Saturday, June 30, 2012
Utekelezaji wa sehemu ya ahadi: ULINZI katika kata ya SINZA
Utekelezaji wa sehemu ya ahadi: ULINZI katika kata ya SINZA
Katika miongoni mwa vipaumbele nane vilivyounda kifupi cha AMUA katika kampeni zangu mwaka 2010 ni suala la ULINZI katika Jimbo zima la Ubungo.
Nashukuru leo 30.06.2012 kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali tumezindua Ujenzi wa kituo cha polisi katika kata ya Sinza.
Uzinduzi huo uliohudhuriwa na wananchi, Mstahiki Meya wa Kinondoni, Yusuph Mwenda na Diwani wa Kata ya Sinza, Renatus Pamba.
Natanguliza shukrani zangu za dhati sana kwa wananchi ambao tumeshirikiana katika mchakato huu, Diwani wa Kata ya Sinza, Renatus Pamba, Mstahiki Meya, Yusuph Mwenda (ambaye ameahidi Manispaa ya Kinondoni itatoa Sh milioni kumi (10) kuchangia Ujenzi).Hii ni baada ya kuhamasishwa na Mbunge na Diwani baada ya Sh Milioni Kumi (10) nyingine kutolewa katika mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo (CDCF)
Maslahi ya Uma Kwanza.
John John MNYIKA
Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA)
30 Juni 2012
Thursday, June 28, 2012
Taifa na Madaktari: Tumefikia hapa tulipo kwa sababu ya Rais Kikwete na Bunge
Sababu ya hali tete ya nchi na maisha ya wananchi kwenye sekta ya afya ni udhaifu wa serikali na uzembe wa bunge. Rais Jakaya Kikwete ajitokeze alitangazie taifa kuunda tume huru ya kuchunguza kutaka kuuwawa kwa Dk. Ulimboka Steven na kutoa ahadi ya kuongeza fedha katika bajeti ya wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ili kushughulikia chanzo cha mgogoro. Spika Anna Makinda aruhusu bunge litumie mamlaka yake ya kuisimamia serikali kusuluhisha.
Taifa limeingizwa kwenye hali tete katika sekta ya afya na maisha ya wananchi wanaotegemea huduma toka hospitali, vituo vya afya na zahanati za umma yapo mashakani.
Tumefika hapa tulipo kutokana na udhaifu wa serikali wa kushughulikia matokeo badala ya chanzo cha mgogoro wake na madaktari na uzembe wa bunge katika kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi kusuluhisha pandembili zinazolumbana kwa gharama ya vifo na nyingi kwa wagonjwa wasio na hatia.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilianza ikashindwa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alijaribu akashindwa, Rais Jakaya Kikwete naye akaingilia kati kuondoa udhaifu uliokuwepo naye anaelekea kushindwa; kwa kuwa wote wanashughulikia matokeo ya mgogoro badala ya chanzo.
Chanzo cha mgogoro wa serikali na madaktari na wananchi kuhusu sekta ya afya ni bajeti finyu inayotengwa na serikali na kiasi kidogo cha fedha kinachotolewa katika sekta hii nyeti, na hivyo kushindwa kuboresha maslahi ya watumishi wa sekta ya afya wakiwemo madaktari kwa upande mmoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kwa upande mwingine.
Rais Kikwete ajitokeze alitangazie taifa kuunda tume huru ya kuchunguza kutaka kuuwawa kwa Dk. Ulimboka na kutoa ahadi ya kuongeza fedha katika bajeti ya wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ili kushughulikia chanzo cha mgogoro:
Hatua ya serikali kukimbilia mahakamani na kutumia kivuli cha mahakama kukwepa kushughulikia madai ya msingi ya madaktari ni kuendelea kushughulikia matokeo na hivyo kuendeleza migogoro na migomo.
Hata kama serikali ikitumia vyombo vya dola kukamata au kujeruhi madaktari, inapaswa kutambua kwamba mgomo wenye madhara makubwa kwa nchi umekuwa ukiendelea chini chini kwa muda mrefu kwenye sekta ya afya nchini na kuchangia vifo vya wananchi kwa magonjwa yanayotibika kutokana na huduma mbovu na kukosekana kwa madawa na vifaa tiba katika hospitali, vituo vya afya na zahanati za umma.
Rais Kikwete anapaswa kujitokeza na kutoa ahadi ya kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuongeza fedha za bajeti ya afya katika mwaka wa fedha 2012/2013 kupitia mkutano wa nane wa bunge unaoendelea hivi sasa ili kushughulikia chanzo badala ya kupanua wigo wa migogoro katika taifa.
Aidha, Rais Kikwete anapaswa kutumia nguvu zake za ukuu wa nchi na uamiri jeshi mkuu kulaani tukio la kutekwa, kuteswa na kutaka kuuwawa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dr. Ulimboka Stephen ambapo baadhi ya watumishi wa serikali na askari wa vyombo vya dola wanatuhumiwa kuhusika. Ili kurejesha imani juu ya Serikali na vyombo vyake badala ya kutegemea jopo la wapepelezi kutoka jeshi la polisi pekee ambalo nalo baadhi ya vituo vyake Jijini Dar es salaam vimetuhumiwa, Rais Kikwete aunde tume huru ya kuchunguza tukio husika ambalo limeongeza madoa kwa nchi kitaifa na kimataifa.
Spika aruhusu bunge litumie mamlaka yake ya kuisimamia serikali kusuluhisha:
Kwa kipindi cha takribani miezi minne nimetumia njia za kibunge kutaka suala la madai ya madaktari lijadiliwe bungeni ili kushughulikia chanzo badala ya matokeo hata hivyo hitaji hilo la kikatiba limekuwa likipuuzwa na kusababisha bunge lizembee kuchukua hatua kwa wakati kuepusha mgogoro na mgomo.
Izingatiwe kwamba katiba ya nchi ibara ya 63 (2) inatamka kwamba “Sehemu ya pili ya bunge (yaani wabunge) ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano, ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba”.
Nawaomba wananchi wa Tanzania waliotutuma kuwawakilisha kumtaka Spika Makinda na wabunge wote kuwajibika kujadili bungeni hali tete ya sekta ya afya nchini na kauli tata za serikali katika kushughulikia hali hiyo. Spika, uongozi wa bunge na wabunge kwa pamoja tutakiwe kukataa visingizio vya serikali vya kutumia mahakama kuathiri haki, kinga na madaraka ya bunge ya kuisimamia serikali juu ya suala la madaktari na hali ya sekta ya afya nchini.
Hivyo; wabunge, umma na wadau wa haki za binadamu tuungane pamoja kutaka Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii iliyoshughulikia suala la madai ya madaktari itolewe bungeni na hadharani na bunge liruhusiwe kutumia mamlaka yake ya kuisimamia serikali kujadili taarifa hiyo na kupitisha maazimio maalum ya kuupatia ufumbuzi mgogoro unaoendelea na pia kuboresha hali ya huduma katika hospitali, vituo vya afya na zahanati inayoendelea kutetereka.
Kanuni ya 64 (1) (c) ya Kanuni za Kudumu za Bunge inayoelekeza kwamba “Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika bunge, mbunge hatazungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama”; inatumiwa vibaya na serikali kuficha udhaifu na kudhibiti mamlaka ya bunge kwa kisingizio cha mahakama.
Hata hivyo, zipo njia zaidi ya nne ambazo umma unaweza kutaka spika na wabunge wazitumie kukwepa bunge kuonekana linazembea kuchukua hatua za kuisimamia serikali na kuokoa maisha ya wananchi katika hatua hii ya dharura.
Mosi, hoja inaweza kutolewa ya kutengua kanuni husika kuliwezesha bunge kujadili Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii kuhusu madai ya madaktari kwa kuwa imekuwa kawaida kwa serikali kutoa hoja za kutengua kanuni wakati mwingine kuilinda serikali na kupunguza madaraka ya bunge. Mathalani, kanuni ya 94 inayolitaka bunge kukaa mwezi Februari kama Kamati ya Mipango kutoa mapendekezo ya mpango wa taifa, ilitenguliwa na matokeo yake ni kuwa serikali iliandaa bajeti ikiwemo ya sekta ya afya na kuwasilisha mwezi Juni bajeti ya serikali isiyozingatia kwa ukamilifu mpango na madai ya madaktari.
Pili, Spika anaweza kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa kanuni 114 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge kutaka kamati husika ya bunge kukutana kwa dharura na kuishauri wa haraka serikali kufuta kesi iliyoko mahakama kuu kitengo cha kazi ili kulipa fursa bunge kutumia madaraka yake ya kikatiba kujadili na kupitisha maazimio ya kuweza kusuluhisha pandembili za mgogoro badala ya mahakama. Uamuzi wa kurejea mahakamani unapaswa kuwa wa mwisho baada ya hatua zingine kushindikana.
Tatu; Spika kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa kanuni ya 114 (17) na 116 kuitaka Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii kupatiwa na kupitia nyaraka zilizowasilishwa mahakamani, na kuandaa taarifa maalum ya masuala yanayoweza kujadiliwa bungeni bila kuingilia suala lililo mahakamani. Izingatiwe kwamba Serikali imefungua kesi dhidi ya Chama Cha Madaktari (MAT) na haijafungua kesi dhidi ya Jumuiya ya Madaktari na Taasisi zingine katika sekta ya afya; hivyo kufunguliwa kwa kesi hiyo hakuwezi kulizuia bunge kujadili masuala mengine yanayohusu madaktari na sekta ya afya nchini.
Nne; Kanuni ya 53 (2) au 47 (1) za Kanuni za Kudumu za bunge inaweza kutumiwa kwa Waziri husika kwamba suala la namna ambavyo serikali imejipanga kutoa huduma katika hospitali kufuatia mgomo wa madaktari unaoendelea au mbunge yoyote kutoa hoja kuhusu hali kwa sasa ilivyo katika hospitali na sekta ya afya kwa ujumla kufuatia kuendelea kwa mgogoro kati ya serikali na madaktari na masuala hayo yakajadiliwe. Izingatiwe masuala hayo hayahusu mgogoro ulioko mahakamani bali ni ya dharura kwa ajili ya kuepusha madhara zaidi kwa wananchi na nchi kwa ujumla wakati taifa likisubiri taratibu za mahakama kukamilika.
Ni muhimu umma ukapuuza taarifa isiyokuwa ya kweli iliyotolewa na Naibu Spika Job Ndugai bungeni tarehe 27 Juni 2012 ya kudai kwa tayari kamati ya huduma za jamii imewasilisha taarifa yake bungeni wakati ambapo taarifa hiyo iliyohusisha kazi ya kubwa ya kamati na matumizi ya ziada ya fedha za wananchi imefanywa kuwa siri hata kwetu wabunge. Naibu Spika Ndugai kwa kauli hiyo amekwepa kutekeleza muongozo wake mwenyewe alioutoa katika mkutano wa sita wa bunge mwezi Februari mwaka 2012 kwamba baada ya kamati kumaliza kazi yake taarifa ingewasilishwa bungeni na kujadiliwa. Tayari nilishamuandikia barua Spika tarehe 27 Juni 2012 kupuuza maelezo hayo ya Naibu Spika na kutoa kwa wabunge na bunge taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii ili wabunge tusiendelee kupokea kauli za upande mmoja wa serikali bila kuwa na maelezo na vielezo vya upande wa pili wa madaktari.
John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma
28/06/2012
CHADEMA yalaani Dk Ulimboka kushambuliwa
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), kimelaani kukamatwa na kushambuliwa kwa viongozi wa madaktari ikiwamo Dk Ulimboka Steven ikieleza kuwa hatua hiyo haiwezi kuwa suluhu bali itachochea zaidi mgogoro wa madaktari na Serikali.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika inaeleza pia kwamba udhaifu wa Serikali kuharakisha kwenda mahakamani kabla ya Bunge kupewa fursa ya kujadili madai ya madaktari na kuisimamia Serikali umelifikisha taifa katika hali iliyopo sasa.
"Nalaani uamuzi wa Serikali wa kutumia vyombo vya dola kukamata na kushambulia viongozi wa madaktari ikiwemo Dk Ulimboka Steven kwa hauwezi kuwa suluhu bali utachochea zaidi mgogoro kati ya madaktari na Serikali," ilisisitiza sehemu ya taarifa hiyo ya Mnyika na kuongeza:
“Nichukue fursa hii kuwaomba madaktari kufanya kila kinachowezekana kuokoa uhai wa wagonjwa katika kipindi hiki kigumu.” Mnyika alisema kuwa ameomba wabunge wapewe nakala ya Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii kuhusu madai ya madaktari na hoja ya taarifa husika iwekwe katika orodha ya shughuli za Bunge katika mkutano wa Bunge unaoendelea ili ijadiliwe na kupitisha maazimio, kuwezesha hatua za muda mfupi, wa kati na muda mrefu kuupatia ufumbuzi mgogoro huo na kuboresha sekta ya afya nchini.
“Natarajia kwamba Spika atawezesha kamati kuwasilisha taarifa yake na Bunge kujadili baada ya Serikali kutoa kauli yake bungeni,”alisema. Mnyika alisema ikiwa wabunge wataelezwa ukweli na kupewa taarifa kamili wataweza kuisimamia Serikali na kuwaeleza ukweli madaktari kipi kinawezekana na kipi hakiwezekani.
Alisema kuwa ingawa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoa maelezo bungeni kuwa Serikali itatoa kauli bungeni kuhusu mgomo huo, Bunge halitaruhusiwa kujadili kauli husika, hivyo kukoseshwa fursa ya kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi.
Tuesday, June 26, 2012
Mchango wangu Bungeni leo, Juni 26, 2012
Mosi, nimeuliza swali la nyongeza la kutaka ofisi ya Rais iwawajibishe watendaji waliozembea kuingiza maelezo na vielelezo vya waajiriwa wapya na waliopandishwa vyeo na kusababisha wachelewe kulipwa mishahara na kulimbikiza madai hali inayochochea migomo na migogoro kati ya wafanyakazi na serikali.
Pili, nimeomba muongozo baada ya kauli ya Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kuhusu kushuka kwa bei ya samaki aina ya Sangara kwenye ukanda wa ziwa Victoria kwa kuwa kauli hiyo ina mambo yenye kuzua mjadala kinyume na kanuni 49 (2) hivyo nikataka muongozo wa spika atumie kanuni ya 116 kuwezesha kamati ya bunge ya mifugo na maji kujadili kauli hiyo na kuleta taarifa bungeni wabunge tuweze kutimiza wajibu wa kuisimamia serikali.
Aidha, nilitaka muongozo kwa kanuni 64 (1) (c) na 116 kuhusu mgomo wa madaktari, suala ambalo nitamwandikia spika na bunge kusuluhisha kwa mujibu wa ibara 63 (2).
John John Mnyika,
Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA)
26 Juni, 2012
Sunday, June 24, 2012
Waraka wa kwanza mwaka 2012 wa Mbunge kwa Wananchi- “Ukweli ni Uhuru”
Waheshimiwa Wananchi
wenzangu,
Amani iwe kwenu,
Kwa kipindi cha wiki
nzima kumekuwepo na mjadala mkali bungeni, kwenye vyombo vya habari, mitandao
ya kijamii na katika taifa kwa ujumla juu ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa
fedha 2012/13 sanjari na yaliyojiri kutokana na kauli niliyotoa bungeni juu ya
udhaifu wa Rais katika usimamizi wa maandalizi na utekelezaji wa bajeti pamoja
na mipango muhimu ya maendeleo. Ukweli ni uhuru!.
Aidha, kupitishwa kwa
Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 na Bajeti ya Mapato
na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 bila marekebisho yoyote ya
msingi pamoja na michango mingi ya wabunge ya kukosoa kumedhihirisha kile
nilicho tahadharisha tangu awali kwamba; kwa kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa
nguvu kubwa kwa Rais juu ya bajeti na uendeshaji wa nchi, udhaifu wa Rais una
athiri maisha ya wananchi. Ukweli ni Uhuru!.
Katika mazingira haya,
udhaifu wa rais na uzembe wa bunge unapandikiza migogoro kati ya wananchi na
serikali kutokana ufisadi na masuala ya maendeleo kutopewa kipaumbele cha
kutosha zaidi ya matumizi ya kawaida lakini pia inachochea pia migomo baridi ya
watumishi wa umma hususun madaktari, walimu na askari kutokana pia na madai yao
ya muda mrefu kutokuzingatiwa kwenye bajeti. Ukweli ni Uhuru!.
Kadhalika udhaifu wa
kanuni za Kudumu za Bunge umefanya wabunge kuwekewa mipaka kwa mujibu wa kanuni
97 (2) ya kuchangia mjadala kuhusu hotuba ya bajeti kwa kuchangia tu mambo ya
ujumla yanayohusiana na hali ya uchumi wa nchi na kwamba mbunge yoyote
haruhusiwi kupendekeza mabadiliko katika makadirio ya mapato na matumizi ya
serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Pia, katiba imempa
mamlaka makubwa Rais juu ya Bunge kwa kuwa Bunge likikataa bajeti ya serikali
kwa mujibu wa Ibara ya 90 (2) (b) moja kwa moja Rais analivunja bunge suala
ambalo huwapa hofu wabunge wengi hususani wa chama kinachotawala na kuwafanya
wapige kura ya NDIO hata kama waliikosoa bajeti husika. Hivyo, udhaifu wa bunge
unachangiwa na ukweli kwamba katiba imeweka nguvu kubwa kwa Rais katika kuvunja
bunge linapokataa bajeti wakati huo huo kanuni zimekataza wabunge kupendekeza
mabadiliko katika bajeti; kwa hivyo wabunge hawana uwezo wa kubadilisha na
wakati huo huo wakikataa bunge linavunjwa, katika mazingira haya udhaifu wa
Rais wa kushindwa kutumia nguvu hizo za kikatiba una madhara makubwa sana kwa
nchi na maisha ya wananchi. Ukweli ni
Uhuru!.
Kwa mantiki hiyo,
katika mchakato wa katiba mpya ni muhimu kwa wananchi kutoa maoni ya kuwezesha
ukuu na uhuru wa bunge katika kuisimamia serikali kwenye mchakato wa bajeti kwa
ajili ya miradi ya maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi. Wakati katiba
mpya ikisubiriwa, ni muhimu kwa marekebisho ya haraka kufanyika katika kanuni
za kudumu za bunge hususani sehemu ya tisa inayohusu utaratibu wa kutunga
sheria kuhusu mambo ya fedha kuanzia kanuni ya 94 mpaka kanuni ya 107 ili
kuongeza nguvu za bunge katika kuishauri na kuisimamia serikali kwa mujibu wa
madaraka ya bunge ya ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba ya sasa. Katika muktadha
huo, nimeanza kufanya uchambuzi ili
kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni. Ukweli ni Uhuru!.
Hata hivyo, hata kwa
kanuni zilizopo sasa udhaifu wa bunge unaongezeka kutokana na maamuzi ya
kizembe mathalani ya kutozingatia matakwa ya kanuni za bunge, mfano Kanuni ya
94 inalitaka bunge ili kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika ibara ya 63
(3) (c) ya Katiba kwa kukaa kama kamati ya mipango katika mkutano wake wa mwezi
Februari ili kujadili na kushauri kuhusu mapendezo ya mpango wa taifa
unaokusudiwa kutekelezwa na serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata, kanuni
ambayo toka niingie bungeni haijawahi kutekelezwa kwa wakati hata mara moja
pamoja na kuwakumbusha wanaohusika kusimamia kanuni. Ukweli ni Uhuru!.
Mwaka huu udhaifu
umekuwa mkubwa zaidi kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha
2012/2013 sanjari na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa
Fedha 2012/2013 tarehe 18 Juni 2012 na kupitishwa siku moja tarehe 22 Juni 2012
hali ambayo imechangia katika kufanya bajeti ya nchi isizingatie kwa ukamilfu
mpango wa taifa wa miaka mitano. Ukweli ni Uhuru!.
Nashukuru kwamba Spika
wa Bunge Anna Makinda amekiri bungeni tarehe 20 Juni 2012 kwamba kulikuwa na
udhaifu wa miaka mingi wa kutozingatia kanuni ya 106 ambayo inalitaka bunge
kujadili muswada wa sheria ya fedha mwishoni baada ya bunge kukamilisha kazi ya
kupitisha muswada wa fedha za matumizi ili kuiwezesha serikali kuongeza vyanzo
vya mapato kama wabunge tulivyopendekeza mwaka 2011 na pendekezo hilo kurudiwa
tena na kamati ya fedha na uchumi tarehe 18 Juni 2012. Ukweli ni Uhuru!.
Izingatiwe kuwa iwapo
sheria ya fedha ingepitishwa tarehe 22 Juni 2012 kama ilivyokuwa imepangwa
awali athari zake zingekuwa kubwa kwa kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu
kubwa kwa Rais juu ya utaratibu wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kwa mujibu
wa ibara ya 99 (1) kwa kuweka masharti kwamba bunge halitashughulikia sehemu
kubwa ya masuala ya fedha isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo
lishughulikiwe na bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye
bunge na waziri. Hivyo, michango na mapendekezo ya wabunge bila Rais mwenyewe
kupendekeza isingeliwezesha bunge kufanya mabadiliko ya kupanua wigo wa mapato
kwa kuwa kwa kuwa mujibu wa ibara 99 (2) (a) (i) udhaifu wa bunge ni pamoja na
kukatazwa kutoza kodi au kuongeza kodi. Ukweli ni Uhuru!.
Hivyo, Kamati ya Fedha
na Uchumi itumie vizuri mwanya wa ibara ya 99 (3) kurejea maoni yake, ya kambi
rasmi ya upinzani bungeni na michango ya wabunge ya mkutano wanne wa Bunge
mwaka 2011 na Mkutano wa nane wa Bunge mwaka 2012 na kufanya marekebisho ya
muswada wa sheria ya fedha kwa kumshauri Waziri. Ukweli ni Uhuru!.
Aidha, ili kuondoa
udhaifu uliopo Rais Kikwete mwenyewe asome kumbukumbu rasmi za bunge (Hansard)
za tarehe 18 Juni mpaka 22 Juni 2012 na kuliongoza baraza la mawaziri
kumwezesha Waziri wa Fedha ya 86 (10)
kuwasilisha muswada wa sheria uliochapishwa upya ukiwa na marekebisho au
mabadiliko yanayopaswa kufanyika yenye kulenga kupunguza kodi katika bidhaa
zenye kuchangia mfumuko wa bei na kupanua wigo wa mapato kwa kuongeza kodi
kwenye vyanzo mbadala tulivyovieleza bungeni. Ukweli ni Uhuru!.
Izingatiwe kuwa nilipotolewa
bungeni tarehe 19 Juni 2012 nilieleza kwa ufupi nilichosema bungeni na nilichotarajia
kusema na kuahidi kwamba nitatoa tamko kamili baadaye; baada ya kujipa muda wa
kutafakari nimefikia uamuzi wa kutoa tamko husika wakati bunge litakapoelekea
kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya
mapato na matumizi ya ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2012/2013; ambapo pamoja
na masuala mengine nitaeleza hatua ambazo Rais anapaswa kuchukua kuwezesha
ahadi alizotoa kwa watanzania kuweza kutekelezwa na serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Kwa sasa niwashukuru
wananchi wa Ubungo, wakazi wa mkoa wa Dar es salaam na watanzania kwa ujumla
walionielewa na kuniunga mkono kupitia maoni yao kwenye mitandao ya kijamii,
simu za mkononi na katika vyombo vya habari. Nawashukuru pia viongozi wa dini,
chama na asasi mbalimbali nje na ndani ya serikali walionipa moyo wa kuendelea
kusimamia ukweli na kuacha unafiki ili kusimamia uwajibikaji wa viongozi kwa
maendeleo ya taifa. Ukweli ni Uhuru!.
Nashukuru pia kwa
mchango wa walinipinga na kunikosoa kutokana na kauli niliyotoa juu ya udhaifu
wa Rais Kikwete, wapo walioeleza kuwa ilitokana na jazba na wengine wameeleza
kuwa ningetumia lugha ya diplomasia kufikisha ujumbe ili kutodhalilisha taasisi
ya urais na kwa kuzingatia utamaduni wetu wa heshima kwa wakubwa na wapo
wachache waliosema kwamba ni matusi kutamka ‘udhaifu wa Rais’. Ukweli ni
Uhuru!.
Wakati mjadala huu
ukiendelea ni rai yangu kwamba rejea ifanyike katika mchango wangu wa tarehe 5
Julai 2011 wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya
Rais kwa mwaka 2011/2012 na rejea kamili pia ifanyike kwenye mchango wangu wa
tarehe 19 Juni 201; na ieleweke kwamba naheshimu taasisi ya urais na umri,
naamini katika matumizi ya lugha ya kidiplomasia, hata hivyo nilitafakari na
kuamua kuusema ukweli kwa lugha ya moja kwa moja ili ujumbe ufike kwa mamlaka
zote zinazohusika na wauchukulie kwa uzito tofauti ilivyokuwa mwaka mmoja
uliopita. Ukweli ni uhuru!.
Niliamini, naamini na
nitaendelea kuamini kwamba kutamka neno ‘udhaifu wa Rais’ sio kumtukana Rais na
wala sio kulitumia jina la Rais kwa dhihaka; hata hivyo kwa kuwa pamekuwepo na
mwelekeo wa propaganda za kudai kuwa kauli hiyo ni matusi na kwa kuwa chanzo
cha propaganda hizo ni udhaifu uliofanywa na Naibu Spika Job Ndugai bungeni wa
kunihukumu kwa kutumia kanuni tofauti na tuhuma iliyotolewa; nakusudia kukata
rufaa dhidi ya uamuzi wake ili kuwe na mjadala mpana wa kibunge utakaowezesha
kumbukumbu sahihi kuwekwa. Ukweli ni uhuru!.
Katiba ya Nchi ambayo
niliapishwa kuilinda pamoja na ubovu wake inatamka katika Ibara ya 63 (2) kwamba
“Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano
ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri
Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa
majukumu yake kwa mujibu wa katiba”. Toka nichaguliwe kuwa mbunge mwaka 2010
kwa nyakati na maeneo mbalimbali viongozi wa vyama, dini, asasi za kiraia,
vyombo vya habari na wananchi wa kawaida wakilalamika kuhusu udhaifu wa Rais na
kutaka atumie nguvu na mamlaka yake ya kikatiba kuiongoza kwa uthabiti serikali
kushughulikia masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yanayolikabili taifa;
niliamua kuendelea kusema bungeni kwa mara nyingine ikiwa ni sehemu ya kutimiza
wajibu wa kibunge wa kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali. Ukweli ni
Uhuru!.
Tarehe 19 Juni 2012
nilieleza bungeni kabla ya kutolewa sababu za kuikataa bajeti na tarehe 22 Juni
2012 nilipiga kura ya hapana ya kuikataa bajeti kwa kutokuweka misingi thabiti
ya kutimiza ahadi ya Rais Kikwete na CCM ya maisha bora kwa kila mtanzania na
badala yake kuongeza ugumu wa maisha kutokana na kushindwa kukabiliana na
matatizo ya mfumuko wa bei. Aidha, kiwango cha fedha kwa ajili ya miradi ya
barabara na maji kwa upande wa jiji la Dar es salaam ikiwemo jimbo la Ubungo ni
kidogo tofauti na kile kilichotajwa na Rais Kikwete na kuingizwa kwenye jedwali
la Mpango wa Taifa wa miaka mitano kwa upande wa miradi ya maendeleo iliyopaswa
kutengewa fedha katika bajeti ya 2012/2013. Ukweli ni Uhuru!.
Pamoja na utetezi
uliotolewa na Serikali juu ya mgongano kati ya tafsiri kati ya kiingereza na
Kiswahili, ukweli utaendelea kubaki kuwa tuliamua kuikataa bajeti kwa kuwa
ilishindwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao
uliwasilishwa na Rais Kikwete na ukapitishwa kwa azimio la bunge ambao ulipaswa
kuiongoza serikali kuweka mkazo katika kuendeleza nchi kwa kutumia fedha za
ndani kwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo kama
zilivyokokotolewa katika mpango husika. Ukweli ni Uhuru!.
Naamini Rais Kikwete anayofursa
ya kurekebisha udhaifu huo kwa kuongeza nguvu zake katika muswada wa sheria ya
fedha kupanua wigo wa mapato na hatimaye kumwezesha Waziri wa Fedha kuwasilisha
bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 107 mapendekezo ya matumizi ya nyongeza ya
fedha za serikali yenye kulenga kuongeza kiwango cha fedha za maendeleo. Kwa
upande wa Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam, serikali kwenye bajeti ya
nyongeza inayopaswa kuwasilishwa iongeze fedha za miradi ya Maji kwa upande wa
Ruvu Juu ikiwemo kutenga fedha za kutosha za ujenzi wa Bwawa la Kidunda, kwa
upande wa Barabara iongeze fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara za
pembezoni za mchujo na za mzunguko za kupunguza msongamano wa magari, na fidia
ya ardhi kwa wananchi wa Kata ya Kwembe wanaopaswa kuhama kupisha ujenzi wa
Chuo Kikuu Muhimbili (MUHAS) Eneo la Mloganzila. Ukweli ni Uhuru!.
Kwa Wasemaji wa CCM
waliodai kwamba nimetoa lugha ya matusi dhidi ya Rais na mwenyekiti wa chama
chao wasome Kitabu cha Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania cha mmoja wa waasisi
wa TANU na CCM Mwalimu Julius Nyerere
ambapo wakati huo taifa likiwa katika mtanziko alimueleza Rais wa wakati
huo kuwa ni ‘kiongozi dhaifu’ katika ukurasa wa 50 na kuendelea kusema katika
Ukurasa wa 51 na namnukuu “Kwa sababu ya minong’ono-nong’ono ya watu wasiiona
mbali kuhusu Rais, na kubabaishwa anakobabaishwa na washauri wake wakuu,
nililazimika kuiambia wazi wazi Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi
kwamba najiona kuwa ninao wajibu wa kumsaidia Rais amalize kipindi chake
salama” . Ukweli ni Uhuru!
Naamini Mwalimu Nyerere
hakumtukana Rais Mwinyi, kwa hiyo kunituhumu nimetukana ni kumtuhumu pia
Marehemu Baba wa Taifa; narudia tena kusisitiza kuwa udhaifu uliojitokeza ni
kutokana na Rais kutokutumia kwa uthabiti nguvu na mamlaka yake kwa mujibu wa
katiba ibara za 33, 34, 35, 36, 37, 38 na 99 juu ya utendaji wa serikali na
utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo. Ukweli ni Uhuru!.
Nimalize kwa kunukuu kitabu kingine cha Mwalimu Nyerere cha miaka ya
mwanzoni mwa 1960 cha TUJISAHIHISHE, “ Makosa yetu mengine hutokana na woga;
woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo
anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga ni ubinafsi. Pengine huwa
tunaogopa sisi wenyewe kulaumiwa au kupata hasara fulani. Pengine twaweza kuwa
hatuna cheo chochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tamaa
yoyote ya kupata cheo fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila
binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo
tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama
maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na
wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila
kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni ubinafsi mbaya sana.", mwisho
wa kunukuu: Ukweli ni uhuru.
Wenu katika utumishi wa umma,
John Mnyika
22 Juni 2012
Bungeni-Dodoma
Friday, June 22, 2012
Lengo la Kuomba Mwongozo - Sakata la Madaktari
Kwanini niliomba muongozo-Sakata la Mgomo wa Madaktari
Leo nilitaka kuomba muongozo wa Spika kwa mujibu wa Kanuni 49 (2) baada ya Waziri wa Afya kutoa kauli juu ya utekelezaji wa madai ya madaktari. Kanuni hiyo inataka kauli isiwe ya kuzua mjadala lakini aliyoyaeleza waziri juu ya uboreshaji wa maslahi ya madaktari yanazua mjadala kwa kuwa yanatofautiana na majibu ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoyatoa bungeni jana, (Juni 21, 2012) na pia hayana uhalisi. Mathalani, wakati serikali ikidai imeongeza posho ya kuitwa kazini (on call allowance) toka Februari, 2012 na kutumia bilioni 7.9 kwa miezi michache, imetenga kwa watumishi wa Afya bilioni 18.9 tu kwa mwaka mzima wa 2012/2013 kiwango ambacho hakitoshi.
Hivyo nilitaka kuomba muongozo Spika awezeshe kauli hiyo ijadiliwe kama ilivyokuwa kwa kauli juu ya fedha za rada. Nakusudia kumuandikia barua Spika kushauri aelekeze kamati ya bunge ya huduma za jamii kauli hiyo ya waziri.
Pia bunge halipaswi kunyimwa fursa ya kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa ibara ya 63 ya kuishauri na kuisimamia serikali kusuluhisha mgogoro na madaktari ili kuepusha mgomo wenye athari kwa nchi na wananchi kwa kisingizio cha kusudio la serikali kupeleka mgogoro mahakama kuu kwa kuwa mpaka leo taarifa iliyotolewa bungeni bado hakuna shauri katika kitengo cha kazi. Hivyo, Spika anapaswa kutoa jukumu kwa kamati husika ya bunge kuendelea na usuluhishi kabla ya serikali kukimbilia mahakamani.
Wabunge tupewe nakala ya taarifa ya majadiliano ya pande mbili yaliyochukua zaidi ya siku 90 badala ya kupewa hotuba ya nusu saa ya upande mmoja wa serikali pekee.
Hata serikali ikizuia mgomo wa wazi kwa zuio la kimahakama ieleweke kuwa mgomo wa chinichini kwa watumishi wa afya ambao una athari ya muda mrefu kwa maisha ya wananchi nchini.
Mwisho, serikali ipunguze matumizi yasiyo ya lazima na ipanue wigo wa mapato.
John John Mnyika.
Mbunge Jimbo la Ubungo (CHADEMA)
22 Juni, 2012

Upinzani Kukataa Bajeti
Gazeti la Majira la tarehe 21 Juni 2012 limebeba kichwa cha habari “Siri ya kukataa bajeti yafichuka: Yadaiwa hilo ni shinikizo la nchi za magharibi; lengo ni kupora gesi, mafuta na madini ya urani”:
Nilipotolewa bungeni tarehe 19 Juni 2012 nilieleza kwamba nitatoa tamko la kina ya sababu za kutoa kauli bungeni kuwa “tumefika hapa kwa sababu ya udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa Bunge na upuuzi wa CCM”; nimeacha mpaka sasa kutoa tamko kuwapa nafasi Rais Kikwete, Wabunge na CCM watafakari mchango niliotoa bungeni na kuchukua hatua zinazostahili za kuondoa bajeti na kuwezesha marekebisho ya msingi.
Wakati nikisubiri hatua hizo amenukuliwa tarehe 21 Juni 2012 Mbunge wa Iramba Magharibi Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM akitoa madai ya uongo ambayo yanaendelea kudhihirisha kile nilichokieleza bungeni; hivyo katika muktadha huo iwapo Rais Kikwete na Bunge halitarekebisha udhaifu uliojitokeza nitaendelea kuungana na wabunge wengine wa upinzani kukataa bajeti na kuchukua hatua zaidi na kutoa tamko la kina siku chache zijazo.
Kwa sasa nieleze tu kuwa Nchemba anapaswa kuyataja kwa majina hayo mataifa ya magharibi na kuwataja kwa majina wabunge na wanasiasa anaodai wamewezeshwa kifedha ili kukataa bajeti kuwezesha kuporwa kwa gesi, mafuta na madini ya urani. Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe anapaswa kutoa kauli kwa umma iwapo maneno hayo ya uzushi ndio msimamo wa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na CCM.
Wananchi ambao wametutuma wabunge kuikataa bajeti wanajua kwamba bajeti hii inakataliwa kwa kutokuweka misingi ya kutimiza ahadi ya Rais Kikwete na CCM ya maisha bora kwa kila mtanzania na badala yake kuongeza ugumu wa maisha kutokana na kushindwa kukabiliana na matatizo ya mfumuko wa bei.
Aidha, wabunge tumekubaliana na maoni ya kambi ya upinzani ya kuikataa bajeti kwa kuwa imeshindwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao ulipitishwa kwa azimio la bunge ambao ulipaswa kuiongoza serikali kuweka mkazo katika kuendeleza nchi kwa kutumia fedha za ndani. Nikinukuu ukurasa wa 92 kifungu cha 4.3.1 “Kwa kuelewa kuwa wakati wote kutakuwa na miradi ya uwekezaji nje ya mpango, serikali kuanzia sasa itakuwa inatenga asilimia 35 ya makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo kila mwaka”. Wabunge tunayakataa makadirio ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kwa sababu Serikali imetenga asilimia sifuri ya mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo.
Ndio maana katika mchango wangu bungeni tarehe 19 Juni 2012 kabla ya kutolewa bungeni nilieleza kwamba nakataa bajeti kwa kuwa bajeti haikuweka vipaumbele vya msingi vya maendeleo ya wananchi na nikataja mifano ya masuala ambayo wananchi wa Ubungo walionituma kuwawakilisha ya kutaka fedha za kutosha kutengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya maji na barabara za pembezoni za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es salaam. Katika mchango huo ambao unaweza kurejewa katika taarifa rasmi za bunge (Hansard) nilieleza namna ambavyo bajeti iliyowasilishwa haitekelezi ilani ya CCM kwa ukamilifu wala kutenga viwango vya fedha kama ilivyotakiwa na mpango wa taifa wa miaka mitano.
Miradi hiyo ya Ubungo na Dar es salaam kwa ujumla ya maji na barabara ilipitishwa na baraza la mawaziri ili kutengewa fedha Mwenyekiti akiwa Rais Kikwete na ilitokana na ahadi za Rais Kikwete lakini haijatengewa fedha za kutosha huku bajeti ikiwa na matumizi mengi ya kawaida yasiyokuwa ya lazima ambayo yangeweza kupunguzwa na kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo. Badala ya Nchemba kufanya propaganda chafu alipaswa kumshauri Rais Kikwete na CCM kutekeleza ahadi na kutimiza wajibu ipasavyo kwa kuiondoa bajeti na kuirejesha baada ya kuifanyia marekebisho ya msingi ili isikataliwe.
Nchemba anapaswa kufahamu kwamba wabunge wa upinzani kabla na hata katika bunge la kumi tumekuwa tukiungana pamoja kupinga ufisadi na kutetea rasilimali za taifa ambazo Serikali ya CCM kwa muda mrefu imeachia zimeporwa na mataifa na makampuni ya kigeni kwa madai ya uwekezaji kutoka nje. Nchemba ni vyema tu akarejea uchambuzi wa wasemaji wa kambi rasmi ya upinzani kuhusu udhaifu wa kisera na kisheria pamoja na mikataba mibovu ambayo inalikosesha taifa mapato kwenye gesi, mafuta na madini ambao umetolewa kwa nyakati mbalimbali.
Hivyo, Serikali isipotoa kauli ya kukubaliana na maoni ya kambi rasmi ya upinzani tuliyoyatoa tarehe 15 Julai 2011 wakati wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013; katika masuala ya gesi, mafuta na madini kwa nafasi yangu ya uwaziri kivuli wa Nishati na Madini nitatumia njia za kibunge katika mkutano huu wa nane wa bunge unaoendelea kusimamia uwajibikaji kwa maslahi ya umma. Nchemba anapaswa kufahamu kwamba kutokana na udhaifu uliopo hivi sasa, Tanzania haina sheria ya gesi asili huku uvunaji wa rasilimali hiyo ukiendelea kiholela na ufisadi uliobainika na kuanikwa hata bungeni mpaka sasa haujashughulikiwa.
Madai ya Nchemba kuwa wabunge wameshiriki kuandaa bajeti katika hatua ya kamati hivyo hawana uhalali wa kuipinga bungeni hayana ukweli wowote kwa kuwa kwenye kamati wabunge hujadili bajeti za Wizara za kamati husika; bajeti kuu hupelekwa baadaye kwa mujibu wa kanuni ya 96 ya Kanuni za Kudumu za Bunge ambayo hata yenyewe kwa mwaka huu haikutekelezwa ipasavyo.
Aidha, ifahamike kwamba wabunge tulikoseshwa fursa ya kutumia ipasavyo mamlaka ya kibunge ya Ibara ya 63 ya katiba ya kuishauri na kuisimamia serikali katika kupanga mipango ya maendeleo kutokana na kanuni ya 94 ya bunge kutokuzingatiwa ambayo ilitaka bunge likae kama kamati ya mipango katika mkutano wa Bunge wa Mwezi Februari kutoa mapendekezo ya vipaumbele na hivyo kufanya mpango huo kujadiliwa hivi sasa wakati mapendekezo ya bajeti yameshaandaliwa bila kuzingatia mpango wa taifa wa miaka mitano.
Wakati nilipohoji kuhusu suala hilo miezi ya Februrari, Machi na Aprili Nchemba hakuwahi kuunga mkono wala kuishauri CCM na serikali kuzingatia hatua muhimu za upangaji wa bajeti ambazo zingeepusha bajeti kukataliwa katika hatua ya mwisho kwa kutokidhi matakwa ya umma.
Kauli ya Nchemba ya kwamba wabunge wa upinzani tunataka kuikwamisha bajeti ili bunge livunjwe twende kwenye uchaguzi imedhihirisha tahadhari niliyoitoa ya kwamba wananchi wasitarajie wabunge wa CCM kuikataa bajeti kwa kuwa ubovu wa katiba ibara ya 90 umetoa mamlaka makubwa kwa Rais ya kulivunja bunge, na kwamba wabunge wengi wa CCM wana hofu juu ya uchaguzi kurudiwa hivyo wataipitisha bajeti kwa kura ya NDIYO hata kama inaongoza ugumu wa maisha kwa wananchi na haiwezeshi utekelezaji wa haraka wa miradi ya maendeleo. Hivyo, suluhisho katika hali hiyo kabla ya mabadiliko ya katiba ni Rais kuondoa udhaifu na kutumia nguvu kubwa aliyonayo kwa mujibu wa katiba kuiondoa bajeti na kuirejesha ikiwa imefanyiwa marekebisho makubwa kwa kuzingatia michango ya wabunge na maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni.
John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
Bungeni-Dodoma (21/06/2012)

Tuesday, June 19, 2012
Msimamo wangu wa sasa juu ya Kauli yangu bungeni!
Nitatoa tamko la kina baadae kuhusu
kilichotokea lakini kwa ufupi ubovu wa bajeti hii ni matokeo ya udhaifu wa Rais
Kikwete, yeye ndiye aliyesaini Mpango wa Taifa wa miaka mitano kama Kiongozi
Mkuu wa Nchi tena kwa wino mwekundu kama Amiri Jeshi Mkuu. Na yeye ndiye
Mwenyekiti wa baraza la mawaziri, bajeti hii iliyoacha kuzingatia mpango wa
Taifa imepita kwenye baraza alilloliongoza, pia kushindwa kutekelezwa kwa
bajeti iliyopita ni matokeo pia ya udhaifu wa taasisi ya Urais.
Pia kwa mujibu wa Katiba Rais ndiye
ambaye anapeleka bajeti bungeni, Waziri mwenye dhamana anapeleka tu kwa niaba.
Rais amepewa mamlaka makubwa juu ya bajeti ibara ya 99 imeweka mipaka kuhusu
mambo ambayo bunge lina mamlaka nayo huku ibara ya 90 inasema bunge likikataa
bajeti rais ana mamlaka ya kuvunja bunge. Hivyo Rais Kikwete anapaswa kuagiza
Waziri wa Fedha bajeti iondolewe irudi kwenye baraza la mawaziri ikafanyiwe
marekebisho!
John Mnyika
19 Juni 2012
Thursday, June 14, 2012
PUMZIKA KWA AMANI MZEE WETU BOB MAKANI
WASIFU WA MZEE MAKANI
Hayati
Bob Nyanga Makani alizaliwa mwaka 1936 katika Hospitali ya Kolandoto,
Shinyanga. Alikuwa ni mmoja wa watoto wengi katika familia ya Mzee
Makani.
Alipokuwa
na umri wa miaka sita, alianza masomo yake kwenye shule ya Msingi
Ibadakuli, Shinyanga. Kama ilivyokuwa kawaida ya Serikali ya Mkoloni
Muingereza hapa Tanzania wakati huo, watoto wa Machifu walipelekwa
kusoma Shule ya Sekondari Tabora, ndivyo ilivyokuwa kwa Hayati Bob pia.
Kutokana
na uhodari wake katika masomo, Mheshimiwa Bob Makani alifaulu na
kupelekwa Chuo Kikuu Cha Makerere, wakati huo kikiwa ni Chuo Kikuu cha
pekee Afrika Mashariki, ambako alifuzu na kupata Shahada ya Kwanza
katika Uchumi (BA Economics).
Hakuridhika
na shahada hiyo. Mwaka wa 1961 alikwenda Chuo Kikuu cha Liverpool,
nchini Uingereza na 1965 akatunukiwa Shahada ya Sheria (LLB). Kwa
mujibu wa Sheria za Uingereza, anayehitimu Shahada ya Sheria ni lazima
vilevile apasi mitihani ya Sheria kwenye Middle Temple, London,
Uingereza na Mheshimiwa Bob Makani alifanikisha hiyo mwaka huo huo na
kurejea nyumbani Tanzania.
Aliporudi
Tanzania aliajiriwa na Serikali kama Mwanasheria wa Serikali kwa muda
mfupi kabla hajapandishwa cheo na kuwa Exchange Control Manager wa
Benki Kuu.
Hapo
ndipo alipokutana na kuwa karibu na Mhe. Edwin Mtei aliyekuwa Gavana wa
Benki Kuu wakati huo. Ndiyo maana haikuwa ajabu lilipoanza vuguvugu la
siasa za mabadiliko nchini mwaka 1966, Mhe. Makani na Mhe. Edwin Mtei
walikuwa pamoja.
Mwaka
wa 1992 mfumo wa vyama vingi vya siasa ulipokubaliwa rasmi nchini, Mhe.
Bob Makani na Mhe. Edwin Mtei walikuwa mstari wa mbele kwenye uundwaji
wa chama cha siasa. Mwaka huo Mhe. Bob Makani alistaafu kazi yake ya
Unaibu Gavana wa Benki Kuu ili aweze kuelekeza shughuli zake zote
kwenye uanzishaji wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mheshimiwa
Bob Makani ni mwasisi wa CHADEMA na ana kadi ya Chama Namba tatu baada
tu ya Mhe. Edwin Mtei, No. I na Marehemu Brown Ngilulupi Kadi No. 2.
Tangu
mwanzo kabisa, CHADEMA kilifaidi mengi kwa utumishi uliotukuka toka
kwake Bob Makani. Kwanza kabisa, CHADEMA kilifaidika na utaalam wake
wa Sheria ambao pamoja na busara zake zilikisaidia chama kutengeneza
Katiba na taratibu za Uongozi/Administrative Structure) ambayo hadi
sasa ni msingi wa aina ya uongozi tuliojenga ndani ya CHADEMA.
Jambo
la pili ni kuwa Mhe. Bob Makani kwanza kwa asili na pili kwa maumbile
yake, alikuwa mtu wa watu. Ijapo ameshika vyeo vikubwa ndani ya
Serikali, Bob alikuwa na kipaji cha kuwaelewa wananchi na kuungana nao
katika kutafuta ubora wa maisha kwa ujumla. Urefu aliomjalia Mwenyezi
Mungu, ulihakikisha anaonekana! Hali kadhalika, kwa ucheshi wake.
Alisikika na kueleweka.
Ni
kwa kutambua uwezo na vipaji vyote hivi, ndiyo maana hapo hapo kwenye
kikao cha Mkutano Mkuu wa kwanza wa CHADEMA Desemba 1991, ndipo Mhe.
Bob Makani akachaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa CHADEMA.
Hali
kadhalika, kutokana na usemi uliopo kuwa KAZI NGUMU MPE MSUKUMA, Chama
nacho hakikuchelewa kumpa Bob Makani kazi ngumu ya kueneza Chama kipya
Tanzania nzima.
Mhe.
Bob Makani alipewa kazi maalum ya kukipeleka chama mikoa ya Morogoro,
Kigoma, Tabora, Singida, Mwanza na Rukwa. Hapa ikumbukwe kuwa wakati
huo, kuanzisha chama kipya ilionekana kama ni uasi au uhaini na kwenye
mikutano mingi ya hadhara kwenye mikoa hiyo, alipokelewa kwa matusi na
mara nyingine matusi na mawe.
Kwenye
mazingira haya magumu na ikizingatiwa kuwa chama hakikuwa na ruzuku,
alitumia rasilimali zake bila uchoyo ili kukijenga kile alichokiamini
kuwa ni chombo cha ukombozi wa wananchi kwa ajili ya maendeleo ya watu.
Sisi
tuliopo CHADEMA leo, tunajua na kuamini kuwa tokana na ujasiri wa
uongozi wa Mhe. Bob Makani kama Katibu Mkuu wa kwanza wa chama, ndipo
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliweza kutamka wazi kuwa CHADEMA ndicho
chama pekee cha upinzani alichoona kina sera na mwelekeo sahihi.
Akakitumia kama mfano wa kukiasa chama chake, CCM kuiga utengenezaji wa
sera zinazoweza kutekelezwa.
Mwaka
wa 1998, Mhe. Bob Makani akachaguliwa kuwa Mwenyekiti Taifa wa CHADEMA,
wadhifa alioshika hadi 2003 alipomaliza muda wake na wakati huo
akaendelea na kazi zake kama mwanasheria wa kujitegemea lakini akibaki
kuwa kiongozi na mshauri wa chama hadi kifo kilipomfikia.
Katika uhai wake Mhe. Bob Makani tokana na uadilifu na utaalam wake aliteuliwa kushika nafasi nyingi za uongozi zikiwemo:-
1.Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ndege Tanzania.
2.Mkurugenzi wa Bodi ya Williamson Diamonds
3.Mkurugenzi Bodi ya Tanzania Breweries
4.Mkurugenzi Bodi ya Benki ya Taifa ya Biashara
5.Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Law Society
Marehemu
alianza kusumbuliwa na uogonjwa wa moyo tangu 2009. Mwaka uliofuata
2010 alipelekwa India kwa matibabu na alipata nafuu kwa muda. Mwaka
huu, Bob Makani alipelekwa Nairobi kwa Operation ndogo lakini baada ya
hapo hakuweza kuendelea na kazi.
Mnamo
saa za jioni tarehe 9 Juni alizidiwa na kukimbizwa Hospitali ya
Aghakhan ambapo alifariki saa saba usiku. Marehemu ameacha wajane,
watoto saba na wajukuu wanane.
Mwenyezi Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya Marehemu Bob Nyanga Makani.
AMINA.
Monday, June 11, 2012
HATUA NILIZOCHOKUWA DHIDI YA WIZARA YA MAJI
Kufuatia
Wizara ya Maji kukaa kimya bila kujibu barua toka Ofisi ya Mbunge kwa
zaidi ya mwaka mmoja, nimeamua kuchukua hatua za kibunge kwa
kuwasilisha kwa Katibu wa Bunge, taarifa na maelezo ya hoja binafsi
kutaka Bunge, katika mkutano unaotarajiwa kuanza tarehe 12 Juni 2012,
lipitishe aazimio ya kuwezesha uwajibikaji wa Wizara husika na mamlaka
zake katika kushughulikia masuala ambayo nimeyaeleza
katika hoja husika.
Ikumbukwe kwamba, tarehe 20 Mei 2012 nilitoa mwito kwa Waziri Profesa Jumanne Maghembe kuueleza umma hatua saba za haraka zaidi za Wizara ya Maji kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam mara baada ya Waziri kurejea ofisini kutoka katika ziara hiyo ya vyanzo vya ruvu juu na ruvu chini na kufanya mikutano na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka
(DAWASA) pamoja na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO).
Nilichukua hatua ya kutoa taarifa kwa umma baada ya Wizara kuwa na utendaji mbovu wa kutojibu barua ambapo katika kipindi cha kati ya mwaka 2011 mpaka 2012 nimeandika jumla ya barua nne kwa Wizara husika kwa niaba ya wananchi kwa nyakati mbalimbali bila kupata majibu yoyote.
Katika ya hatua hizo ambazo Waziri nilieleza anapaswa kuzisimamia katika Wizara ya Maji ni; Mosi, kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya kashfa ya taifa ya kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 ambapo Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji.
Pili; kuwasilisha bungeni Mpango Maalum wa kuboresha huduma za Majisafi na uondoaji wa Maji Taka katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 kwa ajili ya kuidhinishwa, kutengewa bajeti kamili ya utekelezaji wa haraka katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kusimamiwa ipasavyo kwa msukumo wa kibunge badala ya ahadi za ujumla za kwenye ziara.

Tatu; Waziri kueleza hatua zilizopangwa kuchukuliwa kufuatia ziara yake kuhakikisha Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 unawekewa muda wa ukomo wa kukamilika ndani ya miezi mitatu katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa.
Nne; Waziri kukubaliana na pendekezo nililotoa bungeni kwa nyakati mbalimbali la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa thamani ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.
Tano; Waziri kuhakikisha Wizara ya Maji inaisimamia EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali. Aidha, Wizara ya Maji ihakikishe EWURA inaharakisha kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es Salaam.
Sita; Waziri kuwezesha Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on the management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012 iliyotolewa na CAG kabla ya mkutano wa nane wa bunge ulipangwa kuanza tarehe 12 Juni 2012 ili maoni na mapendekezo yazingatiwe wakati wa mchakato wa bajeti.
Saba; Wizara ya Maji kuhakikisha Serikali inawasilisha kwenye mkutano wa tisa wa bunge muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka (Water Supply and Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili kushughulikia upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.
Imetolewa Dar es salaam tarehe 8 Juni 2012 na:
John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
Thursday, June 7, 2012
Operesheni Okoa Kusini:John Mnyika Awapiga Msasa Wana Newala na Nanyumbu Juu Ya Uwajibikaji wa Serikali Kwa Wananchi,Elimu ya Katiba Mpya na Movement For Change( M4C)
Mbunge wa Ubungo(CHADEMA)John Mnyika
Akihutubia na akisikiliza maswali na kutoa somo la kudai uwajibikaji wa
serikali kwa wananchi, elimu ya katiba mpya na M4C, kwa wanakijiji
katika maeneo ya wilaya tofauti za Newala na Nanyumbu
Mbunge wa Ubungo(CHADEMA)John Mnyika Akimsikilzia Katibu wa Tawi wa CUF, Bi. Zaituni baada ya kutoa somo la kudai uwajibikaji wa serikali kwa wananchi, elimu ya katiba mpya na M4C, kwa wanakijiji katika maeneo ya wilaya tofauti za Newala na Nanyumbu.Picha na Habari na Kurugenzi Ya Habari-CHADEMA