Thursday, June 14, 2012

PUMZIKA KWA AMANI MZEE WETU BOB MAKANI



WASIFU WA MZEE MAKANI

Hayati Bob Nyanga Makani alizaliwa mwaka 1936 katika Hospitali ya Kolandoto, Shinyanga.  Alikuwa ni mmoja wa watoto wengi katika familia ya Mzee Makani.
Alipokuwa na umri wa miaka sita, alianza masomo yake kwenye shule ya Msingi Ibadakuli, Shinyanga. Kama ilivyokuwa kawaida ya Serikali ya Mkoloni Muingereza hapa Tanzania wakati huo, watoto wa Machifu walipelekwa kusoma Shule ya Sekondari Tabora, ndivyo ilivyokuwa kwa Hayati Bob pia.
Kutokana na uhodari wake katika masomo, Mheshimiwa Bob Makani  alifaulu na kupelekwa Chuo Kikuu Cha Makerere, wakati huo kikiwa ni Chuo Kikuu cha pekee Afrika Mashariki, ambako alifuzu na kupata Shahada ya Kwanza katika Uchumi  (BA Economics).
Hakuridhika na shahada hiyo. Mwaka wa 1961 alikwenda Chuo Kikuu cha Liverpool, nchini Uingereza na 1965 akatunukiwa Shahada ya Sheria (LLB). Kwa mujibu wa Sheria za Uingereza, anayehitimu Shahada ya Sheria ni lazima vilevile apasi mitihani ya Sheria kwenye Middle Temple, London, Uingereza na Mheshimiwa Bob Makani alifanikisha hiyo mwaka huo huo na kurejea nyumbani Tanzania.
Aliporudi Tanzania aliajiriwa na Serikali kama Mwanasheria wa Serikali kwa muda mfupi kabla hajapandishwa cheo na kuwa Exchange Control Manager wa Benki Kuu.
Hapo ndipo alipokutana na kuwa karibu na Mhe. Edwin Mtei aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu wakati huo.  Ndiyo maana haikuwa ajabu lilipoanza vuguvugu la siasa za mabadiliko nchini mwaka 1966, Mhe. Makani na Mhe. Edwin Mtei walikuwa pamoja.
Mwaka wa 1992 mfumo wa vyama vingi vya siasa ulipokubaliwa rasmi nchini, Mhe. Bob Makani na Mhe. Edwin Mtei walikuwa mstari wa mbele kwenye uundwaji wa chama cha siasa.    Mwaka huo Mhe. Bob Makani alistaafu kazi yake ya Unaibu Gavana wa Benki Kuu ili aweze kuelekeza shughuli zake zote kwenye uanzishaji wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mheshimiwa Bob Makani ni mwasisi wa CHADEMA na ana kadi ya Chama Namba tatu baada tu ya Mhe. Edwin Mtei, No. I na Marehemu Brown Ngilulupi Kadi No. 2.
Tangu mwanzo kabisa, CHADEMA kilifaidi mengi kwa utumishi uliotukuka toka kwake Bob Makani.  Kwanza kabisa, CHADEMA kilifaidika na utaalam wake wa Sheria ambao pamoja na busara zake zilikisaidia chama kutengeneza Katiba na taratibu za Uongozi/Administrative Structure) ambayo hadi sasa ni msingi wa aina ya uongozi tuliojenga ndani ya CHADEMA.
Jambo la pili ni kuwa Mhe. Bob Makani kwanza kwa asili na pili kwa maumbile yake, alikuwa mtu wa watu.   Ijapo ameshika vyeo vikubwa ndani ya Serikali, Bob alikuwa na kipaji cha kuwaelewa wananchi na kuungana nao katika kutafuta ubora wa maisha kwa ujumla.  Urefu aliomjalia Mwenyezi Mungu, ulihakikisha anaonekana!  Hali kadhalika, kwa ucheshi wake.  Alisikika na kueleweka.
Ni kwa kutambua uwezo na vipaji vyote hivi, ndiyo maana hapo hapo kwenye kikao cha Mkutano Mkuu wa kwanza wa CHADEMA Desemba 1991, ndipo Mhe. Bob Makani akachaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa CHADEMA.
Hali kadhalika, kutokana na usemi uliopo kuwa KAZI NGUMU MPE MSUKUMA, Chama nacho hakikuchelewa kumpa Bob Makani kazi ngumu ya kueneza Chama kipya Tanzania nzima.
Mhe. Bob Makani alipewa kazi maalum ya kukipeleka chama mikoa ya Morogoro, Kigoma, Tabora, Singida, Mwanza na Rukwa.  Hapa ikumbukwe kuwa wakati huo, kuanzisha chama kipya ilionekana kama ni uasi au uhaini na kwenye mikutano mingi ya hadhara kwenye mikoa hiyo, alipokelewa kwa matusi na mara nyingine matusi na mawe.
Kwenye mazingira haya magumu na ikizingatiwa kuwa chama hakikuwa na ruzuku, alitumia rasilimali zake bila uchoyo ili kukijenga kile alichokiamini kuwa ni chombo cha ukombozi wa wananchi kwa ajili ya maendeleo ya watu.
Sisi tuliopo CHADEMA leo, tunajua na kuamini kuwa tokana na ujasiri wa uongozi wa Mhe. Bob Makani kama Katibu Mkuu wa kwanza wa chama, ndipo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliweza kutamka wazi kuwa CHADEMA ndicho chama pekee cha upinzani alichoona kina sera na mwelekeo sahihi. Akakitumia kama mfano wa kukiasa chama chake, CCM kuiga utengenezaji wa sera zinazoweza kutekelezwa.
Mwaka wa 1998, Mhe. Bob Makani akachaguliwa kuwa Mwenyekiti Taifa wa CHADEMA, wadhifa alioshika hadi 2003 alipomaliza muda wake na wakati huo akaendelea na kazi zake kama mwanasheria wa kujitegemea lakini akibaki kuwa kiongozi na mshauri wa chama hadi kifo kilipomfikia.
Katika uhai wake Mhe. Bob Makani tokana na uadilifu na utaalam wake aliteuliwa kushika nafasi nyingi za uongozi zikiwemo:-
1.Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ndege Tanzania.
2.Mkurugenzi wa Bodi ya Williamson Diamonds
3.Mkurugenzi Bodi ya Tanzania Breweries
4.Mkurugenzi Bodi ya Benki ya Taifa ya Biashara
5.Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Law Society
Marehemu alianza kusumbuliwa na uogonjwa wa moyo tangu 2009.   Mwaka uliofuata 2010 alipelekwa India kwa matibabu na alipata nafuu kwa muda.  Mwaka huu, Bob Makani alipelekwa Nairobi kwa Operation ndogo lakini baada ya hapo hakuweza kuendelea na kazi.
Mnamo saa za jioni tarehe 9 Juni alizidiwa na kukimbizwa Hospitali ya Aghakhan ambapo alifariki saa saba usiku.  Marehemu ameacha wajane, watoto saba na wajukuu wanane.
Mwenyezi Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya Marehemu Bob Nyanga Makani.
AMINA.
 

No comments: