Tuesday, May 22, 2012

Ufisadi TANESCO, mikataba mibovu na mpango wa dharura wa umeme-majibu kwa Waziri Mpya wa Nishati na Madini

Toka waziri na manaibu waziri wapya wa wizara ya nishati na madini wateuliwe kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini sikutoa maoni yoyote kwa sababu ya kuwapa muda wa kuingia ofisini na kuanza kazi.


Kwa nyakati mbalimbali Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo toka ateuliwe ameeleza kuwa atakuwa waziri wa matendo kuliko maneno, na kwa kuanzia amezungumza kuhusu sekta ndogo ya umeme na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari tarehe 20 Mei 2012 na 21 Mei 2012.

Amenukuliwa akitoa ahadi za maneno kuhusu masuala yafuatayo: Kushughulikia orodha ya watuhumiwa wa ufisadi ndani ya TANESCO; Kusimamia mapitio ya mikataba mibovu kwenye sekta ya umeme; Kuagiza watumike wataalamu wa ndani kabla ya wataalamu wa nje; Kuharakisha utekelezaji wa mipango ya umeme.

Nasubiria kuona matendo na nitahoji utekelezaji wa ahadi husika kwenye mkutano wa nane wa bunge unaoanza tarehe 12 Juni 2012 kwa nafasi yangu ya uwaziri kivuli wa nishati na madini na mbunge wa Jimbo la Ubungo yalipo makao makuu ya TANESCO.

Hata hivyo, katika kuchukua hatua za vitendo kuhusu masuala hayo Waziri wa Nishati na Madini na manaibu wake wapitie kumbukumbu za kibunge na mchango wetu kwa nyakati mbalimbali kwa Wizara ya Nishati na Madini kupata hatua za vitendo zinazopaswa kuchukuliwa kuhusu sekta ndogo ya umeme kwa upana wake; na kwa machache niliyoyanukuu kutoka kwenye vyombo vya habari ni muhimu wakazingatia yafuatayo:

Mosi; kushughulikia orodha ya watuhumiwa wa ufisadi ndani ya TANESCO

Waziri Muhongo azingatie kuwa hii si mara ya kwanza kwa orodha ya watuhumiwa wa ufisadi ndani ya TANESCO kuwasilishwa Wizara ya Nishati na Madini, katika siku za karibuni agizo lingine la kuwasilisha orodha lilitolewa mwaka 2010 na mwaka 2011 wafanyakazi wa TANESCO wakazungumza tena kwa uchungu kuhusu ufisadi ndani ya shirika hilo la umma na mafisadi wanaohusika. Ni muhimu Waziri akarejea pia katika orodha ya siri iliyowasilishwa mwanzo na iwapo kuna majina ya watuhumiwa wa ufisadi yamejirudia kwa mara nyingine tena achukue hatua za vitendo za kuitoa orodha hadharani na pia kutaka maelezo toka kwa vyombo vya uchunguzi vya kiserikali na mamlaka za nidhamu za watumishi hao kupata maelezo ya hatua ambazo zilichukuliwa toka orodha hizo ziwasilishwe.Waziri Muhongo azingatie pia orodha hiyo haipaswi kuhusu watumishi wa TANESCO pekee kwa kuwa ufisadi ndani ya shirika hilo unatokana na msukumo wa ufisadi toka kwa watuhumiwa wa ufisadi wa ndani ya Wizara ya Nishati na Madini na pia wataalamu kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali. Baadhi ya majina yao yametajwa pia bungeni kwa nyakati mbalimbali hivyo anachopaswa kufanya ni kusimamia kwa vitendo utekelezaji wa maazimio yaliyobaki ya bunge ya mwaka 2008 juu ya mkataba baina ya TANESCO na kampuni ya Richmond Development Company LLC na ya mwaka 2011 kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni na kuhusu uendeshaji wa sekta ndogo ya gesi nchini.

Pili; Kusimamia mapitio ya mikataba mibovu kwenye sekta ya umeme

Waziri Muhongo azingatie ahadi za maneno za kufanya mapitio ya mikataba mibovu kwenye sekta ndogo ya umeme zilianza toka mwaka 2008 hivyo anachopaswa kusema ni kueleza hatua za vitendo vilizofikiwa katika kufanya mapitio ya mikataba kwa kurejea rai yangu ya mara kwa mara kuwa toka mijadala miwili muhimu inayogusa sekta ndogo ya umeme kufungwa mwaka 2010 na ni miaka minne toka maazimio yapitishwe na bunge kuhusu masuala husika. Baadhi ya maazimio hayo ni Azimio Na. 3, ambalo liliagiza kwamba “Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC (uliorithiwa na Dowans Holdings S.A.) na ile kati ya TANESCO na IPTL, SONGAS, AGGREKO na Alstom Power Rentals, ipitiwe upya mapema iwezekanavyo kama ambavyo Mikataba ya Madini ilivyopitiwa upya na Serikali”. Iwapo Azimio hili lingetekelezwa kwa ukamilifu wake, gharama za uzalishaji TANESCO na serikali kwa ujumla zinazotokana na matatizo katika mikataba zingepungua. Pia, Azimio Na. 13, “Serikali izihusishe Kamati za Kudumu za Bunge kwenye hatua za awali za maandalizi ya Mikataba mikubwa ya muda mrefu ya kibiashara ili kuondokana na utaratibu uliopitwa na wakati kwamba Mikataba ya Kibiashara ni siri hata kwa walipa kodi wenyewe. Aidha, Serikali ihakikishe kuwa, Kamati zote za Bunge zinapitia Mikataba mikubwa ya muda mrefu ya kibiashara chini ya sekta zao ili kuliondolea Taifa mizigo isiyo ya lazima”. Azimio hili halijaanza kutekelezwa kwa ukamilifu wake matokeo yake ni kwamba serikali katika kipindi cha kati ya mwaka 2008 mpaka 2012 kumeendelea kuwa na usiri katika hatua za awali za maandalizi ya mikataba na pia mikataba mingi mikubwa haijafanyiwa mapitio. Kwa utaratibu wa sasa kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge ya mwaka 1988 pamoja na kanuni na taratibu za bunge, kamati au mbunge anaweza kuomba kwa serikali kupitia kwa ofisi ya bunge nakala ya mikataba baada ya kusainiwa hali ambayo hailiwezeshi bunge kutimiza kikamilifu wajibu wa kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 63 ya kuisimamia serikali katika hatua zote muhimu.Tatu; kuagiza watumike wataalamu wa ndani kabla ya wataalamu wa nje

Namuunga mkono Waziri Muhongo katika azma ya kutumia wataalamu wa ndani kabla ya wataalamu wan je, hata hivyo ni muhimu Waziri akarejea kwenye hotuba yetu bungeni ya tarehe 15 Julai 2011 na kuzingatia masuala ya msingi ya kuwezesha utekelezaji wa agizo hili kwa kuweka mifumo muhimu kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013. Aidha, Waziri Muhongo apanue wigo wa dhana hii ya kuwashirikisha wataalamu na makampuni ya ndani sio tu kwenye kutumia wataalamu washauri bali mkazo uwekwe pia kwenye makandarasi na ununuzi unaofanywa na mashirika na taasisi zilizochini ya Wizara ya Nishati na Madini ikiwemo TANESCO ili kunusuru uchumi wa nchi na kuchangia katika ajira nchini. Hata hivyo, katika kutumia watalaamu hao wa ndani pamoja na kupanua wigo wa wazabuni kutoka ndani, Waziri Muhongo awezeshe ukaguzi maalum ili wataalamu na makandarasi waliohusika katika ufisadi dhidi ya TANESCO na mashirika mengine yaliyochini ya Wizara ya Nishati na Madini waondolewe katika orodha (black listing).

Nne; kuharakisha utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme.

Waziri Muhongo ameahidi kusimamia kwa kusimamia ongezeko la uzalishaji na usambazaji wa umeme na katika kufanya hivyo pamoja na mipango ya muda mrefu atoe taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa Mpango wa dharura wa umeme kabla ya mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 12 Juni 2012.

Waziri Muhongo azingatie kuwa matatizo ya sasa ni matokeo ya udhaifu wa kisera na kiutendaji kuanzia wakati wa Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi na baadaye kwa Rais awamu ya tatu Benjamin Mkapa ambapo TANESCO iliwekwa kwenye orodha ya mashirika ya kubinafsishwa na hivyo serikali kuacha kuwekeza kikamilifu katika uzalishaji wa umeme pamoja na matengenezo ya miundombinu ya usafirishaji na usambazaji. Aidha, ni katika kipindi hicho hicho kuliibuka matatizo pia ya ufisadi kwenye uwekezaji katika sekta ya nishati kama ya IPTL, Kiwira, Net Group Solution nk. Awamu ya nne ya Rais Kikwete nayo ikaongeza zaidi mzigo kwa TANESCO kupitia miradi mingine ya kifisadi kama ya Richmond na sasa kuna tuhuma mpya za ufisadi kuhusu utekelezaji wa Mpango wa dharura wa umeme.

Mpango wa Dharura uliwasilishwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011, ahadi ya serikali ilikuwa kuongeza MW 572 ifikapo mwezi Disemba 2011 na kuweka orodha ya mitambo ya kununua kabla ya oktoba 2012. Pamoja na kuwa na mpango wa gharama kubwa wa dharura ambayo unahusisha kwa sehemu kubwa suluhisho la muda mfupi la kukodi mitambo, bado utekelezaji wa mpango wenyewe nao unasuasua hali inayodhihirisha kuendelea kwa uzembe na udhaifu katika serikali. Hata mitambo iliyofungwa nayo haina uhakika wa kuwa na uwezo wa kuendeshwa wakati wote uliopangwa kutokana na madeni TANESCO ambayo inadaiwa, serikali kushindwa kutekeleza kikamilifu ahadi ilizotoa kwa TANESCO na pia upungufu wa gesi kwa ajili ya kuendeshea mitambo husika na kuwa tishio kwa nchi kuingia gizani katika siku za usoni. Kati ya miradi ambayo utekelezaji wake umesuasua kinyume na ahadi za serikali bungeni ni pamoja na kununua mtambo wa MW 150 wa NSSF na kununua mitambo ya MW 100 wa TANESCO Ubungo.

Kwa upande mwingine, udhaifu wa kutokutekeleza mipango ya uzalishaji wa gesi na makaa ya mawe kwa wakati umesababisha utegemezi mkubwa kwenye matumizi ya mafuta katika mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura. Zaidi ya nusu ya umeme unaozalishwa nchini hivi sasa ambao ni sawa na takribani MW 660 unazalishwa kwa kutumia dizeli, mafuta ya ndege na mafuta mazito hali ambayo imeongeza mahitaji makubwa ya uagizaji wa mafuta toka nje ya nchi. Hii imesababisha mahitaji makubwa ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mafuta na hivyo kuchangia katika kuporomoka kwa thamani ya shilingi. Aidha, ongezeko kubwa la uagizaji toka nje limeathiri urari wa biashara na hivyo kuchangia katika mfumuko wa bei. Hivyo, watanzania hivi sasa wanabeba mzigo wa kupanda kwa bei za bidhaa na gharama za maisha kwa ujumla kutokana na ufisadi kwenye mikataba, ubadhirifu katika matumizi, uzembe katika uongozi na upungufu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali kwenye sekta ya nishati.

Waziri Muhongo arejee tahadhari niliyotoa bungeni kuhusu gharama kubwa za mpango wa dharura wa umeme na kupendekeza vyanzo mbadala vya fedha ambavyo serikali ilivipuuza. Ikumbukwe kwamba tarehe 15 Julai 2011 nilieleza bungeni vyanzo mbadala vya kuongeza fedha katika bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bila kuathiri kwa kiwango kikubwa maisha ya wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla. Tarehe 18 Julai 2011 Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikubaliana na mapendekezo yetu na hivyo wakati anatoa hoja ya kuahirisha majumuisho ya mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini akaahidi kwenda kukata fedha kwenye posho na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima katika bajeti ya serikali ili kuelekeza fedha kwenye mradi wa dharura wa umeme. Hata hivyo, tarehe 13 Agosti 2011 Serikali ikageuka na kuleta mpango wa dharura tofauti ambao ulijikita katika serikali kuidhamini TANESCO kwenda kukopa kwenye mabenki ya kibiashara zaidi ya bilioni 400. Siku hiyo nilirudia kumsomea Waziri Mkuu kumbukumbu ya Bunge (Hansard) ya ahadi yake ya tarehe 18 Julai 2011 ambayo haikuitimiza, inaelekea serikali ilitoa ahadi hewa ndio maana haikutaka kabisa kubadili msimamo.

Waziri Muhongo aonyeshe kwa vitendo kwamba utendaji wa Wizara ya Nishati na Madini umebadilika kwa kurejea masuala muhimu na kuyazingatia kwenye makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2012/2013; kauli yangu kuhusu masuala mengine ya gesi asili, mafuta na madini nitayaeleza katika hatua za baadaye.

Imetolewa tarehe 21 Mei 2012

No comments: