Tuesday, May 1, 2012

WAFANYAKAZI, UWAJIBIKAJI na KESI za UCHAGUZI

Mei Mosi, niko ofisini tukiendelea na kazi lakini nimeona niandike machache kutokana na maswali ambayo nimeanza kuulizwa juu ya maoni yangu kutokana na hotuba ya Rais na juu ya masuala ya kesi za uchaguzi. Mengine zaidi tutaelezana baada ya kazi jimboni;


WAFANYAKAZI: Nawatakia heri katika siku ya wafanyakazi; risala iliyosomwa kwa JK sehemu kubwa ni mambo yaleyale ambayo Rais amekuwa akielezwa na wafanyakazi miaka kadhaa mfululizo , aeleze amefikia wapi kwa takwimu katika nyongeza ya mishahara, punguzo la kodi nk. Mei Mosi ya 2011 alitoa maneno matupu kwa wafanyakazi kuwa wasubiri bajeti, nikasema ilikuwa ahadi hewa na kweli ikiwa ni usanii hata bungeni. Sasa amerudia tena kauli zile zile. Kuhusu mfumuko wa bei, maneno ya Rais yamedhihirisha kwamba tatizo letu kubwa zaidi si la kiuchumi bali ni udhaifu wa uongozi, ufisadi na kutetereka kwa misingi ya utawala wa sheria katika sekta muhimu za nishati na kilimo. Sijaridhika pia na maelezo aliyotoa kuhusu namna serikali inavyoshughulikia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana. Ni vizuri tu Rais akarejea ushauri na mapendekezo yetu kuhusu masuala yote matatu ya wafanyakazi, mfumuko wa bei na ajira kwa vijana tuliyotoa ndani na nje ya bunge kwa nyakati mbalimbali na kuisimamia vizuri serikali kuhakikisha yanatekelezwa.

UWAJIBIKAJI: Kuhusu uwajibikaji kutokana na taarifa za CAG na mijadala ya bungeni, historia aliyoieleza Rais Kikwete ya toka 2007 imedhihirisha nilichokisema siku chache zilizopita kuwa hatuna serikali na mamlaka ya Rais hayatumiki vizuri kwa maslahi ya umma, inaonyesha taarifa zote Rais; hata hizi zilizojadiliwa mwaka 2012 Rais alikuwa nazo toka 2009/2010, angetumia vizuri madaraka yake kwa mujibu wa katiba vyombo vya dola na mamlaka zingine zingeshachukua hatua. Lakini ameendelea kusema tu serikali imepokea mapendekezo kutoka bungeni na inayafanyia kazi huku uzembe na ufisadi ukiendelea kutamalaki katika utumishi wa umma toka Orodha ya Mafisadi (List of Shame) itolewe mpaka sasa. Tuendelee kuunganisha nguvu ya umma kusimamia uwajibikaji mpaka kieleweke.

KESI ZA UCHAGUZI: Nashukuru Mbassa ameshinda Biharamulo, Sumbawanga Mjini tumepata jimbo wazi la kwenda kulikomboa; Ubungo tutakwenda mahakamani kesho kwa ajili ya kupatiwa mwenendo wa kesi (court proceedings) kwa ajili ya kufanya uwasilishaji wa mwisho (final submission) kabla ya hukumu kutolewa. Maslahi ya UMMA kwanza

1 comment:

Anonymous said...

Si mkazi wa jimbo lako wala si mkazi wa Dar, lakini navutiwa sana na huu mpango wako wa kazi!

Mungu akupe afya ili kazi yako iendelee