Tuesday, May 22, 2012

Hatua saba za haraka zinazopaswa kuchukuliwa na Waziri Mpya wa Maji

Toka mabadiliko ya Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya maji yafanyike sikutoa maoni yoyote nikisubiri wateule hao kuanza majukumu yao na kutoa kauli zao kwa umma kuhusu namna walivyojipanga katika kushughulikia matatizo ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam ambalo miaka michache baada mwaka 1961 ulikuwa zaidi ya asilimia 68; hivi sasa miaka 50 baada ya uhuru tumerudi nyuma na upatikanaji ni kwa wastani asilimia 55 tu tena kwa mgawo.


Hali ni mbaya zaidi kuhusu uondoaji wa maji taka ambapo ni chini ya asilimia 10 tu ya makazi ndiyo yaliyounganishwa katika mtandao wa maji taka na hivyo kuleta uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa. Hata katika maeneo yaliyopimwa Jijini Dar es salaam mitandao ya maji taka haijakarabatiwa na kupanuliwa kwa wakati kwa kuzingatia ongezeko la watu suala ambalo lisipochuliwa kwa uzito unaostahili madhara yatatokea katika siku za usoni.

Nilitarajia Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe aanze kazi kwa nguvu ili kurejesha imani juu ya utendaji wake uliochafuka kutokana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika aliyoiongoza awali kugubikwa na tuhuma mbalimbali kwa mujibu wa taarifa za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na madai mengi yaliyotolewa bungeni hususani katika mkutano wanne mwaka 2011 na mkutano wa saba mwaka 2012.

Badala yake amerudia ahadi zile zile kama zilizotolewa na Waziri aliyemtangulia Prof. Mark Mwandosya kwa nyakati na maeneo mbalimbali kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2011 kuhusiana na hatua za utatuzi wa matatizo ya maji safi na maji taka katika Jiji la Dar es salaam ambazo utekelezaji wake unasuasua zaidi ya mwaka mmoja toka zitolewe.

Aidha, siku chache baada kuapishwa Naibu Waziri wa Maji Dk. Binilith Mahenge alifanya ziara ya kutembelea vyanzo vya uzalishaji wa maji na kutoa kauli kuhusu utekelezaji wa miradi, lakini wiki moja baadaye Waziri wa Maji naye akafanya ziara katika vyanzo vile vile na kurudia kauli zenye mwelekeo ule ule ambayo ni matumizi mabaya ya muda na rasilimali nyingine za umma zilizotumika katika ziara hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

Hivyo, baada ya kurejea ofisini kutoka katika ziara hiyo ya vyanzo vya ruvu juu na ruvu chini na kufanya mikutano na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) pamoja na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) natoa mwito kwa Waziri Maghembe kuueleza umma hatua saba za haraka zaidi za Wizara ya Maji kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam.

Katika ya hatua hizo ambazo Waziri Maghembe anapaswa kuzisimamia katika Wizara ya Maji ni; Mosi, kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya kashfa ya taifa ya kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 ambapo Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji.

Pili; kuwasilisha bungeni Mpango Maalum wa kuboresha huduma za Majisafi na uondoaji wa Maji Taka katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 kwa ajili ya kuidhinishwa, kutengewa bajeti kamili ya utekelezaji wa haraka katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kusimamiwa ipasavyo kwa msukumo wa kibunge badala ya ahadi za ujumla za kwenye ziara.

Tatu; Waziri Maghembe aeleze hatua zilizopangwa kuchukuliwa kufuatia ziara yake kuhakikisha Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 unawekewa muda wa ukomo wa kukamilika ndani ya miezi mitatu katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa.

Nne; Waziri Maghembe akubaliane na pendekezo nililotoa bungeni kwa nyakati mbalimbali la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa thamani ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.

Tano; Waziri Maghembe ahakikishe Wizara ya Maji inaisimamia EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali. Aidha, Wizara ya Maji ihakikishe EWURA inaharakisha kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es salaam.

Sita; Waziri Maghembe awezeshe Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on the management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012 iliyotolewa na CAG kabla ya mkutano wa nane wa bunge ulipangwa kuanza tarehe 12 Juni 2012 ili maoni na mapendekezo yazingatiwe wakati wa mchakato wa bajeti.

Saba; Wizara ya Maji ihakikishe Serikali inawasilisha kwenye mkutano wa tisa wa bunge muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka (Water Supply and Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili kushughulikia upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.

Imetolewa tarehe 20 Mei 2012

1 comment:

Anonymous said...

Baba bila maji Kimara Bonyokwa by 2015 sahau kura yangu na wote nitakaoweza kuwashawishi.