyohamishiwa mkataba wa kitapeli wa Richmond; na takribani bilioni 172 kwa ujumla ambazo taifa linawajibika kuzilipa kutokana na kukodisha mitambo hiyo. Hvyo tunarudia tena rai yetu ya kutaka fedha zilizozilipwa kizembe mpaka sasa kurejesghwa serikalini. Kwa vyovyote vile, jitihada za Bwana Lowassa za kuhamasisha ujenzi wa Sekondari Kata, na utumishi wake kama Waziri Mkuu katika kipindi cha miaka miwili, haviwezi kuzidi hasara aliyosababisha katika uchumi wetu kipindi chote tulichokosa umeme wa dharura na wala hailingani na hasara ambayo tunaendelea kuilipa kila siku iendayo kwa Mungu. Maamuzi haya ya Bwana Lowassa yanaendelea kuwaumiza wananchi wote ikiwemo wa Jimbo lake la Monduli ambao wanataabika kwa mzigo wa gharama za umeme.

Tunarudia tena kumkumbusha Rais Kikwete kwamba Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inamtaka Rais kuhakikisha kwamba taratibu zinatengenezwa zitakazojenga maadili na kuongeza imani ya wananchi kwa uadilifu wa viongozi wa umma na katika taratibu za utoaji maamuzi ndani ya Serikali na katika sekta ya umma. Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma vile vile imeweka kanuni zinazotakiwa kuongoza utendaji wa viongozi wa umma: kwamba wanapokuwa madarakani, viongozi wa umma watakuwa waadilifu, wenye huruma, utulivu, umakini na watakaoendeleza viwango vya juu vya maadili ili kujenga na kuendeleza imani ya umma kwa uadilifu wa Serikali. Kuhusiana na utoaji wa maamuzi, viongozi wa umma watatekeleza wajibu wao kufuatana na sheria na kwa maslahi ya umma. Hivyo, taarifa ya Waziri Mkuu Pinda kutokueleza bayana hatua ambazo Bwana Lowassa ameshachukuliwa au atachukuliwa ni ishara kuwa kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa wakati akizungumza na Wazee wa CCM mkoani Dar es Salaam kwamba Bwana Lowassa amepata tu ‘ajali ya kisiasa’, na kumsifu kwa utumishi wake imechangia kumlinda mhusika huyu mkubwa katika sakata zima la RICHMOND. Vijana wa CHADEMA tulitarajia kuwa, baada ya Bwana Lowassa kukiri mwenyewe hadharani kuhusu uzembe wake na matumizi mabaya ya madaraka Rais Kikwete angelekeza hatua za kuchukuliwa dhidi yake badala ya kuendelea kumpamba kama “shujaa wa uwajibikaji’, kinyume na hayo tutaamini kwamba serikali yake inaendeshwa kwa ‘ubia wa kulindana’. Aidha tunarudia kutoa rai kwamba Rais Kikwete kuwafukuza kazi watumishi wote wa umma waandamizi ambao wametajwa na Bwana Lowassa kushiriki uzembe na matumizi mabaya ya madaraka; watumishi ambao walitajwa pia na Kamati Teule ya Bunge lakini mpaka sasa wanaendelea kutumikia nafasi zao mbalimbali. Kwa kuwa Waziri Mkuu Pinda ameshatangaza kwamba kwa wale wateule wa Rais, Kamati yake imeshapeleka suala zima kwake, tunategemea Rais atachukua hatua za haraka ili kuonyesha mfano kwa viongozi wengine wa chini yake wanaotarajiwa kuchukua hatua kwa watumishi wa chini.

Kadhalika tunapenda kuvikumbusha tena vyombo vya dola kwamba Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Kuhujumu Uchumi ya mwaka 1984 inatamka makosa yafuatayo kuwa baadhi ya makosa ya kuhujumu uchumi ni pamoja na yale yote yenye kusababisha hasara kwa mamlaka ya Serikali. Pia Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007 inatamka kuwa ubadhirifu na/au ufujaji wa mali ya umma unaofanywa na watumishi wa umma na Matumizi mabaya ya madaraka kwa ajili ya manufaa binafsi, ni sehemu ya ufisadi. Bwana Lowassa alithibitisha kwamba maneno yake kwamba wapo viongozi waandamizi wa Serikali ambao amewataja kwa majina wamefanya maamuzi ya kifisadi, kitendo chake cha kunyamazia ufisadi huo- kinafanya iwe vigumu kwa yeye kutenganishwa na tuhuma za ufisadi zilizomo katika mchakato mzima wa kupewa tenda kwa kampuni ya Richmond na mambo yote yaliyotokea baada ya Mkataba huo kuhamishiwa kwa kampuni ya Dowans.

Aidha tumefadhaishwa na Taarifa ya Waziri Mkuu Pindi kwamba kujiuzulu kwa Waziri Mkuu na Baadhi ya Mawaziri ilikuwa ni ishara ya hatua ambazo serikali imechukua kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu suala husika. Tunarudia kukumbusha kwamba toka sakata la Richmond lilipoanza zaidi ya mwaka mmoja uliopita tulimtaka Bwana Lowassa kujiuzulu kulinda heshima yake lakini alikaidi na kuitetea kampuni ya Richmond. Uamuzi wa yeye kujiuzulu baada ya kashfa yote kuwa hadharani, umesaidia tu kuilinda serikali ya CCM lakini katu hauwezi kumpatia heshima ya uwajibikaji na wala hakuwezi kuwa ishara ya kwamba Maazimio ya Bunge yameshatekelezwa.

Kwa niaba ya Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), kwa taarifa hii tunarudia kukemea jitihada zozote za kumlinda na kumtangaza Lowassa kuwa shujaa katika taifa letu kwani hali hii ikiachwa kuendelea inatoa mfano mbaya kwa vijana wa Tanzania. Tusingependa kwa namna yoyote katika taifa letu, mtuhumiwa wa ufisadi aliyetajwa pia katika orodha ya mafisadi(list of shame) kulindwa na kuenziwa kama shujaa wa Taifa letu kwani ni kuharibu maana nzima ya ushujaa katika uwajibikaji.

“Inasikitisha kwamba vijana wezi wadogo wadogo wakijazana magerezani. Vijana wamachinga kuendelea kukosa mitaji na maeneo ya kufanyia biashara; wanafunzi wa elimu ya juu wakipandishiwa ada na wengine kukosa mikopo- huku fedha za walipa kodi zikiendelea kuteketea kwa ufisadi na watuhumiwa wa ufisadi wakiendelea kutamba hadharani. Hali hii ikiachwa, itaharibu utawala wa sheria na kuleta matabaka katika taifa letu. Vijana tusingependa kuona nchi yetu inatumbukia kwenye migawanyiko kwa sababu ya kuwalinda watu wachache kwa kisingizio cha haki za binadamu”

Imetolewa tarehe 31 Agosti 2008 safirini Kenya na:

John Mnyika

Mkurugenzi wa Vijana

0754694553



1 comment:

Ngorongoro Lengai Geopark said...

Kipindi hicho Lowasa shetani kwako. Leo ndio malaika wako huyo mkuu.