Saturday, May 12, 2012

Waziri Kigoda anusuru viwanda walivyovibinafsisha kwa kuanza na cha Nguo Urafiki

Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Abdalah Kigoda anapaswa kuweka kipaumbele katika kunusuru viwanda vilivyo katika hali mbaya kutokana na matatizo yaliyotokana na ubinafsishaji pamoja na ufisadi katika mchakato wa uwekezaji ili kuchangia katika kuinua uchumi wa nchi na kuongeza ajira nchini.




Waziri Kigoda atumie nafasi hiyo kurekebisha kasoro ambazo serikali za awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa ambayo yeye alikuwa mmoja wa mawaziri akiwa ofisi ya rais mipango na ubinafsishaji ilizisababisha.



Waziri Kigoda amehusika katika ubinafsishaji wa viwanda, kuratibu urekebishaji wa mashirika ya umma na kusimamia kisera utendaji wa mashirika yaliyobinafsishwa; kuteuliwa uwaziri wa viwanda na biashara kuwe ni fursa kwake ya kurekebisha makosa ya awali.



Nimemkaribisha kutembelea Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kabla ya mkutano wa bunge la bajeti unaotarajiwa kuanza tarehe 12 Juni 2012 ili kushughulikia udhaifu wa kiutendaji, ufisadi dhidi ya mali za kampuni, kulinda maslahi ya wafanyakazi na kushughulikia kasoro katika mchakato wa ubinafsishaji.



Waziri wa Viwanda na Biashara azingatie kuwa matatizo ya kiwanda cha urafiki ni zaidi ya changamoto za kawaida kwa kuwa ni matokeo ya kasoro katika mchakato mzima wa ubinafsishaji, udhaifu wa kiutendaji wa miaka mingi pamoja na ufisadi uliokithiri unaohitaji uchunguzi maalum.



Aidha mchakato wa kutafuta mwekezaji mpya unaoendelea hivi sasa unaohusu kampuni ya China iliyokuwa ikimiliki hisa asilimia umegubikwa na utata na wakati huo huo kuna mchakato mwingine wa kinyemela wa kutaka kuuza hisa asilimia 49 zinazomilikiwa na Serikali kwa niaba ya Watanzania.



Kama inavyofahamika, moja ya viwanda vikubwa vya nguo hapa nchini vilivyojengwa wakati wa Awamu ya Kwanza ya Utawala wa nchi yetu chini ya Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kiwanda cha Nguo cha Urafiki ambacho kilijengwa miaka michache baada ya uhuru kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka nchi ya China. Baadaye kiwanda kilibinafsishwa kiholela na sasa kinaendeshwa kwa ubia kuanzia mwaka 1997 ambapo serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 49 ya hisa huku asilimia 51 zikiwa chini ya kampuni ya nchini China.



Pamoja na kuwa mwenye hisa nyingi ndiye anawajibika zaidi katika uendeshaji wa kiwanda kiuendeshaji na maslahi ya wafanyakazi, serikali kwa kuwa na hisa 49% kwa niaba ya watanzania ina wajibu wa pekee wa kufuatilia kwa karibu hali ya kiwanda kama sehemu ya kulinda viwanda vya ndani, kudhibiti hasara kwa serikali na kuzuia upotevu wa mali za umma. Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka kumi wajibu huu umekuwa hautekelezwi ipasavyo hali ambayo imedidimiza kiwanda kwa kiwango kikubwa na kuathiri uzalishaji pamoja na kupunguza ajira.



Baada ya kubaini hali hiyo tarehe 4 Februari 2011 nilitembelea Kiwanda cha Nguo cha Urafiki Ubungo na kufanya mazungumzo na wafanyakazi pamoja na wawakilishi wa menejimenti. Kutokana na mkutano huo na vyanzo vingine nilipata maelezo ya kina kuhusu hali mbaya ya kiwanda ikiwemo kusimama kwa uzalishaji wa nguo na maslahi duni ya wafanyakazi.



Kufuatia taarifa hizo nilichukua hatua ya kuziandikia mamlaka husika kuweza kuchukua hatua za haraka kunusuru hali ya kiwanda. Kutokana na mamlaka husika kuchelewa kuchukua hatua nilikwenda mbele zaidi kwa kutumia mamlaka ya kibunge kuhoji mawaziri husika wakati wa mkutano wa nne wa Bunge wakati wa kujadiliwa kwa bajeti za wizara mbalimbali mwaka 2011.



Baadhi ya Wizara nilizozitaka kuchukua hatua ni pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha hususani ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika Hodhi la Mali ya Mashirika ya Umma (CHC), Wizara ya Kazi na Ajira na mamlaka zingine. Hatua ambazo zimechukuliwa mpaka sasa zimekuwa za kususua na hazionyeshi kama serikali inayachukulia matatizo ya Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kwa uzito unaostahili.



