Hatimaye leo tarehe 15 Disemba 2011 Samson Mwigamba mmoja wa Waandishi wa Makala aliyefikishwa mahakamani tarehe 8 Disemba 2011 ametoka mahabusu kwa dhamana. Kuchelewa kutoka kwake kumesababishwa na ugumu wa dhamana iliyotokana na aina ya dhamana iliyotakiwa. Awali ilitarajiwa angeshtakiwa kwa kosa la uchochezi hivyo viongozi wa chama walijiandaa kwa dhamana husika. Hata hivyo, hata hivyo alifunguliwa kesi ya jinai namba 289 ya mwaka 2011 yenye mashtaka makubwa zaidi ya kudaiwa kushawishi askari na maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama kutoendelea kutii serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete (kosa lenye mwelekeo wa uhaini).
Mahakamani alidaiwa kutenda kosa hilo tarehe 30 Novemba 2011 kutokana na Makala yake kwenye gazeti la Tanzania Daima Toleo Na. 2553 ambayo inadaiwa kuwa maudhui yake yamekwenda kinyume na kifungu 46 (b), 55 (10)(a) na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kutokana na mashtaka hayo alitakiwa kati ya mdhamini mmoja wapo aweke hati ya nyumba yenye thamani iliyotajwa na mahakama. Kwa kuwa sharti hili lilitolewa tarehe 8 Novemba na kesho yake ilikuwa sikukuu ya uhuru tarehe 9 Disemba hakukuwa na fursa ya kutimiza masharti yote kwa wakati pamoja na jitihada zote zilizofanywa na viongozi husika wa chama.
Hii ni kwa sababu taratibu za dhamana ya hati yenye mali isiyohamishika zinahusisha mali hiyo kufanyiwa uthamini (valuation) na baadaye kufanyiwa tena tathmini ya uthibitisho (verification) hatua ambazo huchukua muda kutokana na urasimu katika mamlaka mbalimbali.
Kwa heshima yake na kwa ajili ya kupanua wigo wa mjadala nimeona niwaletee ujumbe huu ambao nilichangia kwenye mtandao wa Wanabidii tarehe 7 Disemba 2011, siku moja kabla ya Mwigamba kufikishwa mahakamani.
“Nimesoma tena ujumbe ambao Mwigamba aliundika kwenu, najua wengine waliuchukulia kuwa ni mwito wa kawaida tu polisi kwa kuwa mhariri gazeti lililochapa makala yake hakuitwa.
Hata hivyo, vyanzo vyangu ndani ya Jeshi la Polisi vimenieleza kuwa kesho asubuhi Mwigamba anatarajiwa kupelekwa mahakama ya Kisutu kushtakiwa kwa kosa la uchochezi. Taratibu Tanzania inaelekea kuwa dola ya kipolisi (police state), hali ambayo ikifikia itakuwa na athari kubwa kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu.
Sina hakika kama wakuu wetu kwenye vyombo vya ulinzi na usalama wanayafanya haya kwa kwa maelekezo ya Rais kwa mujibu wa ibara ya 33 na 35 ya katiba au ni matakwa tu binafsi.
Kwa vyovyote vile, Rais anapaswa kushauriwa: KAMATA KAMATA KWA ARI, NGUVU NA KASI ZAIDI (ANGUKA); Miaka 50 baada ya Uhuru, tumeanza kurudi katika zile zama za watu kukamatwa na kuwekwa kizuizini.
Tofauti ya wakati huo na sasa ni kwamba sasa hukamatwi kwa kificho, wala huwekwi mafichoni; ni rahisi tu, polisi wanakukamata halafu wanakupeleka mahakamani.
Wanajua baada ya hapo utakuwa tayari umepoteza sehemu ya uhuru wako, utapaswa kwenda mahakamani mara kwa mara. Kesi itachukua muda mrefu kwa polisi hao hao walikuona una kosa wakakupeleka mahakamani kutoa sababu kwamba ‘upelelezi haujakamilika’.
Kosa la Mwigamba linaelezwa kutokana na makala yake aliyoiandika “Waraka kwa Askari wa Tanzania”, anadaiwa kwamba kupitia makala hiyo amewachochea polisi kukaidi amri za viongozi wao na kuwachochea polisi kukataa kutimiza wajibu wao wa kisheria. Suala hili limenifanya noisome makala yake, na baada ya kuisoma naona sasa tunaelekea katika dola ya kipolisi (police state).
Ari, Nguvu na Kasi hii ya Jeshi la Polisi kusoma, kufanya ufuatiliaji na kuchukua hatua dhidi ya ‘wahalifu’ ningeiunga mkono kama ingekuwepo toka wakati Orodha ya Mafisadi (List of Shame) iliposomwa 15 Septemba 2007 pale viwanja vya Mwembe Yanga na baadaye kusambazwa na vyombo vya habari na mitandao mbalimbali. Lakini mpaka leo Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) hakuna hatua za maana alizochukua lakini ana ari, nguvu na kasi zaidi ya kuwakamata na kuwahoji waandishi wa makala nyingine za magazetini.
Kauli ya kwamba si lazima kwa askari kufanya kile ambacho wakubwa wake wanamuamrisha kufanya hata kama anacholazimishwa ni kinyume cha sheria na kinyume cha maadili na haki na kwamba askari polisi watumie pia akili zao kufikiri Mwigamba sio wa kwanza kuiandika au kuisema.
Tanzania inaelekea kuwa dola ya polisi, sio kwa baadhi ya wabunge na wapinzani tu bali hata kwa wananchi wengine na hata katika ya polisi wa juu dhidi ya polisi wa ngazi za chini.
Tukio hili limenifanya nikumbuke mambo kadhaa dhidi ya jeshi letu ya polisi yaliyojiri katika mkutano wa nne wa Bunge.
Mosi; Wakati wa bunge la bajeti nilihoji kuhusu jeshi la polisi juu ya polisi kuwa na maslahi duni, Serikali ikasema bungeni kuwa posho zao (ration allowance) zimeongezwa mpaka laki unusu. Ukweli ni kwamba askari hawalipwi kiwango hicho cha posho, hata hivi sasa pamoja na ufafanuzi kuhusu mgawo wa posho za askari tulioomba bungeni tarehe 28 na 29 Julai 2011.
Kufuatia kauli ya serikali bungeni askari wakaanza kuulizia kuhusu posho hizo na waliowaunganisha wenzao kuhoji wakaitwa ‘wachochezi’; wakuu wa vikosi na vituo wakapewa waraka wa ‘kufuta’ kauli hiyo ya serikali nje ya Bunge na kuchunguza askari wote wanaopandikiza ‘chuki’ kwa wenzao dhidi ya serikali kwa kutumia suala hilo la posho.
Polisi maeneo mbalimbali nchini wakaelezwa kwamba vitendo vya kushawishi askari aliyekula kiapo cha utii kwa serikali kufanya hujuma kama hizo za kudai posho ambayo imeahidiwa bungeni ni hujuma kwa serikali hivyo ni UHAINI.
Pili, kitabu kinachosambazwa na Jeshi la Polisi Mitaani na Vijijini cha “Utii wa Sheria bila Shuruti” ambacho kinaonyesha mwelekeo wa serikali kuanza kuandaa mazingira ya dola ya kipolisi (police state). Kitabu hicho chenye kueleza kuhusu “wajibu wa vyama na watu walioshindwa katika uchaguzi” kinawaasa watanzania dhidi ya wanasiasa na wanaharakati wenye kutumia ‘tabia ya kutumia shida na kero za wananchi kuchochea hasira, munkari na jazba dhidi ya viongozi halali’.
Aidha, kampeni ya “Utii wa Sheria bila Shuruti” inawakumbusha wananchi wajibu wa “Kuepuka kushiriki katika mikutano, maandamano na harakati za kuichokoza mamlaka ya dola, kwa uwasilishaji wa malalamiko au kero kwa njia ambazo zinasababisha bughudha na karaha kwa wengine”.
Kitabu cha “Utii wa Sheria bila Shuruti” kinaeleza kwamba ‘Sheria inampa mamlaka afisa wa Polisi wa himaya inayohusika kusitisha maandamano, mkutano au mkusanyiko wowote endapo atabaini kwamba kuna habari au taarifa kwamba kuendelea kufanyika kwa mkutano kunaweza kusababisha uvunjaji wa amani na kuhatarisha usalama. Na kwamba endapo amri hiyo itaonekana kuupuuzwa kwa namna yoyote hata kama maandamano, mkutano au mkusanyiko ulikuwa ni halali utahesabika kuwa ni haramu. Hivyo hatua za kuwatawanya kwa njia ya shuruti itafuata ikiwemo kuwakamata waandaaji na washiriki na kuwafikisha mahakamani”.
Kifungu hiki kilitumiwa kwenye Mkutano wangu na Wananchi tarehe 5 Novemba 2011 kwa kuvamia katika mkutano halali, kukata nyaya za vipaza sauti, kukamata viongozi waandaji na kuondoka nao pamoja na gari lenye nyaraka mbalimbali za katiba. Maelezo ambayo waliwaeleza awali viongozi hao ni kuwa mkutano haurusiwi kutokana na tishio la ugaidi wa Al Shabab.
Nilipoelezwa nikawaambia viongozi waendelee na maandalizi ya mkutano kwa kuwa Rais hajatangaza hali ya hatari, kama kuna tishio la kawaida la vurugu polisi waje wamejiandaa kufanya kazi yao ya kulinda amani kama ambavyo walikuwa wamejiandaa kulinda mechi zingine za mpira zilizofanyika siku hiyo hiyo ya tarehe 5 Novemba na matembezi ya Mke wa Rais yaliyofanyika DSM wiki hiyo hiyo.
Pamoja na viongozi kukamatwa na vipaza sauti kuchukuliwa kabla ya kufika uwanjani, nilipofika niliendelea kufanya mkutano wa kupata maoni ya wananchi kuhusu muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba na masuala mengine muhimu ya jimbo na taifa kwa ujumla kabla ya kwenda mkutano wa tano wa Bunge ulioanza tarehe 8 Novemba 2011. Nawashukuru askari walioacha kunikamata pamoja na maagizo waliyokuwa wamepewa ya kunikamata.
Kwanini nimeandika yote haya? Sababu ya Mwigamba kuitwa mchochezi ni kuwa amewaambia askari watumie akili zao wasikubali kutumwa kukamata na kupiga watanzania wenzao katika hatua za maandamano ya kupinga sheria ya mabadiliko ya katiba wakati njia za kidiplomasia kupitia mikutano za kutaka sheria hiyo ifanyiwe mabadiliko kabla ya kuanza kutumika zitakapopuuzwa na hatimaye kulazimika kuunganisha nguvu ya umma kupitia maandaamano.
Nimeamua kutafakari kwa sauti wakina Mwigamba wengine mnisikie, kwamba tusipoungana kuwakanya viongozi wetu tunaelekea kuwa dola ya kipolisi na kwenye mchakato wa katiba dola hiyo (Mungu apishie mbali) inaweza kutumiwa na watawala kuvuruga utulivu wetu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hiyo ni dola ya polisi wasiofikiri kabla ya kutenda; polisi wanaofikiri baada ya kutenda kwa kutumwa na watawala walioacha kufikiri na kujikita katika kutoa amri haramu.
