Friday, May 4, 2012

Fidia ya barabara ya Ubungo Kibangu mpaka Makuburi Makoka imeanza kulipwa; nitaendelea kuisimamia serikali kwa hatua zaidi

Fidia kwa wananchi wa wa Kibangu kuwezesha mchakato wa ujenzi wa njia mbadala kwa wakazi wa Mitaa ya Ubungo – Kibangu na mwongozo katika Kata ya Makuburi inaendelea kulipwa kufuatia barabara iliyokuwa ikitumika kuzolewa na maji kutokana na kuwa pembeni ya mto Gide.



Mpaka leo tarehe 3 Mei 2012 jumla ya shilingi 122,543, 264 zimelipwa kwa nyumba chache zilizobaki na yamesalia malipo ya milioni 64 tu ili notisi kwa wakazi waliosalia iweze kutolewa na hatimaye barabara iweze kufunguliwa hatua za matengenezo ziweze kufuata.


Hivyo, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Manispaa ya Kinondoni kuharakisha malipo ili kuepusha gharama za fidia kuongezeka kwa kuzingitia kuwa iwapo malipo yangefanyika kwa wakati mwaka 2010 gharama za fidia zingekuwa milioni 80 tu lakini sasa zimeongezeka mpaka kufikia zaidi ya milioni 180.


Tarehe 26 Januari 2012 nilifanya mazungumzo ya kikazi na wawakilishi wananchi toka Makuburi pamoja na Meya na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na hatimaye nikafanikisha wananchi hao kukutana na watendaji wa Manispaa na fedha zao za fidia kutengwa.

Hata hivyo, kabla ya kukabidhiwa fedha hizo baadhi yao walikataa kiwango ambacho walikuwa wamekubaliana awali kwa maelezo kwamba thamani za nyumba zao zimepanda baada ya serikali kuchelewa kuwalipa kwa miaka mingi, hawajaridhika na kiwango cha riba kilichowapa nyongeza kwa miaka husika kwa kutozingatia bei ya soko.

Niliendelea kufuatilia suala husika kupitia mikutano ya baraza la madiwani tarehe 25 Februari na 28 Februari 2012 na Manispaa iliahidi kufanya majadiliano nao tena kuweza kutoa nyongeza na kufanya malipo mwezi Machi 2012.


Ikumbukwe kwamba Tarehe 7 Februari 2011 nilimuandikia barua Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Mkuchika kumkumbusha kwamba katika Kikao cha kumi na nne cha Mkutano wa Ishirini wa Bunge la Tisa mnamo tarehe 23 Juni 2010 Waziri wa TAMISEMI wa wakati huo aliahidi bungeni kwa niaba ya serikali kukamilisha mchakato wa ujenzi wa njia mbadala kwa wakazi wa Mitaa ya Ubungo – Kibangu na mwongozo katika Kata ya Makuburi , kufuatia njia iliyokuwa ikitumika kuzolewa na maji kutokana na kuwa pembeni ya mto Gide.


Nilitaka ahadi hiyo itekelezwe kwa haraka kutokana na adha ambao wananchi wa eneo husika wanaipata hivi sasa na pia kutokana na ukweli kuwa kuanzia mwaka 2005 kwa nyakati tofauti serikali ngazi mbalimbali imekuwa ikiahidi kujenga njia mbadala kwa ajili ya eneo husika.


Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilishafanya tathmini ya gharama za ukarabati huo ambao utahusisha kazi za ujenga kingo za mto kwa kutumia Gabions kujaza kifusi na kushindilia. Kwa ujumlawake gharama hizo zilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi 836,458,000/=.


Aidha mpaka kufikia Juni 2010 malipo ya nyumba nne yalishafanywa ambayo yaligharimu shilingi 16,240,262/= ambapo wananchi (2) walilipwa fidia zao. Kilichokuwa kimebaki ni kukamilisha utaratibu wa malipo ya nyingine zilizobaki kwa wakazi waliobaki ambazo kwa mujibu wa tathmini ya wakati huo ilikuwa shilingi 80,195,307/=.

No comments: