Wednesday, December 7, 2011

Msimamo wangu juu ya suala zima la Posho!

Kufuatia habari tarehe 28 Novemba kuhusu ‘kupanda kimya kimya kwa posho za wabunge kwa zaidi ya asilimia 150’ tarehe 29 Novemba 2011 nilitoa kauli yangu kama mbunge na katibu wa wabunge wa CHADEMA kuhusu suala husika.

Katika kauli hiyo nilieleza kuwa: “ Wabunge wa CHADEMA hatujapokea taarifa rasmi kwamba masharti ya kazi ya ubunge yamebadilika na kwamba viwango vya posho vimeongezwa. Wala kamati ya wabunge wa CHADEMA haijawahi kuridhia ongezeko lolote la posho ya vikao (sitting allowance) kwa wabunge. Napenda kutumia fursa kusisitiza msimamo wetu wa kutaka posho za vikao (sitting allowance) ziweze kufutwa kwa wabunge na katika mfumo mzima wa malipo ya wakati wa kazi miongoni mwa watumishi wa umma”.

Hivyo, kama mbunge na katibu wa wabunge wa CHADEMA nilitoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kwa niaba ya Serikali na Spika Anna Makinda kwa niaba ya Bunge kutoa kauli kuhusu suala hili ili kuondoa hisia zinazojengeka kwamba ‘wabunge wote tumekaa bungeni na kukubaliana kujiongezea posho ya vikao’.

Kufuatia Spika Makinda kutoa kauli na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari tarehe leo tarehe 7 Novemba 2011 naomba kutoa msimamo wangu kama ifuatavyo:
“ Ongezeko la posho ya vikao lilofanyika linapaswa kusitishwa kwa kuwa limefanyika kinyume na taratibu na pia halina uhalali wowote kimantiki na halijazingatia uhalisia wa maisha ya wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla; nyongeza hiyo ya posho ya vikao ni haramu (Illegitimate).

Bado narudia kutoa mwito kwa Rais Kikwete kutoa kauli wake na wa Ikulu na Ofisi ya Rais kwa ujumla unaacha ombwe lenye athari kubwa kwa serikali na kwa bunge mbele ya wananchi ambao kwa mujibu wa katiba ibara ya nane ndio wenye mamlaka na madaraka.
Aidha, kauli ya Spika Makinda kwamba nyongeza hiyo ya posho za vikao ni kwa sababu ya kupanda kwa gharama za maisha mkoani Dodoma haina ukweli, wala mantiki na ina mwelekeo wa upendeleo.

Nyongeza hiyo ya posho ya vikao ni matumizi mabaya ya madaraka na ni dharau kwa walipa kodi wanaohangaika na kupanda kwa gharama za maisha na athari za ubadhirifu wa fedha za umma. Ni udhaifu kufikiri kwamba suluhisho la kupanda kwa gharama za maisha ni kuongeza posho za kikao; tatizo la kupanda kwa gharama za maisha linapaswa kushughulikiwa kwa kuchukua hatua dhidi ya matatizo ya kiuchumi katika nchi ili kuweza kuwa na tija kwa wananchi wengi ambao ni waathirika zaidi wa kupanda kwa gharama za maisha kuliko wabunge.

Pia, utetezi wa Spika Makinda kuhalalisha upandishaji wa kinyemela wa posho za vikao kwa wabunge haina maana kuwa kama sababu ingekuwa chanzo ni kupanda kwa gharama maisha ingepandishwa posho ya kujikimu (subsistence allowance) ambayo imebaki pale pale 80,000 .

Aidha kufuatia kauli ya Spika Makinda, hatua za kinidhamu zinapaswa zichukuliwe na Rais Kikwete dhidi ya Katibu wa Bunge Dr Thomas Kashilillah ya kutoa taarifa potofu kwa umma kwa kukanusha kwamba ofisi ya bunge haijaongeza posho kwa wabunge na pia kwa kufanya malipo kinyume na taratibu.

Kugongana kwa kauli baina ya Spika na Katibu wa Bunge ni ishara ya kuwepo kwa jambo ambalo linafichwa kuhusu suala hilo la nyongeza haramu ya posho za vikao kwa wabunge na pia ni ushahidi wa taratibu kukiukwa hali ambayo inahitaji kauli kutoka kwa mwenye mamlaka kwa mujibu wa sheria kuhusu masuala ya posho za wabunge ambaye ni Rais.

Pia, katibu wa wabunge anapaswa kutuomba radhi wabunge kwa kauli yake kwamba mabadiliko ya posho za vikao yametokana na mkutano wa wabunge tarehe 8 Novemba 2011 kuiomba serikali ipandishe posho hizo za vikao.

Binafsi nilikuwepo kwenye mkutano huo wa tarehe 8 Novemba 2011 na hakuna uamuzi wowote ambao ulifikiwa wa kuiomba serikali ipandishe posho za vikao. Kilichotokea ni kwamba katika kuchangia maelezo ya serikali na ya bunge kuhusu masuala mbalimbali ya bunge na serikali yaliyojiri baada ya mkutano wa nne wa Bunge na mpangilio wa mkutano wa tano wa bunge, wabunge walipewa fursa ya kujadili taarifa hizo.

Katika kujadili taarifa hizo wapo wabunge wachache waliotoka nje ya hoja za msingi na kuzungumzia kuhusu nyongeza ya posho ya vikao; hata hivyo mkutano huo wa wabunge haukufanya maamuzi yoyote na wala haukukamilika. Kabla ya majina yetu wengine kufikiwa kuweza kuchangia Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye kwa nafasi yake ya kiongozi wa shughuli za serikali bungeni ni mwenyekiti wa mikutano ya wabunge alieleza kwamba muda umemalizika hivyo mkutano na kwamba tarehe nyingine ingepangwa kwa ajili ya kuendelea kujadili masuala mbalimbali yaliyohojiwa na pia kuweza kutoa fursa kwa wabunge wengine kuweza kutoa maoni yao kuhusu masuala hayo.

Katika hatua hiyo Waziri Mkuu Pinda alisoma majina yetu na kueleza kwamba mkutano huo wa wabunge ungeendelea katika tarehe nyingine lakini haukufanyika mkutano mwingine; hivyo katika mkutano wa tano wa bunge uliomalizika wabunge ambao mimi nilishiriki wabunge wote hatujawahi kukaa na kujipangia nyongeza ya posho za vikao kama inavyoelezwa hivi sasa wala.

Pia, wabunge hatujawahi kupatiwa nakala ya muktasari au kumbukumbu wa vikao vya kamati ya uongozi au vya tume ya bunge ambavyo vimekaa na kupitisha nyongeza ya posho ya vikao kutoka 70,000 mpaka 200,000 kama Spika alivyonukuliwa na vyombo vya habari. Ni muhimu watanzania wakazingatia kwamba mwenye mamlaka ya kupandisha posho za wabunge ni Rais na natoa mwito kwa Rais kukataa kupandisha posho za vikao kwa wabunge na badala yake azifute kabisa. Watumishi wote wa umma ikiwemo wabunge hatustahili kulipwa posho za kukaa kwenye vikao vyetu ambavyo mwisho wa mwezi tunalipwa mshahara kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Kufuatia hali hii, kwa kuwa sasa imeshatoka kauli rasmi ya bunge yenye kudhihirisha kwamba posho za vikao zimepandishwa kinyemela badala ya kufutwa kama tulivyotaka awali; tutaitisha kikao cha wabunge wa CHADEMA ili kukabaliana hatua za ziada za kuchukua kwa kuwa ofisi ya bunge na serikali wanaendelea kuingiza posho za vikao kwenye akaunti za wabunge hata baada za kuzipinga.”


Katika kauli yangu ya tarehe 29 Novemba 2011 nilieleza kwamba ni vyema umma ukafahamu kwamba Sheria ya Utawala wa Bunge (National Assembly Administration Act) ya mwaka 2008 kifungu cha 19 kinataja aina ya posho ambazo zinaweza kutolewa kwa wabunge kama ambavyo Rais ataeleza kwa maandishi. Katika kipengele (d) sheria imetaja orodha (i) mpaka (iii) ya posho ambazo wabunge wanastahili kulipwa za usafiri, kujikimu na wasaidizi. Katika orodha hiyo hakuna Posho ya Kikao (Sitting Allowance) ambayo inalipwa hivi sasa kwa kuwekwa kwenye akaunti za wabunge moja kwa moja ambayo kamati ya wabunge wa CHADEMA tunataka ifutwe mara moja kama sehemu ya mchakato wa kubadili mfumo mzima wa malipo ya posho kwa watumishi wa umma.
Kifungu 19 (d) (iv) kimempa mamlaka Rais ya kutoa posho zingine kwa wabunge kwa kadiri atakavyoelekeza; kifungu hiki kimetoa mwanya wa kutolewa kwa waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais wa tarehe 25 Oktoba 2010 wenye kumbukumbu na. CAB111/338/01/83 masharti ya kazi ya mbunge ambao umeeleza viwango vya posho mbalimbali ikiwemo kutoa posho ya vikao (Sitting Allowance).

Hivyo, ofisi ya Rais na Ofisi ya Bunge zinapaswa kuwaeleza watanzania iwapo waraka huo umebadilishwa na sababu za wabunge kutojulishwa kuhusu mabadiliko hayo.
Aidha tarehe 29 Novemba 2011 nilieleza kuwa, iwapo mabadiliko hayo yamefanyika ni muhimu yakasitishwa kwa kuwa zitakwamisha utekelezaji wa mpango wa kufuta posho za vikao (sitting allowance) na kupunguza matumizi ya serikali kama ilivyoelezwa katika Ilani ya CHADEMA ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 pamoja na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliopitishwa bungeni mwaka 2011.

Izingatiwe kwamba uchumi wa nchi hivi sasa unasuasua, serikali ina hali mbaya ya fedha kutokana na kupungua kwa kiwango cha fedha kinachopatikana katika kodi na washirika wa kimaendeleo ukilinganisha na mahitaji ya bajeti; na hivyo kukopa kibiashara kwa ajili ya kuziba nakisi iliyopo.

Kupungua kwa uzalishaji, kiwango cha fedha pamoja na kuongezeka kwa ubadhirifu katika matumizi ya rasilimali za umma kunachangia katika mfumuko wa bei hali inayohitaji mpango wa dharura wa kunusuru uchumi wetu ukaohusisha pamoja na mambo mengine kubana matumizi ya serikali.

“ Binafsi natarajia serikali ije kwetu wabunge na mpango wa kukabiliana na ongezeko la gharama za maisha kwa wananchi badala ya kutuletea mpango wa kutuongezea wabunge posho za vikao huku mwelekeo wa uchumi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ukiwa kwenye hali tete”.

Kamati ya wabunge wa CHADEMA ilikubaliana posho hizo zifutwe kwa kuwa Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 imeeleza kwamba lengo la msingi ni kuondoa posho za vikao (sitting allowance ) hatua ambayo itaambatana na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma kuendana na ujuzi, nafasi, wajibu ili wafanyakazi walipwe kwa haki kwa kile wanachofanya kwa haki. Uamuzi huu ungewezesha pia kuelekeza fedha zaidi katika miradi ya maendeleo.

Ofisi ya Rais na Ofisi ya Bunge zizingatie kuwa Serikali ya CCM imeridhia msimamo huo na kuuingiza kwenye Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano 2011/2012-2015/2016 uliosainiwa na Rais Jakaya Kikwete tarehe 7 Juni 2011 ambao kwenye ukarasa wa 17 unatamka bayana kwamba posho za vikao na nyinginezo zinapaswa kufutwa au kuwianishwa hivyo kuziongeza ni kupuuza mpango huo.

John Mnyika (Mb)
07/12/2011

25 comments:

ebrah said...

nipo nawe bega kwa bega kwa 150% mh Mnyika.kwani gharama za maisha zimepanda dodoma peke yake?na serikali inadai haina pesa sasa hizo wanazipata wap?mimi wazazi wangu mpk leo hawajalipwa mishahara mwezi wa pili kwa madai pesa hakuna i wonder..naomba hao akina wahujumu uchumi muwaandalie mashtaka kwa ubadhilifu wao..

Nchemwa said...

CHADEMA MMEKOSA MSIMAMO WA PAMOJA KUHUSU SUALA ZIMA LA POSHO, WAPO WENZENU WANAOWASALITI MF. JOSEPH SELASIN MBUNGE WA ROMBO, SHIBUDA. NA WANAO PINGA mf. WEWE MWENYEWE MNYIKA, ZITTO KABWE, HALIMA MDEE, MBOWE NA WENGINE! MNAFIKIRI KWA MTANGAMANO HUU MTAWEZA KWELI KUTETEA KWA DHATI KWAMBA INAATHARI KWA TAIFA?

Daniel Lwanji said...

Safi sana kaka, umeonyesha kukomaa kisiasa, wewe umenena, Tunasubiri utendaji zaidi juu ya hili. kutoa tamko tu haitoshi, juhudi za haraka zinahitajika kukomesha hili.

Anonymous said...

UMEELEWEKA KAKA, tuko nyuma yako, na kwa hili tofauti inaonekana kati ya wabunge wa wananchi na wabunge wa manufa yao binafsi....kama kawida yao wanaweza wakalirudisha bungeni na kulipigia kura na kulipitisha lakini sisi wananchi tutakuwa mahakimu wazuri wakati ukifika....

Anonymous said...

Ni wabunge wangapi wa CHADEMA ambao wamepokea posho hiyo ya nyongeza?
Maana inaonesha ni muda mrefu tu imepitishwa kinyemela na kuanza kuingizwa kwenye Akaunti za Wabunge.

Kwa hiyo posho hizo zimeingizwa hata kwenye Akaunti za zitto, mnyika na wengine bila wao kujua?

INATATANISHA HAPA!!

Mrisho's Photography said...

nasema hivi hii nchi imepoteza dira na haina kiongozi, maana kila mtu ni kiongozi na anaweza kuongea chochote, wakati wowote na asifanywe lolote, kwa sababu hakuna mtu yeyote anayeogopwa na wote!!!

Pawa luhende. said...

Maajabu tena ya maamuzi ya chombo cha ngazi ya juu Tanzania!
Posho posho posho.

Anonymous said...

Hili la Posho tu CCM walitakaficha taarifa na mwishowe kukongana semi, Katibu wa Bunge na Spika. Je, la katiba chini ya mamalka ya Rais ambaye chama chake in ndumilakuwili, tutapata katiba haki kweli?

mafube ntibabara said...

Asante mh.Mnyika wakati wanajiongezea 150% wafikirie mfanyakazi ameongezewa % ngapi? Pia sukari,mfanyakazi wa ndani, kodi ya nyumba n.k tunavilipaje kwa wakati huu, waangalie mashirika yanayokopesha wafanyakazi riba wanazotozwa na kodi inayolipwa kila mwezi kutoka kwenye mishahara yetu, watembelee hospitali vituo vya afya vyetu waone kama kuna dawa, waende kwenye shule za bweni washuhudie zinavyofungwa mapema kwa ukosefu wa chakula huku wazabuni wakihangaika bila malipo, shule za kata wamefanya nini kama watoto wanakaa chini? hapo tuachie mbali maabara,walimu na vitabu. Yapo mengi ila kwa ujmla huduma za jamii zimedolola na inatia uchungu sana ila ipo siku yao.

Anonymous said...

Hivi posho zimepanda lini? samahani naomba kuuliza hvi sera ya kukataa posho ni ya mtu binafsi au ya chama? mara ya kwanza mh. zitto ndiye niliyemsikia akigomea posho akitaka zipelekwe kwenye jimbo lake bt bdae ikawa sera ya chama juzi tena alipotoka hospitali nimesikia akilaumu kupanda kwa posho tena akimtaja mh. january kuwa ni mzalendo wa kweli coz yeye amegomea posho, ila pia bunge lililopita nilisikia wabunge wa chadema 2 wakidai posho ndogo na kubeza wanaokataa posho wanavyanzo vingine vya kipata ili nisingependa kutaja majina. so nauliza suala la posho ni zitto pekee ndo wakulisemea na wengine kudakia. shout out to hon. Zitto Kabwe coz we ndo uko real kwa wananchi.

uncle TOM said...

Me zitto namkubali kwa sababu siku zote anaongea ukweli wengine wanafuata mkumbo tu mh. thelathini aliongea bungeni akidai posho ndogo bt kama tulivyowabongo tunasubiri kitu kifanyike ndo tupate pa kuongelea kwanini hatuna utaratibu wa kukemea kabla? posho mmeshakula ndo mnajifanya kuongea sasa hivi. je wale waliokula tayari mtawafanyeje? haya endeleeni kufaidi national cake wenyewe.

ole laizer said...

Tatizo ni usaliti.
Kwanini Shibuda anawasaliti?

Architect said...

Asante mh. kwa tamko lako!ila tunahitaji uvumilivu katika hili,hata wale waroho wanaozitaka kutoka kambi ya CDM basi wasomeshwe ili wawe wapole! Wajue huu ni mkakati wa kuikomboa Tanzania! Baadhi wanasema wanaopinga ni matajili,wanaendesha magari ya kifahali....wametosheka....Lakini mimi naamini katika yote! Maana hata kama wewe si tajili,sidhani tsh 200,000 km zitakutajilisha mara moja! Tuwe na uchungu na Tanzania yetu na Watanzania wake!

MBASAJOHN said...

tuko pamoja kamanda swala hl n vema mkaitsha maandamano nchi nzma il wananchi tutumie haki yetu kikatba kkataa kkandamzwa na wanyonyaj hawa wasio na haya!

Anonymous said...

DOGO ULIANZA VIZURI LAKINI PESA SABUNI YA ROHO ILA SIJUI KAMA UNASEMA AGAINST POLITICAL WILL MAANA SIKU HIZI WANASIASA WOTE MNATAZAMA UPEPO TU VIJANA WANATAKA KUSIKIANI JE WASOMI WANASEMAJE MOST OF THE POLITICIAN HAMKO REAL LABDA ATAWALE MAAIKA

Anonymous said...

maisha yamepanda kwa wabuge tu,kama sipika alivyosema!!wabunge wetu wote mmeshindwa kuwa wazarendo wa nchi hii maana wabunge ndo wanaopitisha kima cha chini cha wafanyakazi kiwe sh 150,000/lakini baadhi yao wanataka kwa siku wchukue sh 200,000/kweli watanzania tuna akili timamu kwa mwezi nitumie sh lakimoja na nusu mie mfanyakazi na mbuge kwa siku achukue sh laki mbili na tuna enda soka moja wote,watanzania tuamuke sasa

Anonymous said...

nimemaanisha malaika politician mmekuwa opportunist kundi kubwa la wanasiasa vijana ni waigizaji wanaangalia upepo unavumaje na ukweli halisi 'logigal but illegal'

Anonymous said...

R.P. Masaule

Mh Mnyika,

Kwa kweli nchi inaelekea pabaya ila naamini ipo siku wenye nchi na wana nchi uvumilivu utawashinda na kuingia barabarani

Anonymous said...

Mh. Mnyika kama kuna uwezekano toeni hoja ya kutokua na imani na spika wa bunge na katibu wake maana wamekiuka sana misingi ya bunge kwa kutaka kuwachonganisha wbunge na wananchi. hoja zilizotolewa na spika wa bunge ni za kitoto sana. ni aibu bunge kuongozwa na watu (spika na katibu wake) mwenye upeo na uelewa mdogo kiasi hicho.

Stella said...

Mhe. Mnyika, uvumilivu wa CHADEMA kwa wabunge wasaliti kama Shibuda uwe wa kiasi na ikiwezekana ufikie kikomo. NIkisoma habari za Shibuda na matukio mbali mbali akiyoshafanya ya kuwasaliti wabunge wenzake wa CHADEMA ninapata hisia kuwa bado yeye ni CCM na alihamia CHADEMA kwa maslahi binafsi. Uvumilivu wenu Makamanda ni kiasi gani? Vinginevyo tutoleeni tamko kumhusu Shibuda ili sisi tunaowaunga mkono katika harakati za ukombozi wa kweli wa nchi yetu tupate habari sahihi kumhusu Shibuda.

Anonymous said...

Mimi nafikiri Mnyika na Chadema mmeeleweka, CCM ndo wanaogawa posho kwa wabunge hata kama hawataki kuzipokea. Nafikiri Chadema mnafanya kazi nzuri bungeni mnastahili kuongezewa posho kuliko hawa CCM. Pamoja na hayo maisha magumu wanamuathiri mtu mwenye kima cha chini cha mshahara kuliko mbunge anayepokea 7M, kwahiyo makinda amepotosha umma kusema kuwa wabunge wanaathiriwa na kupanda kwa gharama za maisha, kimsingi wabunge wanapaswa wapunguziwe posho na mshahara kwa kushindwa kuisimamia serikali ili gharama za maisha zishuke, mmeendelea kupitisha bajet za anasa tu bungeni shame on wabunge wa CCM.

LULANDALA said...

sifikirii kwamba tofauti ya msimamo na mtazamo juu ya suala hili miongoni mwenu linaondoa uharisia kwamba posho za watumishi wa umma ikiwamo wabunge ni mzigo mkubwa kwa taifa letu. hiyo pia haiondoi ukweli kwamba mnatakiwa kukabiliana na tatizo hili kikamilifu kama wawakilishi waaminifu mnaojali maslahi ya kila mtanzania. HAMTAKIWI KULUDI NYUMA HATA KIDOGO KATIKA HILI,, NA MANPASWA KUAMINI KUWA HATA VITABU VITAKATIFU VIMETANGAZA USHINDI JUU YENU KAMA WAPIGANIA HAKI PASIPO UNAFIKI WOWOTE. TOFAUTI HAZIWEZ KUKOSENA, HATA WAMWITAO BWANA BWANA SI WOTE WATAKAOUONA UFALME WA MUNGU..UMMA UNAAMINI KWAMBA MNATAMBUA MATATIZO YA UMMA MFANO HILO LA POSHO NA HASARA ZAKE KWA TAIFA, NA TUAAMINI KWAMBA HICHO NDICHO KILICHOWASUKUMA KUOMBA UWAKILISHI NDANI YA BUNGE.. MUWAJIBIKE KATIKA HILO NA WALA MSIRUDI NYUMAAA. WATAKATIFU NA WATEULE HAWAACHI KUOMBA KWA AJILI YENU ,BE STRONG, GO AHED GOD IS WITH YOU BROTHER, SAY WHAT IS TRUTH, DECIDE WHAT IS RIGHT AND GOD WILL BLESS U IN JESUS NAME...

Sendaro H said...

Wakati mwingine ninakuwa na mashaka na misimamo mnayoonesha kuwa kuna kitu kimejificha nyuma yake.Siungi mkono posho kupanda hata kiduchu ila swali kwenu ni hili!.
MLIKUWA WAPI SIKU ZOTE kumbe posho ina muda mrefu imepanda?.

Anonymous said...

pamoja sana jembee

Anonymous said...

big up Jembe