Akili zao zinadhihirika kwenye kauli zao na za wataalamu wao mathalani kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali bungeni wakati wa kuhalalisha kifungu kwenye sheria ya Mabadiliko ya Katiba chenye kutoa adhabu ya faini isiyopungua milioni tano na isiyozidi milioni kumi na tano au kifungo kwa muda usiopungua miaka mitatu na isiyozidi miaka saba au adhabu zote mbili kwa kwenda kinyume cha sheria hiyo.
Makosa yenyewe ya hukumu hiyo ni pamoja na ‘kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi’ na ‘kuendesha elimu ya mabadiliko ya katiba kinyume na masharti ya sheria’ hiyo. Makosa ya kukusanya maoni na kutoa elimu sasa yametengewa hukumu kubwa kuliko ya mafisadi na ambao wameisababishia hasara serikali. Huo ndio “Utii wa Sheria bila Shuruti” wanaoutaka kwa watanzania. Kwa maneno ya Werema bungeni kuhalalisha kifungu husika “matatizo tuliyonayo sasa ambayo yanasababishwa na watu ambao hawataki kufuata utaratibu kwa mambo ya siasa, inatakiwa kutoa elimu ya kisiasa katika jambo hili la katiba kwamba wapewe adhabu kali; ndiyo maana yake”.
Nawaandikia kuwaomba mjiandae iwe ni wanahabari, wanaharakati, wanasiasa, viongozi wa dini, wanataaluma au wananchi wa kawaida; kuwa mkiwa na mawazo tofauti kuhusu katiba na polisi hawa wa “Utii wa Sheria bila Shuruti” wakaagizwa kuwakamata kwa kutoa elimu ama kukusanya maoni kinyume cha sheria adhabu yenu itakuwa kifungo cha hadi miaka saba au faini ya hadi milioni 15 au vyote. Na polisi jiandae, huu ni wakati wa pekee katika historia taifa letu; miaka 50 baada ya Uhuru wa Tanganyika, muwafunge wananchi wenzenu wanaodai uhuru wa kweli dhidi ya ujinga, umasikini, maradhi na ufisadi kwa kudaiwa na serikali ya mkoloni kuwa ni wachochezi kama alivyofanyiwa Mwalimu Nyerere na TANU au msimame upande wa haki na ukweli.
Na hili halihusu tu maslahi ya taifa ambayo tunawaomba askari myasimamie popte pale mlipo, inahusu pia kusimamia maslahi yenu wenyewe. Wakiitisha mabaraza ya askari, wakiwaambia polisi kwamba mnapaswa kuendelea kulipwa ration allowance ya laki moja tu, kwa mujibu wa waraka wa idara kuu ya utumishi wa tarehe 26 May 2009 wenye kumb. Na. C/AB.129/271/01/E41 waambieni waje watuambia sisi bungeni kwa kuwa walitoa kauli kuwa mnalipwa laki na hamsini; waje waje wafute kauli bungeni tujadili msingi wa wao kukataa kuwalipa haki yenu hiyo kwa mwezi, wakati ni pungufu ya posho iliyoongezwa kinyemela ya mbunge ya siku moja pekee ya kukaa kwenye kikao (sitting allowance).
Mkitumwa kwenye kufanya operesheni haramu na kulipwa viwango duni vya posho kwa kuwapiga watanzania wenzenu kwa maelezo kuwa waraka mwingine wa tarehe 27 Januari 2009 wenye kumb. Na. C/BC. 129/271/01/18 umewaongezea posho kwa 15% waulizeni mbona serikali imeongeza posho haramu kwa wabunge ya kukaa kwenye vikao kwa zaidi ya 150%.
Wakiendelea kuwalipa mishahara midogo huku kima cha chini kikiwa kimeongezeka toka 219,170 mpaka 243,000 tu sawa na ongezeko la 10% huku bei za bidhaa na gharama za maisha zimeongezeka kwa zaidi ya 100% waulizeni uhuru na usawa tulioupigania miaka 50 uko wapi?
Najua wanaendelea kuwaeleza mkiwa kwenye maandalizi ya gwaride la sherehe za uhuru kuwa muendelee kuwa na ‘utii na uvumilivu kwa kuwa serikali haina uwezo’ na kwamba nyongeza hiyo ndogo kupitia waraka wa tarehe 13 Julai 2011 wenye kumbukumbu na. CAC/205/228/01/A/41 imetokana na hali halisi ya uchumi wetu. Muwakumbushe kiwango cha fedha ambacho kinakaribia kufika bilioni 50 kinachotumika kwenye ‘sherehe’ za miaka 50 ya uhuru toka maandalizi yake yaanze mpaka mwisho huku mkiidai serikali malimbikizo ya madeni.
Hali yenu ni sawa na ya walimu, watumishi wa sekta ya afya na kada nyingine za chini katika utumishi wa umma ambapo mtajumuika kwa ‘utii wa bila shuruti’ katika halaiki ya 9 Disemba ‘kusherehekea uhuru’. Hampaswi kugoma kwa kuwa kazi yenu ni wito, lakini msiache kuwafikishia ujumbe watawala; msikubali kutumiwa kuminya haki zenu wenyewe na za wenzenu.
Tekelezeni amri zote halali za ulinzi na usalama wa taifa letu, wakatalieni amri zote haramu zenye kuvunja sheria, kuvuruga amani na kukiuka haki za msingi za binadamu. Tenganisheni kati ya kusimamia maslahi ya taifa na kulinda matakwa ya mafisadi; tambueni kuna amri za watawala kudumisha utawala wao na kuna amri za viongozi kusimamia mahitaji ya umma.
Watawala wameapa kulinda katiba, ambayo ibara ya 8 (a) inatamka wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na serikali itapata madaraka kwa wananchi; ibara ya 9 inawataka wao na serikali wanayoongoza kulinda haki za binadamu, kuendeleza utajiri wa taifa kwa manufaa ya wananchi wote, kuhakikisha serikali na vyombo vyake vyote vinatoa nafasi sawa kwa raia wote bila ubaguzi na kwamba aina zote za dhulma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini. Waambieni wakumbuke kiapo chao, na wasiwalazimishe nyinyi kutii amri zinazokiuka kiapo chao wenyewe.
Msiwaogope wao kuliko wananchi wanaowalipa mishahara yenu kwa kodi zao na ndugu zenu mnaishi nao katika mazingira yenu ya ugumu wa maisha. Kama hamuwaogopi wananchi wenzenu basi walau muogopeni Mwenyezi Mungu anayetaka muenende kwa upendo, haki na ukweli. Sheria kuu kuliko zote ya kuitii sio ya Tanzania; bali ya nafsi zenu na Mungu wetu. Msiwatii wanapowataka mtende dhambi. Kwa maneno ya Mahatma Ghandi, ‘kuweni mawakala wa mabadiliko mnayotaka kuyaona’”.
Kama nilivyoandika miaka michache iliyopita wakati mwanahabari wa gazeti la Mwanahalisi Saed Kubenea aliposhambuliwa; shambulizi dhidi ya mwanahabari ni chambulizi dhidi ya ‘uhuru wa habari’. Hivyo, kamata kamata dhidi ya watoa maoni, ni kamata kamata juu ya ‘uhuru wa kutoa maoni’. Tukio hili lipaswa kuwa chachu ya kuendelea kutoa maoni na kudai uhuru wa kutoa maoni ikiwemo uliopokwa kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Kesi hii ni muhimu kwa taifa kuhusu haki ya msingi ya kibinadamu na kuwasiliana na kutoa maoni, hivyo tuifuatilie kwa karibu mwenendo wake. Aidha, ni wakati sasa wa kuunganisha nguvu ya umma kudhibiti nchi yetu kugeuzwa ‘dola ya kipolisi’.
John Mnyika (Mb)