Monday, December 10, 2012

ORODHA YA AWAMU YA KWANZA: JUU YA MASUALA NA MATUKIO YA UFISADI NA UZEMBE YALIYOHUSU MIKATABA YA MAKAMPUNI YA M/S SANTA CLARA SUPPLIES COMPANY LIMITED NA M/S McDONALD LIVE LINE TECHNOLOGY LIMITED.


Masuala na matukio ya ufisadi na uzembe yaliyohusu mikataba ya makampuni ya M/s Santa Clara Supplies Company Ltd na M/s McDonald Live Line Technology Limited ambayo yamefanyika kinyume na sheria mbalimbali.

Kwa ushahidi wa nyaraka baadhi ya sheria zilizokiukwa ni pamoja na Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2004, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 na sheria nyinginezo. Aidha, masuala na matukio ya ufisadi na uzembe katika mikataba hiyo yamefanyika kinyume na kanuni, miongozo na maadili ya Shirika la Umeme (TANESCO). 

Ufisadi na uzembe umesababishwa na makosa mengine mbalimbali mathalani mgongano wa kimaslahi, utovu wa uaminifu, matumizi mabaya ya ofisi na makosa mengine yaliyo kinyume cha sheria na maadili ya viongozi na watumishi wa umma.

Orodha ya wanaotuhumiwa kuhusika katika ufisadi na/ama uzembe huo 18 ni kama ifuatavyo:

1.   Mhandisi WILLIAM GEOFREY MHANDO

Huyu alikuwa ni mkurugenzi mkuu wa shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na ndiye mtuhumiwa mkuu wa ufisadi unaohusu mikataba tajwa.

Akiwa mkurugenzi mkuu wa TANESCO aliingia mkataba na kampuni ya SANTA CLARA kwa tenda No PA/001/11/HQ/G/011 kuleta vifaa vya ofisini, kwa kipindi hicho kampuni hiyo tajwa hapo juu ilikuwa inamilikiwa na wanahisa ambao ni familia ya Mhando mwenyewe.

Mkataba huo ulisainiwa na mkewe kama mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo ya CLARA, kitendo hicho cha mkurugenzi kuipatia kampuni ya mkewe tenda ni kinyume na maadili ya Tanesco kifungu cha 2.2, ni kinyume na Sheria ya Ununuzi ya umma kifungu cha 33, 73(3) na 73 (5) pamoja na sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu cha 6 (d), (e) kutokana na kuwa na mgongano wa maslahi na utovu wa uaminifu.

Aidha kusaini kwa mkataba huo yeye akiwa mkurugenzi wa TANESCO ni matumizi mabaya ya ofisi, kwa kutumia ofisi ya umma kujinufaisha yeye pamoja na familia yake na kushindwa kusimamia sheria zinazoongoza na kusimamia ununuzi wa umma.

Kwa upande mwingine, aliingia katika makubaliano na Donald George Mwakamele (mkurugenzi na mwanahisa katika kampuni ya McDONALD)  makubaliano ambayo hayaruhusiwi na yenye mgogoro ( Conflicting Joint Venture Agrement) kinyume na maadili ya TANESCO na sheria nyingine za nchi nilizozitaja awali.

Lakini pia akijifanya ni mfanya biashara alisaini na makubaliano na kampuni hiyo makubaliano ya pande mbili ya kutafuta tenda, kununua, kujenga, kufanya matengenezo na kufanya miradi yote inayohusika na umeme. Katika kuwezesha hilo Mhando alikuwa na jukumu la kutafuta miradi ya umeme na endapo ikikamilika pande hizi mbili zinagawana mapato na faida inayotokana na miradi hiyo wakati huo huo yeye akiwa mtumishi wa TANESCO.

Pamoja na kufukuzwa kazi, umma unapaswa kuunganisha nguvu kutaka Mhando achunguzwe kwa makosa ya kijinai kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomhusu na kufunguliwa mashtaka ya kukiuka sheria za nchi.

2.   Bw. HARUN MATTAMBO

Huyu ni Afisa ugavi wa shirika la umeme Tanzania ( TANESCO) amefanya uzembe kwa kushindwa kuhakikisha manunuzi yote yanayofanywa na shirika yanazingatia  taratibu na kutimiza sheria za manunuzi ya umma.

Aliruhusu kufanyika kwa ufisadi na ukiukwaji wa sheria katika kupatikana kwa zabuni na. PA/001/11/HQ/G/011 na kuathiri Shirika la Umeme (TANESCO).

Alipendekeza kampuni ya M/s Mc Donald ipewe mkataba pamoja na kuwa haikuwa imetimiza masharti ikiwemo kukwepa kuwasilisha mahesabu ya fedha yaliyokaguliwa ya mwaka 2009 kama sheria ilivyohitaji.

Matokeo ya uzembe wake wa kuruhusu ufisadi ni kulisababishia hasara Shirika la Umeme (TANESCO) kwa kuwa kampuni hiyo ya Mc Donald ilipatikana bila kushindanishwa na makampuni mengine yaliyokuwa na unafuu na yaliyotimiza masharti.

Umma uungane kutaka Matambo afukuzwe kazi mara moja, na kuchunguzwa kuhusu tuhuma za kufanya uzembe huo kwa lengo la kujinufaisha na kunufaisha washirika wake kwa ajili ya hatua za ziada za kisheria.
     

3.    Bw ROBERT SHEMHILU

Huyu aliwahi kuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa TANESCO na anatuhumiwa kufanya uzembe ulioruhusu ufisadi.

Alifanya makosa ya kuruhusu malipo yaliyofanyika tarehe 5 Septemba 2011 kabla hata ya kusainiwa kwa mkataba na kuruhusu kuletwa kwa vifaa kabla hata ya kusainiwa kwa mkataba katika ya TANESCO na kampuni iliyopewa kinyemela zabuni ya kuleta vifaa.

Alifanya pia makosa ya kuilipa kampuni ya Mc Donald malipo ya juu ya asilimia 30 ya thamani ya mkataba wakati vifungu vya 26 na 54.1 vya mkataba huo (pamoja na kuingiwa kinyemela) vilielekeza malipo ya asilimia 15 tu.

Shemhilu pamoja na kusimamishwa  umma uunganishe nguvu kutaka, afukuzwe kazi mara moja na kuchunguzwa kwa ajili ya hatua za ziada.
      
4.   FRANCE MCHALANGE, NAFTARI KISIGA NA SOPHIA MSIDAI

Hawa walifanya uzembe wa kushindwa kusimamia Sheria ya Ununuzi wa Umma pamoja na maadili kwa kupendekeza kwamba Kampuni ya SANTA CLARA ipewe zabuni ya kuuzia vifaa TANESCO pamoja na kufahamu kuwa kampuni tajwa ilikuwa haijatimiza masharti na kulikuwa na mgongano wa maslahi.

Umma uhakikishe wanachukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na kukiuka sheria ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wa umma kuwajibika kutoa mapendekezo kwa kuzingatia sheria na maslahi ya umma.

5.   Mhandisi DECLAIN MHAIKI na Bw SUKE

Akiwa mtumishi wa umma alizembea na kukwepa kutoa taarifa  kuhusu kukiukwa kwa vigezo na masharti kuhusu zabuni na. PA/001/09/HQ/W/014 na kufanya kampuni ya McDonald Live Line Technology ipatiwe zabuni kinyume cha sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2004.

Aidha alichangia kufanya kampuni hiyo kupewa zabuni pamoja na kuwa haikuwa na uwezo wa kifedha na kuiwezesha kupewa malipo ya asilimia ya ziada kinyume na mkataba. Huyu naye umma uhakikishe wanachukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na kukiuka sheria na mkataba.

6.   Mhandisi D. MHAIKI, S.NKONDOLA, N.NTIMBA.Mhandisi CHEGERE, MAKIA NA MWITA.

Wote kama timu walifanya maamuzi yaliyosababisha kutolewa kwa mkataba na. PA/001/HQ/W/14 wa tarehe 11 Machi 2010 kwa kampuni ya Ms. Donald Live Line Technology bila kuzingatia uwezo wa kitaalamu, kifedha na masharti mengine na hivyo kukiuka sheria ya ununuzi ya umma na kushindwa kulinda maslahi ya taifa.

Hawa wanapaswa kuchukuliwa hatua za kinadhamu ili kudhibiti maamuzi na mapendekezo ya wataalamu katika utumishi wa umma kuingiza mashirika ya umma na nchi katika mikataba mibovu ili kupanua wigo wa uwajibikaji.

7.   FATUMA CHUNGU, ATHANASIUS NANGALI, ELANGWA MGENI

Kundi hili limehusika katika majadiliano na kutoa mapendekezo yaliyowezesha kampuni ya McDonald kupewa mkataba kinyemela.

Iwapo kundi hili lisingefanya uzembe na kusababisha ukiukwaji wa sheria mchakato wa mkataba huo kati ya mwezi Machi mpaka Mei 2009 ungewezesha TANESCO kuingia mkataba na kampuni yenye uwezo na iliyotimiza masharti na kuepusha shirika hilo kupata hasara na kubeba gharama ambazo zingeweza kuepukika.

Ni muhimu wakachukuliwa hatua za kinadhamu ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwa umakini na ueledi ili kuepusha TANESCO kuendelea kufanya majadiliano na kuingia mikataba mingine mibovu yenye kuongeza mzigo wa gharama kwa shirika na hatimaye ongezo la bei kwa wananchi.

8.   LUSEKELO KASSANGA (MKURUGENZI WA FEDHA)

Huyu alibariki ufisadi wa malipo yenye mkanganyiko katika TANESCO kwa kuilipa kampuni ya Santa Clara mapema kabla hata haijafanyiwa tathmini na kupatiwa zabuni.

Malipo yalifanyika kinyemela tarehe 5 Septemba 2011 wakati ambapo tathmini ya zabuni ilifanyika tarehe 23 Septemba 2011, maana yake ni kwamba malipo yalifanywa kabla hata kampuni husika haijapewa kazi kwa mleta vifaa asiye na uwezo na mwenye mgongano wa kimaslahi.

Kassanga anapaswa kufukuzwa kazi na kuchunguzwa kuhusu tuhuma za ziada za kunufaika kutokana na baadhi ya malipo yaliyofanywa kwa makampuni mbalimbali wakati akiwa mkurugenzi wa fedha ili aweze kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria.

6 comments:

Anonymous said...

Hongera sana Mnyika ,chapa kazi...we ni mfano bora wa kijana anayejituma kwa ajili ya nchi yake

Anonymous said...

Those who saw the enemy and run way, will never dare to stand and fight,but those who fight and suffer defeat will surely stand to fight again.

I salute you.

Sanga Fidelis said...

Ndio maana tunapandishiwa gharama za umeme kila mara kumbe kuna wachache wanaopenda kujineemesha. Pia mgawanyo wa bei wa kumuweka mtumiaji anayezidi unit 50 kwa mwezi kuwa kwenye kundi la watumiaji wakubwa ambapo inampasa kulipa bei sawa na mtu mwenye kiwanda nayo si sawa kwani kwa maisha ya sasa kutumia unit 50 ni hali ya kawaida!

Aled Jeras said...

Asante sana ndugu, Ili Tanzania ipige hatua kiuchumi inahitaji pia viongozi shupavu. Kuna baadhi ya viongozi wetu wanaturudisha nyuma. Wao wanapenda tu kutoa vitisho kwamba wataja wenzao wasio waadilifu lakini mwisho hatuoni kitu. Hii ni njia ya kutengeneza mianya ya rushwa. Tunatakiwa tubadilike, ni zama za uwazi na ukweli ndugu zangu.

Unknown said...

ni probaganda za kisiasa tu!

Anonymous said...

The only solution now is to reorganize the company and see a way to have more companies dealing with electricity supply. The change of leadership is not a solution but of course if proven beyond doubt that what has been explained is true for sure these people have to be punished! Tanzanians are carrying a lot of burden for the prosperity of few! these can not be tolerated.