Wednesday, September 19, 2012

Hatimaye ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Maziwa mpaka External pamoja na daraja unaanza!!


Tayari taratibu za zabuni zimeshakamilika na mkandarasi anapaswa kuanza ujenzi. Manispaa ya Kinondoni imeshaweka alama ya "X" katika majengo ambayo yatapaswa kubomolewa kuwezesha upanuzi wa barabara husika unaofanywa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Dar es salaam (TANROADS).

Tarehe 15 Septemba 2012 nilifanya mkutano wa hadhara Jimboni Ubungo kwenye kata ya Makuburi ambapo pamoja na maswali mengine niliulizwa ni lini ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami kutoka Maziwa mpaka External ukiambatana na ujenzi wa daraja katika barabara husika utaanza.

Pamoja na kueleza hatua iliyofikiwa mpaka sasa nilitoa mwito wananchi wote ambayo makazi yao yamewekewa alama ya "X" ikiwa si wavamizi wa barabara wawasilishe kwa Manispaa ya Kinondoni maelezo na vielelezo vyao kwa kuzingatia Wakala wa Barabara Mkoa wa Dar es es salaam (TANROADS) wao wana bajeti ya ujenzi pekee na madai ya fidia kwa wenye uhalali yako chini ya Manispaa ya Kinondoni; tayari 17 Septemba 2012 baadhi ya wananchi wamewasilisha nyaraka zao.

Ikumbukwe pia kuwa kwa kutambua umuhimu wa suala hili nilichukua hatua mbalimbali za kibunge kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2011 ili barabara husika iweze kupandishwa hadhi na kujengwa kwa kiwango cha lami kwa haraka zaidi kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kuliko ilivyopangwa awali.

Niliziandikia mamlaka husika hususan Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuzingatia barabara tajwa katika bajeti kwa lengo la kuchangia katika kupunguza msongamano, Wizara ya Ujenzi awali ilisema serikali kuu haiwezi kushughulikia barabara hiyo kwa kuwa iko chini ya Manispaa ya Kinondoni. Lakini, nikaendelea kuchukua hatua zaidi kwa njia za kibunge na za uwakilishi wa wananchi na hatimaye TANROADS ikaingiza barabara hiyo katika vipaumbele vyake na kutenga fedha za ujenzi wa kiwango cha lami kiasi cha shilingi bilioni 1.2.

Aidha, pamoja na kiwango hicho cha fedha kilichotengwa na TANROADS, tarehe 5 Machi 2012 Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alieleza kuwa amewasilisha maombi mengine kupitia Mfuko wa Barabara (Road Fund) kwa ajili ya ujenzi wa  daraja kubwa zaidi katika barabara hiyo kwenye eneo la Ubungo Kisiwani/External suala ambalo pia kwa nyakati mbalimbali nilihoji utekelezaji wake.

Izingatiwe kwamba tarehe 21 Machi 2012 niliunganisha wananchi kuchangia hatua za dharura za kufanya matengenezo ili kupunguza kero lakini nikasisitza kuwa suluhisho muhimu zaidi ni kupanua daraja la External katika Eneo la Ubungo Kisiwani ili kupunguza msongamano wa magari na kujenga barabara husika kwa kiwango cha lami hatua ambayo sasa inaelekea kuchukuliwa kwa haraka.

John Mnyika (Mb)
18 Septemba, 2012

4 comments:

Anonymous said...

Safi sana mbunge wetu.
Kazi yako tunaiamini na matokeo mazuri yameanza kuonekana.

Anonymous said...

Safi sana mbunge wetu, tunategea kuona utekelezaji mzuri

Anonymous said...

Safi sana mbunge wetu, tunategea kuona utekelezaji mzuri. C. Kanyala

Anonymous said...

Safi mheshimiwa lakini vipi kuhusu barabara ya Mbezi mwisho mpaka Tanki Bovu na Kimara Temboni mpaka Wazo Hill na Goba mpaka Makongo juu kwa kiwango cha lami?