Pamoja na kuitaka serikali kuchukua hatua pia nilitoa mwito kwa kamati husika za bunge kuchukua hatua ambapo kamati ya Viwanda na Biashara iliitikia mwito huo na Novemba 2011 ilitembelea kiwanda na kushuhudia ukweli wa madai ambayo tumekuwa tukiyatoa kuhusu hali mbaya ya kiwanda. Kamati hiyo ilitoa kauli ya kutaka uchunguzi wa ziada ufanyike hatua ambayo haijatekelezwa mpaka hivi sasa.



Izingatiwe kuwa kabla ya Kuingia ubia, Serikali ilifanya ukarabati mkubwa wa mitambo kwa gharama za walipa kodi watanzania. Aidha, mara baada ya ubia serikali ya Tanzania iliingia mkataba mwingine na Serikali ya China wa mkopo wa dola milioni 27 (zaidi ya bilioni 30) kwa ajili ununuzi wa mitambo mipya badala yake kwa sehemu kubwa fedha hizo zikatumika kununua mitambo chakavu.



Matokeo yake uzalishaji ukaanza kupungua na wafanyakazi wakaanza kupunguzwa na hivyo kusababisha kushuka kwa mapato ya serikali na kuongezeka kwa matatizo ya ajira. Pia, kutokana na matatizo hayo baadhi ya mitambo imeondolewa na kuuzwa kinyemela kama vyuma chakavu hali ambayo imesababisha wafanyakazi kupewa likizo wengi bila malipo na wengine kwa malipo pungufu kwa visingizio mbalimbali. Kutokana na hali hiyo nilizitaka Wizara na Mamlaka husika kuchunguza madai hayo na kuongeza ukaribu wa serikali katika uendeshaji wa kiwanda husika.



Kwa upande mwingine maslahi ya wafanyakazi nayo yamezidi kuwa duni badala kuboreshwa baada ya ubia kuingiwa na hivyo kushusha motisha ya ufanyaji wa kazi. Pia wafanyakazi hawalipwi mishahara kwa viwango vipya vilivyotangazwa na serikali katika hatua za awali. Hali hizi zimesababisha migogoro mbalimbali kati ya kampuni na serikali kwa upande mmoja na wafanyakazi walioko kazini na walioachishwa kwa upande mwingine na hivyo kuongeza mizigo ya madeni kupitia hukumu za mahakama, mamlaka zingine na madai lukuki. Kufuatia hali hiyo kudumu kwa muda mrefu zaidi ya miaka kumi, nilitoa mwito kwa Wizara na Mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kumaliza matatizo ya wafanyakazi katika Kiwanda cha Nguo cha Urafiki ili kuelekeza nguvu katika uzalishaji.



Katika mikutano ya tatu na nne ya Bunge kwa nyakati na njia mbalimbali nilizieleza pia Wizara na mamlaka mbalimbali za serikali kuwa hali mbaya ya kiwanda inahusisha pia kukosekana kwa udhibiti katika mali za kampuni na pia kiwanda kuanza kufanya shughuli ambazo ziko nje ya kazi ya msingi ya ubia wa uzalishaji wa nguo. Niliitaka serikali kuchunguza na kuchukua hatua juu ya shughuli zinazoendelea kufanywa na Kiwanda cha Nguo cha Urafiki nje ya mikataba na misingi ya ubia mathalani: upangishaji wa Nyumba za wafanyakazi, upangishaji wa maeneo ya wazi, upangishaji wa maghala ya kiwanda, uuzaji wa nyumba za wafanyakazi, mfano mzuri ni nyumba 50 za THB eneo la Manzese, na ukodishaji wa maeneo kwa ajili ya kufanya biashara ya mafuta. Hali hii imeambatana na uingizaji wa bidhaa za nje kwa mgongo wa kampuni ya Urafiki na zingine tanzu kinyume na ubia wenye msingi wa kulinda na kuendeleza viwanda vya ndani hali ambayo imeleta athari katika uchumi wa taifa na kupunguza ajira za uzalishaji.



Kutokana na hali hiyo nilitoa mwito kwa Serikali kuingilia kati kupitia Wizara ya Fedha hususani Ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) na Wizara ya Viwanda na Biashara kuchukua hatua zinazostahili juu ya kiwanda cha Urafiki. Aidha, kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara kuchukua hatua za kuisimamia serikali ili kuharakisha hatua za kunusuru kiwanda hiki kama ili kuonyesha pia mfano wa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhusu viwanda vingine. Hata hivyo, mpaka sasa hakuna hatua kamili zilizochukuliwa na Wizara na Mamlaka husika hali ambayo imefanya niendelee kutaka uwajibikaji wa serikali hata baada ya mabadiliko ya baraza la mawaziri.



John Mnyika (Mb)

11/05/2012

No comments: