Sunday, July 15, 2012

Majibu juu ya MAJI na hoja binafsi

Jana tarehe 13 Julai 2012 niliuliza swali la nyongeza bungeni kuhusu mtandao wa mabomba maarufu kama mabomba ya wachina kutokutoa maji kwa miaka mingi kwenye maeneo kadhaa ya Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla; nilihoji hatua za dharura za serikali za kuhakikisha mabomba hayo yanatoa maji badala ya kusubiri mpaka Disemba 2014 kama ilivyoelezwa katika hotuba ya Wizara ya Maji, nilihoji pia hatua zilizochukuliwa  kwa waliosababisha uzembe wenye kulitia hasara taifa kwa kuwa mabomba hayo yameanza kuharibika.

Katika majibu serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Maji Dkt. Binilith Mahenge ilieleza kuwa upo uwezekano wa sehemu ya miundombinu kuharibika au kuharibiwa na ili kuepusha hali hiyo serikali inatekeleza miradi ya kuongeza uzalishaji kutoka Ruvu chini, Ruvu juu na vyanzo vingine. Aidha, baada ya miradi hiyo kukamilika mtandao wa mabomba utahakikiwa na kama kuna kasoro zitarekebishwa na pia kama kuna ubadhirifu wowote utakao bainika Serikali itachukua hatua.

Ninachoweza kusema kwa sasa ni kuwa Hotuba ya Waziri wa Maji Prof, Jumanne Maghembe akiwasilisha bungeni mpango na makadirio ya matumizi ya fedha za Wizara ya Maji kwa mwaka 2012/2013 tarehe 9 Julai 2012 na majibu haya ya Naibu Waziri ya tarehe 13 Julai 2012 yanadhihirisha haja ya hoja binafsi niliyoiwasilisha ya kuomba bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam.
Ikumbukwe kwamba Rais Jakaya Kikwete na mawaziri mbalimbali kwa nyakati mbalimbali waliahidi kwamba tatizo la maji kuwa historia katika mkoa wa Dar es salaam mwaka 2013;  kinyume na ahadi hiyo kauli mpya ya Waziri bungeni ni kuwa sasa miradi hiyo inakamilika mwaka 2014. Hata hivyo, uchambuzi wangu kuhusu bajeti iliyopitishwa mwaka 2011/2012 na 2012/2013 inaonyesha kwamba hata lengo hilo la 2014 haliwezi kufikiwa kwa kuwa kiwango cha fedha kilichotengwa ni kidogo pungufu ya kilichopaswa kutengwa kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa maendeleo, hivyo kama mwelekeo wa utekelezaji utakuwa wa kusuasua kama ilivyo sasa matatizo ya maji katika Jiji la Dar es salaam yatadumu mpaka zaidi ya mwaka 2016 tofauti na ahadi zinazotolewa na serikali.
Ikumbukwe kwamba Mwezi Februari 2011 Wizara ya Maji iliandaa waraka maalum wa kuiomba Serikali kutenga kiasi cha shilingi bilioni 653.85 Mpango Maalum 2011-2013 wa kuboresha huduma za majisafi na uondaji wa majitaka katika Jiji la Dar es salaam na kupitishwa na Baraza la Mawaziri lakini kiwango cha fedha kinachotengwa na serikali hakizingatii waraka huo na maazimio ya baraza la mawaziri kwa ukamilifu wake hali ambayo inahitaji bunge kuisimamia serikali kwa haraka.

Aidha, Wizara ya Maji haionyeshi kuichukulia kwa uzito unaostahili kashfa ya Kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 ambapo Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji; hivyo hatua za kibunge zinahitajika katika kuwezesha ukaguzi stahiki.
Kwa upande mwingine, wakati miradi ya muda mfupi ikiendelea kusubiriwa, wananchi wanahitaji maji ya haraka hivyo Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 uwekewe muda wa ukomo wa kukamilika kuwa Oktoba 2012 katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa tofauti na ahadi ya Rais Kikwete aliyoitoa Kimara mwezi Mei mwaka 2010.
Nashukuru kwamba baada ya kueleza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi tarehe 8 Juni 2012 hatua zifuatazo zimechukuliwa na Wizara ya Maji: Mosi, kwa mara ya kwanza Wizara imejibu barua yangu na kueleza hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa za kushughulikia kwa haraka matatizo ya maji katika Jimbo la Ubungo. Pili, Wizara imetoa mrejesho wa utekelezaji wa Mpango wa dharura wa Maji kwa jiji la Dar es salaam.
Hata hivyo, kwa kuwa maelezo na majibu yaliyotolewa hayajashughulikia kwa ukamilifu hatua saba ambazo nilipendekeza Wizara ya Maji ichukue nitaendelea kuchukua hatua katika mkutano huu wa nane unaoendelea kuwasilisha hoja binafsi kuomba bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam.
Izingatiwe kwamba tarehe 8 Juni 2012 nilieleza kwamba nimewasilisha  kwa katibu wa bunge taarifa ya hoja pamoja na maelezo ya hoja; hivyo ninachosubiri hivi sasa ni kujulishwa iwapo hoja husika imekubaliwa kuwasilishwa bungeni katika mkutano wa bunge unaoendelea hivi sasa.
Kati ya hatua hizo saba amabazo bunge ni muhimu likapitisha maazimo ya kuisimamia serikali kwa mujibu wa katiba ya nchi ibara ya 63 (2) na (3) ni pamoja na ; Mosi,  kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya kashfa ya taifa ya kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 ambapo Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji.
Pili; kuwasilisha  bungeni Mpango Maalum wa kuboresha huduma za Majisafi na uondoaji wa Maji Taka katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 kwa ajili ya kuidhinishwa, kutengewa bajeti kamili ya utekelezaji wa haraka katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kusimamiwa ipasavyo kwa msukumo wa kibunge badala ya ahadi za ujumla za kwenye ziara.
Tatu; Serikali kueleza hatua zilizopangwa kuchukuliwa kufuatia ziara ya Wizara ya Maji kuhakikisha Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 unawekewa muda wa ukomo wa kukamilika ndani ya miezi mitatu katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa.
Nne; Serikali kukubaliana na pendekezo nililotoa bungeni kwa nyakati mbalimbali la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa thamani ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.
Tano; Serikali kuhakikisha Wizara ya Maji inaisimamia EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali. Aidha, Serikali ihakikishe EWURA inaharakisha kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es salaam.
Sita; Serikali iwezeshe Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on the management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012 iliyotolewa na CAG kwa haraka ili maoni na mapendekezo yazingatiwe mapema iwezekanavyo.
Saba; Serikali ihakikishe inawasilisha kwenye mkutano wa tisa wa bunge muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka (Water Supply and Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili kushughulikia upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.
Imetolewa Dar es salaam tarehe 14 Julai 2012 na:

John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
Bungeni-Dodoma




No comments: