Thursday, December 23, 2010

Mnyika acharuka kupigwa Mbunge Lema

KATIBU wa kambi ya upinzani bungeni na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amelaani kitendo kilichofanywa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha mjini cha kumpiga Mbunge Godbless Lema na kumtaka Mkuu Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema, kuchukua hatua dhidi ya askari hao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mnyika alisema kitendo kilichofanywa na polisi hao hakipaswi kunyamaziwa na inaonyesha wamefanya kazi hiyo kwa maelekezo, hivyo IGP Mwema anapaswa kuchukua hatua za kinidhamu na za kisheria kwa polisi hao.

Alisema taratibu za kiuchaguzi haziruhusu polisi kuingia katika ukumbi wa uchaguzi na bunduki au silaha hivyo ni hatua ya kujiuliza polisi hao walipata baraka za nani za kuingia ndani ya Baraza la Madiwani wakati uchaguzi ukiendelea?

Aidha, Mnyika alisema ni vema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akatoa kauli juu ya suala hilo kutokana na kitendo hicho kutokea kikiwa chini ya ofisi yake ambayo ndiyo wasimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa (Tamisemi).

“Ni vema Pinda akaliangalia suala hili kwa kwenda mbali zaidi tangu ndani ya ukumbi wa uchaguzi; ni kinyume na taratibu za uchaguzi, ilikuwaje polisi wakaingia na bunduki? Walipata baraka kutoka kwa nani?” alihoji Mnyika.

Alisema pamoja na hilo bado ofisi ya Bunge inawajibika kutoa tamko haraka kwa kitendo kilichofanyika kutokana na kuingilia maslahi ya Bunge na ni kinyume na Katiba.

“Ofisi ya Bunge inapaswa kuchukua hatua zinazostahili; ni taasisi inayostahili kulinda wabunge wake,” alieleza.

Hata hivyo, Mnyika alisema CHADEMA inahitajika kutafakari na kuchukua hatua za kisheria, ili kukomesha vitendo hivyo vinavyoashiria vyombo vya dola kutaka kusababisha umwagaji damu.

“Vyombo vya dola havifanyi kazi bila maelekezo hali inayoonyesha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinahusika na hivyo inatakiwa itoe kauli ya kulaani na kulichunguza jambo hilo,” alisema.

Akizungumza na Kituo cha Televisheni cha TBC1, Kamanda wa Polisi wa Arusha, Thobias Andengenye, alikanusha polisi kuhusika kumpiga mbunge huyo na kudai kuwa baada ya kuachiwa kwa dhamana Lema alipita maeneo waliyokuwepo wapenzi wa chama chake ndipo alipoanguka.


Chanzo- Tanzania Daima (Disemba 2010)

No comments: