Wednesday, February 29, 2012

Ratiba ya mbunge na DAWASCO kwenye kata leo, hatua zaidi zitafuata

Leo Machi Mosi nitakuwa pamoja na DAWASCO katika kata mbalimbali za jimbo la Ubungo kuchukua hatua za kuboresha upatikanaji wa maji kupitia ziara ya kikazi: Sinza (Saa 3-4 As), Mabibo/Makurumla (4-5), Makuburi (5-6), Saranga (6-7 mch), Msigani (7-8), Kwembe (8-9 jn).

Izingatiwe matatizo ya maji katika maeneo mengi ya jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo yamedumu kwa muda mrefu, tumepewa kazi ya kuwawakilisha kuisimamia serikali na mamlaka zake kupunguza kero husika katika kipindi cha muda mfupi; tunao wajibu wa pamoja wa kuziba pengo la miaka 50 katika kipindi cha chini ya miaka 5. Katika kipindi cha mwaka mmoja toka tupewe dhamana na dhima yapo maeneo ambayo tumewezesha yameanza kupewa mgawo wa maji, tuendelee kuunganisha nguvu ya umma zaidi katika mwaka huu wa pili wa 2012 yaongeze maeneo mengi zaidi.

Baada ya ziara hii tutawapa mrejesho kuhusu ratiba ya mgawo wa maji na hatua ambazo DAWASCO itapaswa kuendelea kuchukua. Nitawaeleza pia hatua za ziada ambazo tunapaswa kuchukua za kupanda ngazi kwenye mamlaka zingine hususan DAWASA, EWURA, Wizara ya Maji, Ofisi ya Rais na wadau wengine.

Tuendelee kushirikiana kila mmoja akichukua hatua kwa njia yake, maoni na ushauri pia unakaribishwa, wenye kutaka kuunganisha nguvu ya umma kupitia maandamano ya kuja kwa mbunge nao nawakaribisha; izingatiwe kuwa, maandamano yatayoratibiwa na ofisi ya mbunge kuwalenga wahusika wa juu zaidi yenyewe bado siku yake, tutafikia hatua hiyo iwapo serikali haitashughulikia kwa haraka masuala ambayo yanaweza kufanyika mwezi huu na kuonyesha kwa vitendo dhamira ya kutenga rasilimali za kutosha kwa mipango mingine inayoendelea kutekelezwa. Ni wakati wa mabadiliko ya kweli; tuwajibike. Maslahi ya Umma Kwanza, Twende Kazi.

Hatua nilizochukua kuhusu barabara ya Kibangu-Makoka na fidia ya Riverside

Nilichukua hatua kuhusu barabara Kibangu-Makoka na Januari nilikwenda Makuburi kuchangia matengenezo ya barabara husika , leo nimemweleza diwani kazi iharakishwe na kuhusu fidia ya wananchi wa Riverside Manispaa imenihakikishia kuwa italipwa mwezi Machi 2012; kesho nitakuwepo tena Makuburi kwa ajili ya kufuatilia masuala ya maji.

Kazi ya mbunge ni kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali. Kama sehemu ya wajibu huo nilitumiwa SMS na baadhi ya wananchi wa Kibangu na Makoka katika kata ya Makuburi kuhusu ubovu wa barabara ulioongezeka mara baada ya mafuriko ya mkoa wa Dar es salaam. Pamoja na kuwa barabara hii ni ya ngazi ya mitaa kwa maana ya halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, nilichukua hatua ya kuunganisha nguvu pamoja na diwani na wananchi kwa ujumla.

Izingatiwe kwamba kuhusu barabara hii nilitimiza wajibu wa uwakilishi baada ya kukutana na wananchi wa eneo husika mwaka 2010 na kunitaka niipe kipaumbele katika bajeti, kwa kushirikiana na diwani tulifanya hivyo na hatimaye barabara hii imetengewa fedha takribani milioni 100 kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo na Manispaa ya Kinondoni katika mwaka huu wa fedha 2011/2012.

Hata hivyo, baada ya kupokea malalamiko ya siku za karibuni nilifika tena tarehe 7 Januari 2012 na kufanya mkutano na wananchi katika shule ya msingi Mabibo/Makuburi kwa ajili ya kuanza harambee ya kuunganisha nguvu ya wananchi kufanya ukarabati wa dharura wakati ambapo matengenezo makubwa ya Manispaa yakisubiriwa.

Monday, February 27, 2012

Hatimaye Ujenzi wa Choo cha Kituo cha Mabasi Mbezi Luis Waanza

Jana tarehe 27 Februari 2012 nimefuatilia tena kwa mamlaka husika na kujulishwa kwamba tayari ujenzi wa choo na uzio umeshaanza na kwamba sasa unafanywa na fedha za umma toka TANROADS badala ya Manispaa ya Kinondoni.

Mtakumbuka kuwa mwezi Januari 2012 nilifuatilia kwa nyakati na namna mbalimbali kutaka ujenzi wa choo katika Kituo cha Daladala cha Mbezi Luis uharakishwe. Nimefanya hivyo pamoja na kutambua kwamba kituo husika kimejengwa katika eneo la hifadhi ya barabara (nitachukua hatua zingine kuhusu hili), kinaweza kutumika kwa miaka kadhaa kupunguza msongamano wa magari.

Kwa kuwa kazi ya mbunge ni kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali nilizihoji mamlaka husika ambazo ni TANROADS na Manispaa ya Kinondoni ambazo zilikuwa zirushiana mpira kuhusu ujenzi wa choo. Hatimaye nilijulishwa kupitia bodi ya barabara na RCC kuhusu choo kitajengwa na Manispaa ambayo haikuwa imetenga bajeti husika.

Nilikwenda katika kituo husika cha Mbezi kabla ya kwenda bungeni Januari na kutoa kauli ya kutaka ndani mwezi mmoja ujenzi uwe umeanza na iwapo usingeanza nilieleza kusudio la kuunganisha nguvu ya umma baada ya kutoka bungeni mwezi Februari ili kituo hicho kianze kutumika kupunguza msongamano hata kama choo kitakuwa hakijakamilika.

Nawashukuru wananchi mlioonyesha mwamko wa kufuatilia suala hili kwa karibu na wadau wote ndani na nje ya mamlaka husika mliochukua hatua; Maslahi ya Umma Kwanza.

Thursday, February 23, 2012

DAWASCO umekiuka mikataba; hatua za haraka zinahitajika kuboresha upatikanaji wa maji DSM

Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) imekiuka mikataba miwili muhimu inayoongoza kazi zake na kusababisha matatizo ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ikiwemo maeneo mbalimbali ya Jimbo la Ubungo.

Imenibidi nitoe taarifa hii kwa umma kwa nilitumia taratibu za kawaida za kiofisi tarehe 14 Februari 2012 kuiandikia barua DAWASCO kuchukua hatua kuhusu tatizo la kutozingatiwa kwa ratiba ya mgawo wa maji katika Jiji la Dar es salaam hali ambayo imesababisha kero ya maji katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Ubungo.

Hata hivyo DAWASCO haikujibu barua husika kueleza hatua ambazo imechukua, hivyo natoa mwito wa wazi wa siku tatu kwa DAWASCO kufanya ukaguzi wa mtandao wa maji na kurekebisha kasoro zilizopo na kutoa taarifa kwa umma kuhusu matitizo ya maji yanayoendelea katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo.

Kazi ya mbunge kwa mujibu wa katiba ni kuwawakilisha wananchi, kutunga sheria na kuisimamia serikali hivyo nakusudia kuchukua hatua zaidi za kibunge dhidi ya DAWASCO iwapo haitazingatia masharti ya mikataba husika na kushughulikia matatizo ya maji yanayoendelea hivi sasa katika jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo.

Ikumbukwe kuwa DAWASCO ni shirika la umma lililoundwa kwa tangazo la Serikali nambari 139 la tarehe 20 Mei 2005 kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1992.

Thursday, February 16, 2012

Kanuni za Uchaguzi wa Wabunge wa EAC zirekebishwe

Mihimili miwili ya nchi yaani bunge na serikali inapaswa kutoa uongozi thabiti wenye kuwezesha Tanzania kupata wabunge wanaokubalika na umma wa Bunge la Afrika Mashariki katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kwenye mkutano ujao wa bunge.

Ili kutimiza azma hiyo Spika wa Bunge Anna Makinda anapaswa kuwezesha marekebisho ya msingi ya kanuni zinazosimamia uchaguzi husika kabla ya katibu wa bunge kutoa tangazo la uchaguzi tajwa.

Aidha, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta anapaswa kutoa kwa umma na kwa vyama vya siasa muswada wa sheria ya uchaguzi wa Afrika Mashariki wa mwaka 2011 uliopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki ili uwe msingi wa marekebisho yanayopaswa kufanyika kabla ya uchaguzi husika kufanyika nchini.

Uchaguzi huu una umuhimu wa pekee kwa wananchi wa Tanzania ikiwemo wa Jimbo la Ubungo wakati huu ambapo jumuiya ya Afrika Mashariki ipo katika soko la pamoja na majadiliano ya kuwa na sarafu moja yanaendelea hali ambazo zina athari kwa nchi na wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Izingatiwe kuwa tarehe 10 Februari 2012 wakati wa kuahirishwa kwa mkutano wa sita wa Bunge Spika Makinda ametangaza kuwa uchaguzi wa wabunge wa kuwakilisha Tanzania kwenye bunge la Afrika Mashariki utafanyika katika mkutano wa saba wa Bunge unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 10 Aprili 2012.

Wednesday, February 15, 2012

Kuhusu Kauli za Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma

Kufuatia Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutangaza katika vyombo mbalimbali vya habari tarehe 15 Februari 2012 kwamba wameanza kuhakiki fomu za tamko la mali na madeni kwa baadhi ya viongozi tuliojaza fomu husika, mjadala umeibuka jimboni na katika jamii kuhusu suala hilo na baadhi mmeomba maoni yangu juu ya mchakato huo.

Umma ufahamu kuwa nilitimiza masharti ya kuwasilisha fomu kwa wakati na kutoa tamko kwa mujibu wa sheria, uhakiki ni utaratibu wa kawaida. Pamoja uhakiki, natoa mwito kwa Sekretariati kufanya uchunguzi juu ya viongozi wa umma wenye tuhuma mbalimbali ambao tumewataja kwa majina kwa nyakati mbalimbali. Aidha, kuhusu kufanya marekebisho ya sheria ya maadili ya umma kwa ajili ya kuweka mipaka kati ya biashara na siasa, sekretariati badala ya kurudia tena kufanya utafiti irejee kauli ya serikali bungeni kuwa waraka wa marekebisho ulishaandaliwa tayari na itoe mapendekezo kwa serikali yenye kuwezesha muswada kuwasilishwa katika mkutano ujao wa bunge.

Pamoja na uhakiki wa kawaida, sekretariati ifanye uchunguzi kwa watuhumiwa:

Ni vizuri ikazingatiwa kuwa nilitimiza masharti yanayotakiwa kwa mujibu kifungu cha 9 cha Sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995 ya kujaza fomu za tamko la mali na madeni na ni jambo la kawaida kwa sekretariati kufanya uhakiki wa fomu tajwa na kabla ya kuwa mbunge nimekuwa nikitoa mwito wa mara kwa mara kwa sekretariati kutimiza wajibu husika.

Ni muhimu sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma ikapanua wigo wa uhakiki iongeze orodha ya viongozi wa umma ili walau kwa mwaka iweze kuhakiki sampuli isiyopungua 10% ya viongozi wote wa umma na taarifa ya uhakiki huo iweke wazi kwa umma kuhusu wote wasiotangaza mali kwa mujibu wa sheria au ambao watabainika kutoa taarifa zenye kasoro.

Tuesday, February 14, 2012

DAWASCO kutozingatia ratiba ya mgawo wa maji

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ametoa mwito wa Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) kutoa taarifa kwa umma kuhusu kutozingatiwa kwa ratiba ya mgawo wa maji katika Jiji la Dar es salaam hali ambayo imesababisha kero ya maji katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Ubungo.

Mnyika ametoa mwito huo kupitia kwenye barua yake kwa DAWASCO aliyoiwasilisha leo tarehe 14 Februari 2012 na kutoa rai kwa madiwani wa CCM na CHADEMA katika Jimbo la Ubungo kuwasilisha taarifa za hali ya maji katika kata zao kufuatia malalamiko ya wananchi.

Itakumbukwa kwamba tarehe 5 mwezi Septemba 2011 Mbunge Mnyika alifanya mkutano na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO akiwa na baadhi ya wakazi wa kata mbalimbali kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Ubungo.

Kufuatia mkutano huo DAWASCO ilichukua hatua mbalimbali ambazo ziliboresha mgawo wa maji katika maeneo kadhaa ya Jimbo la Ubungo katika kipindi cha mwishoni mwezi Septamba mpaka katikati ya mwezi Disemba mwaka 2011.

Saturday, February 11, 2012

Nilitaka bunge likae kama kamati ya mipango kuchukua hatua za kunusuru uchumi na kupunguza mfumuko wa bei

Katika kuendelea kutimiza wajibu wa kuisimamia serikali kushughulikia uchaifu wa uchumi wa nchi yetu wa urari tenge kutokana na kuagiza bidhaa nyingi toka nje na upungufu katika uzalishaji na usambazaji wa ndani na kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi nilihoji uongozi wa serikali na bunge sababu za bunge kutokukaa kama kamati ya mipango kama kanuni za bunge zinavyohitaji na badala yake kufanyiwa semina ya hali ya uchumi tarehe 8 Februari 2012.

Nilieleza bayana kwamba matarajio yangu katika mkutano huu wa sita wa bunge ilikuwa ni serikali kuwasilisha bungeni mpango wa haraka wa kunusuru uchumi wa nchi, kupunguza mfumuko wa bei na kudhibiti kuporomoka kwa thamani ya shilingi yetu ukilinganisha na sarafu nyingine badala ya semina ya hali ya uchumi ambapo mada zinaweza zikatolewa na wabunge wakatoa maoni mazuri lakini yasiingizwe katika utekelezaji ya kiserikali na bajeti ya taifa.

Kanuni ya 94 ya Kanuni za Kudumu za Bunge inaelekeza “Ili kutekeleza majukumu yaliyoanishwa katika ibara ya 63(3) (c) ya katiba, Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango katika Mkutano wake wa Mwezi Februari ili kujadili na kushauri kuhusu mapendekezo ya Serikali katika mwaka wa fedha unaofuata”.

Pamoja na kuhoji ni lini mpango utaletwa na kujibiwa na Waziri wa Fedha Mustapha Mkullo na Spika wa Bunge Anna Makinda kuwa mpango utajadiliwa katika Mkutano wa Saba wa Bunge mwezi Aprili; nilitoa pia mawazo yangu kuhusu hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na serikali kwa haraka kupunguza mfumuko wa bei nchini na kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi hali ambayo ni tishio kwa uchumi na usalama wa nchi na maisha ya wananchi kwa ujumla.

Friday, February 10, 2012

Kutoka Bungeni: Sheria ya Katiba; Maji Ubungo na Kiwanda cha Urafiki

Kutoka Bungeni: Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba; Maji Jimboni Ubungo mitaa ya pembezoni na Hatma ya Kiwanda cha Nguo cha Urafiki

09/02/2012 nilichangia kwa maandishi muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2011; katika mchango wangu nilirejea pia msingi wa mapendekezo niliyoyatoa awali wakati wa kuwasilisha taarifa ya hoja binafsi kuhusu mchakato wa katiba mpya na uchambuzi niliofanya mara baada ya kuchapwa kwa muswada wa sheria husika kwa mara ya kwanza: http://mnyika.blogspot.com/2011/04/tamko-la-awali-kuhusu-muswada-wa.html. Nashukuru kwamba hatimaye harakati tulizoanza miaka mingi na zikapata msukumo mwezi Disemba 2010 ya kutaka mchakato wa katiba kuanzia bungeni kupitia kwa bunge kutunga sheria juu ya tume shirishi ya katiba, bunge maalum la katiba na hatimaye katiba kuhalalishwa kwa kura ya maoni zimepiga hatua nyingine kwa marekebisho ya sheria kuwasilishwa bungeni. Hata hivyo izingatiwe kuwa marekebisho ya sheria yaliyowasilishwa bungeni tarehe 09 Februari 2011 ni awamu ya kwanza, kuhusu tume na mchakato wa kukusanya maoni pamoja na kuandaa rasimu. Bado mabadiliko yanahitajika katika awamu ya pili na ya tatu; kuhusu bunge maalum la katiba na hatua ya kutunga katiba na kura ya maoni na mchakato wake kusimamiwa na tume ya uchaguzi. Katika mchango wangu nimeeleza pia kwamba bado kifungu cha 21 pamoja na adhabu kupunguzwa bado ziko juu; hivyo nimeendelea kutaka makosa yatenganishwa kati ya makosa ya kijinai ambayo yanaweza kuhukumiwa kwa kutumia sheria ya adhabu (penal code) na makosa ya kawaida katika mchakato wa kutoa elimu juu ya mabadiliko ya katiba na kukusanya maoni. Adhabu ya makosa ya kawaida inapaswa kuwa ndogo ya kawaida ili kutokufanya wananchi wapate hofu ya kushiriki kwa uhuru kwenye mchakato wa katiba na pia ili kulinda haki za msingi za kikatiba za kupata taarifa na kutoa maoni. Nasikitika kwamba sikuwepo jana jioni na leo asubuhi wakati bunge limekaa kama kamati kuhusu muswada husika kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu; hata hivyo kwa kuwa awamu nyingine zitafuata za marekebisho ya sheria husika, bado ipo nafasi ya kuendelea kufanya marekebisho mengine ya ziada.

Wednesday, February 8, 2012

Kutoka Bungeni: Hadhi ya Barabara DSM; mgomo wa madaktari ; Uchaguzi Afrika Mashariki; Sheria ya Fedha Haramu; utalii na ajira pori la Pande

Kutoka Bungeni: Hadhi ya Barabara DSM; mgomo wa madaktari ; Uchaguzi Afrika Mashariki; Sheria ya Fedha Haramu; utalii na ajira pori la Pande

Katika kuendelea kuwawakilisha wananchi nimeendelea kuisimamia serikali katika masuala yafuatayo:

Leo 08/02/2011 nimeulizwa swali la nyongeza kuhusu barabara za Dar es salaam kwa lengo la kuharakisha uboreshaji wa miundombinu ya pembezoni na kuchangia kupunguza foleni. Kwa muda mrefu kikwazo cha ujenzi wa barabara, madaraja na mifereji kimekuwa ni kiwango kidogo cha fedha ambacho TANROADS Mkoa wanatengewa. Nimetoa mfano wa mfereji wa Malapa Ilala Bungoni ulihitaji tu 2.3 Bilioni kukamilika lakini toka mwaka 2009 mpaka leo ujenzi bado unaendelea ukisuasua; nikata Wizara ya Ujenzi ieleze ni lini barabara za Dar es salaam zitapandishwa hadhi kwa orodha ambayo tulishawasilisha serikalini miaka kadhaa iliyopita ili ziongezewe bajeti ujenzi uweze kuharakishwa? Waziri Magufuli amekiri kweli fedha zilikuwa zikitengwa kidogo, amekubali kuwa ameshapokea orodha ya barabara husika na ameahidi kwamba wataalamu wake wanazipitia na karibuni atatoa taarifa ya barabara zilizopandishwa hadhi. (Swali hili nimeuliza kufuatilia masuala niliyowahi kuyazungumza hapa: http://mnyika.blogspot.com/2012/01/kuhusu-msongamano-wa-magari-dsm-na.html

Aidha, nimeandika barua kwa Spika kuhusu mgomo wa madaktari kama ambavyo mlishauri jana nilipoandika ujumbe huu: http://mnyika.blogspot.com/2012/02/mgomo-wa-madaktari-bungeni-tena-leo.html; kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge cha dharura kinaendelea hivi; nimeshauri hayo mapendekezo saba niliyoyatoa kwenye hiyo barua yazingatiwe na bunge litoe taarifa ya haraka kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa mpaka sasa. Aidha, nimetoa mwito kwa Rais kuweza kutaarifiwa naye kuweza kuingilia kati kwa mujibu wa mamlaka yake ya kikatiba ya kwenye ibara ya 34 na 35.

Tuesday, February 7, 2012

Mgomo wa Madaktari bungeni tena leo; nilitaka hatua hizi zichukuliwe

Leo Mbunge wa Mbozi Geofrey Zambi alitoa hoja ya bunge kujadili suala la mgomo wa madaktari kwa dharura kufuatia taarifa kuwa madaktari bingwa nao wameingia kwenye mgomo. Spika Anna Makinda alizuia hoja hiyo kwa maelezo kuwa suala hilo bado linashughulikiwa na bunge kupitia kamati yake ya huduma za jamii. Baada ya maelezo ya Spika niliomba muongozo hata hivyo sikupatiwa nafasi.

Kimsingi nilitaka kuelieza bunge kwamba maelekezo yaliyotolewa na Naibu Spika Job Ndugai yanahitaji kuongezewa maagizo ya ziada na Bunge ili wadau wote wakawa na imani kwamba suala hili linashughulikia kwa dharura na kwa mwelekeo stahiki hali ambayo itashawishi mgomo kuweza kusitishwa.

Hadidu rejea na ratiba ya kamati inapaswa iwe bayana hivyo kuna umuhimu wa uongozi wa bunge kutoa tamko lenye maelezo ya ziada kwa kuwa kimsingi madaktari walishapoteza imani na namna ambavyo serikali kupitia kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikishughulikia masuala yao.

Aidha, imani hiyo ilipoteza zaidi baada ya uamuzi wa Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii kutoa maelezo yasiyokuwa ya kweli bungeni kuhusu madai ya madaktari na hali ya mgogoro mzima. Bunge na uongozi wa bunge unapaswa kuwa makini katika mazingira ya sasa ili kuepusha uwezekano wa madaktari na wananchi kwa ujumla kupunguza imani pia na namna ambavyo mgogoro huu unashughulikiwa.

Sunday, February 5, 2012

Kutoka Bungeni: Sheria ya Fedha Haramu; vyama vya siasa na tishio kwa mamlaka ya Bunge

Nashukuru wote waliounga mkono marekebisho niliyowasilisha tarehe 03/02/2012 kwenye sheria (The Anti Money Laundering (Amendments Act) 2012 ya kumwingiza msajili wa vyama vya siasa kuwa sehemu ya wadhibiti wa masuala ya fedha haramu. Kwa upande mwingine, nawashukuru wote waliotikia NDIYO (kwa kujua au kutokujua) kuunga mkono marekebisho mengine ambayo niliyawasilisha katika sheria husika ya kuongeza ukubwa wa adhabu kutoka na makosa ya ujumla ya kukiuka Sheria ya Udhibiti wa Fedha haramu.

Katika kuwasilisha hoja hiyo ya marekebisho nilifanya rejea katika Ripoti ya Utafiti ya Juni mwaka 2011 iitwayo “The Political Economy of the Investment Climate in Tanzania” iliyotolewa na “Africa Power and Politics”, ripoti ambayo imefanya rejea pia ya masuala ambayo vyama vya siasa hususan CHADEMA, vyombo vya habari na asasi za kiraia nchini kwa nyakati mbalimbali viliyaibua kuhusu fedha haramu katika siasa nchini hasa wakati wa uchaguzi uliofanywa na CCM na wagombea wake.

Katika hoja hiyo nilisisitiza kuwa tatizo la dola kutekwa (state capture) lina athari kubwa zaidi kwa nchi na maisha ya wananchi hivyo udhibiti wa fedha haramu kwenye kuingiza viongozi madarakani ni suala la muhimu ili kuepusha baadhi ya vyama kama ilivyokuwa kwa CCM kutumia fedha za kifisadi kama za EPA-Kagoda, Deep Green, Tangold na Meremeta katika uchaguzi.

Nilisema kwamba kumuingiza msajili wa vyama vya siasa ambaye amepewa mamlaka ya kudhibiti matumizi ya fedha katika vyama vya siasa, viongozi wake na wagombea wake nyakati zote ikiwemo katika uchaguzi itaongeza nguvu katika utekelezaji wa sheria ya udhibiti wa fedha haramu. Nilifanya hivyo kwa kurejea Election Expenses Act 2010 (Kifungu 4 na 5) na The Political Parties Acti no. 5 ya 1992 (Kifungu cha 13 na 14).

Kutoka Bungeni: Mgomo wa Madaktari; bado hakijaeleweka

Nashukuru kwamba walau tofauti na tarehe 02/02/2012 ambapo Naibu Spika Ndugai alipotosha muongozo nilioomba akadai kuwa ni hoja isiyoungwa mkono na kuipuuza; tarehe 03/02/2012 amezingatia muongozo nilioomba na kutoa mwelekeo ambao umeongeza msukumo katika bunge kufanya kazi yake ya kuisimamia serikali.

Hata hivyo, bado muongozo uliotolewa haujitoshelezi kwa kuwa jukumu hilo kwa kamati ya huduma za bunge halikuelezwa bayana limeanza lini na litamalizika lini. Vyanzo kadhaa vimeeleza kwamba taarifa ya kamati husika itawasilishwa kwenye mkutano ujao wa bunge (Mkutano wa Saba), suala ambalo halipaswi kukubaliwa. Kutokana na uzito na udharura wa mgogoro huu ni muhimu taarifa ya awali ya kamati iliyopewa jukumu ikawasilishwa katika mkutano huu wa sita unaoendelea ili hatua za haraka zikachukuliwa katika kushughulikia madai ya madaktari na kupata taarifa ya kweli kuhusu athari za mgogoro na mgomo ulioendelea ikiwemo vifo vilivyotokea.

Aidha, Kamati husika ingepewa hadidu rejea za wazi ikiwemo ya kufanya kazi ya usulushi na upatanishi katika mgogoro ambao umetokea baina ya madaktari na serikali na pia kuwezesha bunge kusimamia ipasavyo na kwa haraka serikali katika kushughulikia madai ya wafanyakazi.

Kwa upande mwingine, kwa kuwa imebainika wazi kwamba kuna uzembe na udhaifu miongozi mwa watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakiongozwa na Waziri wa Wizara husika ambaye amefikia hatua hata ya kutoa taarifa ya kulidanganya bunge; ni vizuri baada ya Kamati husika kusikiliza pande zote mbili Waziri na watendaji husika walazimishwe kujiuzulu ili hatua za kushughulikia madai ya madaktari na kuboresha huduma za afya katika hospitali za umma zitekelezwe na wateule wengine wenye uwezo na dhamira ya kweli ya kushughulikia matatizo yaliyojitokeza.

Thursday, February 2, 2012

BUNGENI LEO: Mgomo wa madaktari na Sheria ya Bodi ya Mikopo

Asubuhi ya leo Naibu Spika Job Ndugai alitumia kanuni vibaya kuzuia hoja ya dharura bungeni kuhusu mgomo wa madaktari. Kimsingi, sikuwasilisha hoja ila niliomba muongozo wa Spika ili niweze kupatiwa nafasi ya kuwasilisha hoja ya dharura. Kwa kuwa hoja kama hiyo iliwasilishwa juzi na ikaungwa mkono lakini Spika akasema ameshakubaliana na serikali kuwa ingewasilisha kauli. Hata hivyo, jana hakukuwa na kauli ya serikali huku wananchi wakiendelea kupata madhara ya mgomo. Hivyo nikata muongozo kwa kuwa Spika alitumia kanuni ya 49 (2) ambayo kimsingi inatoa mwanya kwa kauli ya serikali kuwasilishwa kwenye wakati atakaoona yeye kuwa na unafaa juu ya jambo linaihusu serikali na lisilozua mjadala. Nilitaka kanuni hiyo isitumike badala yake wabunge tutimize wajibu wa kuisimamia serikali kwa kutumia kanuni ya 47 kuhusu hoja ya dharura. Kwa kuwa ilikuwa muongozo hakukuwa na hitaji la kikanuni la wabunge wengine kuunga mkono lakini akaamua kuilinda serikali kwa kuwa hawakuwa wamejiandaa. Lakini mwishoni ameahidi kuwa kauli ya serikali itatolewa kesho.

Jioni ya leo bunge litajadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali na.2 wa mwaka 2011 ambao kwa sehemu kubwa ukiondoa sheria nyingine unahusu marekebisho ya kimsingi katika sheria ya bodi ya mikopo. Ni kwa bahati mbaya kwamba muswada huu umeletwa na hoja ya kusomwa kwa hatua zake zote tatu katika mkutano mmoja hivyo hakutakuwa na muda wa kukusanya maoni ya wadau kwa upana wake. Ni sehemu ndogo sana ya vifungu vya muswada huu ndio inapaswa kukubalika lakini kwa ujumla muswada huu unakwenda kuingiza mambo ambayo tuliyapinga kwa makongamano, migomo na maandamano yakaondolewa wakati sheria husika inatungwa mwaka 2004. Maudhui ya muswada huu yamenifanya nikumbuke makala ambayo niliandika mwezi kama huu lakini mwaka 2007: http://www.chadema.or.tz/makala/makala.php?id=43 Marekebisho haya yanaenda kuweka mazingira mengine ya migogoro katika elimu ya juu nchini kutokana na masuala ya mikopo kwa wanafunzi. Muswada huu ulipaswa kuja bungeni baada ya ripoti ya Tume ya Rais iliyoundwa tarehe 14 Februari 2011 na kukabidhi taarifa yake tarehe 29 Aprili yenye mapendekezo ya jinsi ya kuboresha utaratibu wa sasa wa ugharamiaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu kuwekwa wazi kwa bunge na kwa umma ili kufanya marekebisho mapana zaidi ya kimfumo.