MBUNGE wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, amelitaka Jeshi la Polisi kushirikiana na wananchi katika kuwafichua majambazi ambao wamekithiri katika maeneo mengi jiji la Dar es Salaam.
Mnyika alitoa kauli hiyo baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti matukio ya ujambazi yaliyokuwa yakifanywa katika eneo la Kimara hivi karibuni ambayo yamezidi kushamiri bila mafanikio; mbunge huyo amelitaka jeshi hilo kuweka nguvu kazi katika maeneo hayo ili kunusuru mali za wananchi pamoja na maisha yao.
Mnyika aliyekuwa katika kikao na wananchi wa kata ya Saranga jana alipokea malalamiko na kero hiyo ambayo imeshindwa kutatuliwa jambo linalohatarisha maisha kutokana na eneo hilo kukumbwa na matukio ya ujambazi kila mara kwa kutokuwa na ulinzi.
Mnyika alimtaka kamanda wa mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, kuchunguza kwa kina sababu za kuwepo kwa ujambazi wa mara kwa mara katika maeneo hayo unaohusisha matumizi ya silaha za moto kwani kumekuwepo na tuhuma za polisi kupokea rushwa kutoka kwa majambazi hao jambo linalosababisha hali hiyo izidi kuendelea.
Mnyika alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa kata ya Kimara kwa kuunga mkono jitihada za kuboresha kituo cha polisi cha Temboni na kujitolea pikipiki mbili, ‘radio call’ na upanuzi wa kituo pamoja na kuendesha harambee kwa ajili ya ujenzi wa choo katika kituo cha polisi ambapo sh 800,000 zilipatikana na ahadi ya mifuko 12 ya saruji ilitolewa.
Wakati huo kamanda polisi wa mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela alitoa wito kwa wananchi kuweka mazingira bora ya ulinzi na usalama kwenye makazi yao ikiwemo kujiandaa na majanga huku polisi wakijitahidi kuweka mikakati ya kuongeza nguvu katika eneo hilo.
Chanzo: Tanzania Daima (Disemba 2010)
No comments:
Post a Comment