Tarehe 8 Disemba 2011 Wizara ya Nishati na Madini imetoa Taarifa kwa Umma kuhusu Maendeleo ya Sekta ya Nishati na Madini. Tunaendelea kuipitia taarifa husika na tutatoa taarifa mbadala kwa umma kama sehemu ya wajibu wa kikatiba wa kuishauri na kuisamia serikali. Hata hivyo, nimeshangazwa na ukimya wa serikali mpaka hivi sasa kuhusu haja ya kutoa kwa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na maendeleo ya sekta ya nishati ambayo inakabiliwa na changamoto nyingi kwa sasa zenye kuathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.
Kuanzia mkutano wa tano wa bunge ulionza tarehe 8 Novemba 2011 ilitarajiwa kwamba serikali ingetoa taarifa bungeni kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba kuhusu mpango wa dharura wa umeme na maendeleo ya sekta ya nishati; hata hivyo suala hilo halikuingizwa kwenye ratiba ya bunge. Baada ya taarifa kutokutolewa bungeni nilitarajia serikali ingetoa taarifa kwa umma lakini mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini haijatoa taarifa husika hivyo natoa mwito kwa Waziri husika kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umema na maendeleo ya sekta ya nishati kwa ujumla.
Mpango wa Dharura uliwasilishwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011, ahadi ya serikali ilikuwa kuongeza MW 572 ifikapo mwezi Disemba 2011. Kati ya hizo, MW 150 ilikuwa zizalishwe kupitia makubaliano baina ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na TANESCO; ilitarajiwa kuzalishwe MW 50 Septemba, MW 50 Oktoba na MW 50 Novemba 2011.
Kimsingi kauli iliyotolewa bungeni kuwa mitambo ilikuwa imepatikana haikuwa ya kweli hivyo ahadi ya kupata umeme huo ilikuwa hewa. Mpaka sasa hakuna hata MW moja ambayo imezalishwa kwa ushirikiano kati ya NSSF na TANESCO. Ujumbe ulipotumwa Marekani kwenda kuona mitambo iliyokuwa inaelezwa kwamba ipo haikukuta mitambo yoyote, walikuta kampuni ambayo haikuwa na uwezo kama ilivyokuwa kwa Richmond Development LLC; timu hiyo ya wataalamu ilibidi kwenda Ufaransa nako ikakosa mitambo ya dharura. Hivyo, fedha nyingi za umma zimetumika kufuatilia ahadi hewa na umeme mpaka sasa haujapatikana.
Ikumbukwe kwamba mpango mwingine wa muda mfupi ulioelezwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011 ni mradi wa kununua mitambo ya MW 100 wa Jacobsen wa gesi asili ambao awali ulikuwa ukamilike 2009/2010 lakini kutokana uzembe ndani ya serikali mradi huo haukukamilika mpaka mwaka 2011. Kuchelewa kwa kununuliwa na kufungwa kwa mitambo hii ambayo ilikuwa ifungwe Ubungo ndiko kuliongeza makali ya mgawo wa umeme kuanzia mwishoni mwa 2010 mpaka mwanzoni mwa mwaka 2011.
Baada ya kuchelewa kwa mradi huu serikali ikakubaliana na mkandarasi kuwa mradi huo ukamilike Juni 2012. Kutokana na ahadi ya MW 150 za dharura toka NSSF kuthibitika kuwa ni hewa, serikali ikarudi tena mezani kufanya majadiliano na mkandarasi wa mradi wa Jacobsen ili kuharakisha utekelezaji uzinduliwe mwezi Disemba 2011 wakati wa ‘sherehe’ za uhuru. Hata hivyo, wataalamu hawakumueleza tena ukweli Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa matarajio waliyompa ya kuzindua mradi huo wakati wa sherehe za uhuru nayo yamethibitika kuwa hewa kwa kuwa sherehe zimepita bila umeme wa nyongeza. Kutokana na hali hii, Rais Kikwete alilazimika kurudia mara kwa mara kwamba asingetoa hotuba ndefu uwanja wa taifa kwenye maadhimisho tarehe 9 Disemba katika siku ambayo wananchi walitarajia mkuu wa nchi azungumze masuala makubwa ya kitaifa ikiwemo suala la umeme na sekta ya nishati wa ujumla.
Kwa upande mwingine, udhaifu wa kutokutekeleza mipango ya uzalishaji wa gesi na makaa ya mawe kwa wakati umesababisha utegemezi mkubwa kwenye matumizi ya mafuta katika mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura. Zaidi ya nusu ya umeme unaozalishwa nchini hivi sasa ambao ni sawa na takribani MW 660 unazalishwa kwa kutumia dizeli, mafuta ya ndege na mafuta mazito hali ambayo imeongeza mahitaji makubwa ya uagizaji wa mafuta toka nje ya nchi. Hii imesababisha mahitaji makubwa ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mafuta na hivyo kuchangia katika kuporomoka kwa thamani ya shilingi. Aidha, ongezeko kubwa la uagizaji toka nje limeathiri urari wa biashara na hivyo kuchangia katika mfumuko wa bei ambao hivi sasa umefikia zaidi ya asilimia 16. Hivyo, watanzania hivi sasa wanabeba mzigo wa kupanda kwa bei za bidhaa na gharama za maisha kwa ujumla kutokana na ufisadi kwenye mikataba, ubadhirifu katika matumizi, uzembe katika uongozi na upungufu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali kwenye sekta ya nishati.
Pamoja na kuwa ahadi za mpango wa dharura bado hazijatekelezwa kwa ukamilifu wake serikali inaendelea kutumia zaidi ya bilioni 2 kila siku kama gharama za mafuta ya kuzalishia umeme suala ambalo linahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina kuhusu vyanzo vya fedha hizo na uhalali wa matumizi ya miradi ya Aggreko International, Symbion Power LLC na IPTL.
Nilionya bungeni kuhusu gharama kubwa za mpango wa dharura wa umeme na kupendekeza vyanzo mbadala vya fedha ambavyo serikali ilivipuuza. Uamuzi wa kukopa katika mabenki ya biashara kwa ajili ya kugharamia mpango wa dharura wa umeme tayari umeshaanza kuathiri Shirika la Umeme (TANESCO), serikali na utaathiri maisha ya wananchi.
Ikumbukwe kwamba tarehe 15 Julai 2011 nilieleza bungeni vyanzo mbadala vya kuongeza fedha katika bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bila kuathiri kwa kiwango kikubwa maisha ya wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla. Tarehe 18 Julai 2011 Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikubaliana na mapendekezo yetu na hivyo wakati anatoa hoja ya kuahirisha majumuisho ya mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini akaahidi kwenda kukata fedha kwenye posho na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima katika bajeti ya serikali ili kuelekeza fedha kwenye mradi wa dharura wa umeme.
Hata hivyo, tarehe 13 Agosti 2011 Serikali ikageuka na kuleta mpango wa dharura tofauti ambao ulijikita katika serikali kuidhamini TANESCO kwenda kukopa kwenye mabenki ya kibiashara zaidi ya bilioni 400. Siku hiyo nilirudia kumsomea Waziri Mkuu kumbukumbu ya Bunge (Hansard) ya ahadi yake ya tarehe 18 Julai 2011 ambayo haikuitimiza, inaelekea serikali ilitoa ahadi hewa ndio maana haikutaka kabisa kubadili msimamo.
Matokeo ya hali hiyo ni hivi sasa serikali kutafuta namna ya kuinusuru TANESCO kwa kubebesha mzigo mkubwa wananchi kwa kuwa hivi karibuni imewasilisha ombi la kupandisha bei ya umeme kwa wastani wa 155% (zaidi ya mara tatu) ya bei ya sasa. Ombi hili likikubaliwa kwa ukamilifu wake litakuwa na athari kubwa sana katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi. Ikumbukwe kwamba Januari 2011 umeme ulipanda bei kwa 18.5% tu lakini kupanda huko kulisababisha mfumuko wa bei, sasa watanzania wajiulize itakuwaje ukipanda kwa 185%. Hata hivyo, ni vigumu kwa EWURA kukubali kupandisha bei kwa kiwango hicho kwa kuwa ikumbukwe kwamba Disemba 2010 TANESCO iliomba kupandisha bei kwa zaidi ya 30% lakini haikukabaliwa. Kukataliwa kupandisha kwa bei kubwa kutaiweka TANESCO njia panda kwa kuwa tayari imeshakopa kwa gharama kubwa katika mabenki ya biashara na pia gharama za uendeshaji wa TANESCO zipo juu kutokana na ufisadi katika mikataba mbalimbali na pia kutokana na madeni makubwa ambayo TANESCO inadai kwa serikali na wateja wengine.
Hivyo, upo uwezekano wa mikopo kushinda kulipwa kwa wakati na TANESCO na madeni kurudi kwa umma kupitia kwa dhamana za serikali. Katika hali hii hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa na Wizara ya Nishati na Madini kutoa taarifa ya kina ya hali halisi ya utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na maendeleo ya sekta ya nishati ili kudhibiti mianya ya uchelewaji na ubadhirifu ambayo imeanza kujitokeza kwa kuzingatia pia mapendekezo ambayo tuliyatoa bungeni.
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
14/12/2011
2 comments:
hivi hali hii itavumiliwa hadi lini? kama alidangaya kwanini asichukuliwe hatua? je sio fedha ya wananchi iliyotumika na kugundua madudu hayo? inafidiwaje hela hiyo iliyotumika bule kuchunguza richmond ya mara ya pili? naomba mjipange mtueleze wananchi tuchukue hatua.
Nakupongeza kwa kuhakikisha serikali intmiza wajibu wake. Naona bado ipo kimya sijui wataeleza lini. Ila mheshimiwa pia hujatoa tamko la kuhusu mafuta ya petrol, diesel. Ni kero kubwa kwa kweli.
Post a Comment