Katika hatua nyingine, Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika ambaye amedokeza kusudio lake la kuwasilisha hoja bungeni katika mkutano wake wa Februari, mwakani, ili liweke utaratibu wa kuanzishwa, kuratibiwa na kusimamiwa kwa mchakato wa katiba mpya kwa kuzingatia matakwa ya umma
Katika mkutano wake na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bw. Mnyika alisema ameona kuna haja ya kuwasilisha hoja hiyo mapema kuliko alivyokuwa amepanga awali, baada ya kuona dalili za suala hilo 'kupelekwa katika njia zenye kasoro' ambazo ziliwahi kutumika huko nyuma na matokeo yake kupuuzwa.Bw. Mnyika ambaye pia ni katibu wa Kamati ya Wabunge wa CHADEMA, alisema kuwa itakuwa si sahihi kwa hoja ya katiba mpya kuchukua mkondo wa 'kuundiwa tume au kamati ya rais au jopo la wataalamu washauri,' bali itakuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwani vitu kama hivyo viliwahi kuundwa lakini mapendekezo yake yakaishia 'kutupwa kapuni na watawala.' "Zipo sababu kadhaa ambazo zimenisukuma kuona umuhimu wa kulipeleka suala hilo bungeni sasa, ili lichukue mkondo wa bunge, kwanza katiba ni sheria, tofauti yake na sheria zingine yenyewe ni sheria mama.
"Ibara ya 63 (2) na (3) zinaeleza kuwa bunge lina mamlaka ya kutunga sheria pia ibara ya 98 (1) si sheria tu, bunge lina mamlaka ya kufanya mabadiliko ya katiba...hivyo kuna haja ya mjadala huu kuchukua mkondo wa bungeni, ndiyo uende serikalini, kisha urudi bungeni. Lakini pia katiba ni mkataba kati ya watawala na watawaliwa, viongozi na waongozwaji au serikali na wananchi.
"Sasa kama ndivyo hivyo kwenye mkataba wa namna hii ambapo mwenye mali ambaye ni mwananchi anatoa mamlaka ya kusimamiwa mambo yake kwa serikali, lazima yeye awe na kauli kubwa juu ya uendeshwaji wa masuala hayo...ibara ya 8 (1) ya katiba inasema kuwa wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote na madaraka, wajibu wa serikali ni kuleta ustawi kwa niaba yao," alisema Bw. Mnyika na kuongeza;
"Ibara ya 63 (2) inasema kuwa bunge litafanya kazi kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali, hivyo basi bunge na wabunge ambao ndiyo wawakilishi wa wananchi, wanaosimama badala ya wenye mali wanapaswa kujadili na kutoa maelekezo kwa serikali."Sababu ya tatu ni kuwa huu sasa si wakati tena wa kuendelea kuliundia tume au kamati za rais suala hili, imeshafanyika sana huko nyuma na historia inaonesha kuwa hazikutimiza matakwa ya wananchi.
"Iliundwa tume ya chama, enzi zile za chama kimoja, wakati wa Mwalimu Nyerere mwaka 1976, maarufu kwa jina la Tume ya Thabit Kombo, ndiyo iliyokuja na mapendekezo ya katiba hii mbovu tuliyonayo, yenyewe ilipeleka mapendekezo straight foward (moja kwa moja) kwa Halmashauri Kuu ya chama wakati huo, kisha bunge likayajadili kwa saa tatu na kupitisha.
Bw. Mnyika aliongeza kuwa kila 'joto' la mjadala wa katiba mpya linapopanda, watawala walioko madarakani wamekuwa wakijaribu kuuzima au kupindisha hoja kwa kuunda tume, kamati au jopo na kisha kuishia 'kuweka viraka' badala ya kufanya kulingana na matakwa ya wananchi.
"Ukiacha hiyo Tume ya Thabit Kombo, mwaka 1983 kulikuwa na joto kubwa la mjadala juu ya katiba hii ya mwaka 1977 ambao ndio mjadala wa katiba mpya ulizaliwa kabisa, serikali ikaamua kufanya marekebisho madogo na kuingiza haki za binadamu mwaka 1984...mwaka 1991 ikaundwa Tume ya Nyalali juu ya mfumo wa vyama vingi, lakini kwa jinsi ilivyokusanya maoni ikaona kuna umuhimu wa kuwa na katiba mpya.Bw. Mnyika alisema kuwa mapendekezo hayo ya Tume ya Nyalali juu ya kuandikwa upya kwa katiba na juu ya sheria 40 mbovu yalipuuzwa, isipokuwa lile la kuruhusu mfumo wa vyama vingi kwa sababu ilikuwa ni tume ya rais na yeye kwa mujibu halazimiki kusikiliza ushauri wa mtu yeyote.
"Mwaka 1998 pia ikaundwa tume nyingine ya rais, Tume ya Jaji Kisanga, Tume ya White Paper, tume ya serikali nyingine badala ya tume ya wananchi, rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa alipuuza ushauri wa katiba mpya, tena akaibeza kuwa ilifanya zaidi ya ilichokuwa imeagizwa kufanya, badala yake serikali ikachukua mapendekezo ya rais kuwa na mamlaka ya kuteua wabunge 10 na lile la kuondoa ulazima wa mshindi wa urais kushinda kwa asilimia zaidi ya asilimia 50 ya kura zote.
"Marekebisho hayo ya mwaka 2000 kwa maoni yangu yakaturudisha nyuma zaidi badala ya kwenda mbele...suala la kuunda tume, mbali ya kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma, lakini pia si njia mwafaka kwa sababu rais kwa mujibu wa ibara ya 37 (1) halazimiki kufuata ushauri wa mtu yeyote...lakini pia hii si hoja ya rais wala serikali ni hoja ya wananchi," alisema Bw. Mnyika.
Alisema kuwa kwa hoja yake hiyo ambayo atakuwa ameikamilisha ndani ya juma moja, kisha kuiwasilisha siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa bunge unaotarajia kujadili hoja hiyo kama zinavyosema kanuni za bunge, ataliomba bunge lianzishe mchakato huo kwa kuisimamia na kuishauri serikali juu ya njia sahihi, na baadaye serikali iitishe mkutano mkuu wa taifa wa kikatiba.
"Kisha kuundwe tume ya kisheria itakayojumuisha watu mbalimbali, si jopo la wataalamu tu, kuratibu maoni ya Watanzania kwani katiba ni mali ya wananchi si ya wataalamu pekee, baada ya hapo ifuatie kura ya maoni itakayojumuisha wananchi wote kufikia mwafaka wa kitaifa juu ya suala hilo.
Alisema kuwa pamoja na kuwa alikuwa na sababu zingine nyingi za kutaka kuwasilisha hoja hiyo ndani ya miaka mitano bungeni, lakini moja ya sababu zilizomfanya aamue kuipeleka katika bunge la Februari, mwakani ni pamoja na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye alisema juma lililopita kuwa atamshauri Rais Jakaya Kikwete aunde jopo la wataalamu kisha watoe mapendekezo ya marekebisho ya katiba lakini si kuandika katiba mpya.
Alisema sababu zingine ni pamoja na kukumbana na swali la mahitaji ya katiba mpya na Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyo huru katika karibu kila mkutano wake wakati wa kampeni za uchaguzi, ambapo alikuwa akiahidi kuwa atakapopewa nafasi ataitumia kuwasilisha hoja bungeni ili mchakato uanze kwa manufaa ya Watanzania, hivyo kuwa hoja ya wapiga kura wake.
Chanzo: Majira-20/12/2010
No comments:
Post a Comment