Jana jumapili tarehe 6 Mei 2012 nimekabidhi zaidi ya vitabu mia saba (700) kama ishara ya kuanzisha Programu ya Taarifa iitwayo “Toa Kitabu Kisomwe”, hii ni miezi mitatu baada ya kusambaza kwa wananchi wa jimbo la Ubungo vitabu 4500 ikiwa ni pamoja na nakala za katiba ya nchi na vitabu kuhusu mchakato wa katiba mpya; na kufanya jumla ya vitabu ambavyo nimesambaza mpaka sasa kuwa zaidi ya elfu tano (5,000).
Lengo ya Programu ya Taarifa ya “Toa Kitabu Kisomwe” ni kusambaza jumla ya vitabu visivyopungua elfu hamsini (50,000) ndani ya Manispaa ya Kinondoni katika kipindi cha mwaka ili kuchochea uhuru wa kifikra na kuchangia katika ustawi wa wananchi.
Kwa mtazamo wangu akili na vipaji ambavyo kila mwanadamu amejaliwa ndiyo mtaji mkuu wa kujikwamua kimaisha. Hivyo kushirikiana kuwezesha elimu bora na uhuru wa kifikra ni msingi muhimu wa kuchochea maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla.
Elimu bora sio majengo pekee bali ni pamoja na walimu bora na mazingira bora ya kusomea na kujifunzia yenye vifaa vya kujifunzia na vitabu vya kiada na ziada.
Hivyo, harakati za kusimamia uwajibikaji wa serikali kuu, serikali za mitaa na mamlaka nyingine zinazohusika na sekta ya elimu hususani kwenye shule, vyuo na vyuo vikuu vya umma zinapaswa kuendelezwa.
Tuendelee kuhakikisha rasilimali zinazotengwa ikiwemo ruzuku ya elimu ya msingi na sekondari na mikopo ya elimu ya juu zinakuwa za kutosha, zinatolewa kwa wakati na zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kudhibiti mianya ya ufisadi.
Wakati, tukisimamia uwajibikaji huo wa serikali tutambue masuala matatu muhimu; mosi, jukumu la kuboresha mazingira ya elimu kwenye elimu rasmi ya darasani sio wa serikali pekee bali ni wajibu wa wote katika jamii.
Pili, izingatiwe kuwa sehemu kubwa ya wananchi hawajapata elimu rasmi hivyo ni muhimu kuwa na mifumo ya elimu kwa njia nyingine mitaani na vijijini ili kuchochea zaidi maendeleo.
Tatu, hata kwa wenye elimu rasmi inafahamika kuwa elimu haina mwisho hivyo kila mmoja ana wajibu wa kujisomea ili kuendeleza uhuru wa kifikra.
Katika muktadha wa masuala hayo matatu, niliungana na Asasi ya Maendeleo Ubungo (Ubungo Development Initiative-UDI) kuzindua Programu ya Taarifa inayohusisha kukusanya vitabu vya kiada na vya ziada kutoka wa watu mbalimbali na taasisi mbalimbali na kuvisambaza katika taasisi za elimu kwa ajili ya wanafunzi kusoma na maeneo maalumu kwa ajili ya wananchi kujisomea.
Mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema kwamba ukimpa mtu samaki umemlisha kwa siku moja lakini ukimfundisha kuvua umemlisha kwa maisha yake yote. Nikisisitiza mantiki ya msemo huo naweza kusema pia kwamba ukimpa mtu chakula cha kawaida umemshibisha kwa muda mfupi lakini ukimpa chakula cha kifikra umemuwezesha kwa muda mrefu; huu ndio msingi utakaoongoza Programu ya Taarifa; “Toa kitabu kisomwe”.
Kupitia programu hii tunaomba taasisi au mwananchi yoyote mwenye kitabu chochote popote ambaye yuko tayari kukitoa ili kisomwe iwe ni cha kiada au cha ziada awasiliane UDI ili iweze kufikisha kitabu hicho kwa walengwa.
Ukipenda unaweza kuweka saini kwenye kitabu hicho kama kumbukumbu kuwa taasisi yenu au wewe ndiye uliye “Toa kitabu Kisomwe” au unaweza pia kutueleza kitabu hicho unapendekezwa kipelekwe wapi ndani ya Manispaa ya Kinondoni ili kiweze kusomwa kwa ufanisi.
Sisi mpango wetu ni kusambaza vitabu hivyo kwenye maktaba za shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kwa upande wa elimu ya kiada na kusambaza kwenye maktaba za jumuia, ofisi za serikali za mtaa, taasisi za kijamii na vijiwe vya kudumu kwa upande wa elimu ya ziada.
Naamini kwamba kwenye kaya mbalimbali za Manispaa ya Kinondoni vipo vitabu makabatini au masandukuni ambavyo ama ni vya kiada vilivyoachwa baada ya walengwa wa awali kupanda ngazi moja ya elimu kutoka ile ambayo walikuwa wakisoma au ni vya ziada ambavyo tayari wahusika walishavitumia na vinaweza kuwa na mchango mkubwa kwa walengwa wengine wenye kuvihitaji hivyo; “Toa Kitabu Kisomwe”.
Aidha, naamini pia kwamba Jiji la Dar es salaam lina makao makuu ya taasisi mbalimbali ambazo hutoa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kusambaza nchini lakini wakati mwingine hushindwa kuwafikia walengwa katika ngazi ya chini jijini hivyo UDI kwa kuwa taasisi ya ngazi ya chini inaweza kuwa kiungo kizuri cha kuwezesha vitabu husika kuwafikia walengwa; “Toa Kitabu Kisomwe”.
“Toa kitabu kisomwe” kupitia ofisi ya UDI iliyopo Kimara Kona au wasiliana na UDI kupitia Afisa Taarifa (0768503331 au 0715745874) au barua pepe ubungo2005@yahoo.com kutoa kitabu husika.
Nilitumia pia fursa hiyo kuitaka serikali kutoa kauli kuhusu hatua iliyofikiwa katika kusambaza vitabu na vifaa vingine vilivyonunuliwa kutokana fedha iliyorejeshwa baada ya ufisadi wa Rada kubainika.
Pia, nilitoa pia mwito kwa wananchi katika mchakato wa maoni ya katiba mpya kuhakikisha haki za elimu na taarifa zinatolewa kikamilifu na kulindwa kikatiba tofauti na katika katiba mbovu ya sasa ambayo imetaja haki hizo na kuziwekewa mazingira ya kupokonywa na serikali kujitoa katika wajibu wa kisheria wa kuhakikisha zinapatikana. Wakati mabadiliko hayo yakisubiriwa serikali iharakishe kuwasilisha bungeni muswada wa sheria ya uhuru wa taarifa ambayo ni nyenzo muhimu ya kupambana na ufisadi na kuchochea maendeleo nchini.
5 comments:
HILI NI JAMBO JEMA MP NITASHIRIKI KWA KADIRI NIWEZAVYO
Big up JJM, spread more fire
Hili ni moja ya mawazo chanya sana mkuu...
Taifa lolote haliwezi kusonga mbele kama watu wake hawasomi,ELIMU ndio mama wa ukombozi wowote ule.umeonyesha njia,big up sana.mh.mnyika.
Nadhani tukimaliza tunahitaji kuanzisha/kufufua maktaba za wilaya na ikibidi tuwe na maktaba kila kata,lazima TUSOME na TUSOME kwa bidii,TUSOME AU TU WATUMWA WA WATU WENGINE.
Post a Comment