MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) ameahidi kuisadia shule ya mchepuo wa Kingereza ya Kings iliyoko Kata ya Goba wilayani Kinondoni, Dar es Salaam kutatua kero ya umeme inayoikabili.Mnyika alitoa ahadi hiyo mwishoni mwa wiki kwenye mahafali shuleni hapo na kuongeza kuwa pamoja na shule hiyo kujiwekea nishati ya umeme inayotumia nguvu za jua kama msingi wa maendeleo bado nishati hiyo haitoshi kutokana na ukweli kwamba nguvu yake ni ndogo katika matumizi.
“Katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia tunatakiwa kutumia mitandao mbalimbali ikiwamo kompyuta, intaneti na printa sasa umeme huu wa jua hauwezi kufanya yote hayo; kikubwa katika umeme huu ni kuwasha taa tu,” alisema Mnyika.
Aidha, aliwataka wakazi wa eneo hilo wajiorodheshe kwa lengo la kujua idadi yao kisha atalifuatilia kwa kukutana uongozi wa Shirika la umeme nchini (TANESCO), kuwafahamisha kuwa kuna jamii kubwa inahitaji huduma hiyo.
Katika hatua nyingine Mnyika alishiriki katika kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike na wa kiume wa shule hiyo.
“Kwa hili la ujenzi wa bweni nawapongeza sana, kwani litakapokamilika litasaidia kupunguza uchelewaji wa wanafunzi kufika shuleni pia litawafanya wanafunzi kuwa karibu na mazingira ya shule,” alisema Mnyika.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment