Sunday, July 1, 2012

MAONI YA MBUNGE WA UBUNGO KUHUSU HOTUBA YA MH. DKT. JAKAYA KIKWETE RAIS WA TANZANIA KWA WANANCHI TAREHE 30 JUNI 2012




Leo tarehe 1 Julai 2012 kumesambazwa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari hotuba ya Mh. Dkt. Jakaya Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wananchi inayotajwa kutolewa tarehe 30 Juni 2012.

Kufuatia hotuba hiyo na kufuatia mwito kutoka wachangiaji wa mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kutaka maoni yangu kuhusu hotuba husika, naomba nichukue fursa hii kutoa maoni kwa nafasi yangu ya ubunge kuhusu hotuba tajwa kama ifuatavyo:

Hotuba hiyo ya Rais imeibua mjadala na masuala ambayo yanahitaji kujadiliwa bungeni katika mkutano wa nane wa Bunge unaoendelea hivyo, serikali isiendelee tena kutumia kisingizio cha mahakama kulizua bunge kujadili masuala husika wakati yenyewe inayajadili na kuyatolea maelezo na maelekezo pamoja na kuchukua hatua hususani kuhusu suala la mgomo wa madaktari.

Hotuba hiyo ya Rais ukindoa suala la usafirishaji haramu wa watu nchini inaelekea kuwa ndiyo kauli ya Serikali ambayo Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliahidi kwamba ingetolewa bungeni lakini baadaye serikali ikasema haitatoa kauli. Uamuzi wa Serikali kuitoa kauli hiyo kupitia hotuba ya Rais una mwelekeo wa kukwepa wabunge wasijadili hotuba husika na pia wasitimize wajibu wa kikatiba wa ibara 63 (2) wa kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi.

Hivyo, Ofisi ya Rais na Ikulu wanapaswa kutoa maelezo kwa umma sababu za Rais kutolihutubia taifa tarehe 30 Juni 2012 kama ilivyotangazwa katika baadhi ya vyombo vya habari vya kielectroniki na badala yake hotuba ya Rais kusambazwa tarehe 1 Julai 2012 kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari na iwapo masuala ya hotuba hiyo kuhusu mgomo wa madaktari ndiyo yale ambayo Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikusudia kuyaeleza bungeni.

Aidha, kwa kuwa bunge litajadili mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kuanzia kesho tarehe 2 Julai 2012 na kuendelea ni muhimu wabunge wakajadili pia masuala ambayo Rais ameyaeleza kwa taifa na kutimiza wajibu wa kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) wa kuishauri na kuisimamia serikali.

Kuhusu Usafirishaji Haramu wa Binadamu Nchini
Ni vizuri hotuba ya Rais imeeleza wazi kwamba tukio la Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine kukutwa wamekufa si la kwanza kutokea hapa Tanzania kwa kuwa kwa kipindi cha miaka kumi kumekuwa na ongezeko la usafirishaji haramu wa binadamu katika taifa letu kupitia mipaka ya mikoa mbalimbali hapa nchini. Kwa mbinu yoyote ile ambayo imetumika, matukio haya yanaashiria kwamba mipaka yetu haipo salama kwa kuwa kama malori na vyombo vingine vya usafiri vyenye watu wasio na hati za kuingilia nchini wanaweza kuingia kwa wingi kwa nyakati mbalimbali tafsiri yake ni kwamba nchi iko kwenye hatari ya kuingiziwa pia vitu vingine haramu ikiwemo madawa ya kulevya na silaha hali ambayo ni tishio kwa usalama wa nchi na maisha ya wananchi. Ni vizuri Rais amekutana tarehe 27 Juni 2012 na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuzungumzia tukio hilo; hata hivyo, zaidi ya kuwapongeza vyombo vya dola kwa kazi nzuri ya kudhibiti shughuli za biashara haramu, nilitarajia kwamba Rais kwa mujibu wa mamlaka yake ya ibara ya 33 (2) ya mkuu wa nchi, kiongozi wa serikali na amiri jeshi mkuu angeagiza uchunguzi ufanyike kuhusu udhaifu uliojitokeza na kuagiza hatua kuchukuliwa kwa walishindwa kudhibiti hali hiyo katika mipaka ambayo biashara haramu ya usafirishaji wa watu inapitia. Izingatiwe kwamba mianya hii katika mipaka yetu ina athari pana sio katika suala hili tu bali pia katika usalama wa maisha ya wananchi kama ilivyo katika mikoa ya Kigoma, Kagera na kwingineko ambapo uhai wa wananchi na mali zao uko mashakani kutokana na uvamizi toka kwa wahamiaji haramu. Aidha, athari za hali hiyo zimejitokeza katika usambazaji wa chakula toka kwenye hifadhi ya taifa ambapo pamoja na Serikali kutumia zaidi ya bilioni 27 kusambaza mahindi na nafaka nyinginezo bei za bidhaa hizo katika Soko la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo hazikushuka kutokana na vyakula hivyo kutoroshwa na kuuzwa nje ya nchi kutokana na udhaifu katika ulinzi kwenye mipaka.

Hivyo, ni muhimu wabunge wakati wa mjadala wa bajeti ya ofisi ya Rais wataka kuongezeka kwa uwajibikaji na usimamizi wa utawala wa sheria ili kudumisha amani nchini.

Hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa ni pamoja na bunge kuisimamia serikali kuhakikisha idara ya usalama wa taifa inafanya kazi kwa ufanisi zaidi katika kuvisaidia vyombo vingine vya dola kulinda mipaka ya nchi na pia matatizo ya maslahi katika vyombo vya ulinzi na usalama yanatatuliwa ili vyombo husika viweze kufanya kazi bila baadhi ya maofisa wake kujihusisha na vitendo vya ufisadi na kuruhusu biashara haramu za aina mbalimbali.

Kuhusu Mgomo wa Madaktari

Kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi sasa; hotuba ya Rais imeendeleza kauli za upande mmoja ambazo zimekuwa zikitolewa na serikali kuhusu mgogoro huo bila taifa kupewa fursa ya kupata maelezo na vielezo vya upande wa pili; hivyo kuwa serikali imetoa kauli yake hadharani badala ya bungeni au mahakamani, ni muhimu pia taarifa ya kamati ya bunge ya huduma za jamii iliyoshughulia suala hilo na kukutana na pande zote mbili itoe taarifa yake bungeni na kwa umma.

Katika hotuba yake Rais amewaeleza kwa kiwango kikubwa wananchi namna ambavyo madaktari wanasababisha mahangaiko kwa wagonjwa wengi na kusababisha vifo kwa wengine lakini hakueleza kabisa mchango wa serikali katika kusababisha hali hiyo. Hivyo, kwa kuwa pande zote mbili zinachangia katika athari zinazoikumba nchi na wananchi kutokana na mgomo; ni muhimu chombo cha tatu kikaingilia kati kuwezesha ufumbuzi kupatikana na chombo hicho ni bunge ambalo ndilo lenye wajibu wa kuisimamia serikali. Jitihada za kuwalazimisha madaktari kurejea kazini bila majadiliano ya pande mbili mbele ya chombo cha kuisimamia serikali kushughulikia chanzo cha mgogoro huo zinaweza kuleta ufumbuzi wa muda mfupi na athari za muda mrefu.

Ieleweke kwamba hata madaktari wakisitisha mgomo wa wazi kutokana na amri ya mahakama na agizo la Rais, migogoro katika ya serikali na watumishi wa umma wenye kusababisha migomo baridi ya chinichini ina madhara ya muda mrefu kwa taifa.

Mathalani, kutokana na migomo baridi na huduma mbovu katika sekta ya afya wananchi wa kawaida wamekuwa wakifa kutokana na magonjwa yanayotibika.

Migomo ya chini kwa chini ya walimu na mazingira mabovu yamekuwa yakisababisha kudidimia kwa elimu katika shule za umma; mwanafunzi aliyehitimu masomo yake bila kujua kusoma na kuandika hana tofauti na mgonjwa anayekufa kwa kukosa huduma.

Hali hii ya kugoma kusiko kwa wazi imeenza kujipenyeza mpaka kwa askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuachia mianya ufisadi na kushindwa kusimamia utawala wa sheria kama ivyodhihirika kwa kuongezeka kwa vitendo vya biashara haramu katika taifa letu.

Rais amewaeleza wananchi kuwa kati ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika vikao sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari na kwamba katika mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa na pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana wa pamoja kwa mambo saba. Hata hivyo, katika masuala matano yaliyobaki, Rais hakueleza kwa wananchi nini ambacho serikali ilikuwa tayari kutoa kwa kila madai na kwa kiasi gani badala yake ameonyesha tu kwa ujumla kwamba madai hayo hayatekelezi.

Aidha, kufuatia hotuba hii ya Rais Madaktari nao wana wajibu wa kuueleza umma msingi wa madai yao na kwa kiwango gani walikuwa tayari kushuka kutoka katika madai yao ya awali, kinyume na hayo itaonekana kwamba madaktari waliingia katika majadiliano wakiwa na msimamo wa kutaka madai yao pekee ndiyo yakubaliwe wakati ufumbuzi wa mgogoro wa pande mbili hupatikana kwa win win (give and take).

Ni vizuri ikafahamika kwamba katika majadiliano, pande zote mbili huwa na mapendekezo yake; hivyo upo uwezekano kwamba yapo madai ambayo madaktari wameyatoa ambayo serikali haina uwezo wa kuyatimiza kwa kiwango walivyopendekeza na yapo ambayo serikali imeyakataa wakati ambao ina uwezo wa kuyatekeleza hata ikiwa kwa kiwango pungufu ya kile kilichopendekezwa na madaktari.

Suluhu katika mgogoro kama huo ambao kila upande una mapendekezo yake linapaswa kufanywa na vyombo vya usuluhishi; hata hivyo kuwa suala hili linahusu mgawanyo wa rasilimali za nchi na bajeti ya serikali, chombo chenye mamlaka ya kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi ni bunge.

Na kwa kuwa kamati ya bunge ya huduma za jamii ilikutana na pande mbili, ilikuwa muhimu kwa serikali kabla ya kupeleka shauri mahakamani kurejesha kwamba suala husika bungeni ambalo ndilo lenye wajibu wa kupendekeza vipaumbele vya mpango wa serikali na ndilo lenye kuidhinisha bajeti ya matumizi ya serikali.

Uamuzi wa serikali kukimbilia mahakamani kabla ya majadiliano ya bunge umechangia katika kusababisha mgomo wa madaktari, hivyo ushauri wangu kwa Rais Kikwete ni kwa serikali kufuta kesi iliyoko mahakamani ili bunge lipewe fursa ya kujadili ripoti yake kamati yake na kupitisha maazimio ya kuwezesha suluhu kati ya serikali na madaktari.

Mahakama iwe ni hatua ya mwisho baada ya mihimili miwili muhimu ya serikali na bunge kushindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro unaoendelea wenye athari kwa nchi na maisha ya wananchi.

Rais Kikwete ameeleza taifa kwamba Serikali imeongeza sana bajeti ya sekta ya afya kutoka shilingi bilioni 300 2005/2006 hadi shilingi trilioni 1.2 mwaka 2011/12; hata hivyo serikali inapaswa pia kulieleza taifa namna ambavyo kiwango hicho cha fedha kinapungua ukiweka kizio (factor) cha kushuka kwa thamani ya shilingi na mfumumo wa bei ukilinganisha mwaka 2005 na 2012.

Ukweli ni kwamba bajeti ya Sekta ya Afya bado ni ndogo kwa kuwa serikali haijatimiza bado azimio la kutenga asilimia 15 kwa ajili ya bajeti ya afya pia, hata kiwango hicho cha ongezeko la fedha hakijaleta matokeo ya kutosha kutokana na matumizi kuelekezwa kwenye baadhi ya maeneo yasiyokuwa ya kipaumbele na kuwa na utegemezi wa kiwango kikubwa cha fedha za wahisani ambazo kwa mwaka huo wa 2011/2012 aliourejea Rais Kikwete hakikutolewa kwa kiwango kilichoahidiwa. Hivyo, Rais Kikwete awezeshe kuongezwa kwa fedha za ndani kwenye bajeti ya afya kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Katika madai mengine Rais Kikwete ameeleza kwamba pande mbili zilifikia makubaliano nusu nusu, hali ambayo inaashiria kwamba madaktari wana hoja ambazo zinahitaji majadiliano hivyo, ni muhimu bunge likapewa nafasi ya kujadili kuweza kuwakilisha pande zote mbili za serikali na madaktari kuhusu nini kinawezekana na nini hakiwezekani ili kulinusuru taifa na mgogoro unaoendelea.

Rais Kikwete ametumia kwa kiwango kikubwa madai ya madaktari ya ongezeko la mshahara kujaribu kuwachonganisha wananchi na madaktari kwa kuwa na madai yasiyotekelezeka. Hata hivyo, ni muhimu ikafahamika kwamba sio madaktari pekee ambao wana mgogoro na mwajiri wao yaani serikali kuhusu kiwango cha mshahara bali pia watumishi wengine wa umma ikiwemo walimu.

Nyongeza iliyotolewa na serikali ya kati ya asilimia 15 na 20 kwenye mwaka wa fedha 2012/2013 ni tofauti na ahadi ambazo serikali imekuwa ikitoa kwa wafanyakazi za kuongeza mishahara na kupunguza kodi katika mishahara. Rais Kikwete na serikali warejee maoni na mapendekezo ya kambi rasmi ya upinzani kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na 2012/2013 kuhusu nyongeza za mishahara kwa watumishi wa umma na vyanzo mbadala vya mapato vya kuongeza kwa ajili ya kuwa na uwezo wa kutimiza mahitaji. Uwiano wa sasa wa matumizi ya mishahara kuwa asilimia 48 ya bajeti badala ya uwiano mzuri wa asilimia 35 kuwa mishahara na na asilimia 65 zitumike kugharimia huduma na shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na taifa; ni matokeo ya udhaifu wa serikali katika kupanua vyanzo vya mapato, kupunguza matumizi ya kawaida yasiyo ya lazima na kuongeza fedha katika miradi ya maendeleo hali ambayo Rais Kikwete kuliwezesha bunge kuisimamia serikali na kuirekebisha.


Kuhusu Suala la Dkt. Steven Ulimboka

Rais Kikwete ameeleza wananchi kuwa ameelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane; hata hivyo kauli hii inaashiria kukubaliana na hatua iliyochukuliwa na jeshi la polisi kuunda jopo la kuchunguza.

Nilitarajia Rais Kikwete kwa kutambua uwepo wa madai ya polisi kutuhumiwa kuhusika katika jaribio la mauji ya Dr Ulimboka angetangaza kuunda tume huru ya uchunguzi au walau angeongeza nguvu katika jopo la uchunguzi lililoundwa kwa kuunda timu ya maafisa waandamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama na usalama pamoja na wadau wengine kutoka taasisi huru.

Rais Kikwete anapaswa kutumia madaraka yake kwa mujibu wa katiba kuunda tume huru ambayo inadhihirisha kwa vitendo kwamba watuhumiwa hawajichunguzi wenyewe na kuwezesha matokeo ya uchunguzi kuaminika.

Narudia kuwasihi madaktari kuendelea kuokoa maisha ya wananchi katika kipindi hiki kigumu lakini wakati huo huo Rais Kikwete aiongoze serikali kuepusha athari zaidi katika sekta ya afya ya kuwa na mgogoro na madaktari kwa kuliwezesha bunge kujadili suala hili na kulipatia ufumbuzi ikiwemo kupitia nyongeza ya bajeti ya Wizara ya Afya. Nimemwandikia barua Spika Anna Makinda akiwa ni mkuu bunge kama muhimili mmojawapo wa dola kuweza kuchukua hatua stahili, naomba pande zote zizingatie maoni yanayotolewa na wabunge kwa niaba ya wananchi kwa maslahi ya taifa.

Maoni haya yametolewa leo tarehe 1 Julai 2012 na:

John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma

6 comments:

Unknown said...

Na Lingine kama kweli serikali haina hela kwanini isitangaze kupunguza mishara na malupulupu yote kwa asilimia hata ishirini tu kwa viongozi wote hasa wa kisiasa? kama yupo anayelipwa sh 18 miliion kwanini ishindikane kwa madaktari? Hata katika familia kama baba unalia hali kwamba hela hamna na ukashiriki kula kiporo asubuhi na kula dona kwa Maharage, watoto watakuelewa tu. Lakini kama unawambia watoto hela hamna na unarudi usiku umelewa baada ya kula sijui wapi huko watoto hawatakulewa. Au watoto wanadai daftari za kwendea shule unasema hela hamna lakini unazidi kushona suti tu hutaeleweka hata kidogo. Kwa hiyo kama serikali kweli inaamnini haina hela(siamini) ya kuwalipa madaktari na walimu haki zao itangaze wote wenye mishahara zaidi ya 3.5m wapunguzwe!

Anonymous said...

Kwani Lazima Kila kitu anachofanya aseme?

The other day ukasema ni dhaifu, why - sababu mawaziri wake wamefanyaje fanyaje sijui. Na wewe tukuite dhaifu kwa kufuata kila msimamao wa Chadema.

We ua kila njia ya kuwasilian an Rais, kama una nia nje na nchi hii, you could have been the fore-player kwa kutoa assistance kwa Rais.

Example, : Mtumie maoni yako, then publish kuwa nimetumia Mheshima Rais maoni haya, sio hapo kakaoosea, huku hakutakiwa kufanya vile, plase amesema hovyo....WHY?

Be an example to others.

You have to ask your self why most CCM members are great supporters of Zitto...... When you get the answer, rethink of my advice........

GARABA said...

nakushukuru kwa mchango wako mkubwa leo bungeni............... Japo mwenyekiti alitaka kukunyanyasa.

Anonymous said...

Mnyika,
Tafadhali fuatilia suala la Mkurugenzi wa TANROAD Eng. Mfugale kutengenezewa barabara inayoenda mpaka kwake tu wakati barabara inayoenda mpaka Saranga ni mbovu ile mbaya. Hii itakuwa rushwa ya makampuni anayoyapa tenda au Ubinafsi wa viongozi wa serikali uliobobea. Yaani imetengenezwa mpaka nyumbani kwake tu. Hii nchi tunapoelekea sio kuzuri kabisa.

Anonymous said...

Anony wa kwanza
Haya ni maoni yake kwa nafasi yake ya Ubunge.
We all differ, maoni yangu yanaweza kutofautiana au kukubaliana kwa kiwango fulani.
hiyo kumwambia mbona wabunge wa CCM wanamkubali ZITTO..who is wabunge wa CCM mpaka wawe reference point???....
Mnyika hongera, na maoni yako ni muhimu yanatakiwa kuchambuliwa na kufanyiwa kazi pale inapobidi.

Mimi binafsi maoni yangu, mfumo wa malipo wa wafanyakazi au watumishi wa umma yanabidi kuangalia upya, tayari unaonekana ni matatizo matupu.
Makundi katika jamii, yanayofaa kulipwa viwango vya juu vya mishahara na iwe hivyo hasa sekta ya elimu na afya.
Mfano: one of my colleagues ni mhindi, anadai nchini india kazi ya ufundishaji una mshahara mnono na marupurupu mazuri in short its a hot cake job similar to udaktari/utabibu/uuguzi, malipo yao yako juu haswa zaidi ya wanasiasa (i.e viongozi wa serikali na wabunge). Lakini anadai kupata hizo kazi ni mbinde mpaka mtu afuzu na kuwa mwalimu au daktari si kazi ndogo. Mfumo/procedure iliyopo ya mtu kupitia ili afuzu kupata hizo kazi ni ngumu..meaning at the end wanahakikisha anae kuwa mwalimu au daktari then ni mwalimu na daktari haswa kwa uwezo alionao ambapo anakuwa amepitia hatua nyingi za kupimwa/kutahiniwa kwa vitendo na nadharia na amefuzu. Kwamba huyu sasa amefuzu kutoa tiba kwa wananchi au amefuzu kutoa elimu inayofaa kwa wananchi. Akishafuzu basi anakikishiwa mazingira bora na maslahi bora ili afanye kazi yake kwa ufanisi.
Uthibitisho wa haya maelezo si uongo matokeo yake ktk nchi ya India tunayaona katika hizi sekta mbili. India wako mbele sana katika Elimu na afya na wanazidi kupiga hatua. Elimu yao ni bora na vile vile huduma zao afya. Ni kwa sababu walijikita katika kuhakikisha mizizi ya hizi ya sekta inapatiwa udongo wa rutuba na maji ya kutosha.
Lakini hali isivyo hapa TZ, wale wanaofeli ndio tunaona wanaenda kusomea ualimu..honestly speaking considering ELIMU ni asset kubwa ya maendeleo lakini tunaruhusu waliofeli ndio wasome ualimu. Ni kwa nini? kwa sababu maslahi na mazingira ni ya ovyo, so yule aliyefaulu na akili zake hata kidogo wazo la kuwa mwalimu haliko katika kichwa chake. Vile vile na udaktari, ingawa kusomea kwake ni kugumu lakini at the end maslahi na mazingira ni duni, na ndio usikute tumepoteza watu wengi katika fani nyingine lakini walipendelea kuwa matabibu ila walikuwa put off na maslahi na mazingira baada ya kumaliza masomo yao.
So kwa kusema hivyo; we really need to revamp the health and education sector kwa manufaa ya vizazi vijavyo. Au sivyo ili taifa linaaangamia hivi tunaliangalia.
Viongozi hawako tayari kubadili mifumo ambayo haileti tija na badala yake tunaona tu maamuzi mengine yanatolewa kama vile kukomoana. Mind you, its our great grand children and their children who will suffer.
LETS CHANGE FOR THE BETTER!!

Anonymous said...

Bila kuwa na chama chochote kila tanzania, na bila kufungamana na upande wowote lile nasema yafuatayo.
Mh mnyika unachokisema na kufanya si bali tu kisa upo ndani ya chama cha chadema ni kwamba uko sawa na kwa binadamu mwenye akili timatu, anaejali jamii yake, kuiheshimu na kutambua mchango wake ikiwa ni pamoja na kumuogopa MUNGU wake anapsawa kusema ukweli kwa namna yoyote ile hasa katika mambo ya kimsingi. Ki ufupi mimi ni kijana mdofo sana ila nina maswali haya, tena ingekua vizuri myika uyasome na ukawaulize watu hawa. Je ingekua mhe Rais mwanaye ridhiwani ama huyu miraji ama ally wametekwa angeishia kusema tu ataelekeza nguvu? Uko wapi ubinadamu, uko wapi kumuogopa MUNGU wetu. je huu ndo uislamu na mafunsisho ya dini aliyopitia raisi wetu mpaka kule jeshini.? Swali hili liende kwa IGP wetu pia pamoja na wasaidizi wake wote. Swali la pili hao watekaji wasioukua na akili na kupelekeshwa bila kutumia akili ya kuzaliwa sawa na kutukana wasaidizi wa mama zao kwanini labda wasingetafuta kuteka watoto wa hawa mafisadi wa nchi hii wenye kashfa waziwazi anagalau warudishe pesa zetu badala ya kutafuta maskini msema kweli. Nahisi ni ukosefu wa akili maana kama kweli wanahisi wanaitaji peace kwa nchi wangeanza na hawa wezi wa nchi yetu kina lowassa,karamagi na wengi neo. Mbona wanapeta mpaka sasa? mbona hawabugudhiwi ama kwakua pesa zao nimewafunga midomo wote mpaka watekaji wenyewe. Hao watekaji na wambea wote wanaotumikishwa kama wapumbavu mpaka kukosa value ya utu wao kama watasoma huu ujumbe nasema hivi. Mbona kuna watu wengi wanaotakiwa kutekwa na wanazagaa nchini bila hofu? and msidhani kuteka kutaogopesha watu maana hamtawamaliza soon things will erupt with no control. Keep it up bro