Wednesday, December 29, 2010

Mnyika awasilisha taarifa ya hoja binafsi kuhusu katiba mpya

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika, leo anawasilisha taarifa ya hoja binafsi kuhusu mchakato wa Katiba Mpya kwa Katibu wa Bunge.

Mnyika alisema jana kuwa atawasilisha hoja hiyo kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge kifungu cha 55 (1) kwa ajili ya Bunge kupitisha maazimio ya kuweka utaratibu wa kiusimamizi na wa kisheria wa kuratibu mchakato mzima wa kuandikwa kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nichukue fursa hii kufafanua kuhusu upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watu kupitia baadhi ya vyombo vya habari mara baada ya kueleza kusudio langu la kuwasilisha hoja binafsi kuhusu Katiba mpya. Mimi kama mbunge ninapokwenda kuwasilisha hoja binafsi kuhusu Katiba mpya nafanya hivyo kama sehemu ya kutimiza wajibu wa kuwawakilisha wananchi na kulinda ukuu wa Katiba katika taifa letu.

“Hoja binafsi ninayokwenda kuiwasilisha ni kwa ajili ya Bunge kwenda kutimiza wajibu huu wa Kikatiba ambao wabunge wote tumeapa kuulinda na kuutetea; kufanya hivyo hakuwezi kuwa tendo la ’unafiki’ moja ya gazeti lilivyoeleza (sio Tanzania Daima),” alisema.

Alieleza kuwa kumewakuwapo na upotoshoji unaoeleza kuwa anakusudia kwenda kuwasilisha rasimu ya Katiba mpya bungeni kupitia hoja binafsi na kueleza kuwa hilo si jukumu la mtu mmoja, chama, taasisi au dini bali ni jukumu la Watanzania wote.

Mnyika alieleza kuwa anachowasilisha ni hoja binafsi kwa ajili ya Bunge kuazimia kuweka utaratibu utakaoanzisha, kusimamia na kuwezesha serikali kuratibu mchakato wa Katiba mpya utakaohakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu kuandika Katiba kupitia tume inayohusisha wadau, elimu kwa umma, mkutano mkuu wa taifa wa Katiba na kura ya maoni.

“Mtu binafsi, taasisi, chama au dini kila kimoja kinaweza kuwa na maoni yake kuhusu Katiba ambayo kinaweza kuyatoa kwa njia ya taarifa au hata kuandaa rasimu sifuri, lakini hatimaye lazima tuwe na mfumo wa pamoja ili kuweza kuwa na makubaliano ya kitaifa kwa kuwa Katiba sio mali ya chama chochote, dini yoyote au mtu yeyote bali ni sheria mama na mkataba kati ya wananchi na serikali,” alisema.

Alieleza kuwa suala la Bunge kuweka maazimio na utaratibu ikiwemo kutunga sheria ya kuratibu mchakato wa mabadiliko ya Katiba ni la muhimu na la haraka wakati huu ambapo tayari makundi mbalimbali ya kijamii yamejitokeza na kuweka misimamo yao wazi ya kutaka Katiba mpya na mengine kutangaza kuanza kuandika miswada ama rasimu ya Katiba husika.

Aidha, mbunge huyo alionya kutokuwapo na utaratibu wa haraka na wa pamoja kila mdau atakwenda kwa mfumo wake, kunaweza kuzalisha mpasuko katika jamii kutokana na suala la Katiba mpya.

“Sio jambo baya makundi ya kijamii kuandaa rasimu sifuri za Katiba, lakini kama kila kundi likaandaa rasimu yake halafu utaratibu wa kuunganisha maoni ya makundi mbalimbali kupitia chombo kinachokubalika na kinachohusisha wadau wote kuchelewa, taifa linaweza kuingia kwenye malumbano; ndio maana ni muhimu kwa utaratibu huo kuwekwa kupitia mkutano wa Bunge wa Februari,” alisema.

Wakati huohuo, mbunge huyo aliwataka wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kutoa maoni kuhusu rasimu sifuri ya katiba iliyopitishwa na Kongamano la wadau Februari 17 mwaka 2007, baada ya kuwasilishwa na Kamati ya Wataalamu iliyoongozwa na Dk. Sengondo Mvungi.

Katika kongamano hilo pamoja na kueleza ubora wa rasimu hiyo sifuri ukilinganisha na Katiba inayotumika hivi sasa wajumbe walieleza kasoro zilizopo kwenye rasimu sifuri ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho kabla ya rasimu husika kukabidhiwa katika vyombo vya maamuzi.

“Hivyo, tunakaribisha maoni ya umma kuhusu rasimu husika inayopatikana kwenye tovuti www.chadema.or.tz, maoni yatumwe kupitia info@chadema.or.tz au yatumwe moja kwa moja kwa kamati ya madai ya Katiba mpya,” alieleza mbunge huyo.

Muda mrefu sasa, kumekuwa na vuguvugu la madai ya kuwepo kwa Katiba mpya kutoka kwa taasisi mbalimbali, viongozi wa dini na wanasiasa. Joto hilo liliongezeka baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31 wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilipoamua kuvalia njuga madai ya Katiba mpya.

Kilio hicho cha CHADEMA kimekuwa kikipata watu wanaoikiunga mkono wakiwamo wanasiasa mashuhuri nchini, viongozi wa dini, asasi zisizo za kiserikali na wananchi wa kawaida.


Chanzo: Tanzania Daima 27/12/2010

No comments: