Thursday, February 2, 2012

BUNGENI LEO: Mgomo wa madaktari na Sheria ya Bodi ya Mikopo

Asubuhi ya leo Naibu Spika Job Ndugai alitumia kanuni vibaya kuzuia hoja ya dharura bungeni kuhusu mgomo wa madaktari. Kimsingi, sikuwasilisha hoja ila niliomba muongozo wa Spika ili niweze kupatiwa nafasi ya kuwasilisha hoja ya dharura. Kwa kuwa hoja kama hiyo iliwasilishwa juzi na ikaungwa mkono lakini Spika akasema ameshakubaliana na serikali kuwa ingewasilisha kauli. Hata hivyo, jana hakukuwa na kauli ya serikali huku wananchi wakiendelea kupata madhara ya mgomo. Hivyo nikata muongozo kwa kuwa Spika alitumia kanuni ya 49 (2) ambayo kimsingi inatoa mwanya kwa kauli ya serikali kuwasilishwa kwenye wakati atakaoona yeye kuwa na unafaa juu ya jambo linaihusu serikali na lisilozua mjadala. Nilitaka kanuni hiyo isitumike badala yake wabunge tutimize wajibu wa kuisimamia serikali kwa kutumia kanuni ya 47 kuhusu hoja ya dharura. Kwa kuwa ilikuwa muongozo hakukuwa na hitaji la kikanuni la wabunge wengine kuunga mkono lakini akaamua kuilinda serikali kwa kuwa hawakuwa wamejiandaa. Lakini mwishoni ameahidi kuwa kauli ya serikali itatolewa kesho.

Jioni ya leo bunge litajadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali na.2 wa mwaka 2011 ambao kwa sehemu kubwa ukiondoa sheria nyingine unahusu marekebisho ya kimsingi katika sheria ya bodi ya mikopo. Ni kwa bahati mbaya kwamba muswada huu umeletwa na hoja ya kusomwa kwa hatua zake zote tatu katika mkutano mmoja hivyo hakutakuwa na muda wa kukusanya maoni ya wadau kwa upana wake. Ni sehemu ndogo sana ya vifungu vya muswada huu ndio inapaswa kukubalika lakini kwa ujumla muswada huu unakwenda kuingiza mambo ambayo tuliyapinga kwa makongamano, migomo na maandamano yakaondolewa wakati sheria husika inatungwa mwaka 2004. Maudhui ya muswada huu yamenifanya nikumbuke makala ambayo niliandika mwezi kama huu lakini mwaka 2007: http://www.chadema.or.tz/makala/makala.php?id=43 Marekebisho haya yanaenda kuweka mazingira mengine ya migogoro katika elimu ya juu nchini kutokana na masuala ya mikopo kwa wanafunzi. Muswada huu ulipaswa kuja bungeni baada ya ripoti ya Tume ya Rais iliyoundwa tarehe 14 Februari 2011 na kukabidhi taarifa yake tarehe 29 Aprili yenye mapendekezo ya jinsi ya kuboresha utaratibu wa sasa wa ugharamiaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu kuwekwa wazi kwa bunge na kwa umma ili kufanya marekebisho mapana zaidi ya kimfumo.

9 comments:

Anonymous said...

Wananchi sasa wanalazimishwa kuingia barabarani na kuiondoa serikali hii dharimu kwa mawe na nyenzo nyingine za jadi . yaanai kwa kuwa wao hawatibiwi hapo muhimbili ndio wanaona hakuna haja ya angalau kusikia yanayotokea?

Mathias P. Lyamunda said...

Mh. Mnyika, Kimsingi serikali hii inanyanyasa wanafunzi na pia inanyanyasa wanafunzi waliokopeshwa na Board ya mikopo. Nimetafakari sana vitisho vinavyotelewa kwa waliokopeshwa na bodi, kuwa watazuiliwa hata kusafiri au hata kupata huduma za kibenk, hivi wanatumia sheria gani kutoa hivi vitisho! Je, Sheria ya hati za kusafiria inatoa masharti gani kwa mtanzania kupata hati ya kusafiria? Je inataja kudaiwa na bodi kutakufanya mtu asipewe hati ya kusafiria?

Mh. Mnyika kimsingi sisi vijana ambao tulisomeshwa na bodi na sasa tumeajiriwa tunalipa kodi kubwa sana kila mwezi kama PAYE, ambayo ni mchango mkubwa sana kwa bodi ya mikopo ambayo inatumia kodi za wananchi kukopesha wanafunzi! Lakini pia mwajiri wangu alikwisha peleka taarifa zangu kwa bodi toka mwaka 2008, lakini hakupata mrejesho wowote wala maelekezo yoyote kuto bodi ya mikopo, kitendo kinachoonesha utendaji kazi usioridhisha wa bodi! Nakuomba Mh. utembelee maeneo mbalimbali ukusanye maoni ya wanafunzi na yale ya wadaiwa!

NuKtA said...

Kimsingi Mh. Mnyika nimeunga mkono hoja yako kuiona kuwa ni ya msingi na zaidi ya hiko nimeingiwa na hofu kubwa kuona Kiongozi mwenye dhamana ya kuliongoza Bunge anauona mgomo wa Madaktari ni sawa na migomo mingine kama wafanyakazi wa Reli, walimu, wanafunzi n,k hii migomo mingine inazo altenatives na mingine yawezekana kuituliza kisiasa kama wenye hoja zao hawajachoshwa na ahadi tamu za kisiasa zisizotekelezeka. hii hali inapelekea wasomi wengi kuhama nchi kwakuto kuthaminiwa na kurudishwa nyuma kiuchumi kama CCM haiamini iwaulize waendao kutibiwa nje kama hawabongi kiswahili na madaktari wa huko walikokwenda kutibiwa.
Kimsingi kanuni hizi za kudumu za Bunge zimetungwa chini ya Ibara ya 89 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, sasa kifungu alichokitumia Makamo Spika nikutaka kwa makusudi kabisa kulifanya suala hili linalofanana na janga ambalo Bunge lingepaswa kulipokea kama la dharula lionekane ni la kawaida tu. hapa kanuni ni ya 47 na inapata nguvu kwenye kanuni ndogo ya 2 inaposisitiza udharura wa jambo lenyewe kwamba Hoja ya namna hiyo itakuwa ni maalumu na inaweza kutolewa wakati wowote hata kama majadiliano yatakuwa yanaendelea. sasa Makamo spika anapotumia kanuni ya 49 ni upotoshaji wa makusudi wa hoja za msingi. jamani tujiweke sawa 2015 vijana tujiungeni na harakati mbalimbali tuikomboe hii nchi. Ni hayo tu Mh. Mnyika. ni mimi Mpiganaji Kamanda, Prof. Mwaimu.

Elinasi said...

Bodi ya mikopo haijawahi kuwa serious,pamoja na matatizo ya sheria kuwepo ila hakuna uwajibikaji pale,wengi pengine hawajui hata majukumu yao..mwezi wa 11 tulipeleka majina yetu kama wafanya kazi ili waanze kutukata deni ila mpaka leo hakuna hata taarifa kutoka kwao..

Anonymous said...

Kaka Mnyika serikali hii ni tatizo kubwa kiasi cha kufanya politics katika mambo ya msingi, imefuatilia poroja zote za Ndugai ndipo nika pata picha ni bunge la namna gani tunalo.WATANZANI SIASA NI TAALUMA TUSIKUBALI TENA KUBURUZWA NA WANASIASA WASIOWATAALUMA YA SIASA.

Theophil said...

Ndugai hawezi kuruhusu kaui ya serikali ijadiliwe kwani ni msumari kwake. Kumbukeni madaktari wamegoma kwa sababu ya maslahi mabovu ambayo serikali haiwezi kuyatoa kwao huku ikiweza kuyatoa kwa wabunge wasio waaminifu kama huyo Ndugai ambaye analilia posho yake iongezeke

Mathius said...

Ndugai ni zao la ufisadi, unategemea atafanya kinyume na waliomtuma/muweka? Mungu atupe uhai 2015 tulifutilie mbali hili kundi la wanyang'anyi tuanze kuijenga tanzania yetu mpya!

Anonymous said...

Ni masikitiko yangu kuwa bado hoja bungeni zinajadiliwa na kutafuta wingi wa watu ambao kimsingi NI UCHANGA wa siasa. Nilikushihudia Kaka Mnyika ukitoa hoja hii ya msingi ambayo kwa uelewa wa kawaida HAPAKUTEGEMEWA kuwepo wa kupinga hoja hii. Hivi ccm na serikali yao WANAWAPENDA wananchi wa nchi ipi. Kiumbe hai si rahisi kupoteza mifumo yote ya fahamu. hata kama hawaoni "walopinga hoja" hata kusikia/ kuhisi juu ya suala hili la mgomo wa maDr. Kiukweli moto alouwasha Bw. Pinda ni mkubw zaidi ya ule wa mwanzo. Ni lazima viongozi kutambua wanaongea nini kwa rika lipi na matokeo yake ni yapi

immanuel said...

Kimsingi wananchi wamechoshwa sana na hoja na mambo yasiyo na tija kwa taifa bali kwa maslahi ya vyama. wazee wamejaa bungeni na kila kukicha vijana wanazidi kuwa watumwa kwa wazee ambao muda wao wa kustaafu umefika ila wanalindwa lindwa tu kwa maslahi ya mafisadi wachache. Juzi wakati Mh.Nchimbi akiwakilisha hoja bungeni kuhusu vijana kuna baadhi ya wazee walizima tv zao na wengi waliiunga mkono kinafiki huku wakijua wazi kwamba hilo si lengo lao. Ccm wamekuja na hoja hii ili kutafuta tu kura za vijana 2015. Sasa vijana watambue hoja ile ni mtego wa kuwakamata wao katika uchaguzi ujao.Kuna mbunge alihoji kuhusu ucheleweshwaji wa hoja hii na kiukweli hakukuwana jibu la maana la kueleweka zaidi ya kujikanyaga kanyaga kama kawaida yao mimi nauhusisha moja kwa moja ucheweshwaji huo na uchaguzi ujao, nawaasa vijana kuuona mtego huu na kutowapa kura viongozi wanaojipenda wenyewe na kutotambua uraia wao.