Wizara ya Nishati na Madini inayoongozwa na Waziri William Ngeleja ieleze wananchi hatua iliyofikiwa katika kuboresha mifumo ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi kuhusu utafuataji na uchimbaji wa madini ya urani ili kuhakikisha umiliki, manufaa na usalama.
Aidha Wizara ieleze hatua ambazo zimefikiwa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya serikali ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu mauzo na mabadilishano ya umiliki yaliyofanyika baina ya kampuni ya Australia (Mantra Resources) na Kampuni ya Urusi ya ARMZ Uranium Holding kampuni tanzu ya Rosato; kama ambavyo nilihoji Bungeni tarehe 15 Julai 2011.
Pia hatua iliyofikiwa na serikali kufanya marekebisho ya sheria kuweka mipaka ya kiwango cha wigo wa mikopo katika mitaji katika madini kwenye mahesabu ya kodi, kuwezesha kuondolewa kwa riba ya mikopo kwa makampuni yanayohusiana na kuhakikisha kodi ya mauziano ya makampuni makubwa ya madini ya kimataifa hata kama yamefanyika nje ya nchi.
Itakumbukwa kwamba kwa nafasi yangu ya Uwaziri Kivuli wa Nishati na Madini nilieleza masikitiko yetu juu ya maamuzi ya serikali ya kuendelea na hatua za mbele katika utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani bila kukamilisha maandalizi ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi yanayohitajika suala ambalo litaachia mianya ya upotevu wa mapato kwa taifa kama ilivyokuwa kwenye madini mengine na pia itahatarisha usalama.
Tarehe 15 Julai 2011 nikataka serikali itoe maelezo ya kina kuhusu mauzo na mabadilishano ya umiliki yaliyofanyika baina ya kampuni ya Australia (Mantra Resources) na Kampuni ya Urusi ya ARMZ Uranium Holding kampuni tanzu ya Rosato. Mauzo hayo ambayo yanaelezwa kimataifa kuwa yamefanyika kwa bei ya dola 1.16 ambayo ni zaidi ya trilioni 2. Mauzo hayo yamehusisha kuhamishiana umiliki wa maeneo ya Tanzania Mkuju River (Mbamba Bay) na Bahi Kaskazini (Dodoma). Iwapo tungepata asilimia 30 tu ya mauzo hayo kama kodi taifa letu lingepata 600 bilioni ambayo ni fedha nyingi kuliko bajeti nzima ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka.
Izingatiwe kwamba eneo husika lina madini ya urani takribani paundi 108 sawa na asilimia 77 ya uchimbaji wote wa urani kwa mwaka juzi. Hii ni aibu kwa taifa linalokwenda nje kuomba huku ikiachia bwerere fursa za rasilimali za ndani na kufikia hatua hata ya mbuga za wanyama kuvamiwa kwa uchimbaji usio kuwa na tija ya moja kwa moja kwa watanzania walio wengi.
Kwa upande mwingine niliitaka serikali ichukue hatua za kudhibiti ukwepaji kodi na kuongeza mapato ya serikali katika mwaka wa fedha 2011/2012 kwa Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Wizara nyingine zinazohusika: Kutunga Sheria ya kuhakikisha kwamba mikopo kwenye makampuni ya uwekezaji wa madini katika mahesabu ya kodi isizidi 70% ya mtaji; Kutunga Sheria kuhakikisha kwamba riba ya mikopo kwenye makampuni yanayohusiana haitaondolewa kwenye mahesabu ya kodi; Kufanya marekebisho ya sheria kuhakikisha kwamba kodi ya mtaji (capital gains) inatozwa katika mauziano ya makampuni yote ya madini ambayo mali zake au uwekezaji wake uko nchini hata kama mauziano hayo yamefanyika nje ya nchi.
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
26/03/2012
1 comment:
Habari John. Kazi nzuri kupaza sauti ili wezi wajue kuna watu, lakini kazi kubwa inayotakiwa kwa sasa ni kupata rasilimali watu zaidi wenye uwezo na ujasiri wa kulinda, kutetea, na kusimaimia mali asili ya taifa letu. Kupeana habari ni njia nzuri ya kuelimishana na kuamshana. Vijana wa taifa la Tanzania watambue ujana ni leo, taifa tulitakalo liandaliwe wakati uliopo, kwa nguvu ya pamoja tutaweza kuzuia matumizi mabaya ya maliasili yetu, tutaweza kuzuia uvamizi wa ardhi, na akili zetu pia. Vijana waweze kuhoji na kuchukua uamuzi stahiki pale pasipo na jibu ridhisha.
Post a Comment