Gazeti la Majira la tarehe 21 Juni 2012 limebeba kichwa cha habari “Siri ya kukataa bajeti yafichuka: Yadaiwa hilo ni shinikizo la nchi za magharibi; lengo ni kupora gesi, mafuta na madini ya urani”:
Nilipotolewa bungeni tarehe 19 Juni 2012 nilieleza kwamba nitatoa tamko la kina ya sababu za kutoa kauli bungeni kuwa “tumefika hapa kwa sababu ya udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa Bunge na upuuzi wa CCM”; nimeacha mpaka sasa kutoa tamko kuwapa nafasi Rais Kikwete, Wabunge na CCM watafakari mchango niliotoa bungeni na kuchukua hatua zinazostahili za kuondoa bajeti na kuwezesha marekebisho ya msingi.
Wakati nikisubiri hatua hizo amenukuliwa tarehe 21 Juni 2012 Mbunge wa Iramba Magharibi Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM akitoa madai ya uongo ambayo yanaendelea kudhihirisha kile nilichokieleza bungeni; hivyo katika muktadha huo iwapo Rais Kikwete na Bunge halitarekebisha udhaifu uliojitokeza nitaendelea kuungana na wabunge wengine wa upinzani kukataa bajeti na kuchukua hatua zaidi na kutoa tamko la kina siku chache zijazo.
Kwa sasa nieleze tu kuwa Nchemba anapaswa kuyataja kwa majina hayo mataifa ya magharibi na kuwataja kwa majina wabunge na wanasiasa anaodai wamewezeshwa kifedha ili kukataa bajeti kuwezesha kuporwa kwa gesi, mafuta na madini ya urani. Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe anapaswa kutoa kauli kwa umma iwapo maneno hayo ya uzushi ndio msimamo wa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na CCM.
Wananchi ambao wametutuma wabunge kuikataa bajeti wanajua kwamba bajeti hii inakataliwa kwa kutokuweka misingi ya kutimiza ahadi ya Rais Kikwete na CCM ya maisha bora kwa kila mtanzania na badala yake kuongeza ugumu wa maisha kutokana na kushindwa kukabiliana na matatizo ya mfumuko wa bei.
Aidha, wabunge tumekubaliana na maoni ya kambi ya upinzani ya kuikataa bajeti kwa kuwa imeshindwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao ulipitishwa kwa azimio la bunge ambao ulipaswa kuiongoza serikali kuweka mkazo katika kuendeleza nchi kwa kutumia fedha za ndani. Nikinukuu ukurasa wa 92 kifungu cha 4.3.1 “Kwa kuelewa kuwa wakati wote kutakuwa na miradi ya uwekezaji nje ya mpango, serikali kuanzia sasa itakuwa inatenga asilimia 35 ya makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo kila mwaka”. Wabunge tunayakataa makadirio ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kwa sababu Serikali imetenga asilimia sifuri ya mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo.
Ndio maana katika mchango wangu bungeni tarehe 19 Juni 2012 kabla ya kutolewa bungeni nilieleza kwamba nakataa bajeti kwa kuwa bajeti haikuweka vipaumbele vya msingi vya maendeleo ya wananchi na nikataja mifano ya masuala ambayo wananchi wa Ubungo walionituma kuwawakilisha ya kutaka fedha za kutosha kutengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya maji na barabara za pembezoni za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es salaam. Katika mchango huo ambao unaweza kurejewa katika taarifa rasmi za bunge (Hansard) nilieleza namna ambavyo bajeti iliyowasilishwa haitekelezi ilani ya CCM kwa ukamilifu wala kutenga viwango vya fedha kama ilivyotakiwa na mpango wa taifa wa miaka mitano.
Miradi hiyo ya Ubungo na Dar es salaam kwa ujumla ya maji na barabara ilipitishwa na baraza la mawaziri ili kutengewa fedha Mwenyekiti akiwa Rais Kikwete na ilitokana na ahadi za Rais Kikwete lakini haijatengewa fedha za kutosha huku bajeti ikiwa na matumizi mengi ya kawaida yasiyokuwa ya lazima ambayo yangeweza kupunguzwa na kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo. Badala ya Nchemba kufanya propaganda chafu alipaswa kumshauri Rais Kikwete na CCM kutekeleza ahadi na kutimiza wajibu ipasavyo kwa kuiondoa bajeti na kuirejesha baada ya kuifanyia marekebisho ya msingi ili isikataliwe.
Nchemba anapaswa kufahamu kwamba wabunge wa upinzani kabla na hata katika bunge la kumi tumekuwa tukiungana pamoja kupinga ufisadi na kutetea rasilimali za taifa ambazo Serikali ya CCM kwa muda mrefu imeachia zimeporwa na mataifa na makampuni ya kigeni kwa madai ya uwekezaji kutoka nje. Nchemba ni vyema tu akarejea uchambuzi wa wasemaji wa kambi rasmi ya upinzani kuhusu udhaifu wa kisera na kisheria pamoja na mikataba mibovu ambayo inalikosesha taifa mapato kwenye gesi, mafuta na madini ambao umetolewa kwa nyakati mbalimbali.
Hivyo, Serikali isipotoa kauli ya kukubaliana na maoni ya kambi rasmi ya upinzani tuliyoyatoa tarehe 15 Julai 2011 wakati wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013; katika masuala ya gesi, mafuta na madini kwa nafasi yangu ya uwaziri kivuli wa Nishati na Madini nitatumia njia za kibunge katika mkutano huu wa nane wa bunge unaoendelea kusimamia uwajibikaji kwa maslahi ya umma. Nchemba anapaswa kufahamu kwamba kutokana na udhaifu uliopo hivi sasa, Tanzania haina sheria ya gesi asili huku uvunaji wa rasilimali hiyo ukiendelea kiholela na ufisadi uliobainika na kuanikwa hata bungeni mpaka sasa haujashughulikiwa.
Madai ya Nchemba kuwa wabunge wameshiriki kuandaa bajeti katika hatua ya kamati hivyo hawana uhalali wa kuipinga bungeni hayana ukweli wowote kwa kuwa kwenye kamati wabunge hujadili bajeti za Wizara za kamati husika; bajeti kuu hupelekwa baadaye kwa mujibu wa kanuni ya 96 ya Kanuni za Kudumu za Bunge ambayo hata yenyewe kwa mwaka huu haikutekelezwa ipasavyo.
Aidha, ifahamike kwamba wabunge tulikoseshwa fursa ya kutumia ipasavyo mamlaka ya kibunge ya Ibara ya 63 ya katiba ya kuishauri na kuisimamia serikali katika kupanga mipango ya maendeleo kutokana na kanuni ya 94 ya bunge kutokuzingatiwa ambayo ilitaka bunge likae kama kamati ya mipango katika mkutano wa Bunge wa Mwezi Februari kutoa mapendekezo ya vipaumbele na hivyo kufanya mpango huo kujadiliwa hivi sasa wakati mapendekezo ya bajeti yameshaandaliwa bila kuzingatia mpango wa taifa wa miaka mitano.
Wakati nilipohoji kuhusu suala hilo miezi ya Februrari, Machi na Aprili Nchemba hakuwahi kuunga mkono wala kuishauri CCM na serikali kuzingatia hatua muhimu za upangaji wa bajeti ambazo zingeepusha bajeti kukataliwa katika hatua ya mwisho kwa kutokidhi matakwa ya umma.
Kauli ya Nchemba ya kwamba wabunge wa upinzani tunataka kuikwamisha bajeti ili bunge livunjwe twende kwenye uchaguzi imedhihirisha tahadhari niliyoitoa ya kwamba wananchi wasitarajie wabunge wa CCM kuikataa bajeti kwa kuwa ubovu wa katiba ibara ya 90 umetoa mamlaka makubwa kwa Rais ya kulivunja bunge, na kwamba wabunge wengi wa CCM wana hofu juu ya uchaguzi kurudiwa hivyo wataipitisha bajeti kwa kura ya NDIYO hata kama inaongoza ugumu wa maisha kwa wananchi na haiwezeshi utekelezaji wa haraka wa miradi ya maendeleo. Hivyo, suluhisho katika hali hiyo kabla ya mabadiliko ya katiba ni Rais kuondoa udhaifu na kutumia nguvu kubwa aliyonayo kwa mujibu wa katiba kuiondoa bajeti na kuirejesha ikiwa imefanyiwa marekebisho makubwa kwa kuzingatia michango ya wabunge na maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni.
John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
Bungeni-Dodoma (21/06/2012)
No comments:
Post a Comment