Monday, June 11, 2012

HATUA NILIZOCHOKUWA DHIDI YA WIZARA YA MAJI

Kufuatia Wizara ya Maji kukaa kimya bila kujibu barua toka Ofisi ya Mbunge kwa zaidi ya mwaka mmoja, nimeamua kuchukua hatua za kibunge kwa kuwasilisha kwa Katibu wa Bunge, taarifa na maelezo ya hoja binafsi kutaka Bunge, katika mkutano unaotarajiwa kuanza tarehe 12 Juni 2012, lipitishe  aazimio ya kuwezesha uwajibikaji wa Wizara husika na mamlaka zake katika kushughulikia masuala ambayo nimeyaeleza
katika hoja husika.

Ikumbukwe kwamba, tarehe 20 Mei 2012 nilitoa mwito kwa Waziri Profesa Jumanne Maghembe kuueleza umma hatua saba za haraka zaidi za Wizara ya Maji kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam mara baada ya Waziri kurejea ofisini kutoka katika ziara hiyo ya vyanzo vya ruvu juu na ruvu chini na kufanya mikutano na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka

(DAWASA) pamoja na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO).

Nilichukua hatua ya kutoa taarifa kwa umma baada ya Wizara kuwa na utendaji mbovu wa kutojibu barua ambapo katika kipindi cha kati ya mwaka 2011 mpaka 2012 nimeandika jumla ya barua nne kwa Wizara husika kwa niaba ya wananchi kwa nyakati mbalimbali bila kupata majibu yoyote.


Katika ya hatua hizo ambazo Waziri nilieleza anapaswa kuzisimamia katika Wizara ya Maji ni; Mosi, kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya kashfa ya taifa ya kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 ambapo Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji.


Pili; kuwasilisha bungeni Mpango Maalum wa kuboresha huduma za Majisafi na uondoaji wa Maji Taka katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 kwa ajili ya kuidhinishwa, kutengewa bajeti kamili ya utekelezaji wa haraka katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kusimamiwa ipasavyo kwa msukumo wa kibunge badala ya ahadi za ujumla za kwenye ziara.

Tatu; Waziri kueleza hatua zilizopangwa kuchukuliwa kufuatia ziara yake kuhakikisha Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 unawekewa muda wa ukomo wa kukamilika ndani ya miezi mitatu katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa.

Nne; Waziri kukubaliana na pendekezo nililotoa bungeni kwa nyakati mbalimbali la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa thamani ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.


Tano; Waziri kuhakikisha Wizara ya Maji inaisimamia EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa
DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali. Aidha, Wizara ya Maji ihakikishe EWURA inaharakisha kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es Salaam.

Sita; Waziri kuwezesha Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on the management of water
distribution in urban areas) ya Januari 2012 iliyotolewa na CAG kabla ya mkutano wa nane wa bunge ulipangwa kuanza tarehe 12 Juni 2012 ili maoni na mapendekezo yazingatiwe wakati wa mchakato wa bajeti.

Saba; Wizara ya Maji kuhakikisha Serikali inawasilisha kwenye mkutano wa tisa wa bunge muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka (Water Supply and Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili kushughulikia upungufu uliojitokeza katika
utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.
Imetolewa Dar es salaam tarehe 8 Juni 2012 na:

John Mnyika

Mbunge wa Jimbo la Ubungo

No comments: