Thursday, February 3, 2011

RIPOTI YA KONGAMANO LA MAJI JIMBO LA UBUNGO TAREHE 31.01.2010

Utangulizi:
Kongamano la maji jimbo liliandaliwa na Ofisi ya Mbunge jimbo la ubungo ambalo lilifanyika katika ukumbi wa Chuo cha Maji Ubungo (Rwegalulila). Kongamano lilikua na mada kuu mbili; Mosi ni sera, sheria na mikakati ya sekta ya maji safi na maji taka- fursa na changamoto kwa wananchi wa jimbo la ubungo. Pili, hali halisi ya upatikanaji wa maji jimbo la ubungo na wajibu wa wadau mbalimbali katika kukabiliana na tatizo la maji.

Zaidi ya wadau 200 walishiriki kongamano na kupata fursa ya kujadili hatua zinazoweza kuchukuliwa katika kukabiliana na kero zinazohusu sekta ya maji katika muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.

Pamoja na kuwa wadau muhimu kama Dawasco na Wizara ya Maji walitumiwa mwaliko kushiriki na kutoa mada katika kongamano hilo cha kushangaza hawakuweza kushiriki kabisa na sababu zilizotolewa hazikua na msingi wowote lakini kongamano liliendelea na kufikia kutoa maazimio.

Wadau waliohudhuria:
Pamoja na wadau wakuu kwa maana ya Wizara ya Maji na Dawasco kushindwa kufika na kutoa mada lakini wadau zaidi ya 200 waliweza kuhudhuria na kushiriki katika kongamano, hawa ni pamoja na wawakilishi kutoka wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wirara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia na Watoto, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Kinondoni, Ewura, Ofisi ya Ubunge Jimbo la Ubungo, Maafisa Watendaji, Madiwani, Wenyeviti wa Mitaa mbalimbali, Asasi za kiraia kama HakiElimu, Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Asasi ya Maendeleo Ubungo (UDI), Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT) na wadau wa maendeleo kama Care International, Wawakilishi wa Uongozi wa Chuo cha Maji pamoja na wanafunzi, Vyombo vya Habari pamoja na wananchi mbalimbali.

Mjadala:
Mwenyekiti wa kongamano alianza kwa kuchokoza mjadala kwa kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali kama ifuatavyo;
i. Kinachotakiwa kufanyika kutatua kero ya maji katika jimbo la Ubungo: mwenyekiti aligusia mipango ya muda mrefu ya utatuzi wa kero ya maji kama ilivyoainishwa katika ripoti ya Mkukuta ya July 2010 kuwa kero ya maji inatakiwa kuwa imekwisha ifikapo mwaka 2013. Pia kuchimba visima vikubwa Kimbiji na bwawa la Kidunda kama ahadi iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 24.05.2010 alipotembelea Kimara na pia tarehe 17.10.2010 na 28.10.2010 alirudia ahadi hiyo hiyo. Hili kwa Mwenyekiti/ Mbunge ni suluhisho la muda mrefu

ii. Tafiti zilizofanywa na watu mbalimbali; mwenyekiti aligusia kuwa wapo wananchi ambao ni wakazi wa jimbo la ubungo ambao kwa umoja wao na kuguswa na tatizo sugu la maji waliamua kufanya tafiti zao za kitaalamu ambazo zililenga kutatua kero ya maji na kugundua kuwa kwa siku wananchi katika jiji la Dar es Saalam wanahitaji kutumia lita 450,000 milioni kwa siku lakini kwa sasa ni lita 300,000 milioni ndizo zinazozalishwa. Kwa maana hiyo lita 150,000 milioni ni pungufu ya mahitaji yanayohitajika kwa ajili ya kukidhi haja ya huduma hii. Hata hivyo tafiti hizo hizo zinaonyesha kuwa 50% ya maji yanayozalishwa kwa sasa yanapotea bila kuwafikia wananchi. Hata hivyo mwenyekiti alishauri kuwa ili kuanza kutatua kero hii ya maji kwa muda mfupi ni vizuri sasa mikakati ikawekwa ili kuzuia upotevu huo wa maji ambao ni wa kiasi kikubwa sana. Upotevu huu wa maji husababishwa na viunganishi visivyo halali katika mtambo wa Ruvu juu ambao hufikia 15% kwa mtambo husika pekee.

iii. Ziara ya Mbunge makao makuu Dawasco; katika ziara ya Mbunge makao makuu ya Dawasco mnamo tarehe 19 Januari 2011 na kuelezwa pamoja na mambo mengine kuwa kero ya maji katika jimbo la ubungo husababishwa na mazingira ya kijiografia ambapo kuna miinuko inayosababisha maji kutokufika maeneo hayo kutokana na presha ya maji kuwa ndogo. Mwenyekiti/ Mbunge alishauri kuwa Liongezwe “tank” lingine au lile la Uluguruni ambalo halifanyi kazi lianze kutumika. Kama tatizo ni “pump” ya kusukuma maji ili kuwe na presha ya kusukuma maji ni vizuri “pump” inunuliwe ili kutatua kero ya maji kwa muda wa kati.

iv. Vioski vya maji; ilishauriwa na mwenyekiti kuwa vibanda hivi vya kuuzia maji ambavyo vipo na vimefungwa vifunguliwe na pia viongezwe vingine katika maeneo mbalimbali ya jimbo. Pia bei ya maji katika vioski hivi idhibitiwe ili kuepuka upangaji wa bei holela ambao huwaathiri wananchi ambao ndio watumiaji wakubwa wa huduma hii. Hili lilishauriwa kuwa suluhisho la muda mfupi.

v. Ujenzi wa visima, changamoto kubwa iliyopo katika ujenzi wa visima ni kuwa maeneo mengi ni ya miinuko kwa hiyo inabidi kuchimba visima kwa kina kirefu ambapo husababisha kutumia kiasi kikubwa cha fedha. Pia maji yanayopatikana katika maeneo mengi ni ya chumvi hivyo kuwa ni changamoto nyingine.

vi. Suluhisho la muda wa kati; mwenyekiti alidokeza kuwa sehemu kubwa ya jimbo la Ubungo inahudumiwa na mtambo wa Ruvu juu kasoro maeneo ya Goba, Mburahati na Mabibo ambayo huhudumiwa na mtambo wa Ruvu chini. Pia mwenyekiti aligusia kuwa serikali ya Marekani kupitia mpango wa MCC imetoa fedha kwa ajili ya kuongeza bomba lingine likini fedha hizo hazitoshi kwa kuwa hazifiki hata bilioni 200. Ili kupata suluhisho la muda wa kati mwenyekiti aliwaomba washiriki kujadili; Je hatuna vyanzo mbadala katika mapato ya serikali ili kutatua tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam?

vii. Majukumu ya wadau; mwenyekiti alipendekeza majukumu kwa wadau wachache katika kutatua kero ya maji;

 Manispaa ya Kinondoni: mwenyekiti alitoa pendekezo kwa Manispaa kujenga visima kwenye maeneo ya pembezoni na kushauri kuwa kwa mwaka jana Manispaa ilitarajia kujenga visima 7 idadi ambayo alisema ni ndogo sana kulingana na mahitaji yaliyopo.

 Ewura: sheria inayounda Dawasa inawataka Ewura kudhibiti matumizi na bei ya maji kwenye miradi iliyopo chini ya jumuia za wananchi lakini changamoto kubwa iliyopo ni utekelezaji, na aliwakaribisha washiriki kwa ajili ya mjadala juu ya swala hilo.

 Vyombo vya habari: wanatambulika kama wadau muhimu sana katika swala la huduma ya maji. Mwenyekiti aliwaomba wanahabari kushughulikia kwa karibu swala la maji ili kuleta msukumo wa uwajibikaji na hatimae kutatua kero hii ya muda mrefu.

MAAZIMIO YA KONGAMANO
Baada ya mjadala mrefu uliodumu kwa takribani masaa matatu ukiendeshwa na Mwenyekiti ambaye pia ndiye aliyechokoza mada husika, kongamano lilifikia maazimio yafuatayo kwa ajili ya kutatua kero ya maji katika jimbo la ubungo;

i. Kongamano limelaani kitendo cha Dawasco kutohudhuria na kutoa mada bila sababu ya msingi huku wao wakiwa ni wadau wakubwa wanaolalamikiwa na wananchi katika kadhia hii nzito na ya muda mrefu sana. Juhudi kubwa ilifanywa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo kuwasiliana na Dawasco Makao Makuu na waliahidi kushiriki na kutoa mada lakini mpaka siku ya kongamano ofisi haikupokea ujumbe wa aina yoyote kuhusu ushiriki wao. Mawasiliano yalifamyika tena siku hiyo ya kongamano na ndipo walipokiri kuwa hawatashiriki kwa kuwa kazi yao ni ya kitaalamu na hivyo hawatakiwi kushiriki makongamano ya kisiasa. Hata hivyo kongamano hilo halikuwa la kisiasa bali wadau mbalimbali bila kujali dini au itikadi za vyama walishiriki na kutoa maoni yao na hata mamlaka ya serikali Ewura walishiriki, wawakilishi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto nao pia walishiriki na kutoa maoni. Kwa kuzingatia hayo ndipo kongamano lilipofikia uamuzi wa kuwalaani Dawasco kushindwa kushiriki katika kongamano hilo lenye kutoa mwelekeo/utatuzi wa tatizo sugu la maji.

ii. Utendaji wa Dawasco utazamwe upya kimuundo
ili kuleta ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi. Hii ni kutokana na maeneo mengi kukosa maji huku wananchi wakiendelea kulipia bili za maji, hakuna mgawo wa maji ulio rasmi kwa maeneo yote ambapo huchangia maeneo mengine kuwa na maji muda mwingi na mengine kukosa kabisa, watendaji wa Dawasco kuwajibu vibaya wananchi pindi wanapofuatilia matatizo ya maji, watendaji wa shirika hilo kuwa na ushirikiano na wafanyabiashara wa maji nahata wengine kutuhumiwa kumiliki magari yanayouza maji. Haya na mengine yaliwafanya washiriki kuazimia kuwa kuna haja ya kulifanyia shirika tajwa maboresho makubwa ili kukidhi mahitaj ya wananchi.

iii. Watu wanaotumia bomba ambazo wameziunganisha na bomba kuu la maji bila idhini ya shirika (illegal connections) wafichuliwe mara moja na kuchukuliwa hatua na mianya hiyo ya upotevu wa maji ifungwe ili kuwezesha maji kuwafikia wananchi walio wengi. Hii ni pamoja na malalamiko yaliyotolewa kuwa wapo wafanyabiashara waliojiunganishia maji kwa ajili ya kuwauzia wananchi wanaokosa huduma hiyo. Vile vile maeneo ya Kibamba maji yanatumiwa kumwagilia bustani za michicha na miche ya miti, hii ni kwa sababu ya uunganishwaji kiholela wa maji katika bomba kuu.

iv. Wananchi wenye “pump” binafsi za kuvutia maji; hawa nao watazamwe upya kwa sababu wanafanya maji mengi kubaki katika maeneo yao na hivyo kufanya wale wasokua na kifaa hicho kupata maji kidogo au kukosa kabisa. Hali hii inawafanya wachache kuhodhi huduma ya maji na kufanya wengi kuzidi kutaabika. Hivyo swala hili linahitaji kutazamwa upya na ikiwezekana wazuiwe kutumia vifaa hivyo.

v. Sera ya Maji; hitaji la mabadiliko katika Sera ya Maji ili kuyatoa maeneo mengi ya Jimbo la Ubungo kutoka kuwa kwenye miradi ya maji vijijini na kuwa kwenye miradi ya maji mjini. Hii ni kutokana na maeneo mengi ya jimbo kushindwa kunufaika na miradi mingi ya maji kwa kuwa sera inayatambua kama maeneo ya vijijini.

vi. Kamati za Maji kila kata ziundwe upya na zipewe nguvu ya kisheria tofauti na sasa ambapo huwa zinakua za muda kutokana na mradi husika (interim committees). Madiwani walipewa jukumu la kuhakikisha sheria ndogondogo zinatungwa ili kuzipa nguvu kamati za maji. Pia kongamano liliazimia kuwa kamati ziwe zinapeleka ripoti Manispaa kuhusiana na hali halisi ya upatikanaji wa maji ili mamlaka husika zichukue hatua za haraka.

vii. Mradi wa barabara katika Kata ya Manzese uliharibu miundombinu ya Maji na bado ukarabati wa kurudisha mabomba yaliyoharibika haujafanyika. Kongamano liliazimia kuwa miundo mbinu yote iliyohariwa ifidiwe na kurudishwa ili wananchi waendelee kupata maji.

viii. Maeneo ya miinuko mabwawa na visima vya maji vijengwe ili kuwaondolea wananchi kero ya kukosa maji kwa sababu ya kijiografia.

ix. Mitaa mipya itengewe maeneo ambayo ni maalumu kwa maji taka; hii ni kwa sababu jimbo la ubungo kuna mitaa mingi sana ambayo ni mipya na haina maji taka. Hii itatunza mazingira lakini pia itazuia magonjwa ya mlipuko.

x. Kata ya Kwembe haina miundombinu ya maji kabisa na hivyo wananchi kuendelea na kupata adha ya kununua maji ya madumu kwa bei ghali sana. Pia Msakuzi maji yanauzwa shilingi 500 hali inayofanya wananchi kuishi maisha magumu sana.

xi. Vyanzo vya maji vitumike vizuri hii ikiwa ni pamoja na wananchi kuwa na utamaduni wa kuhifadhi maji ya mvua kitaalamu.
xii. Ewura; Pamoja na kuwa Ewura wana uwezo wa kudhibiti bei ya maji katika vioski na sehemu zinazomilikiwa na jumuia za wananchi bado nguvu kubwa iongezwe kuhakikisha maji yanauzwa kwa bei iliyokubaliwa. Na pia uandaliwe utaratibu wa kudhibiti pia bei za wafanyabiashara ya maji ambao hununua kwa bei ya jumuia na kuuza maji hayohayo kwa wananchi kwa bei kubwa mno.

xiii. Nguvu ya pamoja ya wananchi inahitajika ili kubuni miradi ya maji na pia kuweka mikakati ya kila mara na kushirikisha mamlaka husika kutatua tatizo hili.

xiv. Kongamano linatoa muda wa mwezi mmoja kwa Dawasco kuanza kutatua kero ya maji kwa hatua za muda mfupi ili kupunguza kero ya maji. Wakishindwa kufanya hivyo Mbunge wa Jimbo la Ubungo atalazimika kuwasilisha hoja binafsi Bungeni kuhusiana na tatizo hili katika kikao cha mwezi Aprili 2011.

HITIMISHO
Kamati ya maji ya kongamano iliundwa ikiwa na mwakilishi mmoja kutoka kila kata 14 za jimbo na pamoja na madiwani wote kutokana na wadhifa wao na hivyo kufanya idadi ya wajumbe kufikia 28. Kamati itashughulikia utekezaji wa maazimio na pia kuibua kero mbalimbali za maji katika maeneo ya jimbo la Ubungo. Kamati itafanya kazi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo.

4 comments:

Anonymous said...

makongamano kama haya ya kujadili na kutafuta ufumbuzi wa maji yangefanyika awali tatizo hili sio kwa ubungo tu bali nchi nzima. hongera sana ngd mbunge kuonyesha njia. na DAWASCO wapo bado kwy sera ya chama kimoja--mawazo mgando. nami pia nachukua fursa hii kuwashutumu

PM CHUO CHA MAJI. said...

Kwanza nitoe shukrani zangu kwa Mbunge kwa kushirikisha wananchi kutatua matatizo yanayo wakabili.
Kwani jimbo la UBUNGO ndio ilipo wizara ya maji,achuo cha maji na wasomi mbalimbali wa nchi hii wanapatikana hapa lakini linakabiliwa changamoto ya maji MH fatilia kwa makini miradi mbalimbali ya maji na mipango endelevu ya maji huko bungeni ili tuondokane na aibu hii ya miaka hamsini tangu uhuru!

Unknown said...

hongera sana endelea kuwafahamisha wananchi kujua mahitaji yao ya msingi.

Anonymous said...

Nakupongeza kwa juhudi unazofanya mh. Mb, kitu ambacho kimekosekana kwenye hiyo report ni time frame, ni vizuri kuweka time frame ili iwe rahisi kufanya monotoring na evaluation na itakuwa rahisi kujua ni wapi hapafanyi kazi sawa. Kila la kheri!