Saturday, December 18, 2010

Mnyika atoa asilimia 20 ya mshahara kuchangia elimu

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika, amesema ameanza kutekeleza ahadi yake ya kutenga asilimia 20 ya mshahara wake kwa ajili ya Mfuko wa Elimu katika jimbo hilo.

Akizungumza katika kongamano la Vijana Wasomi wa Vyuo Vikuu jana lililofanyika katika ukumbi wa River Side Dar es Salaam, alisema kwa kuwa wakati wa kampeni alitoa ahadi hiyo, ameona ni vyama akaanza nayo kwa kuwa ina manufaa kwa kukuza elimu na kuwa na wasomi wengi nchini.

Mnyika aliwashukuru vijana pamoja na wananchi kwa ujumla kwa kumuunga mkono ambapo aliwaahidi kufanya kazi na hata wasiomuunga mkono wakati wa uchaguzi lengo likiwa kuiinua Ubungo.

“Uchaguzi umekwisha nawashukuru kwa kuniunga mkono nitafanya kazi na wote, ninyi na hata ambao hawakuniunga mkono nawaomba wananchi wote wazee na rika zote pamoja na watendaji wote wa serikali na viongozi wa vyama mbalimbali tushirikiane pamoja katika kuutumikia umma na kuwezesha maendeleo,” alisema Mnyika.

Alisema wananchi wa Ubungo mwenye tatizo au ushauri ofisi ya mbunge imeanza kufanya kazi na iko ndani ya jengo la Wilaya ya Kinondoni, lakini pia atafungua ofisi ya ziada ambayo itakuwa inashughulika na kutoa elimu kwa vijana, wanawake na makundi mengine ya kijamii.

Katika kongamano hilo wataalamu vijana waliwasilisha mada mbalimbali za namna ya kutekeleza mipango ya kushughulikia masuala yanayowagusa wananchi katika sekta za elimu, ajira, maji, miundombinu, usalama, uwajibikaji, ardhi na afya.

Chanzo: Tanzania Daima (Asha Bani)

No comments: