Wednesday, December 28, 2011

Serikali itake Israel waombe radhi; tukijiheshimu, tutaheshimiwa

Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inaitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa tamko juu ya kauli ya Waziri wa Ulinzi wa Israel ya kwamba nchi yetu si ya muhimu wala ya maana.

Waziri Barak alifanya mahojiano na Radio Israel na kutoa kauli ambayo imenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari vya nchi hiyo wiki iliyopita kuwa “ Germany, France and England are not Tanzania, Mauritania or Tripolitania…..these are very important, very relevant countries and we don’t have an interest in increasing tensions with them or making them bitter enemies”.

Kwa kauli hii serikali ya Israel inaiona Tanzania sio nchi ya muhimu wala ya maana hata kufikia hatua ya kuilinganisha na eneo tu ndani ya Libya linaloitwa Tripolitania.

Tunamtaka Waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa, Benard Membe kuitaka serikali ya Israel kuomba radhi kufuatia kauli hiyo au kueleza wazi iwapo mazungumzo hayo ya Waziri Barak ni msimamo wa nchi hiyo kuhusu uhusiano wa kidiplomasia wa mataifa yetu.

Barua pekee ya balozi wa heshima wa Tanzania nchini Israel, Kasbian Nuriel Chirich kwenda kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Avigdor Lieberman ya kulaani matamshi hayo ya Waziri Barak na kumkaribisha mwakilishi wa Israel kutembelea Tanzania haitoshi kuifanya serikali ya nchi hiyo kutambua athari za kidiplomasia za kauli iliyotolewa.
Aidha kwa kuwa serikali imekuwa ikieleza kwamba Tanzania ina mahusiano mazuri ya kiulinzi na Israel, ni muhimu pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dr Hussein Mwinyi akaeleza umma iwapo kauli hiyo ya Waziri Barak ndio msingi wa mahusiano yaliyopo kati ya nchi zetu kuhusu ulinzi na usalama.

Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa inachukua fursa hii kurudia kuwakumbusha watanzania kwamba kupuuzwa huku kwa nchi yetu katika medani ya kimataifa kunatokana na sera mbovu ya mambo ya nje chini ya utawala wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tanzania imepoteza heshima katika siasa za dunia kutokana na diplomasia yetu kujikita katika kuomba omba kimataifa; pamoja na kuwa kimaneno na maandishi serikali inazungumza kuhusu diplomasia ya kiuchumi, kivitendo mahusiano yetu yamejengeka katika misingi ya utegemezi, kupungua kwa urari wa kibiashara na kuachia mianya ya uporwaji wa rasilimali.

Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa inatambua kwamba wakati wa uongozi wa awamu ya kwanza wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania ilikuwa na heshima na sauti kimataifa sio tu katika jitihada za ukombozi kusini mwa Afrika bali pia katika mahusiano ya kisiasa, kiuchumi na kijamii baina ya nchi za kusini na mataifa mengine duniani.

Hali ya Tanzania kupoteza sauti katika medani ya kimataifa imedhihirika pia hivi karibuni katika mkutano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi (COP 17) uliomalizika hivi karibuni nchini Afrika Kusini; wakati nchi yetu ikiwa ni miongoni mwa waathirika wakubwa zaidi wa mabadiliko ya tabia nchi. Iwapo hatua hazitachukuliwa kurejesha heshima na sauti ya Tanzania kimataifa maamuzi mengi yatafanyika yenye athari kwa wananchi wengi bila ushiriki wao thabiti kama yanayoendelea hivi sasa kuhusu Mikataba ya Kiuchumi na Nchi za Jumuia ya Ulaya (EPA) yenye madhara kwa wakulima na wenye viwanda nchini.

Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa inatoa mwito kwa watanzania kuendelea kuunganisha nguvu ya umma kusimamia uwajibikaji na kufanya mabadiliko ya kimsingi ya kiuongozi, kisera na kimfumo ya kitaifa ili kuweza kurejesha nafasi na heshima ya Tanzania kimataifa katika mazingira ya sasa ya ushindani wa kiuchumi, kiulinzi, kijamii na kisiasa.

Kauli ya Waziri Barak nimuendelezo tu wa mataifa mbalimbali kuifanya Tanzania na baadhi ya nchi nyingine za Afrika kuwa hazina heshima wala sauti katika siasa za kimataifa kama ambavyo Serikali za Uingereza na Marekani zimeweka masharti yenye mwelekeo wa ukoloni mamboleo kuhusu masuala ya ushoga na usagaji.

Hatua za kupinga kauli za kudharauliwa na kulazimishwa mambo tusiyoyataka ziende sambamba na kudhibiti mianya yote ya ufisadi wa kimataifa, uwekezaji uchwara na kutetereka kwa misingi wa utawala wa kisheria masuala ambayo yanasababisha migogoro na pia rasilimali za nchi kutokutumika kwa manufaa ya wananchi walio wengi; tukijiheshimu, tutaheshimiwa. 

Wenu katika Demokrasia na Maendeleo,

John Mnyika (Mb)

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa (CHADEMA)

15 comments:

Filipo Lubua said...

Lini Tanzania itaheshimika kimataifa? Nashindwa kuamini kuwa nchi isiyokuwa na amani kama Israel inatoa matamshi hayo ya dharau. Hapa ndipo ninapotambua kuwa kweli heshima ya nchi haiji kwa ukosefu wa vita na maradhi, kama wanavyosisitiza viongozi wengi wa Tanzania; bali heshima ya nchi yoyote, kimataifa, itakuja kama nchi husika ina uchumi uliothibitika, pamoja na siasa zinazolenga kulinda na kuheshimu maamuzi ya raia wake. Ni kweli kabisa, kitendo cha Tanzania kuwa na Rais ambaye ni ombaomba asiye na aibu, kinatufanya tudharaulike machoni mwa nchi nyingine, hata zile ambazo hazijawahi kuionja amani ambayo tunajivunia kila siku.

Mkama, A said...

Hapa umenena mkuu! Ila wasiwasi wangu ni hii serikali yetu sidhani kama wanaweza kutoa kauli ya kijasiri ya kusimia hadhi ya taifa letu.
Binafsi na mshukuru balozi wetu wa heshima kwa hilo tamko lake japokuwa nae hajaweka mambo sawa. Serikali hii inabidi tuhakikishe katiba mpya inaainisha vigezo maalumu kwa kwa kazi maalumu na hasa mawaziri na makatibu wakuu pia ipo haja ya wabunge pia.

Blessings said...

Hili jambo la mahusiano yetu na Israel ni la kihistoria na si vema kutoa tamko bila ya kujua kwanza sababu za Israel kutokuwa na balozi wao katika nchi yetu na sisi kukosa balozi anayewakilisha nchi yetu katika Israel ikiwa kweli hatuna.

Kwa hali hiyo ni dhahiri kuwa tayari hatuna mahusiano mazuri na Israel kwa kuwa hawana mwakilishi kwetu na sisi hatuna kwao.

Tukirejea kwenye historia tutaelewa kisa chote. Hii ni changamoto kwa wizara inayohusika na mahusiano ya kimataifa kuchunguza na kujua tuna tatizo gani na nchi hiyo miongoni mwa nchi zote duniani. Ubalozi wao kwanini haupo kwetu?, Kuna siku nilisikia katika majibu ya waziri kuwa balozi wa Israel aliyepo nchini Kenya eti ndiye ambaye anatumika na huku Tanzania. Binafsi sijaridhika na jibu hilo kwa kuwa sidhani kama kuna nchi nyingine ambayo balozi aliyepo Kenya ndiye ambaye anahusika na Tanzania pia.

Kwa haraka sipendi kusema sisi tumepuuzwa na Israel bali ninapenda tuangalie suala la mahusiano yetu kuwa yalishakuwa na dosari hata kabla ya kauli hiyo.

Tukiacha kauli hiyo ya Israel pamoja na kwamba siungi mkono tamko lolote kutolewa na nchi yetu kujibu kauli ya waziri huyo wa Israel bali ninasisitiza mahusiano yarejeshwe na ubalozi wao uwepo kwetu na sisi tuwe na wetu kwao.

Mbali na hilo; Naunga mkono; kwamba heshima yetu kimataifa imeshuka na tunahitaji viongozi wazalenda na wenye kujali hadhi ya nchi yetu Kimaifa.

Blessings said...

Wapendwa rafiki; baraka katika nchi yetu inategemea sana tunavyosema na tunavyohusiana na nchi ya Israel. Biblia iansema Atakayembariki Israel atabarikiwa na atakayemlaani Israeli atalaaniwa. Kama nchi yetu itailaani Isreal kwa namna yoyote tutajipatia laana. Hii ni sheria katika ulimwengu wa roho. Kwa wale wanaoamini Biblia wataniunga mkono. Wale wasioamini wanisamehe lakini wanikubali kwa kuwa ni ukweli ambao tusipozingatia tukatamka tu chochote kuhusiana na Israel kwa sababu ya uhuru wa kusema chochote tulionao tutaangukia katika laana kubwa.

SIYO WAZO LINALOHITAJI KUPIMWA KITAALUMA NI LA KIIMANI. KAMA HUAMINI SIKUHUKUMU.

Anonymous said...

Jamani, hili swala lisiende kiushabiki, mambo kama haya yakitokea Watanzania tunapaswa kuwa kitu kimoja na si kuingiza mambo ya vyama au dini zetu, huyu waziri wa Israel amekosa adabu, tena amekosa adabu sana mpuuzi huyu, anafikiria nini kusema hivi, je leo Tanzania kama nchi ikianza biashara na Iran na tukawauzia uranium yetu atasema kuwa Taznania si chochote? Hizo hasira zao za kutokuwa na Ubalozi hapa Tanzania zisiwe sababu bana.

Taznania, tangia enzi ya Mwalimu Nyerere iliamua kutokuwa na Ubalozi na hii nchi kwa sababu ya msimamo wa Israel kuikalia kimabavu Palestine... Sasa kwa kuwa hawa jamaa ni watu wa visasi hawajalisahau ilo na ina wauma sana sana kuona nchi maskini kama hii kuwa na msimamo kama huo.

Najuwa kuna watu kama jamaa yangu hapo, anadai kuwa atakaye ibariki Israel basi naye atabarikiwa na kweli tunaona hizo nchi ambazo zinaiunga mkono Israel jinsi zilivyo barikiwa, maana tunashuhudia ushoga na usagaji ukitete hadharani na hata kuzipita zile nchi za Sodoma na Gomora, maana Sodoma na Gomora zilifanya ufisadi wa wanaume kuingiliana wenyewe kwa wenyewe lakini hawakufikia hatua za wanaume au wanawake kuoana wenyewe kwa wenyewe, kweli USA na UK zimebarikiwa, leo hii imepitishwa sheria Uko Amerika kuruhusu wanajeshi wa kimarekani kuwa si kosa kufanya mapenzi na wanyama (bestiality), hao ndio waliobarikiwa maana hata ngono kinyume na maumbile ni sawa tu kwao.

Basi hao wanaoitetea Israel kwa mujibu wa imani zao wajuwe kwamba wameramba garasa, maana Israel haiwatambui Wakristo wala Waislam, kwao hakuna kiumbe kilicho bora zaidi ya myahudi, na ndio maana wakamtesa na kusurubu Yesu Kristo...

Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake.
Matthew 21:43
Haya ni maneno ya Bwana Yesu Kristo.

Na wakipata nafasi basi angalia hizi youtube video: http://www.youtube.com/watch?v=6Ek5G6337yU na hii: http://www.youtube.com/watch?v=JA6vRC1xW_c

Au atafute hizi heading uko youtube:
"We killed Jesus, and we're proud of it"
Mocking Jesus on Israeli TV - צליבת ישו - The Crucifixion of "Yeshu"

Firoz Datoo said...

Tumebanwa kila upande hatuna pa kufurukuta, viongozi wengi wa sasa ni waoga,pamoja na umasikini wetu tulioutaka wenyewe kwa kuwakabidhi wageni rasilimali zetu kwao,namkumbuka mwalimu aliweza kuwakosoa waziwazi pale alipoona heshima ya Tanzania inawekwa rehani.

Anonymous said...

ni sawa huo nu udhalilishaji lakini, heshima ina anza chini, kwenye majimbo. ikiwa kila mmbuhe angejitahidi kutengeneza jimbo lake ili liwe mfano naamini nchi nzim ingekuwa na heshima.
Namaanisha hata Mh Mnyika una nafasi ya kujenga heshima katika nchi hii, ikiwa wewe utahakikisha wananchi wa ubungo wana maji, barabara za mitaa nzuri, unasaidia katika kukuza ajira binafsi kwa vijana wajasilia mali nk nadhani watu wataheshimu jimbo jimbo lako. n kila mbunge akifanya hivyo nadhani nchi nzima itaheshima.

lakini tatizo ni kwamba tunakalia siasa badala yaa maendeleo, hata kama leo raisi akisimama na kukemea hayo matamshi ya waisraeli kwa tanzania , bado haitasaidia ikiwa nyinyi tuliowachagua hamtaleta maendeleo, na mtarudi tena 2015, kutudanganya then nyie mtaendelea kuishi maisha mazuri,magari ya kifahali, mishahara minono,wakati sisi tunabaki na afadhali ya jana... maisha magumu hata, usafiri tabu kila siku kuminyana kwenye madalala.

naaandika haya kwa uchungu kwani tulitazmia mabadiliko makubwa kwako Mh Mnyika lakini mwaka sasa unaisha kaka. 2015 si mbali,achana na mambo yasiyo na tija kwa wananchi wako wa ubungo, post mikakati ya kuwakomboa wananchi wako wa ubungo, post kama hizi za kashafa za waisraeli, hazimgusi mwananchi wa kawaida wa hapa ubungo ambaye hajui leo atakula nini , huku alisimama juani kukuchagua, kulinda kura na ukashinda ..kila la kheri

taniwatani said...

israel haijakurupuka kwa kauli yake ya kusema tanzania si kitu na hawana "interest"! hili lifahamike kwamba tanzania ina msimamo thabiti kuhusu palestina! ni majuzi tu palestina ilipeleka ombi UN kutambuliwa, japo ilishindikana lakini katika nchi za mwanzo kutamka kuiunga nkono palestina ni Tanzania na tufahamu hilili ndilo linalofanya moyo wa israel kuwa na kidonda kwa Tanzania!

Anonymous said...

these are very important, very relevant countries and we don’t have an interest in increasing tensions with them or making them bitter enemies”.

KWA KAULI HII!!!! WAKO SAHIHI. Hivi kweli unategemea ISRAEL inaweza ikapingana na UK, FRANCE AU GERMAN kwa kuwa upande wa TANZANIA na ukichukulia nchi yetu ni ya tatu kwa kuomba duniani!!??

WAKO SAHIHI, HAINA HAJA YA KUTUOMBA RADHI KWA KUTUAMBIA UKWELI!!

Katikiro Moshi Mujaya said...

Mimi kwa ufupi sana nasema tumejitakia.
Tumejitakia kutukanwa; tumejitakia kudharauliwa.

Anonymous said...

Ndugu yangu John, heshima ya Taifa lolote kama ilivyo heshima ya mtu binafsi mume au mke itajengeka kutokana na muhusika kujitengenezea mazingira chanya (kujiheshimu) au hasi (kutokujiheshimu). Kitendo cha Tanzania kuamua kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Israel wakati bado taifa hilo likiendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na wakati huo huo kukataa katakata kuachia kukalia ardhi ya Waarabu iliyojitwalia kwa mabavu mwaka 1967, si tu kwamba ni kuwasaliti wale wanyonge wa Palestina tuliokuwa tumeapa maiak chungu nzima kwamba tungelikuwa nao upande mmoja bali ni kujidhalilisha.
Tanzania inakosa nini kwa kutoitambua Israel na kuitaka iache ubabe usio na maana? Hivi akina Membe na wenzake wanapokutana na Wapalestina wanawaambia nini hasa kimebadilika tangu Mwalimu kung'atuka kiasi cha kuifanya tanzania iikumbatie Israel na kuwatosa Wapalestina?
Hili bakuli la omba omba linatufanya tukaombe kila mahali hata kwa shetani ili mradi atupe makombo kidogo tusife njaa. Aibu! Aibu! Aibu kubwa sana.

Shoochik said...

Ndugu yangu John, heshima ya Taifa lolote kama ilivyo heshima ya mtu binafsi mume au mke itajengeka kutokana na muhusika kujitengenezea mazingira chanya (kujiheshimu) au hasi (kutokujiheshimu). Kitendo cha Tanzania kuamua kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Israel wakati bado taifa hilo likiendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na wakati huo huo kukataa katakata kuachia kukalia ardhi ya Waarabu iliyojitwalia kwa mabavu mwaka 1967, si tu kwamba ni kuwasaliti wale wanyonge wa Palestina tuliokuwa tumeapa maiak chungu nzima kwamba tungelikuwa nao upande mmoja bali ni kujidhalilisha.
Tanzania inakosa nini kwa kutoitambua Israel na kuitaka iache ubabe usio na maana? Hivi akina Membe na wenzake wanapokutana na Wapalestina wanawaambia nini hasa kimebadilika tangu Mwalimu kung'atuka kiasi cha kuifanya tanzania iikumbatie Israel na kuwatosa Wapalestina?
Hili bakuli la omba omba linatufanya tukaombe kila mahali hata kwa shetani ili mradi atupe makombo kidogo tusife njaa. Aibu! Aibu! Aibu kubwa sana.

Shoochik said...

Tujiulize swali la msingi kwamba hivi siasa yetu ya mambo ya nje ni ipi? Hivi tunatengeneza sera ya mambo ya nje kwa kuangalia nini hasa? Hivi tumefikia mahali hatuwezi hata kuwa na uhuru wa kukemea maovu? Israel anafanya anachotaka dhidi ya Wapalestina na tunakaa kimya hatuthubutu hata kusimama hadharani na kukemea? Tunashindwa hata kubweka tu potelea mbali tusiwe na meno yenye nguvu ya kung'ata?
Watu wanaonewa na Wamarekani tunakaa kimya? Libya imevamiwa hapa tumegugumia na hata tulipojifanya kwamba tunatoa tamko halikuwa na nguvu kwa sababu unayemkaripia ndiye ameshika funguo za hazina yako.
Aibu hii ni lazima ikomeshwe kwa vijana kusimama kidete na kujitahidi kurejesha heshima ya taifa letu heshima ambayo ilikuwa inawafanya watu wanasimama kutusalimia popote duniani tulipokuwa tunakwenda licha ya kwamba tulikuwa hatuchimbi dhahabu wala kuwa na gesi kama ilivyo sasa. Masikini jeuri anayejivunia utu wake anaheshimika mara milioni moja kushinda tajiri ombaomba asiyekuwa na msimamo katika maisha.
John, endelea kuwaamsha Watanzania wa kizazi kipya watambue nini maana ya uzalendo na utangamano wa kimataifa.

Marcel M. said...

However weak we may be in any arena,as a country we have right to and should claim to be respected. Besides, I have not seen directly the insult in the statement quoted. Would someone clarify by giving the source document.

Kheri said...

Kwa kweli kauli hii imetoka kwa mtu asiye na adabu, mpuuzi na mtu wa kulaaniwa kwa kauli za kishenzi. Kuchanganyikiwa kwao kwa maisha ya kumangamanga tangu kuumbwa kwa dunia sio tatizo letu. Watuache sie wenye nchi nzuri hata kama viongozi wetu wana mapungufu lakini Mungu kaipendelea sana nchi hii, anailinda na ametupa busara ya utu na tunaishi na majirani zetu vizuri, hatuna bifu na mtu na hatufungamani na mtu yeyote. Alaaniwe aliyejipa jina la Baraka wakati alipaswa kuitwa Mikosi. John nakuunga mkono