Thursday, January 9, 2014

Kauli ya awali kuhusu ongezeko la bei za umeme

Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), katika kikao chake cha tarehe 10 Desemba 2013 pamoja na mambo mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja hatua ambayo itaongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi na itaathiri uchumi wa nchi.

Maamuzi hayo yamefikiwa kufuatia tarehe 11 Oktoba 2013, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa EWURA. TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari 2014 na asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015.

Vilevile TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi ya kitanzania.

Maamuzi hayo ya Bodi ya EWURA ambacho ni chombo cha Serikali yamethibitisha kwamba Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo alisema uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013 alipowahakikishia wananchi kwamba bei ya umeme haitapanda hata baada ya TANESCO kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha bei ya umeme.


Aidha, kwa kuwa leo tarehe 9 Januari 2014 Waziri Muhongo amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kwamba sekta ya nishati sio porojo; natoa mwito kwake kuanza kwanza kujirekebisha yeye mwenyewe kwa kuacha porojo na uongo na kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuzuia utekelezaji wa maamuzi ya kupandisha bei ya umeme ambayo yataongeza ugumu wa maisha kwa wananchi kinyume na ahadi ya maisha bora kwa kila mtanzania iliyotolewa na CCM.

Pia, kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini natoa mwito kwa wote wenye kuathirika na maamuzi hayo ndani ya wiki moja kuanzia sasa watume maoni na mapendekezo yao kwa barua pepe kupitia anuani mbungeubungo@gmail.com

Maoni na mapendekezo hayo yanaweza pia kutumwa njia nyingine za kuwasiliana na Ofisi ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Maoni na mapendekezo hayo yahusu athari ambazo wamezipata na/au wanatarajia kuzipata kutokana na maamuzi hayo na mapendekezo ya hatua ambazo wanataka zichukuliwe.

Narajia kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wananchi mbalimbali hususan kutoka pia kwa wateja wa TANESCO ambao wamepandishiwa bei katika makundi yafuatayo: 

Kundi D1: Hili ni kundi la wateja wadogo wa majumbani, hasa vijijini, ambao hutumia wastani usiozidi wa Uniti 75 kwa mwezi. EWURA imeongeza wigo wa mahitaji ya umeme na kufikia uniti 75 kwa mwezi, kwa kile kilichoelezwa kuwa lengo likiwa ni kuongeza idadi ya wateja wa TANESCO wanaoweza kulipa kidogo kwa matumizi ya umeme kwa kiwango hicho, na pia kuwahamasisha kutumia zaidi umeme. Awali kundi hili lilikuwa linatunia wastani wa matumizi ya uniti 50 kwa mwezi. Bei mpya ni shilingi 100 kwa uniti moja, kutoka shilingi 60 za sasa, sawa na ongezeko la shilingi 40.

Kundi T1: Hili ni kundi la watumiaji wakubwa wa umeme majumbani, biashara ndogondogo, mashine za kukoboa na kusaga nafaka, taa za barabarani, mabango n.k. Bei iliyoidhinishwa ni shilingi 306 kwa uniti moja, ikiwa ni ongezeko la Shilingi 85 ya bei ya sasa. TANESCO ilipendekeza ongezeko la shilingi 131.

Kundi T2: Hili ni kundi la watumiaji umeme wa kawaida ambao hupimwa katika msongo wa volti 400, na ambao matumizi yao ya wastani kwa mwezi ni zaidi ya uniti 7,500 wateja wafanyabiashara kubwa, viwanda vya kati. Bei ya nishati iliyoridhiwa ni shilingi 205 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 73 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza ongezeko la shilingi 145 ya bei ya sasa.

Kundi T3-MV: Hili ni kundi la wateja wakubwa kama viwanda vikubwa waliounganishwa katika msongo wa kati (Medium Voltage). EWURA imeidhinisha bei ya nishati kwa kiwango cha shilingi 166 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 45 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza ongezeko la shilingi 148 kwa uniti moja.

Kundi T3-HV: Hili ni kundi la wateja wakubwa waliounganishwa katika msongo wa juu (High Voltage – Voti 66,000 na zaidi) ikiwa ni pamoja na ZECO, Bulyanhulu, na Twiga Cement. Bei iliyoidhinishwa ni shilingi 159 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 53 la bei ya sasa. TANESCO waliomba ongezeko la shilingi 80 kwa uniti moja.

Mara baada ya kupokea maoni na mapendekezo hayo, pamoja na hatua ambazo nitachukua kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nitawasilisha pia mapendekezo kwa Kambi Rasmi ya Upinzani kuchukua hatua za kibunge na CHADEMA kuchukua hatua za nje ya Bunge ili kunusuru uchumi wa nchi na kutetea maslahi ya wananchi.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini 
09/01/2014

8 comments:

Unknown said...

Ukweli athari ni kubwa sana maana uwezo wa kununua umeme umepungua sana. Mfana jana nimenunua umeme wa Tshs. 20,000/ nikapata unit 35 tu wakati kabla ya ongezeko hela hiyo hiyo ilinipatia unit 74! Kwa matumizi ya nyumbani kwangu hii ina maanisha umeme kwa siku 3 tu, unit 10 kwa siku!! Kwa wiki umeme wa shil. 40,000; kwa mwezi ni Tshs. 160,000/- Wapangaji wanatugomea ongezeko hili!! Hawaelewi!! Lazima tuone athari kwa uchumi mazingira nk

Anonymous said...

Kwa kipindi hiki tunachopambana na grobal walming inabidi tanesco wafanye mambo mawili ambayo ni ya msingi. Moja kuhakikisha wanasambaza umeme vijiji vyote. Pili kupunguza bei ya umeme. Hayo mambo yatasaidia ktk kuzuia matumiz ya mkaa na kuni.

PENHE said...

maelezo wanayotoa ya kuendesha shirika kwa hasara ni pamoja na taasisi nyingi za serikali ikiwapo wizara kutokulipia huduma wanazotumia. Matumizi ya Luku ni bora kwa kila anayetumia huduma itasaisia kupatikana kwa fedha zao na si kukimbilia kupandisha gharama za umeme sababu tunajua hata gesi ikiaanza kutumika kuzalisha umeme gharama hazitashuka. Hili linaonekana dhahiri kwenye bei ya sukari ambayo tangu imepaanda wakati wa mavuno haba haijawahi shuka na wafanyabiashara wetu wakililia kutokuagizwa kwa sukari nje wakati wao wanahozi kwenye maghala wakihitaji ihadimike wauze kwa gharama ya juu. Umeme unauzwa zanzibar, zanzibar nao wanashirika lao wanalipa ankara za umeme kwa shirika au na wao wanatumia kana kwamba wanazalisha wao?

Unknown said...

Mnyika ,mimi ni mshabiki wa chadema lakini si mwanachama na kamwe siwezi kuwa mwanachama wa chama chochote kwa kuwa vyama una na tbia ya kubadilika baada ya kufikia ngazi flani mfano ni ninyi wenyewe. umeme umeshapanda mara kadhaa (3 au zaidi) tangu wewe uwe Mbunge,na katika mara zote uwa unaongea na hakuna kinachobadilika ,kimsingi uwa unakamilisha wajibu wako tu wa kuongea lakini hakuna mabadiliko au faida ya yale tunayoongea.mfano kuna kipindi tuliambiwa umeme ungepanda kwa miezi sita tu na baada ya hapo ungerudi kama bei kalya ya ongezeko hilo lakini paka sasa hakuna kilichopunguzwa zaidi ya bei kuongeza. wasi wasi wangu ni juu ya uwezo wako wa kutatua tatizo hili kwa kuwa sijawahi kuona ukifanikiwa kila unapojaribu kulipigania hili.

yote ya yote ungera maana unajitahidi kuwasiliana nasi .


Soori said...

Binafsi sijui kwa nini serikali ya chama dhalimu cha ccm hawana huruma kwa wananchi wake.
Wanatakiwa wajiulize umeme umepanda asilimia 75 kwa watumiaji wa kawaida je?mishahara na vipato vya hawa watu vimepandishwa asilimia ngapi?
We need changes watanzania 2015 is just around the corner tutawaadhibu kwa kura.

Anonymous said...

Nimewahi kuhudhuria mara mbili mikutano ya EWURA ya kukusanya maoni ya bei ya umeme na maji. Mara zote jina la Mnyika limetajwa pamoja na yeye kutokuwepo kutokana na shinikizo analotoa la bei kushuka. Mara zote mbili bei ziliongezeka kidogo lakini si kwa kiwango ambacho TANESCO waliomba. Safari hii sikumsikia sana Mnyika kabla zaidi ya ujumbe alioandika wakati wa mgawo ambao alidokeza pia Serikali inakusudia kupandisha bei ya umeme na kututaka tupinge. Kamanda, je; kwa kuja sasa unaweza kushinikiza wabadili? Wapunguze?

Unknown said...

Kimsingi ongezeko la bei ya umeme halijazingatia maisha halisi ya mtanzania kwani gharama hizo ni kubwa ukilinganisha na maisha ya mwanananchi wa kawaida,TANESCO kwa miaka mingi imekua haifanyi vizuri ktk kujiendesha hii inatokana na mikataba mibovu ambayao serikali kupitia TANESCO imekua ikisani sambamba na rushwa iliyokithiri ktk taasisi hiyo, kutokana na hali hiyo TANESCO imeamua kuongeza bei kwa kudanganya umma kwamba ongezeko hilo ni kwa ajili ya kujiendesha na kuboresha huduma.Watanzaia wenzangu tulipinge hili kwanza umeme sio wa uhakika na huduma sio bora,pili EWURA wamekua wakiibeba Tanesco kwa kutoruhusu ushindani dhidi ya kampuni nyingine

Unknown said...

Kimsingi ongezeko la bei ya umeme halijazingatia maisha halisi ya mtanzania kwani gharama hizo ni kubwa ukilinganisha na maisha ya mwanananchi wa kawaida,TANESCO kwa miaka mingi imekua haifanyi vizuri ktk kujiendesha hii inatokana na mikataba mibovu ambayao serikali kupitia TANESCO imekua ikisani sambamba na rushwa iliyokithiri ktk taasisi hiyo, kutokana na hali hiyo TANESCO imeamua kuongeza bei kwa kudanganya umma kwamba ongezeko hilo ni kwa ajili ya kujiendesha na kuboresha huduma.Watanzaia wenzangu tulipinge hili kwanza umeme sio wa uhakika na huduma sio bora,pili EWURA wamekua wakiibeba Tanesco kwa kutoruhusu ushindani dhidi ya kampuni nyingine